MWONGOZO WA KARATASI YA KWANZA NATHARI, UFAHAMU NA USHAIRI: SIMON T KAWAIDA NA JOHNPAUL ARIGUMAHO.

UDURUSU WA KARATASI YA KWANZA

P320/1

Ufahamu

Nathari

Ushairi

Simon T Kawaida

na

Johnpaul Arigumaho

@2022

 SEHEMU A: UFAHAMU

Ufahamu ni zoezi la kusoma, kuchambua, kutalii pamoja na kuchunguza maana na muktadha wa kifungu cha habari. Ni hali ya kusoma kwa makini kwa ajili ya kuelewa maana iliyomo katika ibara kwa kukadiria muktadha wa kifungo husika.

UMUHIMU WA UFAHAMU

  • Humsaida msomaji kuelewa kifungu cha habari.
  • Huimairisha uwezo wa msomaji wa kufikiri na kutekeleza mambo
  • Humsaidia msomaji kupanua msamiati wake
  • Humpa msomaji uwezo wa kuchanganua na kuchambua muktadha wa habari
  • Huhifadhi historia
  • Hupitisha ujumbe kwa kizazi baada ya kingine.
  • Huburudisha msomaji/ jamii
  • Hukuza stadi za lugha hasa kusoma.

VIPENGELE VYA UFAHAMU/ STADI ZA LUGHA

  • Kusoma
  • Kuandika
  • Kuzungumuza
  • Kusikiliza  

KUSOMA

Kusoma ni zoezi la kupitia kifungu cha habari ili kuelewa na kufahamu ujumbe uliomo kwa ajili ya kujibu maswali yatokanayo na kifungo husika.

AINA ZA KUSOMA

  • Kusoma kwa ufahamu
  • Kusoma kwa ziada

KUSOMA KWA UFAHAMU

Katika kusoma kwa ufahamu, mwanafunzi azingatie mambo yafuatayo;

  • Asome kwa ufasaha
  • Asome kwa makini
  • Asome kimya kimya
  • Asome upesi
  • Asome kimakusudi; asome huku akijaribu kutafuta viini/ mambo muhimu katika kifungu cha habari
  • Asome huku akibaini ujumbe, maudhui, mafunzo yaliyomo katika ibara.

Tanbihi: Kuna mambo yanayozuia kusoma kwa ufahamu, mambo hayo yanajulikana kama; vizuizi, pingamizi, au changamoto za ufahamu.

Msomaji msomaji yeyote anastahili kuepukana na vizuizi vya kusoma kwa ajili ya kufahamu wakati wa kusoma kifungu cha habari.

vizuizi hivi ni pamoja na;

  • Kutumia vionyeshi kama vile vidole wakati wa kusoma
  • Kusoma kwa sauti/ mnongono
  • Kurudiarudia mafungu ya maneno yaliyosomwa kabla ya kumaliza kifungu kizima
  • Kupekuapekua mafungu ya habari kama mtu anayesoma gazeti.
  • Mwendo wa kichwa kutoka kushoto hadi kulia wakati wa kusoma.

UTARATIBU WA KUFUATA WAKATI WA KUJIBU MASWALI

  • Soma maswali uliyopewa kutokana na kifungu cha habari
  • Soma kifungu cha habari kwa makini
  • Soma tena maswali huku ukitafuta viini/ mambo muhimu katika maswali hayo.
  • Soma kifungu cha habari mara ya pili huku ukipiga misitari mahali ambapo viini ulivyovipata katika maswali vinapopatikana.
  • Soma kifungu cha habari mara ya tatu huku ukilinganisha majibu na maswali yaliyoulizwa.
  • Andaa majibu yako huku ukirejelea namna maswali yalivyoulizwa.
  • Sasa andika majibu yanayolingana na maswali kwa ukamilifu.

SEHEMU B: NATHARI

Nathari ni tawi la fasihi linalotumia lugha ya kimaelezo, kimfululizo, lugha ya mjazo au lugha ya insha kuwasilisha ujumbe.

NYANJA AMBAMO NATHARI HUWEZA KUCHOPOLEWA

Tamthilia

Riwaya

Insha

Hadidhi fupi

Hadithi/ ngano

HADITHI/ NGANO

Hadithi au ngano ni utungo wenye visa vinavyosimuliwa kwa hadhira lengwa ili kupitisha ujumbe.

AINA / VIPERA VYA HADITHI

  1. Khurafa / hurafa.

Hizi ni hadithi ambazo wahusika wake ni wanyama. Hadithi za aina hii, huangaziatabia za binadamu kupitia kwa wanyama. Wanyama hupewa uwezo wa kibinadamu kama vile kuongea, kufanya kazi, kufikiri, kuoa N.k

  • Hekaya.

Hizi ni hadithi za kustajaabisha. Mhusika mmoja huwa mjanja au mwerevu kuliko wengine.

  • Visakale

Hadithi za mashujaa wanaosifiwa katika jamii. Angalau mashujaa hawa huwa wamepigania jamii zaokatika vita dhidi ya jamii nyingine au katika vita vya kuikomboa jamii.

  • Usuli.

Usuli husimulia asili / chanzo cha jambo Fulani kwa kuelezea kwa nini jambo hilo hutokea au kwa nini liko kama lilivyo. Kwa mfano, kwa nini binadamu hufariki?,kwa nini binadamu hana mkia? N.k

  • Visasili.

Hizi ni ngano zinazoelezea asili / chanzo cha jambo Fulani. Visasili huelezea jinsi au namna jambo lilivyotokea. Kwa mfano, binadmu alitoka wapi?

Ukimwi ulianzaje?

  • Ngano za mazimwi.

Wahusika katika ngano za aina hii ni mazimwi, majini, au majitu.

  • Ngano za mtanziko

Katika aina hii, mhusika huwa katika hali ambapo hawezi kufanya uamuzi wa kuchagua kati ya vitu/ hali mbili zinazotatiza.

ANWANI/ KICHWA CHA NATHARI

Kichwa cha habari ni kiini/ jambo muhimu linalozungumziwa katika habari.

SIFA ZA KICHWA

  1. Huandikwa kwa herufi kubwa.
  2. Huwa na maneno machache yasiyozidi sita
  3. Huhusiana na kiwiliwili
  4. Huandikwa kwa lugha ya mjazo/ maelezo

UTARATIBU WA KUTUNGA KICHWA

  1. Soma kifungu cha habari kwa makini
  2. Jaribu kuchunguza muktadha wa habari.
  3. Linganisha aya ya kwanza (utangulizi) na aya ya mwisho (tamati) kwa kutafuta muhtasari/ kiini
  4. Toa kiini/ muhtasari (jambo muhimu) linalozungumziwa katika habari
  5. Unda kichwa kinacholinga na muktadha wa habari uliyopewa huku ukirejelea sifa za kichwa kizuri.

TAMATHALI ZA USEMI

Tamathali za usemi zinagawika katika sehemu kuu mbili, yaani;

  1. Mbinu / fani za lugha
  2. Mbinu za sanaa

MBINU/ FANI/ MAPAMBO YA LUGHA

Huu ni uteuzi wa maneno ili kuifanya lugha iwe ya kuvutia au kupendeza.

Mbinu au fani za lugha ni pamoja na;

  1.  Tanakali za sauti

Hii ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti, au yanayoonyesha jinsi kitendo kinavyofanyika. Kwa mfano;

  • Cheka kwa!Kwa!Kwa!
  • Lia kwi! kwi! kwi!
  • Bweka bwe! bwe! bwe!
  • Funika gubigubi!
  • Lala fo! fo! fo!
  • Tashbihi

Hii ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili au hali mbili kwa kutumia maneno ya kulinganisha kama vile; mithili ya, utadhani, ungefikiri, sawa na, mfano wa, kama Nk. Kwa mfano;

  • Nguruma kama samba.
  • Tembea mithili ya sungura.
  • Alivyozungumza ungedhani ni mfalme.
  • Alikuwa mnene mfano wa ndovu.
  • Walivyomsifu ungefikiri wamjua.
  • Isitiari/ Isitiara

Mbinu ya kulinganisha vitu viwili kwa kutumia kitenzi kisaidizi “ni”

au “kuwa”. Kwa mfano;

  • Sara ni simba.
  • Juma alikuwa nguzo yetu.
  • Yesu ni ngome yangu.
  • Jazanda

Ni kulinganisha vitu viwili moja kwa moja bila ya kuuinganisha kiunganishi chochote. Jazanda hutumia lugha ya mafumbo.

  • Maisha bila mapenzi; chai bila sukari
  • Mtoto mwenye kiburi; ardhi yenye mwamba.
  • Elimu bila mali; mti usio na majani.
  • Taashira

Matumizi ya lugha ya ishara kuwasilisha ujumbe fulani. Jina au kitu hutumika kumaanisha kingine chenye uhusiano nacho. Kwa mfano;

  • Mwokozi wa mawazo- pombe
  • Simba wa mwituni- mtu mkali
  • Kamusi yenye miguu- mtu mwerevu
  • Mkono wa chuma- utawala/ udikteta.
  • Mchezo wa wakati- siasa
  • Taswira

Matumizi ya lugha inayojenga picha za hali au jambo fulani akilini mwa msomaji au msikilizaji.

  • Tashhisi/ Uhaishaji

Mbinu ya kukipa kitu, hali, au mnyama sifa za kibinadamu; kama vile kulima, kufikiri, kusoma, kuandika, kuimba Nk.

Kwa mfano;

  • Sharia zimemchunga kwa macho makali.
  • Ng’ombe wangu ameanza kulalamika.
  • Chuku

Ni mbinu ya kutumia maneno yenye kutilia chumvi kitu au hali fulani kwa ajili ya kusisitiza ujumbe au kusifia kitu. Kwa mfano;

  • Sifa ni mrembo kama malaika.
  • Bwaba suhula alikuwa gwiji wa magwiji.
  • Kelele zake zikazidi mpaka zikawakera wafu.
  • Takriri

Mbinu ya kurudiarudia neno au maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Kwa mfano;

  • Nasema nenda, nenda mjinga wee!
  • Alicheka akacheka mpaka tumbo lilipoanza kumuuma.
  • Sitaki sitaki sitaki kusikia mambo yako.
  1.   Inadi.

Mbinu ya kurudiarudia maneno kwa ajili ya kumdharau, kukejeli, kubeza au kumkasirisha mtu.

  1.    Kejeli.

Mbinu ya kumdharau au kumbeza mtu.

  1.    Majazi.

Tabia, hadhi, kazi, mwenendo au matendo ya mtu kuambatana na jina lake.

Mifano ya majina ni kama;

  • Majuto
  • Mapepe
  • Mateso
  • Matege
  • Kijakazi
  • Karisa
  1.  Lakabu

Mbinu ya mhusika kubandikwa jina na wahusika wengine au yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia, hadhi, mwenendo, kazi, au matendo yake.

  1.  Semi

Fungu la maneno linalotumiwa kutoa maana nyingine badala ya ile ya maneno husika katika kifungu. Kuna aina mbili za semi, yaani;

  1. Nahau

Nahau ni semi ambazo huwa na kitenzi katika muundo wake. Kwa mfano;

  • Kula kalenda
  • Mwaga unga
  • Bugia chumvi nyingi
  • Lala kifudifudi
  • Enda segemnege
  • Kata roho
  • Vunjika moyo
  • Misemo

Msemo ni semi ambazo hazina kitenzi katika muundo wake. Mara nyingi misemo huundwa kutumia nomino/ majina. Kwa mfano;

  • Kifo cha mbwa
  • Kitendo cha samba
  • Wahenga na wahenguzi
  • Chanda na pete
  • Macho na pua
  • Macho ya mwewe
  • Pua ya paka
  • Usingizi wa maisha.
  1.    Methali

Maneno ya hekima yenye maana fiche au maana inayofumba. Kwa mfano;

  • Hatesi mtesa akafululiza.
  • Fadhila za punda ni mateke
  • Mpanda ngazi hushuka.
  • Siku za mwizi ni arubaini.
  • Mama wa kambo si mama.
  1.    Maswali ya balagha/ Tashtiti

Haya ni maswali yanayoulizwa na mwandishi au mhusika yasiyohitaji majibu. Kwa mfano;

  • Umenichukia mimi?
  • Kweli nimekuwa maskini?
  • Baba yangu amefariki?
  •  
  •    Uzungumzi nafsiya.

Mhusika huzungumza peke yake aama kwa kuongea au kuwaza/ kufikiri ndani ndani.

  1.    Utohozi

Hii ni mbinu ya kuswahilisha maneno ya lugha ngeni ili yatamkike kama ya Kiswahili. Kwa mfano;

  1. Kiingereza                                                        Yaliyotoholewa
  2. Skirt                                                                                     sketi
  3. Computer                                                                           kompyuta
  4. Aeroplane                                                                           eropleni
  5. Shirt                                                                                     shati
  6. Radio                                                                                    redio
  • Kiarabu                                                                              Yaliyotoholewa 
  • Hakk                                                                                      haki
  • Bustan                                                                                   bustani
  • Bint                                                                                        binti
  • Khmsin                                                                                  kheri/ heri
  • Ardh                                                                                       ardhi
  1.    Mazda

Mbinu ya kurefusha maneno ili kusawazisha mizani. Kwa mfano;

Mazda                                                                                      Kiswahili Sanifu

  • Kinapendekeza                                                                   kinapendeza
  • Taabu                                                                                   tabu
  • Enenda                                                                                 enda
  • Muana                                                                                  mwana.
  •    Inkisari

Mbinu ya kufupisha maneno ili kusawazisha mizani na vina. Kwa mfano;

Inkisari                                                                                    Kiswahili Sanifu

  • Sende                                                                                   usiende
  • Pendo                                                                                   upendo
  • Penzi                                                                                     mapenzi
  • Twali                                                                                     tulikuwa
  • Nali                                                                                        nilikuwa
  •    Ritifaa

Kuzungumza na mtu aliyefariki au asiyekuwepo kana kwamba yupo karibu na mzungumzaji. Kwa mfano;

  • Mama huko uliko sitakusahau.
  • Mbona ulifariki mapema?
  •  Matumizi ya lahaja

Hivi ni vilugha vya wasemaji mbalimbali wa Kiswahili kutokana na ama mahali wanakoishi, kiwango cha ustaarabu au miingiliano ya Kiswahili na lugha nyingine karibu na wasemaji wa Kiswahili. Kwa mfano;

  1. Kiungwana                                                                          Kiswahili sanifu
  2. Mayi                                                                                      maji
  3. Kuya                                                                                       kuja
  4. Vala                                                                                        vaa
  5. Yulu                                                                                        juu
  • Kirufiji                                                                                   Kiswahili sanifu
  • Ntu                                                                                         mtu
  • Habali                                                                                     habari
  • Nzuli                                                                                        nzuri
  •  Kuboronga lugha

Mbinu ya kutobanwa na kanuni za lugha sanifu.

  1. Kuchanganya Ndimi                                                                  Kiswahili Sanifu
  2. Ng’ombe hiing’ombe huyu
  3. Kipofu hiki                                                                                   kipofu huyu
  4. Mtu ya kimathi                                                                           mtu wa kimathi
  • Kubadilisha Mpangilio Wa Maneno         Kiswahili Sanifu
  • Ya nyuma sehemu                                                                    sehemu ya nyuma
  • Unalia mbona?                                                                          Mbona unalia?
  • Huko alienda                                                                              alienda huko
  • Sana amelia                                                                                amelia sana
  •    Tabdila

Mbinu ya kubadili umbo/ tahajia ya neno kwa ajili ya kusawazisha vina. Kwa mfano;

       Tabdila                                                                                             Kiswahili Sanifu

  • Kabidha                                                                                        kabidhi
  • Juwa                                                                                              jua
  • Fikiriya                                                                                          fikiria
  •    Tasfida

Mbinu ya kuficha maneno ambayo ni vigumu kutamka; kuficha aibu.

Mfano ameenda kwa haja ndogo hutumiwa badala ya kuweka neno zito la aibu “kukojoa au kunya”

  •  Mseto/ kuchanganya ndimi

Kuweka neno la lugha ngeni katika sentensi ya Kiswahili kwa mfano;

  • Mwangalie huyo brown
  • Nakupenda sana uncle
  •    Kuhamisha ndimi

Kuingiza sentensi au kifungu cha lugha ngeni katika kazi ya kiswahiil. Kwa mfano;

  • Baba yako ni mtu mzuri sana. He is a very happy man.
  •    Nidaa (!)

Mbinu ya kutumia alama ya mshangao. Kwa mfano;

  • Kumbe ni wewe!
  • Toka hapa mzoga wee!
  • Amekufa!
  •    Dailojia

Mbinu ya wahusika wawili au Zaidi kusemeza katika kazi ya fasihi. Mbinu hii hujitokeza moja kwa moja katika tamthilia.

  •    Monolojia

Mbinu ya kutumia lugha ya masimulizi, maelezo, katika fasihi. Mbinu hii hutumika sana katika nathari.

MBINU ZA SANAA

Hizi ni mbinu ambazokuzitambua unastahili kusoma anghalau kazi nzima ya fasihi. Hizi ni pamoja na;

  1. Taharuki

Hali ya kuweka msikilizaji / msomaji katika hali ya kutaka kujua ni nini kikichofuatia.

  • Sadfa

Kugonga kwa vitendo viwili vinavyohusiana kama kwamba vilikuwa vimepangwa japo havikupangwa.

  • Mbinu rejeshi/ kisengere nyuma

Mhusika au mwandishi huelezea kisakilichokuwa kimetendeka kabla ya kile anachosimulia.

  • Utabiri/ kisengere mbele.

Mbinu ya kuangazia mbele kwa kutabiri jinsi mambo yatakavyokuwa siku zijazo.

  • Ndoto/ njozi

Mbinu ya kutumia ndoto kutabiri mambo yatakayotokea.

  • Nyimbo za mashairi

Hizi ni sauti za lahani zinazotumikakuburudisha msomaji/ msikilizaji.

  • Upeo wa juu

Matukio kufanyika kulingana na mapendekezo au matarajio ya msomaji/ msikilizaji.

  • Upeo wa chini

Matukio kufanyika kinyume na matarajio au mapendekezo ya msomaji/ msikilizaji.

  • Kinaya

Mbinu ya wahusika kufanya mambo kinyume na matarajio ya msomaji.

  1.  Matangulizi

Mbinu ya kuanza kazi ya fasihi kwa kuanza na sehemu ambayo ingetumiwa katikati au mwishoni.

MTINDO WA NATHARI

Mtindo wa nathari huzingatia mambo yafuatayo;

  1. Aina ya wahusika:
  2. Binadamu
  3. Wanyama
  4. Ndege
  5. Mazimwi
  6. Malaika. Nk
  • Aina ya hadithi:
  • Khurafa
  • Hekaya
  • Visakale
  • Usuli
  • Visasili
  • Mtanziko. Nk
  • Muundo wa hadithi
  • Msago ( muundo wa moja kwa moja)
  • Muundo rukia
  • Hadithi changamano
  • Muundo rejea/ matangulizi
  • Nafsi:
  • Nafsi ya kwanza
  • Nafsi ya pili
  • Nafsi ya tatu

TONI

Toni ni sauti ya kiwango cha juu na chini. Toni huwa ama ya mwandishi au mhusika katika kazi ya fasihi.

AINA ZA TONI

Toni ni za aina mbili, yaani;

  1. Toni ya juu
  2. Toni ya chini

Tanbihi: Toni huathiriwa na hisia/ hali na mazingira aliyomo mhusika au mwandishi. Kwa mfano;

  • Toni ya juu ya furaha
  • Toni ya chini ombelezi
  • Toni ya chini bembelezi
  • Toni ya juu chochezi
  • Toni ya juu chokozi
  • Toni ya chini ya huzuni
  • Toni ya chini ya huruma
  • Toni ya chini nyenyekevu
  • Toni ya juu ya uchungu
  • Toni ya juu changamfu
  • Toni ya chini ya mapenzi
  • Toni ya juu ya kuamrisha
  • Toni ya juu ya majigambo
  • Toni ya juu ya hasira.

HISIA

Hisia ni hali inayomuathiri mhusika/ mwandishi au msomaji kwa namna fulani.

AINA ZA HISIA

Hisia ni za aina mbili yaani;

  1. Hisia hai
  2. Hisia za kubuni

HISIA HAI

Hizi ni hisia ambazo humkumba msomaji au msikilizaji wakati wa kusikiliza/ kusoma kifungu cha habari. Hisia hai ni pamoja na;

  • Hisia ya mapenzi
  • Hisia ya huzuni
  • Hisia ya uchungu
  • Hisia ya huruma
  • Hisia chukivu
  • Hisia ya hasira.

HISIA ZA KUBUNI

Hizi ni hisia ambazo msomaji au msikilizaji humpachika mhusika au mwandishi baada ya kutambua hali au mazingira aliyomo. Hisia za kubuni ni pamoja na;

  • Hisia ya uchungu
  • Hisia ya hasira
  • Hisia ya huruma
  • Hisia ya mapenzi
  • Hisia chukivu
  • Hisia huzuni
  • Hisia ya fedheha

HALI/ MAZINGIRA YA MWANDISHI/MHUSIKA

Ni namna mhusika/ mwandishi anavyoonekana. Kwa mfano;

  • Hali ya machafuko
  • Hali ya mawazo
  • Hali ya ulevi
  • Hali ya majuto
  • Hali ya majigambo
  • Hali ya huzuni
  • Hali ya wasiwasi
  • Hali ya mtanziko
  • Hali ya furaha
  • Hali changamfu
  • Hali nyenyekevu
  • Hali ya mapenzi
  • Hali ya maombolezi
  • Hali ya fedheha.

MTAZAMO

Mtazamo ni mawazo ya mtu juu ya jambo fulani. Mtazamo ni wa aina mbili, yaani;

  1. Mtazamo hasi

Huu ni mtazamo duni au mbaya kuhusu jambo fulani

  • Mtazamo chanya

Huu ni mtazamo mzuri kuhusu jambo fulani.

DHAMIRA/ NIA/ NASABA/ MADHUMUNI/ MAKUSUDI/ MALENGO/ SHABAHA/ MATARAJIO YA MWANDISHI

Dhamira ni kile kitu kilichomsukuma mwandishi kuandika kazi yake. Mtunzi/ mwandishi anaweza kuwa na dhamira ya kuonya, kutahadharisha, kukemea sifa potofu, kuelimisha, kuzindua, kuliwaza. Nk

SEHEMU Ch:  USHAIRI

Ushairi ni kazi ya Sanaa inayotumia lugha ya mkato au lugha teule na mpangilio wa maneno unaokiuka sheria au kanuni za sarufi.

AINA ZA USHAIRI

Ushairi huainishwa katika aina mbili yaani;

  1. Mashairi arudhi/ mashairi ya kimapokeo/ mashairi ya kijadi
  2. Mashairi huru/ masivina/ mapingiti
  1. MASHAIRI ARUDHI/ MASHAIRI YA KIMAPOKEO/ MASHAIRI YA KIJADI

Mashairi arudhi ni mashairi ambayo huzingatia arudhi/ sharia/ kanuni za utunzi.

Kanuni za utunzi wa mashairi ni zifuatazo;

  • Urari wa vina
  • Ulinganifu wa mizani
  • Mpangilio wa mishororo
  • Mpangilio wa vipande
  • MASHAIRI HURU/ MASIVINA/ MAPINGITI

Haya ni mashairi ambayo hayafuati arudhi za utunzi wa mashairi.

ISTILAHI/ VIPENGELE VYA KISHAIRI

Istilahi ni msamiati wa maneno yanayotumika katika uwanja wa ushairi. Kwa mfano;

  1. Shairi (mashairi)

Shairi ni utungo wa sanaa unaotumia lugha teule na mpangilio wa maneno usiofuata sharia/ kanuni za sharia.

  • Ubeti (beti)

Hiki ni kifungu cha maneno kinachoundwa kwa idadi fulani ya mishororo.

  • Kina (vina)

Vina ni silabi za namna moja au zenye matamshi mamoja zinazopatikana mwishoni mwa kila mshororo.

  • Mizani

Mizani ni silabi zilizomo katika mshororo.

  • Kipande (vipande)

Ni kisehemu kimoja cha mshororo kinachogawika kwa kutumia kipumuo (mkato).

Kila kipande hupewa jina kutokana na nafasi yake au mwanya kinamokaa katika mshororo.

  • Ukwapi– kipande cha kwanza katika mshororo
  • Utao– kipande cha pili katika mshororo
  • Mwandamizi– kipande cha tatu katika mshororo
  • Ukingo– kipande cha nne katika mshororo
  • Mshororo (mishororo)

Huu ni msitari mmoja wa maneno katika ubeti. Mishoror hutofautishwa katika ubeti kama vifuatavyo;

  • Mwanzo/ fatahi/ kifunguo– mshororo wa kwanza katika ubeti.
  • Mloto– mshororo wa pili katika ubeti.
  • Mleo/ Mlea– Mashororo wa tatu katika ubeti.
  • Kituo– Mshororowa mwisho.

Tanibihi: kituo huainishwa katika mikondo miwili, yaani.

  1. Kibwagizo/ kiitikio/ pambio/ mkarara/ bahari

Kibwagizo ni mshororo unaorudiwarudiwa katika kila ubeti.

  • Kimalizio/ kiishio

Huu ni mshororo wa mwisho unaobadilikabadilika.

  • Bahari

Neno bahari linaelekeza maana nne katika ushairi, yaani;

Maana 1: Bahari ni tanzu au majina ya mashairi kama vile; Mtiririko, mathnawi, ukawafi, ukara. Nk

Maana 2: kituo cha utenzi huitwa utenzi.

Maana 3: vina vya kituo cha utenzi pia huitwa bahari.

Maana 4: bahari ni jina jingine kumaanisha kibwagizo.

  • Diwani

Diwani ni kitabu cha mashairi.

  • Utoshelezi

Ni ukamilifu wa mawazo au fikra katika kila ubeti.

  1.  Muwala

Ni mtiririko na mpangilio wa mawazo na visa kutoka ubeti hadi mwingine.

  1.  Muktadha

Ni namna jambo limetumiwa/ zungumziwa katika kifungu cha maneno.

  1. Urari

Urari ni ulingano, usawa, au mpangilio maalum wa vipengele fulani katika utungo. Urari huzingatia mambo kama:

  • Uwiano/ urari wa vina.
  • Ulinganifu wa mizani
  • Ulinganifu wa vipande
  • Mpangilio wa mishororo
  1.  Lugha ya mkato/ lugha teule

Hii ni lugha iliyobanwa, finyangwa, borongwa, teuliwa au ilyochanganywachanganywa.

  1.  Lugha ya nathari

Hii ni lugha ya mjazo, mfululizo au lugha ya maelezo. Ni lugha yenye matumizi ya kanuni au sharia za sarufi.

  1.  Uchambuzi

Ni kuzungumzia maandishi kwa kufafanua nje na ndani.

SIFA ZA MASHAIRI

  • Mashairi huimbika au hughanika
  • Hutumia lugha teule au lugha ya mkato
  • Hukiuka kanuni za sarufi
  • Hutumia maneno yanayonata pamoja na kuvutia.
  • Hutumia mapigo au sauti za lahani
  • Huzingatia mbinu za utunzi.

UMUHIMU WA MASHAIRI

  • Huhifadhi historia kwa vizazi vya mbele.
  • Huhamasisha jamii
  • Huzindua na kuliwaza jamii.
  • Huelimisha na kutoa maarifa kuhusu jambo fulani
  • Hukuza ukwasi wa lugha
  • Hupisha ujumbe
  • Huonya, hushauri, hutahadharisha pamoja na kutoa mwelekezo kuhusu maadili ya jamii.
  • Hukemea na kukejeli sifa potofu

AINA ZA MASHAIRI

Mashairi ya Kiswahili huainishwa kulingana na idadi ya mishororo iliyomo katika beti za shairi. Aidha, shairi haliwezi kuwa la aina mbili. Zifuatazo ni aina mbalimbali za mashairi.

  1. Tathmina (umoja)

Shairi la mshororo mmoja katika kila ubeti.

  • Tathnia (uwili)

Shairi la mishororo miwili katika kila ubeti.

  • Tathilitha (utatu)

Shairi la mishororo mitatu katika kila ubeti.

  • Tarbia (unne)

Shairi la mishororo mine katika kila ubeti.

  • Takhmisa (utano)

Shairi la mishoror sita katika kila ubeti.

  • Tasdisa (usita)

Shairi la mishororo sita katika kila ubeti.

  • Usaba (tasbia)

Shairi la mishororo saba katika kila ubeti.

  • Unane  (naudia)

Shairi la mishororo minane katika kila ubeti.

  • Utisa (telemania)

Shairi la mishororo tisa katika kila ubeti.

  1.  Ukumi (taashuri)

Shairi la mishororo kumi katika kila ubeti.

BAHARI ZA MASHAIRI

Bahari ni tanzu au majina ya mashairi. Mashairi hupewa majina kutokana na;

  1. Idadi ya mizani katika mshororo
  2. Mpangilio wa vina
  3. Idadi ya vipande
  4. Mpangilio wa maneno

BAHARI KUTOKANA NA IDADI YA VIPANDE

  1. Utenzi (tenzi)

Hili ni shairi la kipande kimoja. Tazama michoro

Ubeti wa kwanza:               ………………………………………

                                             ………………………………………

                                              ……………………………………… 

Ubeti wa pili:                        ……………………………………..

                                                  …………………………………….

                                                  …………………………………….

  • Mathnawi

Shairi la vipande viwili katika kila ubeti. Tazama michoro

Ubeti wa kwanza:                     ………………….,    …………………….

                                                  ………………….,     ……………………

                                                  ………………….,      ……………………

                                                  ………………….,     …………………….

Ubeti wa pili:                           ………………….,     …………………….

                                                   …………………,      …………………….

                                                   …………………,       ……………………

                                                    ………………..,       ……………………

  • Ukawafi

Shairi la vipande vitatu katika kila ubeti. Tazama michoro.

Ubeti wa kwanza:                 

 ……………….,    ………………..,     ………………….

  ……………….,    ………………..,    …………………

   ….………………,     ……………….,    ……………….

Ubeti wa pili:                          

 ……………….,     ……………….,       ………………

 ………………..,     ……………….,     ……………..

  ………………..,     ……………….,      ……………..

  • Mauve/ bantudi

Shairi la vpande vinne katika kila ubeti. Tazama michoro

Ubeti wa kwanza:               

Ukwapi

……………,   ……………….,   ………………..,  ……………….

……………..,   ……………….,    ………………..,   ………………

 ……………..,    ………………,    …………………,    ……………..

Ubeti wa pili:

……………..,   ……………….,   …………………,    ………………

……………..,   ……………….,   …………………,   ……………….

……………..,    ………………,    …………………,   ………………

BAHARI KUTOKANA NA MPANGILIO WA VINA

  1. Mtiririko.

Shairi ambalo vina vyote vya ndani na vya nje hukaririwa/ hurudiwarudiwa kutoka mwanzo hadi mwisho wa shairi. Tazama michoro.

Ubeti wa kwanza:

 …………………………….ta, ……………………………pa

  …………………………….ta, ……………………………pa

 …………………………….ta,   ……………………………pa

Ubeti wa pili:

…………………………….ta,   …………………………….pa

…………………………….ta,   ……………………………pa

…………………………….ta,   ……………………………pa

  • Ukara

Shairi ambalo vina vya kipande kimoja vinakaririwa/ vinatiririka na vya kipande kingine vinabadilikabadilika/ vinahitilafiana. Tazama michoro.

  1. Ubeti wa kwanza:

………………………ka,   ……………………..sa

 ………………………ka,   ……………………..sa

  ………………………ka,   ……………………..sa

  • Ubeti wa pili:

   ……………………..ka,    …………………….ta

    ……………………..ka,    …………………….ta

    ………………………ka,   …………………….ta

Mfano wa pili

  • Ubeti wa kwanza:               

 ……………………….ma,   …………………na

            ……………………….ma,   ………………….na

            ……………………….ma,    …………………na

             Ubeti wa pili:

……………………….te,   ……………………na

 ………………………te,    ……………………na

  ………………………te,    ……………………na

  • Ukaraguni

Shairi ambalo vina vyake vyote vya nje na vya ndani hubadilikabadilika kutoka mwanzo hadi mwisho wa shairi. Tazama michoro

Ubeti wa kwanza:

………………………..tu,   …………………….pi   

………………………..tu,   …………………….pi

………………………..tu,   …………………….pi

Ubeti wa pili:

  ………………………..ka,   ……………………la

   ………………………..ka,    …………………..la

    ………………………..ka,    …………………..la

  • Mkararaguni

Shairi ambalo kila ubeti hwa na vina vyake kivyake. Vina vikipatikana katika ubeti mmoja haviwezi kupatikana tena katika ubeti mwingine hadi mwisho.

Kawaida ya mkararaguni ni kwamba vina vyote vya nje na vya ndani hubadilikabadilika kutoka mwanzo wa shairi hadi mwisho.

BAHARI KUTOKANA NA IDADI YA MIZANI

  1. Kisarambe

Shairi la mizani kumi na sita katika mshororo, yaani; (-8, -8). Kwa mfano;

(Ba-do sa-fa-ri ni nde-fu), (wa-sa-fi-ri tu-si-cho-ke)

( -8 )                                         ( -8 )

  • Kikai

Shairi la mizani kumi na mbili. Shairi la kikai lina mikondo mitatu yaani;

  1. Kipande cha kwanza huwa na mizani nane na cha pili huwa na mizani nne, yaani;   (-8, -4). Tazama mfano;
  2. (Bi-na-da-mu     a-te-nda-ye), (ma-te-ndo-ye)

                                      (-8)                                   (-4)

  • Kipande cha kwanza huwa na mizani nne na cha pili huwa na mizani nane, yaani;   (-4, -8). Tazama mfano;
  • (Si-ki-li-za),(e-we   mu-e-nye   ki-bu-ri)

(-4)                              (-8)

  • Vipande vyote viwili huwa na mizani sita sita, yaani; (-6, -6). Kwa mfano
  • (Mu-we-za   na   mwe-ma),  (ni-m-nye-nye-ke-le)

                                   (-6)                                          (-6)

BAHARI KUTOKANA NA MPANGILIO WA MANENO

  1. Kikwamba

Hili ni shairi ambalo neno au maneno hurudiwarudiwa katika mwanya maalum. Neon laweza kurudiwarudiwa mwanzoni mwa kila mshororo, katikati, au mwishoni mwa kila mshororo. Pia laweza kujitokeza mwanzoni mwa kila ubeti.

MIKONDO YA KIKWAMBA

  • Neno kujitokeza mwanzoni mwa kila mshororo. Kwa mfano;

Ubeti wa kwanza:        jiwe……………..,    …………………..

                                     Jiwe……………..,    ………………….

                                     Jiwe……………..,    ………………….

                                     Jiwe……………..,     ………………….

Ubeti wa pili:              jiwe………………,     ………………….

                                     Jiwe………………,     ………………….

                                     Jiwe………………,     ………………….

                                     Jiwe………………,      …………………

  • Neno kujitokeza katikati ya mshororo. Kwa mfano;

Ubeti wa kwanza:     

 ……………mama,    ………………….

  …………..mama,     ………………….

   …………..mama,     ………………….

Ubeti wa pili:

  ………….mama,     ………………….

………….mama,     ……………………

………….mama,     …………………….

  • Neno kujitokeza mwishoni mwa kila mshororo. Kwa mfano;

Ubeti wa kwanza:

………………………,    ……………..jina

………………………,    ……………..jina

………………………,    ……………..jina

Ubeti wa pili:

………………………,    ……………..jina

………………………,    ……………..jina

………………………,    ……………..jina

  • Neno kujitokeza mwanzoni mwakila ubeti. Kwa mfano;

Ubeti wa kwanza:      chema……………,    ……………………

                                      ………………………,    ……………………

                                      ……………………….,    …………………..

                                      ……………………….,    ……………………

Ubeti wa pili:              chema…………….,    ………………………..

                                      ……………………….,    ……………………

                                      ……………………….,    ……………………

                                      ……………………….,    ……………………

  • Pindu/ Mkufu

Pindu ni shairi ambalo neno au maneno ya mwisho katika kipande hufanywa neno au maneno ya kwanza katika kipande kinachofuatia.

MIKONDO YA PINDU

  • Mizani mbili katika neno la mwisho la kipande kinachotangulia kufanywa neno la kwanza katika kipande kinachofuatia. Kwa mfano;

 …………………..madhehebu,   hebu…………………………………

 …………………………..wajibu,    jibu………………………………..

 …………………….mahabubu,    bubu………………………………..

 …………………………..sahibu,     hibu………………………………

 …………………………..sababu,     babu……………………………..

……………………………katibu,      tibu……………………………….

……………………………nasibu,      sibu……………………………….

  ………………………….skurubu,      rubu……………………………..

  • Neno la mwisho katika kituo cha ubeti unaotangulia kufanywa neno la kwanza katika ubeti unaofuatia. Tazama michoro.

         ………………………………………,    …………………………………….

          ………………………………………,    …………………………………….

         ………………………………………,    …………………………………….

          ………………………………………,    …………………………hakomi.

 Hakomi………………………..,     ……………………………………….

   …………………………………….,     ……………………………………….

  ……………………………………..,    ……………………………………….

    ……………………………………..,    ……………………………………….

  • Kipande cha mwisho cha kituo katika ubeti unaotangulia kufanywa kipande cha kwanza katika ubeti unaofuatia. Tazama michoro

         …………………………………….,    …………………………….

         ……………………………………..,   …………………………….

         ……………………………………..,    …………………………….

           ……………………………………..,    yako mbeleni mauti.

           Yako mbeleni mauti,     ……………………………………..

          …………………………….,     ………………………………

          …………………………….,     ………………………………

           …………………………….,     ……………………………..

  • Mkarara

Neno, kipande, au mshororo hurudiwarudiwa mwanzoni mwa kila ubeti na kukaririwa mwishoni mwa ubeti huo.

BAHARI NYINGINEZO

  1. Sakarani

Ni shairi la bahari Zaidi ya moja.

  • Msuko

Ni shairi la kituo kifupi.

  • Sabilia

Shairi ambalo lina kituo kinachobadilikabadilika. Shairi lenye kimalizio/ kiishio katika kila ubeti.

  • Ngonjera

Shairi la majibizano kati ya wahusika wawili au Zaidi.

  • Malumbano

Shairi la mjadala; mshairi mmoja hujitokeza waziwazi kumpinga mshairi mwingine.

  • Madhuma

Shairi ambalo ukwapi hutoa hoja na utao suluhisho.

  • Guni

Shairi lenye kasoro au lenye makosa ya arudhi za utunzi wa mashairi.

  • Mashairi huru/ masivina/ mapingiti

Mashairi yasiyofuata arudhi/ sharia/ kanuni za utunzi.

UHURU WA MSHAIRI/ KIBALI CHA MSHAIRI/ IDHINI YA MSHAIRI/ UKIUKAJI WA SARUFI

Mshairi ana uhuru Fulani usioruhusiwa katika maandishi mengine. Uhuru huu humuwezesha mtunzi kukiuka lugha wakati anapobanwa na sharia za sarufi. Vifuatavyo ni vipengele vya uhuru wa mshairi.

  1. Kuboronga sarufi

Huu ni uhuru wa kuchanganya ngeli pamoja na kubadilisha mpangilio wa maneno kwa lengo la kusawazisha vina.

  1. Kuchanganya ngeli

Kiswahili sanifu                                                            kuboronga sarufi

  • Magari hayo                                                            magari hizi
  • Waya huu                                                                 waya hii
  • Ng’ombe hawa                                                        ng’ombe hizi
  • Mtu huyu                                                                  mtu huu
  • Kitabu hiki                                                                 kitabu hii
  • Kubadilisha mpangilio wa maneno

Kiswahili sanifu                                                             kuboronga sarufi

  • Sehemu ya nyuma                                                    ya nyuma sehemu
  • Babu analia sana                                                       amelia sana babu
  • Moyo umejaa pendo                                                moyo pendo umejaa
  • Mbona umelimatiya?                                               Umelimatiya mbona?
  • Nakupenda tena asana                                               tena sana nakupenda
  • Mazda

Ni uhuru wa kurefusha maneno kwa ajili ya kuzidisha mizani katika neon bila kupotosha maana asili. Mazda huhusisha mambo yafuatayo.

  1. Kutumia maneno ya umbo ndefu badala ya yale ya umbo fupi.

Kiswahili sanifu                                                                mazda

  • Mke                                                                                  harimu
  • Wimbo                                                                             kasida
  • Mtu                                                                                   kaumu
  • Neno                                                                                 kauli
  • Mwisho                                                                            hatima
  • Kuzidisha silabi za neno. Kwa mfano;

Kiswahili sanifu                                                               mazda

  • Jini                                                                                 ajinani
  • Remba                                                                           rembesha
  • Tabu                                                                               taabu
  • Tanzia                                                                            taanzia
  • Pulika                                                                             pulikiza
  • Mwendawazimu                                                          muendawazimu
  • Enda                                                                               enenda
  • Inkisari

Huu ni uhuru wa kufupisha maneno kwa ajili ya kupunguza mizani na kusawazisha vina. Inkisari huhusisha mambo kama;

  1. Kupunguza silabi katika neno. Kwa mfano

             Kiswahili sanifu                                                            inkisari

  • Niambie                                                                       nambe
  • Ameenda                                                                     meenda
  • Kinaniletea                                                                  chanetea
  • Upuuzi                                                                          upuzi
  • Huenda                                                                         hwenda
  • Tuendelee                                                                    twendelee
  • Waite                                                                             wete
  • Naondoka                                                                     nondoka
  • Mueleze                                                                        mweleze
  • Alikuwa                                                                          yali
  • Tulikuwa                                                                        twali
  • Kuunganisha maneno mawili kuwa moja. Kwa mfano;

Kiswahili sanifu                                                           inkisari

  • Mti wako                                                                    mtiwo
  • Hadhi yake                                                                 hadhiye
  • Mke wake                                                                   mkewe
  • Mwana wangu                                                           mwanangu
  • Baba yako                                                                   babako
  • Unasema nini?                                                           Unasemani?
  • Kutumia maneno ya umbo fupi badala ya yale ya umbo ndefu. Kwa mfano;

Kiswahili sanifu                                                           inkisari

  • Siku zote                                                                       abadi/ daima
  • Hata kidogo                                                                  asilani
  • Hana chochote                                                             hanani
  • Sina chochote                                                               sinani
  • Tabdila

Uhuru wa kubadilisha umbo/ tahajia ya neno bila kupunguza wala kuzidisha mizani kwa lengo la kupata vina. Kwa mfano;

Kiswahili sanifu                                                           tabdila

  • Jua                                                                                juwa
  • Yai                                                                                 yayi
  • Ua                                                                                 uwa
  • Oa                                                                                 owa
  • Kabidhi                                                                         kabidha
  • Maharagwe                                                                 maharagi
  • Jumuiya                                                                        jumuia
  • Fua                                                                                fuwa
  • Endea                                                                            endeya
  • Fikiria                                                                            fikiriya
  • Utohozi

Huu ni uhuru wa kuswahilisha maneno ya lugha ngeni ili yatamkike kama ya Kiswahili. Kwa mfano;

Kiingereza                                                                  utohozi

  • Time                                                                         taimu
  • Comuter                                                                  kompyuta
  • Skirt                                                                          sketi
  • Station                                                                     stesheni
  • Television                                                                televisheni
  • Dictator                                                                    dikteta
  • Robot                                                                        roboti
  • Phone                                                                       foni
  • Tone                                                                          toni
  • Radio                                                                         redio
  • Video                                                                          vidio
  •  Tractor                                                                      trekta
  • Radiator                                                                     redieta
  •  

              Kiarabu                                                                       utohozi

  • Hakk                                                                       haki
  • Bustan                                                                    bustani
  • Bint                                                                         binti
  • Khamsin                                                                 hamsini
  • Kherr                                                                       kheri
  • Ardh                                                                         ardhi

UCHAMBUZI WA MASHAIRI

Uchambuzi wa mashairi unazingatia mambo kama;

  1. Muundo wa shairi.
  2. Mtindo wa shairi
  3. Lugha ya nathari.

MUUNDO WA SHAIRI

Muundo ni sura ya nje na ndani ya shairi. Katika muundo wa shairi tunazingatia mambo kama;

  1. Umbo la shairi.
  2. Mtindo wa lugha
  3. Maudhui
  4. Ujumbe
  5. Mafunzo
  6. Dhamira ya mwandishi
  7. Mbinu/ fani
  8. Ukwasi wa lugha

UMBO LA SHAIRI

Umbo ni sura ya nje ya shairi. Umbo huzingatia jinsi shairi lilivyoumbwa kwa kuzingatia vipengele kama;

  • Kichwa cha shairi
  • Idadi ya beti
  • Mizani
  • Idadi ya mishororo katika kila ubeti
  • Idadi ya mizani katika mishororo
  • Idadi ya vipande
  • Mpangilio wa vina
  • Kituo.

NAMNA YA KUJIBU UMBO LA SHAIRI

  1. Shairi hili lina kichwa ambacho ni …………… (andika kichwa cha shairi katika herufi kubwa)
  2. Shairi hili lina beti ………………………….. ( taja idadi ya beti katika shairi kwa ujumla)
  3. Shairi lina mishororo ……………………. ( taja idadi ya mishororo katika kila ubeti), kwa hiyo ni la …………………….. ( taja aina ya shairi)
  4. Shairi lina mizani ………………………………. ( taja idadi ya mizani katika mishororo)
  5. Shairi lina vipande ………………………. ( taja idadi ya vipande), kwa hiyo ni la ………………………. ( taja bahari kulingana na idadi ya vipande)
  6. Shairi hili lina kimalizio/ kiishio ( ikiwa kituo kinabadilikabadilika)
  7. Shairi hili lina kibwagizo ambacho ni …………………… (andika kibwagizo ikiwa kipo)
  8. Shairi lina vina vya kati na vya mwisho vinavyotiririka kwa hiyo ni la mtiririko.

Au

           Shairi lina vina vya ndani na vya nje vinavyobadilikabadilika kwa hiyo ni la

Ukaraguni

           Au

           Shairi lina vina vina vya kipande kimoja vinatiririka na vya kingine                

Vinabadilika kwa hiyo ni la ukara.( eleza ni kipande kipi kilicho na vina

Vinavyobadilikabadilika na ni kipi chenye vina vinavyotiririka.

MAUDHUI

Maudhui ni mambo muhimu yanayozungumziwa katika kazi ya fasihi. Maudhui ni jumla ya visa, fikra na matendo katika kazi ya fasihi.

UJUMBE

Ujumbe ni habari iliyowekwa wazi mtunzi/ mshairi kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu jambo fulani.

MAFUNZO/ MAADILI

Haya ni mambo anayojifunza msomaji au msikilizaji baada ya kusoma au kusikiliza kifungu Fulani cha habari.

DHAMIRA/ MALENGO/ NIA/ MADHUMUNI/ SHABAHA/ MAKUSUDI/ NASAHA/ MATARAJIO YA MTUNZI

Dhamira ni kile kitu kilichomsukuma mtunzi kutunga kazi yake. Mtunzi wa shairi anaweza kuwa na lengo la kuelimisha, kuonya, kutahadharisha kunasihi. Nk

MTINDO WA LUGHA/ MATUMIZI YA LUGHA

Mtindo wa lugha au matumizi ya lugha hurejelea namna mtunzi anavyotumia mbinu za lugha katika shairi.

UKWASI WA LUGHA/ UBINGWA/ UHODARI/ UMAARUFU/ UKAKAMAVU WA MTUNZI

Huu ni uwezo wa mshairi/ mtunzi kutumia lugha fulani bila kuhusisha fasihi ya lugha nyingine.

Tanbihi:  Mwanafunzi akiulizwa kuchambua ukwasi wa lugha, azungumzie mbinu nyingine isipokuwa utohozi, mseto pamoja na kuhamisha ndimi kwa kuwa mbinu hizi tatu zinahusisha lugha ngeni katika Kiswahili.

MTINDO WA SHAIRI

Mtindo wa shairi huhusisha mambo kama;

  1. Aina ya shairi
  2. Bahari ya shairi

NAMNA YA KUCHAMBUA MTINDO

  1. Mshairi ametumia mtindo wa tarbia kwa sababu shairi lina mishororo minne katika kila ubeti. ( ikiwa shairi lina mishororo minne)

            Au

           Mshairi ametumia mtindo wa tathlitha kwa sababu shairi lina mishororo

           Mitatu katika kila ubeti. (Ikiwa shairi lina mishororo mitatu). Nk

  • Mshairi ametumia mtindo wa mathnawi kwa sababu shairi lina vipande viwili. ( ikiwa shairi lina vipande viwili)

           Au

           Mshairi ametumia mtindo wa ukawafi kwa sababu shairi lina vipande vitatu.

           (Ikiwa shairi lina vipande vitatu)

Tanbihi: taja bahari nyinginezo kwa kufuata njia hii.

LUGHA YA NATHARI

Nathari ni maandishi ya kutumia lugha ya maelezo, mjazo, mfululizo, lugha ya insha au lugha ya kawaida yenye kutii kanuni za sarufi.

MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA KUANDIKA KATIKA LUGHA YA NATHARI.

  • Mshororo hubadilishwa kuwa sentensi.
  • Ubeti hubadilishwa kuwa aya.
  • Vipande na vina huondolewa.
  • Kanuni za sarufi hurejelewa.
  • Nathari hutumia lugha ya kawaida.
  • Mtu anaweza kutumia maneno yake mradi tu asipotoshe maana.
  • Lugha ya kishairi pamoja na uhuru wa mshairi huondolewa.

UTARATIBU WA KUFUATA WAKATI WA KUANDIKA KATIKA LUGHA YA NATHARI

  • Soma ubeti au beti ulizoagizwa kuandika katika lugha ya nathari.
  • Fafanua muktadha wa ubeti ulioagizwa kuandika katika lugha ya nathari.
  • Toa/ fafanua ujumbe uliomo katika ubeti ulioagizwa kuandikwa katika lugha ya nathari.
  • Toa kiini/ jambo muhimu linalozungumziwa katika ubeti ulioagizwa kuandikwa katika lugha ya nathari.
  • Panua kiini/ jambo muhimu kwa kutumia maneno yako bila kupotosha maana asili.
  • Andika kazi yako katika aya moja.

Tanbihi: ikiwa umeagizwa kuandika beti mbili au Zaidi katika lugha ya nathari, andika kila ubeti katika aya yake kivyake.

5 thoughts on “MWONGOZO WA KARATASI YA KWANZA NATHARI, UFAHAMU NA USHAIRI: SIMON T KAWAIDA NA JOHNPAUL ARIGUMAHO.

Leave a reply to Mwalimu Arigumaho Johnpaul Cancel reply