Nadharia ni mpango wa mawazo yanatungwa kutekeleza jambo Fulani. TUKI (2004) wanafasiri nadharia kuwa ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani.
Wafula na Njogu (2007) wanafafanua na kupambanua nadharia kuwa jumla ya maelekezo yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu. Wanadokeza zaidi kuwa dhana hii hurejelea istilahi ya kijumla inayomaanisha mwongozo unaomwelekeza msomaji wa kazi ya fasihi kuifahamu kazi hiyo vizuri katika vipengele mbalimbali vya kazi ya fasihi na namna vinaunganika kuleta umoja katika kazi husika. Kwa mfano jinsi maudhui hulingana na mandhari au jinsi mandhari yanavyolingana na wahusika katika kazi ya fasihi.
Kulingana na maelezo ya Wafula R. M (2004) nadharia husheheni mwongozo wa mikakati ya usomaji wa kazi ya fasihi na hucheza nafasi ya dira katika kuhakiki na kufanya unamuzi fulani.
Wamitila (2003) anaeleza kuwa nadharia hutumiwa kumaanisha kauli za kijumla au kaida zinazomwongoza msomaji katika ufasiri wa maana uliopo katika fasihi. Kwa mfano katika kuelewa maudhui katika kazi ile ya fasihi.
Fauka ya hayo, anasema kuwa ni njia ya kisayanzi inayohusika na kanuni za kijumla na zinazohusika katika utatuzi waswala fulani katika kazi ya kifasihi na pia ni nyenzo ya kufikia malengo fulani ya kiusomi. Nadharia za kuhakiki hata hivyo ni nyenzo tu ya kutusaidia kulifikia lengo fulani na kila nyenzo huwa na ubora na udhaifu. Vilevile nadharia huzuka katika mazingira maalum ambayo yana wasifu na utamaduni mahususi. Hii ni kumaanisha kuwa, hatupaswi kupotoshwa na nadharia kiasi cha kutotambua kuwa zina udhaifu wa kuvimulika vipengele fulani vinavyohusiana na lugha na fasihi zetu.
Nadharia za kuhakiki vilevile huathiriana sana. Huwa vigumu kuongea kuhusu swala la ubunifu katika nadharia yoyote ya kuhakiki. Madai haya yenye mashiko yametambuliwa na wasomi maarufu kama vile Wellek.
Zaidi ya hayo, nadharia hizi zimegawika katika makundi mengi kutegemea malengo na mbinu zake. Kunazo zinazomulika maswala ya kiulimwengu yanajitokeza katika fasihi, kuna zinazohusiana na saikolojia kama vile saikolojia changanuzi, kuna zinazohusiana na visasili, kuna zinazojihusisha na maswala ya jamii, za umuundo wa fasihi miongoni mwa zingine nyingi. Baadhi ya nadharia hizi ni kama vile, nadharia za kisosholojia, za kifeministi, semiotiki, naratolojia n.k..
NADHARIA YA UFEMINISTI.
Ufeministi ni dhana itokanayo na neno la kilatini ‘femina’ linalomaanisha mwanamke. Dhana hii inarejelea uwakilishaji wa haki za wanawake kufuatana na imani ya usawa wa kijinsia. Imejikita sana katika mwamko wa wanawake unaolenga kupigania na kukomesha udhalimu dhidi yao na kufichua matatizo wanayoyapitia katika jamii.
Mbatiah (2001) anaeleza kuwa Ufeministi ni nadharia ya fasihi ambayo inajishughulisha na utetezi wa haki za wanawake dhidi ya ugandamizwaji katika jamii yenye mfumo uliodhibitiwa na wanaume. Kulingana na mawazo yake, nadharia imedhamiria kuupigania ukombozi wa mwanamke kutokana na pingu za kitamaduni, kiuchumi, kidini, kijamii na kisiasa. Pingu anazozirejelea ni misimamo ya itikadi ya kiume ya ubabedume.
Mawimbi ya kifeministi yalianza kuvuma ulimwenguni katika karne ya 19 na yakashika nguvu miaka ya 60 na 70 ya karne ya 20. Kulingana na Ntarangwi (2004) nadharia ya Ufeministi iliibuka katika muungano wa ukombozi wa wanawake uliopamba moto katika miaka ya sitini huko Marekani. Wakati huo, wanawake hasa wa Kimagharibi walianza kuzungumzia matatizo yao kwa kuyaandika. Kwa uwazi na ubayana maswala ya kifeministi yalishika mizizi miaka ya sitini. Kulikuwa na jitihada mbalimbali za kupigania usawa baina ya wanaume na wanawake ingawa hazikuchapishwa kama anavyodai Bonny Onyoni (2002).
Kwa mfano, katika nchi ya Ufaransa kuanzia mwaka 1789 hadi mwaka 1795, inadaiwa kulikuwa na maandamano ya wanawake kutetea kudunishwa walichokiita ‘Msimbo wa Napoleon’. Katika tetesi zao, walidai kuwa kiongozi Napoleon alikuwa amesema kuwa, akili za wanawake ni dhaifu zikilinganishwa na za wanaume. Kwa hivyo, wanawake walifaa kupewa elimu ya kiwango cha chini kama ya ushonaji. Hili lilipelekea wanawake hao kuandamana wakitaka madai hayo kutupiliwa mbali.
Marekani Kaskazini mwaka wa 1848 pia kulikuwa na kundi la wanawake lililoungana katika juhudi za kuleta ukombozi wa wanawake. Kulifanyika mkutano jijini New York ambapo wanawake walitangazwa kuwa huru katika misingi ya kukubaliwa kupiga kura, kupewa elimu ya kutosha, kupewa nafasi sawa za kufanya biashara, usawa wa kupata fidia, usawa wa kisheria na kupata ajira. Ithibati za kimaandishi za kifeministi zenye utaratibu na zilizowekea msingi nadharia ya ufeministi ni ‘A vindication of the Rights of Women’ ya Mary Wollstonecraft (1792) na ‘A Room of One’s Own ya Virginia’ Woolf (1929).
Mary Woollstonecraft ni mwandishi aliyeasisi mazungumzo kuhusu maswala ya wanawake na kulalama kuhusu hali wanawake walikuwa wanapitia katika jamii. Simone de Beauvoir katika kazi yake ya ‘The Second Sex’ mwaka wa 1952 alichangia pakubwa maendeleo ya uhakiki wa kifeministi. Katika kazi yake alibainisha, kukosoa na kupiga vita asasi zilizomdhalilisha au kumdunisha mwanamke. Alizifafanua asasi zinazowadunisha wanawake kama vile dini, ndoa na utamaduni. Beauvoir anasema kuwa dini humkandamiza mwanamke kwa kumfundisha kunyenyekea.
Ndoa nayo imejengwa kwenye misingi na imani ya uwezo mkubwa alionao mwanamume akilinganishwa namwanamke. Kulingana naye ndoa, humsawiri mwanamke katika tamathali hasi na duni.
Mwandishi mwingine ni Kate Millett katika kazi ya ‘Sexual Politics’ anaonyesha athari kubwa katika historia ya Ufeministi. Millett aliwashambulia sana waandishi wanaume kama vile Henry Miller, Norman Miller, Jean Gennet na D.H.Lawrence kutokana na jinsi walivyowasawiri wahusika wa kike. Kutokana na aliyoyagundua katika kazi hizo, Millett anabainisha kuwa miundo ya kijamii pamoja na asasi zake zinashirikiana kumkandamiza mwanamke.
Millett vilevile anaikosoa mikabala ya saikolojia changanuziya Sigmund Freud kwani ina mapendeleo makubwa kwa mfumo wa ki-ubabedume. Mwanasaikolojia huyu alidai kuwa mtoto wa kike huanza kujichukia mara tu anapogundua kuwa hana kiungo cha kiume. Hali hii husababisha alichokiita `wivu’ wa zubu’. Kutokana na wazo la’wivu wa zubu’ la Freud, Millet anaeleza kuwa wivu uliopo ni wa uwezo alio nao mwanamume kutokana na muundo wa kijamii. Mwanamke anakuwa na wivu wa kinachoashiriwa na hilo zubu wala sio zubu kama kiungo cha mwili.
Hali kadhalika, msomi wa Kinigeria Bi. AbiodunOgundipe-Leslie (1994) anasema kuwa wanawake wamepewa majukumu duni na yanayosawiriwa kwa ubaya kama vile kuwa wachawi na wanaume nao husawiriwa kuwa werevu, wenye nguvu na kuaminika na wenye uwezo wa uongozi kwa kuzaliwa. Ogundipe-Leslie anaeleza hali kama hii huchangia kumdunisha na kumtesa mwanamke katika jamii.
Nadharia ya Ufeministi, imegawika katika matapo mbalimbali kutegemea vigezo mbalimbali.
Wafula na Njogu wanaeleza kuwa matapo haya hubainishwa kupitia njia za kiitikadi na kimaeneo. Mkabala wa kiitikadi unahusu mitazamo mitatu ambayo ni, Ufeministi Huru, Ufeministi wa Kijamaa na Ufeministi wa Kimapinduzi.
- Ufeministi Huru hutetea usawa kati ya wanawake na wanaume katika ngazi zote za maisha.
- Ufeministi wa Kijamaa hujishughulisha na ukosoaji wa jamii na kuwahimiza wanaume kushiriki katika malezi ya watoto na kazi nyingine ambazo kimapokeo zimechukuliwa kuwa kazi za wanawake.
- Ufeministi Kimapinduzi humchukulia mwanamume kama adui mkubwa zaidi wa mwanamke. Huhusisha ukandamizwaji wa mwanamke na tofauti za kimaumbile. Pia hushikilia kuwa wanawake wanapaswa waitawale miili yao na hata wasiolewe.
Njia ya kuainisha matapo ya Ufeministi kimaeneo huhusisha Ufeministi na maeneo ya kijiografia. Waainishaji wa kimaeneo ni Mary Eagleton (1991) na Ross Murfin (1991).
Wanaugawa ufeministi katika matapo manne yaani,
- Ufeministi wa Kifaransa,
- Ufeministi wa Kingereza,
- Ufeministi wa Kimarekani na
- Ufeministi wa Kiafrika.
Ufeministi wa Kifaransa unalenga kufafanua jinsi lugha hutoa maana ya mtumiaji wake. Wanadai kuwa lugha kama inavyotumiwa ni zao la taasubi za kiume. Wanasema kuwa lugha inampendelea mwanamume kuliko mwanamke. Jazanda za kuelezea uwezo, nguvu na mamlaka ni za kiume na ilhali zile zenye kusawiria ulegevu na kutoweza ni za kike.
Ufeministi wa Kimarekani unahusishwa na kazi ya Mary Ellman “Thinking about Women” (1968). Mary aliangalia jinsi wanawake wanasawiriwa kwa namna mbalimbali katika kazi zilizoandikwa na wanaume na jinsi wanaume walivyoendeleza usawiri huo hasi wa wanawake katika kazi zao.
Betty Friedan katika “The Feminine Mystique” (1963) anachunguza maisha ya mwanamke ambayo anasema ni jambo lisiloeleweka na wanaume na pia wanawake wenyewe. Tapo hili linashikilia kwamba, wanawake wana namna yao ya kipekee ya kuandika na kujieleza.
Aidha, wanasema kuwa kuna dhamira zinazorudiwarudiwa katika tungo za wanawake. Wanashugulikia kazi za fasihi zilizotungwa na wanawake na pia wanaume maadamu zinaongea juu ya wanawake.
Ufeministi wa Kiingereza huchukulia kuwa, mambo yakihistoria na siasa ndiyo huathiri matendo ya wanawake. Tapo hili lilidhamiria kuwashirikisha wanafunzi katika maswala ya kufanya uamuzi na kuondoa dhuluma dhidi ya jinsia ya kike.
Ufeministi wa Kiafrika ulihusishwa na bara la Afrika. Wanawake wa Kiafrika walisisitiza zaidi upinzani dhidi ya utamaduni unaomnyima mwanamke nafasi ya kutekeleza malengo yake. Miongoni mwa vitengo vya utamaduni huu ni ; desturi na mila zinazomdhalilisha kama vile kuonewa kwa mwanamke asiyezaa, kukosa uwezo wa kuchagua kuwa mke au mzazi wa mwanajamii, tohara na ukeketwaji wa wanawake pamoja na kimya cha kulazimishwa.
Millett (1977) anasema kwamba Ufeministi wa Kiafrika umetokana na utamaduni katika jamii iliyojikita katika kilimo na ushiriakiano wa kijamii. Umejengeka katika misingi thabiti ya kumhusisha mwanamke katika shughuli tofauti za jamii bila kuangalia asasi zinazotawaliwa na mwanamume. Kulingana na Millett, Ufeministi wa Kiafrika husisitiza usawa katika shughuli za jamii na utoaji uamuzi kwa wanawake na wanaume.
Mihimili ya kimsingi ya nadharia ya Ufeministi
Nadharia hii inanuia kuwasawazisha wanadamu kwa upande wa jinsia na utamaduni na kupigania jamii mpya yenye msingi katika amali za kibinadamu na wala si za kimaumbile na za kijadi. Vilevile ni mtazamo unaokuza na kuendeleza hisia za umoja wa wanawake kama kundi linalodhulumiwa.
Aidha, lengo muhimu la nadharia hii ni kuvumbua na kuziweka wazi kazi za sanaa zilizotungwa na wanawake ambazo zimepuuzwa kwa sababu ya utamaduni unaompendelea mwanamume.
Pia inanuia kuchunguza historia ya fasihi ya jadi ya kike na kuwamulika waandishi wa kike waliotambua hali za wanawake na ambao wanaweza kuchukuliwa kama vielelezo kwa wasomaji wao.
Mbatiah anaeleza kuwa lengo kuu la uhakiki wa kifeministi na hasa Ufeministi wa Kiafrika ni kuzua mikakati ambayo itaangazia kutathmini jinsia ya kike, mitazamo, thamani na matakwa ya wanawake sio tu katika fasihi, bali nyanja zote za maisha ya binadamu.
Nadharia hii hunuia kuzindua mwamko kwa wanawake na jinsi wanavyojiona na uhusiano wao na watu wengine.
NADHARIA YA UDHANAISHI
Nadharia ya udhanaishi huangalia maisha ya mwanadamu.
Hujikita katika kuhakiki fujo na udhaifu wa maisha ya mwanadamu, upweke na usiri unaomkumba, kiroho na hofu kubwa anazozipitia, utupu na ubwege wa maisha, swala la uhuru, kifo na hatimaye uhusiano uliopo baina ya binadamu na Mwenyezi Mungu.
Nadharia hii imetafasiriwa na kupambanuliwa na wataalamu mbalimbali. kama vile;- Kimani Njogu na Rocha Chimerah (1999) wanafasiri Udhanaishi kuwa nadharia ambayoinajibidisha na dhana ya Maisha. Wasomi hawa wanajaribu kuuliza swali la kifalsafa kuwa Maisha ni nini?. Kwa undani wanajikita kutafiti nafasi ya mwanadamu ulimwenguni.
Kwa upande mwingine, Wamitila, K. W. (2003) Katika Kamusi ya fasihi Istilahi na nadharia anaeleza kuwa “Udhanaishi ni dhana inayotumiwa kuelezea falsafa ya kuwako na Maisha.
Dhana hii inatumiwa kueleza Maono au Mitazamo unaohusiana na hali ya Maisha ya binadamu, nafasi na jukumu lake ulimwenguni na uhusiano wake na Mungu.
Wanjala Simiyu (2012) kwa upande mwingine katika Kitovu cha fasihi simulizi anasema kuwa Udhanaishi ni falsafa au Mtazamo wa Maisha ulio na kitovu chake katika swali kuwa, anaeleza kuwa maisha ni nini na yana maana gani kwa binadamu?, ni kwa njia gani mwanadamu anaweza kuyabadilisha maisha yake yaliyojaa dhiki, mashaka na huzuni.
Nadharia ya udhanaishi ni falsafa inayoshugulikia maswala kuhusu maisha; ni mtazamo unaokagua hali ya nafasi ya mtu katika ulimwengu anamoishi na pia ni falsafa inayozungumzia uhusianao uliomo kati ya mtu na mungu na iwapo mtu anapaswa kuamini kuwepo kwa mungu.
Vilevile, inatusaidia kuhakiki maisha ya mwanadamu anayeishi katika ulimwengu uliojaa shida na matatizo mengi ambayo yanayosababishwa na binadamu mwenyewe. Shida zinayoyapitia ni kama vita, njaa na uchumi kuzorota, kukosa kazi, ajali barabarani. Matatizo haya yanafanya mwanadamu kukata tamaa na kushuku iwapo kweli mungu yuko.
Waasisi wa nadharia hii ni wanafalsafa Soren KierKegaard wa Ki-Den, Mjeruani Friedrich Nietzsche, Martin Heidegger na Gabriel Marcel.
Kulingana na Kieregaard mtu haishi kwa nguvu zake mwenyewe kwa kuwa kuna nguvu zinazomtawala ambozo ni za mungu. Anaendelea kuwa binadamu anapoishi hutenda dhambi na ili apate utulivu wa kiroho inambidi atubu dhambi hizo. Wanaamini kuwepo kwa mungu kwa binadamu wote.
Mwanafalsafa huyu anaeleza kuwa binadamu ni kikaragosi cha nguvu zilizomuumba ni katika kuzicha mtu huyu hupata utulivu wa kiroho .Kulingana naye, udhanaishi ni dhana ya hofu pale ambapo binadamu huogopa adhabu kutoka kwa mungu kwa hivyo amefunikwa na wasiwasi hataki na kumkosea mungu na kuhimiza ubinafsi wa binadamu.
Friedrich Nietzche (1927) katika kazi yake ya joyful wisdom” asema kuwa mungu amekufa. Tamko hili lake pamoja ca misimamo ya wenzake vinakuwa misingi muhimu ya kuzuka kwa udhanaishi wa ukanaji mungu.
Nadharia hii ilishika sana baada ya vita vikuu vya dunia ambapo watu walikata tamaa maishani. Kulingana na wanafalsafa walioshikilia dhana hii walidai kuwa mtu anapozaliwa, hujipata ametumbukia katika ombwe la aina fulani.Vilevile mtu yuko huru kuishi tu na kukabiliana vilivyo na ulimwengu unaomzunguka.
Mwandishi Kezilahabi ni muasisi wa nadharia hii katika Kiswahili kwa kuwa kazi zake nyingi zimejikita katika maisha ya binadamu, kama vile Dunia uwanja wa fujo, Rosa Mistika miongoni mwa zingine.
Mihimili ya Udhanaishi. Nadharia hii imejengeka katika nguzo kadhaa kama ilivyoasiriwa na wanafalsafa mbalimbali. Kwa kuwa ilizalishwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza vya Dunia, wakati binadamu alikaa kukata tamaa, imejikita katika mihimili ifyatayo;
Kwanza baadhi ya wanaudhanaishi wanatilia mkazo matatizo halisi yanayomsibu mwanadamu na wanakwepa imani ya kinjozi juu ya imani ya kuishi.
Kulingana wasomi wa Kijerumani Heidegger na Jaspers, watu walikata tamaa kwa kuwepo kwa wasiwasi na hofu kwa sababu ya giza la fujo na mapambano ya silaha.
Wanafalsafa hawa pia hawaamini uwepo wa Mungu na uumbaji wake wa ulimwengu. Kwa kuzingatia maafa yaliyokuwa yakiwasibu wanadamu wakati wa vita vya dunia. Madai haya yalipata mashiko miongoni mwawanafalsafa waliodai kuwa iwapo mungu angalikuwepo basi hangeruhusu watu kuendelea kutenda uovu na kuwanyanyasa watu waso hatia.
Udhanaishi inatambua uhuru wa watu wa uchaguzi na hatua ya wazi katika mambo mawili. Tu kwa njia ya uchaguzi wao wa kuchukua hatua, watu wanaweza kutambua kwamba bure, kwa sababu asili ya binadamu ni waliochaguliwa na matendo yao wenyewe kuamua.
Vilevile, nadharia hii huamini katika juhudi za mtu binafsi kujisaka au kupambana na maisha huishia katika umauti. Inashikilia kuwa binadamu imejaa mateso na pindi tu binadamu anapozaliwa hivyo basi huwa amejipata katika ulimweng wa mateso na shida hivyo basi kifo tu ndiyo huwa hatima ya kila kitu.
Hali kadhalika, hujadili hali kama vile mashaka na uchovu wa mambo mbalimbali yanayotutatiza maishani na jinsi yanavyoathili maisha ya yetu.
Maudhui yanayotajwa na wadhanaishi ni kama vile uhuru wa mtu binafsi, uwezo wake wa kujifikilia na kujiamlia. Udhanaishi unafafanua jinsi uhuru wa binadamu umeshikwa na pingu za utamaduni wa jadi na mila. Kulingana na washikilizi, ni bora kutambua umuhimu wa kuchagua na kutenda kulingana na uchaguzi na kujitolea majukumu ya maisha.
Pia hujadili na kugusia maudhui ya ukengeushi ambapo binadamu huwa amekata tamaa au amekosa uhakika maishani. Huwa imembidi kubadilika na kuanza maisha ambayo ni kinyume.
Nadharia hii kwa ufupi inayarejelea maisha ya binadamu, uhusiano wa binadamu katika ulimwengu na masaibu.
Uhakiki wa fasihi.
Uhakiki ni kitendo cha kuchambua kazi ya kifasihi, kifani na kimaudhui ili kupata ujumbe uliomo katika kazi hiyo. Uhakiki ni kitendo cha kusoma kazi ya fasihi asilia inayoweza kuwa riwaya, tamthilia au ushairi, kisha kueleza na kufichua mambo ambayo yamefichika katika kazi hizo. Uhakiki wa fasihi hushughulikia vipengele vikuu viwili ambavyo ni fani na maudhui.
Uhakiki pia ni kitendo cha kutafakari, kuchambua na kufafanua kazi ya fasihi ili kuweka bayana maadili na ujumbe uliomo katika kazi hiyo.
Uhakiki ni kitendo cha kutathmini,kueleza na kuanisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya kifasihi kwa kuongozwa na kaida maalumu.
Nakwahivyo, mhakiki ni mchambuzi na mfafanuzi wa kazi za kifasihi. Mhakiki sharti asome au aisikize kazi ya fasihi kwa makini ili aweze kuihakiki.
Katika fani tunachunguza vipengele vifuatavyo:
- miundo
- wahusika.
- Lugha
- mandhari
- maudhui.
- Jina la kitabu pamoja na picha yake
Katika maudhui tunachunguza vipengele vifuatavyo:
- Dhamira
- ujumbe
- migogoro
- msimamo
- falsafa.

Kongole kazi nzuri
LikeLike
Asante ndugu
LikeLike
kazi bora sana Asante sana mkuu endelea. Nyuma haturudi.
mwalimu N Deposit
LikeLike
ASANTE SANA MWALIMU DEPOSIT. NYUMA HATURUDI
LikeLike
Asante sana mwalimu Deposit
LikeLike