NDOTO YA JUMA
Juma alikuwa mvulana mdogo aliyekulia katika kijiji cha Nkoma, Wilaya ya Mbale. Katika kijiji chao, nyumba nyingi zilijengwa kwa matope na ziliezekwa kwa nyasi au mabati. Watoto walikuwa wanapenda kuchezea nje bila viatu, wakikimbia mashambani kama swala wanaoikimbia upepo na kuruka kwenye madimbwi ya maji baada ya mvua.
Siku zote, Juma alikuwa akisikia watu wakizungumza kuhusu Kampala, mji mkubwa wenye majengo marefu, magari mengi na maisha ya kisasa. Kwa akili yake ndogo, Kampala ilionekana kama mbinguni lakini yeye hakuwahi kufika huko.
Siku moja, baba yake alikuja nyumbani akiwa na barua. “Juma, mjomba wako Karim amekuandikia barua. Anataka uende kumtembelea Kampala!” Baba yake alisema kwa furaha.
Juma aliruka kwa furaha na kucheka hadi mbavu zipasuke! “Kweli baba? Nitakwenda Kampala?” aliuliza kwa mshangao.
Mama yake alimtazama kwa upendo. “Sasa utajifunza mambo mapya, lakini kumbuka kuwa na nidhamu na kumheshimu mjomba wako,” alisema huku akimpakia nguo kwenye mfuko wake mdogo.
Asubuhi ya safari, Juma aliamka mapema na kuvaa nguo zake mpya. Lakini lilikuwa jambo la kushangaza kwake kuvaa viatu kwa mara ya kwanza! Miguu yake ilikuwa haijazoea, hivyo alitembea kwa shida kidogo kama kuku aliyevalishwa viatu.
Baba yake alimchukua boda boda stage kumpeleka kituo cha basi cha YY Coaches mjini Mbale. Juma alikuwa na hofu lakini pia alifurahia upepo uliokuwa ukipiga usoni mwake walipokuwa wakienda kwa mwendo wa kasi kwenye boda boda.
Walipofika katika kituo cha basi, baba yake alinunua tiketi na kumpa kondakta wa basi. “Juma, utakapofika, mjomba wako atakupokea kutoka kituo cha basi cha Namayiba. Usijali, uwe makini,” alisema baba yake kwa upole.
Basi lilianza kujaza abiria, wengi wao wakiwa wanazungumza Kigisu, lugha ya Kibukusu, na Kisamya ambazo Juma aliielewa vizuri. Wengine walikuwa wakizungumza kwa sauti kubwa, wakicheka na hata kupeana viazi vilivypikwa na Muhogo iliyochomwa vizuri. Kwa Bahati mbaya, Juma alikuwa na chakula chake alichopikiwa na nyanya yake katika majani ya ndizi.
Hatimaye, basi la YY liliondoka Mbale likielekea mjini Kampala likiangazia milima na mabonde sehemu za Kamonkoli. Juma alishangazwa na mazingira mazuri ya basi na televisheni iliyokuwa ikichezwa basini.
Walipokaribia Mukono, Juma aliona mabadiliko makubwa. Ghafla, lugha ya Kigisu haikusikika tena bali watu wote walikuwa wakizungumza Kiganda! Juma hakuelewa Kiganda, hivyo alibaki kimya akisikiliza kwa makini lakini bila kuelewa chochote. Ilikuwa kama kila mtu alikuwa akizungumza kwa haraka, sauti zikichanganywa kama nyuki katika mzinga wao.
Ghafla, sauti nzito yenye harufu kali ya pombe ilimkatiza mawazo. “Eh we, kijana wa kijijini, mbona unanuka jasho kama ng’ombe wa soko?” Juma aliinamisha kichwa chake kwa heshima, lakini harufu ya pombe ilizidi kumchoma puani. Mukwasi, mwanamume mwenye sura iliyojaa ukali na macho mekundu kama damu, alimkodolea macho huku akicheka kwa dharau. “Unatoka wapi? Nkoma? Aaah! Hawa watu wa kijijini, mnaingia mjini kama mnaenda kuona miujiza!” Aliendelea kumkejeli huku abiria wengine wakihisi aibu. Lakini Juma alikaa kimya, akishikilia uvumilivu wake kama mti unaostahimili upepo mkali.
Lakini dakika chache baadaye balaa ilimshukia Mukwasi. Basi lilipofika kwenye kona kali, ghafla dereva alishika breki na chupa ya pombe aliyokuwa ameificha mfukoni ilianguka na kuvunjika. Pombe ilimwagika basini na harufu mbaya ikajaa ndani ya basi. Abiria waligeuka kumtazama kwa hasira. “Huyu mtu ana matatizo gani?” Mmoja wao aliuliza kwa ukali.
Abdu mwislamu ambaye yeye na pombe hawapendani hakuvumilia mnuko wa pombe. Alitoka ghafla na kumshika Mukwasi mkono na kumkaripia, “Kama huwezi kuheshimu wenzako, shuka upate special!” Kwa aibu, Mukwasi alikaa kimya, akikunja uso wake kama mtoto aliyekamatwa akifanya makosa. Juma alitabasamu kwa ndani akijua kwamba subira ni silaha ya wenye busara.
Alikuwa akishangaa, “Kwanini lugha inabadilika ghafla?”
Lakini jambo lililomvutia zaidi lilikuwa Colline Hotel, hoteli kubwa iliyosimama kwa fahari karibu na barabara. Ilikuwa na mwangaza wa kuvutia sana mud awa saa moja jioni na majengo yake yalikuwa makubwa sana! Juma aliinua macho kupitia dirisha la basi karibu aanguke chini na kusema kwa mshangao na kwa sauti ya juu, “Hii ni nyumba au kasri la mfalme wa Buganda Kabaka Mutebi?”
Basi lilipoendelea na safari, Juma aliona kitu kingine cha kushangaza—Namboole Stadium! Siku zote alipokuwa kijijini Nkoma, babu yake alikuwa akiisikiliza Radio Mbale, na jina Namboole Stadium lilitajwa mara kwa mara kwenye matangazo ya michezo.
Lakini leo, kwa macho yake mwenyewe, aliiona! Uwanja huo mkubwa ulisimama kifahari, ukimkodolea macho kana kwamba ulikuwa ukimkaribisha kwa tabasamu. Mwangaza wake ulipenyeza hadi kumulika eneo la Kireka kote. Majengo yake yalionekana yamejawa na uhai, yakimwita Juma kwa sauti ya kimya kimya.
Juma alijikuta akitabasamu, moyo wake ukilipuka kwa furaha. “Hakika, sikio halidanganywi na hadithi, lakini jicho huona ukweli!” Aliwaza huku akiendelea kutazama kwa mshangao, akihisi kana kwamba alikuwa ameingia katika ndoto nzuri isiyo na mwisho.
“Kweli hii ndiyo Namboole?” alijiuliza kwa mshangao. Ilikuwa kubwa sana, rangi ya manjano na nyeupe iking’aa sana kama dhahabu. Alihisi kama ndoto.
Baada ya muda mfupi, basi liliingia Kampala. Barabara zilikuwa zimejaa magari mengi, watu walitembea haraka kama mawimbi ya bahari na majengo yalikuwa marefu kuliko yote aliyowahi kuona. Aliendelea kutazama tazama na kushangaa. Macho yake yalikuwa hayatosheki, maana kweli mgeni njiani huona mengi.
Mjomba wake Karim alikuwa akimsubiri katika kituo cha basi cha Namayiba. “Karibu Juma!” alisema huku akimkumbatia kwa furaha.
Nyumbani kwa Mjomba Karim
Walifika nyumbani kwa mjomba wake, na Juma akashangaa tena! Nyumba hiyo ilikuwa kubwa na nzuri, ikiwa na rangi za kupendeza, vioo vikubwa viling’aa kama nyota angani, na bustani iliyojaa maua yenye harufu nzuri kama marashi ya waridi.
Walipoingia ndani, Juma aliona sebule yenye makochi laini yaliyomfanya ahisi kama amekalia mawingu. Chumba cha kulala kilikuwa na kitanda kikubwa chenye shuka safi na nyeupe pee kama theluji. Shuka zilikuwa zimepangwa kwa umaridadi huku chumba cha maakuli kikiwa na meza ndefu na viti vya kisasa tunavyoona kwenye redio.
Jikoni, Juma aliona jiko la gesi, jokofu lilikuwa limejaa vinywaji matunda mazuri sana yanayopendeza. Bafu lenye bomba la mvua lililotoa maji ya moto na baridi wakati ukihitaji. Ungeongea tu halafu maji yajipike maramoja yajimwage pale unawe….maisha yalikuwa superb….
Juma alihisi kama ameingia katika ulimwengu wa maajabu, mahali ambapo kila kitu kiling’aa kama dhahabu, harufu ya hewa ilikuwa tamu kama asali na kila kona ya nyumba ilimfanya ahisi kama mfalme katika kasri lake la kifalme!
Alikumbuka jinsi alivyosimama nje ya nyumba yao siku moja, akitazama mbingu iliojaa nyota. Aliwaza, “Kampala ni wapi? Kuna nini huko?” Katika mawazo yake, aliiona Kampala kama nchi ya nyingine, iliyojaa majengo marefu yanayofika mawinguni, magari yanayoruka hewani na watu wanaovaa mavazi ya kifahari. Kila wakati alipomsikia mtu akisema amekwenda Kampala, moyo wake ulipiga kwa kasi mara mia katika dakika moja akihisi kana kwamba anapaswa kuwa sehemu ya safari hiyo kubwa. Lakini sasa, ndoto hiyo iligeuka kuwa kweli!
Siku zilipita haraka. Juma alijifunza mambo mengi mjini. Alitembea na mjomba wake katikati ya jiji, aliona maduka makubwa na taa zinazowaka usiku kucha kama nyota mbinguni.
Siku moja mjombake aliamua kumchukua Juma Pamoja na Watoto wake wengine kwa wiikendi kama ilivyokawaida yao. Waliamua Kwenda Akamwesi Mall Kyebando karibu na kwao nyumbani. Walifurahia chakula kama kuku, Samaki, nyama ya mbuzi na aiskrimu. Juma ilikuwa mara yake ya kwanza kuonja hivi vyote, alikuwa amezoea mboga za mashambani na unga wa mtama.
Siku hiyo ya wikendi, familia ya mjomba ilikuwa na shughuli nyingi ikiwemo kuogelea. Walikuwa wamepanga kwenda kwenye swimming pool na Juma alijua kuwa hii ingekuwa ni mara yake ya kwanza kuogelea kwenye bwawa la kisasa la mjini.
Watoto wa mjomba wake walikuwa wamevaa mavazi ya kuogelea ya kisasa, huku wakicheka na kujiandaa kwa furaha. Juma alijua kuwa hali ilikuwa tofauti na alivyokuwa amezoea kijijini ambapo angevua nguo na kuogelea uchi kwenye mto wa Nkoma. Alikuwa amezoea maji ya mto ambako hakukuwa na haja ya mavazi.
Alijivua haraka haraka akiwa na furaha na akaenda kuelekea bwawani akijua kuwa alikuwa tayari kwa kuingia. Aliweka mguu mmoja kwenye bwawa la maji safi na baridi, na alikuwa tayari kuingia yote. Lakini kabla hajazidi, mhudumu wa bwawa alikimbia kwa haraka akamshika kwa nguvu na kusema kwa sauti kubwa, “Hapana, hapana! Hapa siyo kijijini! Lazima uvae mavazi ya kuogelea!” Watu wote wazazi wa Watoto na dada pamoja na kaka zake wakiangusha vicheko. Walimuona Juma mtoto wa miaka kumi na tano kijibastola kikibembeabembea kama matawi ya miti ikiyumbishwa na upepo. Vicheko karibu viwaue.
Juma aliguswa na kushangaa. Alijua kuwa alikuwa amekosea, lakini hakuwa na ufahamu wa jinsi watu wa mjini walivyoishi. Watoto wa mjomba wake walicheka kwa kejeli wakimwambia, “Hapa siyo mto Nkoma huko kijijini, Juma! Hapa tunavaa mavazi!” Watoto walichanganya Kiingereza kingi ambacho, “Juma hakuelewa vizuri. Juma hapa we use swimming costumes please”!
Walikuwa wanacheka, lakini walijua kuwa Juma alikuwa tu akijivunia tabia yake ya kijijini. Mhudumu alimuonyesha mavazi ya kuogelea, akimsaidia kumvalisha polepole. Juma alijua kuwa alikuwa amekosea lakini alipenda kuendelea kujifunza na alikubali kwa aibu kidogo.
Baada ya kumaliza, alijua kuwa alikuwa tayari kwa kuogelea kama watoto wa mjomba wake. Aliingia kwenye bwawa. Waliogelea kwa furaha wakicheka na kushindana, huku Juma akifurahi kwa kuona jinsi alivyokuwa anajivunia kuwa sehemu ya familia ya mjomba wake mjini.
Baada ya wiki mbili mjini, ulikuwa ni wakati wa kurudi kijijini. Juma aliaga mjomba wake na kupanda basi la YY Coaches kurudi Mbale.
Aliporudi kijijini Nkoma, watoto wote walimzunguka wakitaka kusikia hadithi kuhusu Kampala.
Maswali ya mazoezi
- Fafanua madhari ya dondoo hili.
- Eleza mbinu ambazo mwandishi ametumia kuwasilisha ujumbe wake.
- Eleza sifa za wahusika angalau wawili kutokana na dondoo hili.
- Ni maudhui yapi yanayojitokeza katika dondoo hili?
- Unaposoma dondoo hili, unajifunza nini kutokana na mhusika Juma?
- Dondoo hili linaonesha mabadiliko ya Juma katika uhusiano na watu wa mjini. Kwa upande wako, unadhani ni muhimu kwa vijana kujua na kuelewa tamaduni mbalimbali? Kwa nini?

Shukrani Kaka, kiswahili Leo , kiswahili kesho
LikeLike
Nyuma haturudi
LikeLike