MSITU MKALI

SURA YA KWANZA
Sarah aliwaza na kuwazua namna ya kukaribia msitu mkubwa wa Mabira. Msitu unaoogopwa na kila mtu katika jamii ya Namasagali. Msitu wa miujiza kulingana na hadihti za wahenga. Kila mtu katika eneo la Namasagali alikuwa analala saa kumi na mbili jioni kujihadhari na wanyama wakali kutoka msitu huo.

Hadithi na masimulizi ya kale yalikuwa yanazingatia sana kutahadharisha watu kuhusu msitu huo. Watoto wa kike wangemaliza kazi zao mapema saa kumi na moja ili wasishambuliwe na pepo za miungu pamoja na wanyama wakali kutoka msitu huo. Ulikuwa muda wa saa tatu asubuhi na wazazi wake Sarah walikuwa wameenda kwa supermarket kununua mkate kunywa chai.

Sarah aliamua maramoja kutekeleza ndoto yake ya muda mrefu ya kugundua siri ya msitu uliokuwa karibu na nyumba yao. Sarah na wazazi wake walikuwa wanaishi karibu na msitu wa miujiza. Msitu huu ulikuwa unaitwa Mabira. Sarah alitamani kugundua siri ya msitu huu. Kila usiku msitu ulikuwa unatoa sauti za mshangao kama sauti ya gari la trekta. Msitu ulikuwa unatoa harufu nzuri kama ya nyama ya kuku muda wa usiku.

Siku moja, Sarah aliamua kutembea kwenda kwa msitu wa Mabira. Sarah alikuwa na kibegi chake kidogo kilichopakiwa na mkate wa kula, maji na maziwa ya kunywa pamoja na kitabu na kalamu vya kuandika. Kwa ujasiri aliingia kwenye msitu mkubwa huo. Msitu ulimkaribisha kwa upepo mzuri na harufu nzuri ya maua.
Aliingia kwa ujasiri bila kuogopa. Alianza kutazama mbele na nyuma ili asiwe anafuatiliwa na simba wakali. Sauti za simba zilikuwa zinasikika mbali na msitu. Sauti za tumbiri zilikuwa zinasikika sehemu ya mkono wake wa kulia. Wawindaji walikuwa pia wanaendelea kupiga kelele za kukimbiza wanyama. Baadaye kidogo, kimya kikubwa kilikuwa katika msitu mzima. Sarah hakusita wala kuogopa, aliendelea na safari yake kugundua siri ya msitu. Alifika katikati mwa msitu akasikia sauti mti ukianguka pu. Sarah aliogopa kidogo lakini akakumbuka lengo lake la kwenda msituni ni kugundua siri ya msitu.
Msitu huo ulikuwa unaogopwa na kila mwanajamii kwa sababu wahenga walikuwa wanautumia kama msitu wa kiuchawi. Wahenga babu na babu wa eneo hilo walikuwa wanaogopa hata kuukaribia msitu huo kwa sababu baadhi ya wenzao walikuwa wanaenda huko bila kurudi. Msitu huo iliaminiwa kuwa maadui wa taifa na jamii nzima wanajificha huko. Msitu ulikuwa miongoni mwa mahali ambapo hata wanajeshi wa taifa walikuwa wanaogopa kutembelea. Wanyama wakali wote wakiwemo simba, chui, mbwa mwitu, nyoka wakali, punda, tembo na wengine.
Msitu ulikuwa wa maajabu kwamba wahenga walisimulia kwamba, kiongozi wao wa kitamaduni aliyejulikana kwa jina la Rubasharaza aliingia wakati mmoja. Alirudi baada ya miaka kumi na mitano. Kiongozi huyo alikuwa na videvu vikubwa na nywele za kushinda simba. Alikuwa anaonekana kama mnyama na pia alikuwa anatoa sauti kama ya simba. Jambo hili liliwafanya wote wahenga kuogopa na kuheshimu msitu huo bila kuukaribia hata.
Sarah alianza kuwaza na kuwazua, “Nimetoka nyumbani bila mtu yeyote kujua nimefika mahali mbapo sijui. Mama na baba zangu wamepika chai tayari na chakula cha mchana. Mimi ninaenda wapi? Sina simu wala betri ya simu kupigia mama na baba nyumbani. Muda unakaribia saa kumi na mbili jioni. Nitarudi nyumbani namna gani? Simba wakali nikiwakuta nitafanya nini? Giza karibu litakuja. Mungu aniongoze lakini sitarudi nyuma wala kuogopa”
Sarah alipoingia ndani zaidi, alikutana na Kuchakuro mdogo. Kuchakuro alimkaribisha kwa sauti ya chini akisema “karibu mtoto mdogo, umefika mahali pa miungu na utaliwa”. Kuchakuro alikuwa mwepesi na alimkaribisha Sarah katika msitu. Sarah hakuogopa wala kutikishwa. Alisimama imara na umri wake mdogo. Kuchakuro kila mara alionekana akiruka kutoka mti mmoja hadi mwingine. Alikuwa kiumbe mwenye urafiki na punde wakawa marafiki na Sarah. Walianza mazungumzo pamoja huku Kuchakuro akimwonyesha sehemu kuu za msitu.

Baada ya masaa machache ya kuzuru katika msitu, Sarah na Kuchakuro walikutana na mto wa bluu unaometameta. Ilikuwa wazi sana na tena wangeweza kuona samaki wenye rangi nyingi wakiogelea chini. Upande wa pili wa mto huo, waliona ua zuri la rangi ya upinde wa mvua.
Sarah alishangazwa na ua hilo na kuamua kulichukua. Lakini alipokaribia, sauti nzito ilitoka upande wake wa kulia ikisema, “Ni nani anayethubutu kugusa maua ya upinde wa mvua?” Alikuwa Dubu mkubwa wa rangi nyeusi si si si.

SURA YA PILI

Mwendo wa ulikuwa wa kusismua na kuogopesha. Sarah aliogopa sana baada ya kuona Dubu. Alimwambia Dubu kwamba hakulenga kusababisha matatizo/madhara yoyote. Dubu alisema kuwa maua ya upinde wa mvua yalikuwa maua ya Miungu. Maua haya yanapaswa kuachwa bila kuguswa. Sarah alielewa na kuahidi kuacha kugusa tena. Sarah aliomba msamaha moja kwa moja. Dubu akawa rafiki wa Sarah pia.

Muda uilipofika saa moja za jioni, Sarah aligundua kwamba alikuwa amepotea. Dubu alipoona wasiwasi wake, alijitolea kumsaidia kutafuta njia ya kurudi nyumbani. Sarah alikuwa na Kuchakuro nyuma yake na Dubu akiongoza mbele. Wote watatu walianza safari yao.
Katika njia, walikutana na shida/changamoto nyingi. Walivuka daraja la mbao na lilikuwa linatetema sana kama mgonjwa wa malaria, walipanda vilima vyenye mwinuko mkubwa sana kama mlima wa Rwenzori. Sarah na marafiki zake walikabili na hadithi mbaya za kuogopesha. Lakini kupitia ushirikiano na ujasiri walifaulu na kushinda vyote. Safari yao ilikuwa nzuri lakini mbaya kwa namna nyingine. Walienda wakipiga gumzo na kushauriana. Kuchakuro alimshauri Sarah “Ukifika nyumbani, jaribu kupata muda unawe kwa sababu umetmebea safari ndefu bila kuoga”

Katika safari yao, Sarah alijifunza mambo mengi ya maisha. Alijifunza kuheshimu viumbe wa kiasili, kuwa jasiri, na kusaidia wengine wenye uhitaji. Zaidi ya hayo yote, alielewa maana ya kweli ya urafiki. Urafiki usio wa siku hizi wa nipe nikupe lakini urafiki wa dhati.

SURA YA TATU
Hatimaye, walifika ukingo/mwisho wa msitu. Sarah alikuwa alikuwa anatazama nyumbani kwao. Sarah aliwashukuru Dubu na Kuchakuro kwa msaada wao na akaahidi kuwatembelea tena. Aliwaahidi kupenda na kuzidi kuwaombea mazuri maishani. Aliwashukuru pia kwa mioyo yao wa kusaidia bila malipo. Sarah aliwaza moyoni, “Mungu ni mwema, kwenda mahali ambapo sijui. Watu nisiojua wakanitendea haki! Sitawasahau na tena lazima mimi niwe na tabia kama hizi maishani mwangu” Akiwa na kumbukumbu nyingi moyoni pamoja na upendo, aliwapungia mkono akisema “kwaheriiiiii, Mungu awabariki katika maisha yenu”.
Sarah alitemeba kwa mwendo wa haraka/kasi hadi nyumbani na kulala.
Usiku huo akiwa amelala kitandani, Sarah alifikiria kuhusu msitu wa miujiza wa Mabira. Haukuwa tu msitu mzuri lakini mahali pa burudani, urafiki, na kujifunza. Alijua kwamba siku zote atafurahia matukio ya kimiujiza aliyokabili siku hiyo.

Siku iliyofuata, Sarah aliamka akiwa na furaha. Alijua kulikuwa na matukio mengi zaidi yakimngojea kwenye msitu wa miujiza huo. Saraha alitamani tena kukutana na Dubu pamoja na Kuchakuro na kuchunguza mengi zaidi kuhusu msitu wa Mabira.
Baada ya muda, Sarah akawa mgeni wa kawaida kwenye msitu wa miujiza huo. Alijifunza kuwasiliana na wanyama, kuelewa njia zao, na kuheshimu nyumba zao. Msitu ukawa sehemu ya maisha yake na tena nyumba yake ya pili.
Matukio ya Sarah msituni yalimfundisha mambo mengi. Alijifunza kuwa jasiri, kuwa mkarimu, na kuwa mwenye heshima. Alijifunza kwamba kila kiumbe, haijalishi ni mdogo au mkubwa kwa kiwango gani, kina jukumu katika dunia/ulimwengu. Sarah aliongea haya yote baada ya kuona jinsi alivyokaribishwa na wanyama porini. Sarah aliwaza “baadhi ya wanayama ni wakarimu na wazuri kuliko binadamu tunaoishi nao”

Siku nyingine, Sarah aliamua kurudi msituni kuona marafika zake Dubu na Kuchakuro. Alipokuwa anatembea, alikutana na mtoto wa paka. Mtoto wa paka huyu alikuwa amepotea msituni. Alichukua kipusi huyo akampeleka kwa Dubu na Kuchakuro. Wote walifanya pamoja kusaidia kipusi huyo kupata mama yake.
Tukio hilo lilimfanya Sarah atambue kwamba, angeweza kuleta mabadiliko katika jamii hata yawe madogo kiasi gani. Sarah alifikria kuwa mtu wa kuwasaidia watoto katika jamii yake hasa wasio na chakula, wato ambao hawana mavazi, watoto ambao hawana karo/pesa za shule na wengine wenye uhitaji. Aliendelea kuahidi kwamba Mungu akimsaidia, atajenga shule ya mayatima katika kijiji chake cha Namasagali. Shule yake itaitwa “Namasagali hope orphans’ school”. Sarah aliahidi pia, kujenga hospitali kuu katika eneo la Namasagali. Hospitali yake itaitwa “Namasagali hope orphans’ hospital”. Sarah alisema haya yote kwa sababu ya upendo na ushirikiano aliopata kutoka marafiki zake wanyama Dubu na Kuchakuro.
Kuanzia siku hiyo, Sarah alianza kupenda na kuheshimu ulimwengu na viumbe pamoja na mimea. Alikuwa hapendi watu wanaokata miti au kuchoma misitu kwa sababu ya makaa. Alianzisha kundi la wapiganizi wa haki za ulimwengu. Mkoa mzima ulianza kuheshimu ulimwenu na viumbe hai wote.

Miaka ilipopita, Sarah alikua akawa msichana mkuu lakini upendo wake kwa ulimwengu na viumbe haukuisha. Alikuwa mlinzi wa misitu kutopata madhara. Pia, alishirikisha watoto wengine kwa kusimulia hadithi zake kuhusu ulimwengu na viumbe. Alifanya jukumu kubwa la kuwatia wenzake moyo kuheshimu na kulinda asili/ulimwengu na viumbe wote.
Hadithi ya Sarah ilienea mbali zaidi. Watoto kutoka pande zote walikuja kusikia hadithi zake za msitu wa kimiujiza. Walitiwa moyo na ujasiri wake, ukarimu wake, na heshima yake kwa ulimwengu na viumbe asili. Wengi wao walitaka kuwa kama Sarah.

Upendo wa Sarah kwa msitu na ulimwengu asili ulikuwa mzuri sana. Upendo wake ulileta mabadiliko makubwa katika jamii na taifa zima. Watoto walianza kupanda miti, kusafisha mito na kulinda wanyama. Walitambua kwamba wao pia wangeweza kuwa walinzi wa asili, kama Sarah.
Urithi wa Sarah uliishi kwa muda mrefu. Msitu wa miujiza ulistawi na kuheshimiwa katika nchi yote. Kila mtu alianza kuheshimi viumbe vyote hasa vya msituni. Hadithi za matukio yake ziliendelea kutia moyo vizazi vipya. Sarah msichana mdogo kutoka Namasagali katika ukingo wa msitu aliacha mabadiliko makubwa katika jamii na taifa zima.

Msitu wa miujiza wa Mabira umesimama hadi leo kwa sababu ya upendo na kujitolea kwa Sarah. Msitu huo hadi sasa ni mahali pa kuburudukia, kujifunza, na kujenga urafiki. Mahali pa kusimulia hadithi ya msichana mdogo Sarah na safari yake ya kimiujiza.
Kwa hiyo, hadithi ya Sara inaendelea katika kunguruma kwa majani, mlio wa ndege, na minong’ono ya upepo.
Msitu huo unaendelea kutukumbusha umuhimu wa heshima, ujasiri, na urafiki. Na juu ya yote, inatukumbusha majukumbu ya kila mmoja wetu hapa duniani.

Maswali:
1. Kwa kuzingatia novella ya Msitu mkali hapo juu, taja majina ya wahusika katika hadithi.
2. Baada ya kusoma hadithi hii, umejifunza nini/ umepata mafunzo gani? Toa hoja sita kwa kutoa mifano kutokana na novella.
3. Sarah na mhusika mkuu katika novella hii. Taja sifa zozote tano za Sarah kulingana na novella. Thibitisha hoja yako kwa kutoa mfano kutokana na novella.
4. Mwandishi wa novella ametumia baadhi ya mbinu za lugha. Taja mbinu angalau nne ambazo mwandishi ametumia katika hadithi hii.

2 thoughts on “MSITU MKALI

Leave a reply to NinsiimaAgnes Cancel reply