Walimu wa Kiswahili Nchini Uganda: Changamoto na Njia za Kuimarisha Mafundisho

UTANGULIZI

Katika karne ya ishirini na moja, lugha ya Kiswahili imeendelea kupata hadhi ya kipekee si tu kama chombo cha mawasiliano bali pia kama kiungo muhimu cha ujumuishaji wa kikanda, hususan katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Uganda, kama mwanachama wa Jumuiya hiyo, imechukua hatua za kisera na kitaasisi kuimarisha nafasi ya Kiswahili katika mifumo yake ya elimu. Mwaka 2019, Kituo cha Kitaifa cha Maendeleo ya Mitaala (NCDC) kilifanya Kiswahili kuwa somo la lazima kwa wanafunzi wa shule za sekondari ya chini (Lower Secondary) katika mtaala mpya ulioanza kutekelezwa rasmi mwaka 2020. Hatua hii iliungwa mkono na agizo la Baraza la Mawaziri lililotangaza Kiswahili kuwa lugha rasmi ya pili ya taifa na somo la lazima katika ngazi ya sekondari.

Hata hivyo, licha ya juhudi hizi za kisera, walimu wa Kiswahili nchini Uganda wanakumbana na changamoto nyingi zinazohatarisha mafanikio ya utekelezaji wa mtaala mpya. Moja ya changamoto kuu ni kupuuzwa kwao katika mchakato wa ajira unaoendeshwa na Tume ya huduma za elimu (Education Service Commission) (ESC).

Mara kadhaa, nafasi za ajira zinazotangazwa na ESC huwa hazitoi vipaumbele kwa walimu wa Kiswahili, au zinaonyesha idadi ndogo ya nafasi ukilinganisha na masomo mengine na pengine hulenga walimu walio tu na stashahada na kuacha walio na shahada.

Hili linawakatisha tamaa wahitimu wa Kiswahili na kudhoofisha mtazamo chanya wa taaluma hii. Zaidi ya hayo, walimu waliopo shuleni hukosa rasilimali za kufundishia, hushindwa kupata mafunzo endelevu ya kitaaluma na hufanya kazi katika mazingira yasiyo na uungwaji mkono wa kijamii, ambapo jamii nyingi bado huiona lugha ya Kiswahili kwa mtazamo hasi.

Makala hii inalenga kuchambua kwa kina changamoto hizo kwa kuangazia uzoefu halisi wa mwalimu wa Kiswahili katika Uganda ya leo na kutoa mapendekezo ya kisera na kimkakati yatakayosaidia kuinua hadhi na ufanisi wa ufundishaji wa Kiswahili katika mazingira ya sasa.

CHANGAMOTO KUU ZA MWALIMU WA KISWAHILI NCHINI UGANDA

1. Mitazamo hasi ya Jamii kuhusu Kiswahili

Katika jamii nyingi nchini Uganda, lugha ya Kiswahili bado haijapata hadhi inayostahili licha ya kuwa lugha ya pili rasmi kisheria. Wazazi, wanafunzi na hata baadhi ya viongozi wa shule huendelea kuliona somo la Kiswahili kama lisilo na manufaa ya moja kwa moja kimasomo wala kikazi, jambo linaloathiri kwa kiasi kikubwa msimamo wa jamii kuhusu umuhimu wake.

Wanafunzi wengi huchukua somo hili kwa shingo upande huku wazazi wakihusisha Kiswahili na matumizi ya mitaani, biashara zisizo rasmi au hata uhalifu kutokana na historia ya kijeshi ya lugha hii nchini. Hali hii huathiri kwa kiwango kikubwa ari ya wanafunzi kujifunza na motisha ya walimu kufundisha.

Ripoti ya Twaweza East Africa (2016) ilibainisha kuwa kiwango cha uelewa wa wazazi juu ya nafasi ya Kiswahili katika mfumo wa elimu ni cha chini mno, hali inayoendeleza mitazamo hasi. Mwalimu wa Kiswahili analazimika kuibua mbinu za ziada za kusisimua ili kuvutia wanafunzi kuchukua Kiswahili katika kidato cha tatu na nne, hali inayoongeza mzigo wa kazi kuliko walimu wa masomo mengine yenye hadhi ya juu kijamii kama Kiingereza, Fizikia, Hisabati na masomo mengine ya sayansi.

2. Ukosefu wa Rasilimali za Kufundishia na Kujifunzia

Pamoja na Kiswahili kufanywa kuwa somo la lazima katika mtaala wa sekondari ya chini, shule nyingi nchini Uganda bado hazina vifaa vya kutosha vya kufundishia na kujifunzia somo hili. Katika shule nyingi za vijijini na hata mijini, walimu wa Kiswahili hulazimika kutumia vitabu vichache vilivyopo au kujitengenezea nyenzo za kufundishia zisizo na ubora wa kitaaluma.

Maktaba nyingi hazina vitabu vya Kiswahili vya mtaala mpya, na mara nyingi walimu hulazimika kufundisha kwa kubuni au kuazima nyenzo kutoka kwa shule nyingine. Vilevile, kuna upungufu wa matumizi ya kidijitali yaliyoandaliwa kwa Kiswahili ambayo yangesaidia kufundisha somo hili kwa mbinu bunifu zinazolenga kizazi cha sasa kinachovutiwa zaidi na teknolojia. Ukosefu huu wa rasilimali huathiri mbinu za ufundishaji, ubora wa somo na hata matokeo ya wanafunzi. Katika baadhi ya maeneo, hata kamusi za msingi au vifaa vya kielimu kama projekta havipo kabisa kwa ajili ya somo la Kiswahili.

3. Kupuuziwa Katika Ajira na Uhamisho wa Walimu

Changamoto kubwa na ya kushangaza inayomkumba mwalimu wa Kiswahili ni kupuuzwa kwake katika mchakato wa ajira na uhamisho wa walimu wa sekondari unaofanywa na Kamisheni ya huduma za elimu nchini Uganda (ESC). Licha ya Kiswahili kutambulika kama somo la lazima, nafasi za ajira kwa walimu wa Kiswahili hutangazwa kwa idadi ndogo sana au kupuuzwa kabisa ukilinganisha na masomo mengine. Hali hii husababisha upungufu mkubwa wa walimu wa Kiswahili katika shule nyingi, huku waliopo wakibeba mzigo wa kufundisha madarasa mengi bila msaada.

Kwa mfano, katika baadhi ya matangazo ya ajira yaliyochapishwa kati ya mwaka 2021 na 2024, idadi ya nafasi kwa walimu wa Kiswahili ilikuwa ni ya chini mno au haikutajwa kabisa, tofauti na masomo hasa ya kisayansi. Hili limepelekea baadhi ya walimu wa Kiswahili kukata tamaa, wengine kubadilisha taaluma na wengi kuendelea kufanya kazi katika sekta zisizo rasmi. Kutotambuliwa huku kunadhalilisha taaluma ya Kiswahili na kuathiri hadhi ya mwalimu katika jamii ya kielimu nchini Uganda.

4. Ukosefu wa Mafunzo Endelevu ya Ualimu (Continuous Professional Development – CPD)

Katika mazingira ya elimu yanayobadilika kila uchao, walimu wanapaswa kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuhuisha mbinu zao za ufundishaji, kuboresha ujuzi wao wa kitaaluma na kuendana na mahitaji ya mtaala mpya. Hata hivyo, walimu wa Kiswahili nchini Uganda mara nyingi hukosa fursa za mafunzo endelevu ya ualimu. Mtaala mpya wa sekondari ya chini unaolenga kujifunza kwa msingi wa umilisi (competency-based curriculum) unahitaji mbinu mpya za ufundishaji zinazojikita katika kazi shirikishi, teknolojia, tathmini endelevu na maudhui jumuishi.

Kwa bahati mbaya, walimu wa Kiswahili hawajapewa mafunzo ya kutosha kuhusu namna bora ya kufanikisha utekelezaji wa mtaala huu. Ripoti ya Taasisi ya Mafunzo ya Walimu (Teacher Training Education Project, 2023) ilionyesha kuwa zaidi ya 60% ya walimu wa Kiswahili waliohojiwa hawakuwahi kushiriki mafunzo yoyote ya mtaala mpya tangu kuanzishwa kwake mwaka 2020. Hali hii hupelekea walimu kufundisha kwa mazoea ya zamani, kushindwa kutumia mbinu bunifu na hivyo kupunguza ufanisi wa ufundishaji. Ukosefu huu wa CPD pia unawanyima walimu fursa ya kujifunza kutoka kwa wenzao, kusambaza mbinu bora na kujenga mtandao wa kitaaluma unaowawezesha kukua katika taaluma yao.

5. Kutotumika kwa Teknolojia kwa Ufanisi Katika Kufundisha Kiswahili

Katika karne ya 21, teknolojia imekuwa nyenzo kuu ya kuimarisha elimu kupitia njia mbalimbali kama ujifunzaji wa mtandaoni, matumizi ya video, simulizi za kidijitali na majukwaa ya kijamii ya kielimu. Hata hivyo, katika mazingira ya shule nyingi za Uganda, hususan maeneo ya vijijini, mwalimu wa Kiswahili hukumbwa na changamoto ya kutotumia teknolojia kwa ufanisi kwa sababu ya ukosefu wa vifaa, maarifa, au miundombinu. Wakati baadhi ya masomo kama Hisabati, Biolojia, na Kiingereza yameanza kunufaika na maudhui ya kidijitali yaliyoandaliwa na NCDC au mashirika ya elimu kama Kolibri na UNESCO, Kiswahili bado ni nyuma.

Matokeo yake, walimu hulazimika kutegemea ubao, nakala chache za vitabu, au masimulizi ya mdomo, jambo linalopunguza ubunifu na mvuto wa somo kwa wanafunzi wa kizazi cha kidijitali cha leo. Zaidi ya hayo, tafiti za ndani kama ile ya Makerere Institute of Social Research (2022) zinaonesha kuwa walimu wengi wa Kiswahili hawajapewa mafunzo ya kutumia vifaa vya TEHAMA (ICT) katika ufundishaji, jambo linaloongeza pengo la maarifa ya teknolojia katika lugha. Hii inawafanya walimu kuwa nyuma katika kutumia video za kielimu, audiobooks, mifumo ya tafsiri, au hata programu za mawasiliano kama Google Classroom na Zoom kwa madhumuni ya kufundisha Kiswahili kwa njia ya kisasa.

6. Mzigo mkubwa wa kazi kwa walimu wa Kiswahili kutokana na ukosefu wa ajira rasmi

Katika shule nyingi za sekondari nchini Uganda, serikali imekosa uwezo wa kuajiri walimu wa Kiswahili waliohitimu na waliosajiliwa, licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya walimu wasioajiriwa. Hali hii imepelekea mzigo mkubwa kwa walimu wachache waliopo kwenye ajira rasmi ambao mara nyingi hulazimika kufundisha madarasa mengi zaidi ya uwezo wao, jambo linalopunguza ubora wa ufundishaji. Kwa mfano, mwalimu mmoja wa Kiswahili anaweza kufundisha zaidi ya madarasa saba, kila darasa likiwa na wanafunzi zaidi ya 80, hali inayochangia uchovu wa mwalimu na kushindwa kumfuatilia mwanafunzi mmoja mmoja kikamilifu.

Ripoti ya Tume ya Huduma za Elimu (Education Service Commission, 2023) na tafiti za Taasisi ya Utafiti ya Elimu (Education Policy Review Uganda, 2023) zinaonesha kuwa zaidi ya 55% ya walimu wa Kiswahili waliostahili kuajiriwa bado wako nje ya mfumo wa ajira ya serikali. Serikali haijatekeleza kikamilifu jukumu lake la kuajiri walimu hawa, jambo ambalo limeleta mzigo usio wa kawaida kwa walimu waliopo. Hali hii siyo tu inaathiri ubora wa elimu bali pia huathiri motisha na ufanisi wa walimu waliopo kwa sababu wanajisikia kutothaminiwa na kukumbwa na kazi nyingi zaidi ya uwezo wao.

MIKAKATI YA KUTATUA CHANGAMOTO

1. Kuongeza ajira rasmi kwa walimu wa Kiswahili kupitia Tume ya Huduma za Elimu (ESC)

Ili kushughulikia changamoto ya uhaba wa walimu wa Kiswahili katika shule za sekondari nchini Uganda, serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kwa kuajiri walimu waliomaliza mafunzo yao hasa walimu wa ngazi ya shahada na uzamili. Tangu mwaka 2020, ambapo Kiswahili kilianzishwa rasmi kama somo la lazima katika mtaala mpya wa sekondari ya chini, kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya walimu wa Kiswahili; hata hivyo, utekelezaji wa ajira rasmi umekuwa hafifu.

Tume ya Huduma za Elimu (Education Service Commission) inapaswa kupewa rasilimali na mamlaka ya kutangaza nafasi za ajira kila mwaka kwa walimu wa Kiswahili. Kuongeza ajira kutasaidia kupunguza mzigo mkubwa wa kazi kwa walimu waliopo, kuboresha uwiano kati ya walimu na wanafunzi na kuinua kiwango cha ufundishaji wa Kiswahili katika shule za umma. Aidha, mpango wa kuajiri walimu unatakiwa kuzingatia maeneo ya vijijini ambako upungufu wa walimu ni mkubwa zaidi. Utafiti wa Education Policy Review Uganda (2023) unapendekeza kuanzishwa kwa mfuko maalum wa ajira kwa masomo yanayopanuka kimkakati kama Kiswahili ili kusaidia utekelezaji wa mtaala kwa ufanisi.

2. Kutoa motisha na marupurupu kwa walimu wa Kiswahili

Moja ya hatua muhimu ya kuboresha hali ya ufundishaji wa Kiswahili nchini Uganda ni kuhakikisha kuwa walimu wa somo hili wanapewa motisha ya kutosha. Walimu wa Kiswahili wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutothaminiwa ikilinganishwa na walimu wa masomo mengine kama sayansi ambao hata serikali imewaongeza mshahara na mara nyingi hupewa marupurupu ya ziada. Ukosefu huu wa motisha umeathiri ari ya walimu na kusababisha baadhi yao kutafuta ajira mbadala au kushindwa kujituma kikamilifu katika kazi zao.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Michezo (MoES) inapaswa kuweka sera za kutoa marupurupu ya ziada kwa walimu wa Kiswahili, hasa wale wanaofundisha katika mazingira magumu au shule zenye uhaba mkubwa wa walimu. Aidha, ni muhimu kuanzisha mpango mkakati wa kutambua walimu wanaofanya kazi kwa ubunifu na kujitolea kwa dhati kupitia tuzo, vyeti vya kutambuliwa au kupandishwa madaraja mapema. Hatua hizi zitaleta motisha ya ndani (intrinsic motivation) na kusaidia walimu kuboresha utendaji wao wa kazi.

3. Kuwajengea walimu wa Kiswahili uwezo kupitia mafunzo endelevu ya kitaaluma (CPD)

Mojawapo ya changamoto kuu zinazowakabili walimu wa Kiswahili ni ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara yanayolenga kuendeleza ujuzi na mbinu zao za kufundisha. Mafunzo Endelevu ya Kitaaluma (Continuous Professional Development – CPD) ni muhimu ili kuhakikisha walimu wanabaki na maarifa ya kisasa, hasa kwa muktadha wa mabadiliko ya mitaala kama ule wa sekondari ya chini ulioanza mwaka 2020 chini ya usimamizi wa NCDC. Walimu wengi wa Kiswahili nchini Uganda walikosa ushiriki wa kutosha katika mafunzo haya, jambo lililosababisha changamoto katika utekelezaji wa mtaala mpya.

Ili kuziba pengo hili, serikali inapaswa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu, vyama vya walimu wa Kiswahili kama vile Watetezi wa Kiswahili Uganda (WAKIU), Chama cha Kiswahili taifa Uganda (CHAKITAU) na mashirika ya kimataifa kama Twaweza na UNESCO kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa walimu wa Kiswahili. Mafunzo haya yawe ya vitendo, yakiwapa walimu fursa ya kujifunza mbinu mpya za kufundishia lugha, matumizi ya teknolojia katika darasa, tathmini ya wanafunzi na ujifunzaji unaomlenga mwanafunzi. Aidha, mafunzo haya yafanyike kwa awamu na maeneo tofauti (kwa mfano kila baada ya muhula mmoja) na yawe na uthibitisho rasmi kama kupewa cheti cha kumaliza (certificate of completion) ili kuongeza thamani ya kitaaluma kwa mshiriki.

Kwa kuongezea, walimu wa Kiswahili wanapaswa kupewa fursa za mara kwa mara za mafunzo ya kitaaluma (Continuous Professional Development) na kuhimizwa kushiriki katika warsha, semina na makongamano ya Kiswahili ili kuendeleza ujuzi wao na kuwa sehemu ya maendeleo ya lugha hiyo katika kanda nzima ya Afrika Mashariki.

4. Kuimarisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia Kiswahili

Serikali kwa kushirikiana na NCDC na Bodi ya Kitaifa ya Mitihani ya Uganda (UNEB), inapaswa kuwekeza katika kuchapisha na kusambaza vitabu bora vya Kiswahili vilivyowekwa kwa mujibu wa mtaala. Pia, kuna haja ya kuendeleza mifumo ya kidijitali kama maktaba za mtandaoni au programu za kielimu zinazowawezesha walimu na wanafunzi kupata maudhui ya Kiswahili kwa urahisi. Mbali na vitabu, shule zinahitaji vifaa vya ziada kama kamusi, rekoda za sauti, vifaa vya video na hata vifaa vya michezo ya kuigiza kwa lengo la kukuza ujifunzaji wa Kiswahili kwa njia shirikishi.

Vile vile, Bodi ya kitaifa ya mitihani (UNEB) ikishirikiana na NCDC waweke njia mbadala za kuelimisha walimu na wanafunzi wa Kiswahili misingi ya utathmini na njia za kupita Kiswahili. Tatizo lililotokea mwaka wa 2024 katika matokeo ya mithani ya kitaifa ni kwamba, Kiswahili kama somo halikupitwa na wanafunzi wengi nchini. Jambo hili lilichangia pakubwa sana kupunguza idadi ya wanafunzi wanaochukua Kiswahili kama chaguo lao/somo la hiari kidato cha tatu. Mambo kama haya kwa somo kama Kiswahili ambalo lina historia mbaya hutatiza maendeleo yake nchini Uganda na linastahili kusuluhishwa haraka iwezekanavyo.

5. Kuimarisha Ushirikiano Kati ya Walimu wa Kiswahili Kupitia Mitandao ya Kitaaluma

Ushirikiano wa kitaaluma kati ya walimu wa Kiswahili ni msingi muhimu wa kubadilishana maarifa, uzoefu na mbinu bora za kufundishia. Hata hivyo, walimu wengi wa Kiswahili nchini Uganda hawana fursa ya kushiriki katika mitandao ya kitaaluma inayowawezesha kujifunza kutoka kwa wenzao. Ukosefu huu wa ushirikiano umesababisha baadhi yao kufundisha kwa kutumia mbinu zilizopitwa na wakati au kushindwa kushughulikia changamoto zinazowakabili kwa ufanisi.

Ni muhimu kwa Wizara ya Elimu, mashirika yasiyo ya kiserikali na vyama vya walimu kama WATETEZI WA KISWAHILI UGANDA (WAKIU) kuimarisha na kupanua mitandao ya walimu wa Kiswahili kwa njia ya warsha, makongamano na makundi ya mtandaoni (online forums) ya kitaaluma. Mitandao hii iwawezeshe walimu kushiriki mijadala, kubadilishana zana za kufundishia na kujifunza mbinu mpya kama vile ujifunzaji wa kidijitali, mawasiliano kwa njia ya mitandao ya kijamii na tathmini ya wanafunzi.

Aidha, mitandao hii inaweza kutumika kama njia ya kushawishi sera kwa mfano kuwasilisha hoja kwa serikali kuhusu ajira, vifaa vya kufundishia, au nafasi za mafunzo. Ushirikiano huu utawafanya walimu wa Kiswahili wahisi kuwa sehemu ya jamii ya kitaaluma inayothamini mchango wao, hivyo kuongeza motisha na kuimarisha ubora wa somo hili katika shule za sekondari nchini Uganda.

6. Kuanzisha Klabu za Kiswahili katika Shule kwa Lengo la Kukuza Upenzi wa Lugha

Uanzishaji wa klabu za Kiswahili katika shule ni mojawapo ya mbinu bora za kukuza hamasa na upendo wa wanafunzi kwa lugha ya Kiswahili. Katika shule nyingi nchini Uganda, wanafunzi hukosa fursa za nje ya darasa zinazowawezesha kutumia Kiswahili kwa hali ya mazoea, jambo linaloathiri ufasaha wao na uelewa wa matumizi halisi ya lugha. Klabu za Kiswahili huweza kutoa jukwaa la mazoezi ya kuzungumza, uandishi wa ubunifu, michezo ya kuigiza, mashairi, mijadala na hafla mbalimbali za Kiswahili.

Kwa mujibu wa tathmini ya mashirika ya elimu kama Uwezo Uganda, ujifunzaji wa lugha yoyote huhitaji mazingira ya vitendo, ambapo mwanafunzi anatumia lugha kwa namna ya mawasiliano ya kila siku. Klabu za Kiswahili zinaweza kujikita katika kusaidia wanafunzi kukuza ustadi wa kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika—stadi nne kuu za lugha.

Ili kuhakikisha ufanisi wa klabu hizi, Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Michezo (MoES) kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (MEACA) inapaswa kuzijengea uwezo na kuzifadhili rasmi. Ufadhili huo unaweza kuchukua sura ya msaada wa kifedha kwa ajili ya vifaa vya kufanyia shughuli, mafunzo kwa walezi wa klabu, pamoja na uratibu wa mashindano ya kitaifa kama vile insha, ushairi na michezo ya kuigiza. Shughuli hizi zitawapa wanafunzi jukwaa la kuonyesha vipaji vyao huku wakikuza mazoea ya kutumia Kiswahili kwa ufasaha.

7. Kushirikisha Vyombo vya Habari Katika Uendelezaji wa Kiswahili

Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuhamasisha matumizi na hadhi ya lugha yoyote katika jamii. Katika muktadha wa Uganda, vyombo vya habari kama redio, runinga, magazeti na majukwaa ya kidijitali vinaweza kuwa nyenzo muhimu ya kueneza na kuimarisha matumizi ya Kiswahili, hasa kwa vijana na jamii kwa ujumla. Hata hivyo, lugha ya Kiswahili bado haijapewa uzito unaostahili katika vyombo vingi vya habari nchini Uganda ukilinganisha na Kiingereza na Luganda.

Kwa mfano, ni vituo vichache vya redio na runinga vinavyotangaza vipindi kwa Kiswahili kwa ukawaida, na idadi ya wanahabari waliobobea katika Kiswahili ni ndogo. Hali hii huathiri mitazamo ya kijamii kuhusu lugha hii, ambapo wengi huihusisha na wasio na elimu ya juu au watu wa tabaka la chini. Ili kubadili hali hii, ni muhimu kwa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuanzisha sera na kampeni mahsusi za kuhamasisha matumizi ya Kiswahili katika vyombo vya habari.

Kampeni hizi zinaweza kujumuisha mafunzo kwa wanahabari kuhusu uandishi wa Kiswahili sanifu, uzinduzi wa vipindi vya redio na runinga kwa Kiswahili, pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya Kiswahili katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya elimu, burudani na taarifa. Pia, ni vyema kuanzishwa mashindano ya uandishi wa habari kwa Kiswahili au vipindi vya ubunifu vinavyochochea matumizi ya lugha hii.

Hatua hii itasaidia kupanua hadhira ya Kiswahili, kuimarisha matumizi yake katika maisha ya kila siku, na kuinua hadhi yake kitaifa na kikanda.

Hitimisho

Changamoto zinazowakumba walimu wa Kiswahili katika karne ya 21 nchini Uganda ni changamoto zinazohitaji kushughulikiwa kwa haraka na kwa ushirikiano wa wahusika wote, ikiwemo serikali, taasisi za elimu, walimu wenyewe, na wadau wa lugha. Kukabiliana na changamoto hizi ni muhimu ili kuhakikisha kuwa Kiswahili kinaendelea kuwa lugha yenye thamani kubwa katika mfumo wa elimu na jamii kwa ujumla, na ili kuendeleza mahusiano ya kijamii na kiuchumi ndani ya Afrika Mashariki.

Ninawahimiza walimu wa Kiswahili kushirikiana kwa karibu, kubadilika na kukubali mbinu mpya za ufundishaji, na kuendelea kujifunza ili kuendana na mabadiliko ya taaluma. Ushirikiano huu utasaidia kuleta tija zaidi darasani na kukuza lugha ya Kiswahili kwa ufanisi zaidi.

Mwisho, ni lazima tukumbuke maneno ya mshairi maarufu, “Lugha ni daraja la mawasiliano na utamaduni.” Kwa hiyo, tukitunza na kuendeleza Kiswahili, tunajenga daraja thabiti la kuunganisha watu wa kanda yetu na kuzalisha fursa mpya za maendeleo kwa vizazi vijavyo.

4 thoughts on “Walimu wa Kiswahili Nchini Uganda: Changamoto na Njia za Kuimarisha Mafundisho

  1. Shukrani mheshimiwa kwa kusambaza injiri ya lugha ya kiswahili……Kiswahili Leo kiswahili kesho…..

    Like

  2. Ni changamoto kweli je, Kuna namna yoyote naweza shirikiana katika mchakato huo wa kueneza somo la kiswahili Huko Uganda?
    On Sun, Jun 8, 2025, 6:51 AM Jifunze Kiswahili na mwalimu Johnpaul

    Like

Leave a reply to Nuwagaba Dickens Cancel reply