MWONGOZO WA TAMTHILIA YA CHEMA CHAJIUZA-Innocent Agume.

MWONGOZO KAMILIFU WA TAMTHILIA YA CHEMA CHAJIUZA.

MWALIMU JOHNPAUL ARIGUMAHO.

arigumaho810@gmail.com.0778514179.

INKSIRI

MwongozoKamilifu wa Chema Chajiuza ni kazi ambayo imejadili kwa muhtasari ploti au muundo wa tamthilia ya Chema Chajiuza ukionyesha kila kitendo na kila onyesho visa vikuu vilivyotendeka.Pia, wahusika na sifa zao tukirejelea kurasa wanapojitokeza, maudhui pamoja na ufafanuzi vipatikanamo tamthiliani chema Chajiuza bila kusahau mbinu za kifani na kisanaa mwandishi alizotumia kupamba lugha ili kukamilisha ujumbe wake.

TABARUKU.

Natabaruku kazi hii kwa mama yangu mpendwa Bi katekista Katushabe Beatrice na wowote wanaojali.

Pia, bila kuwasahau wataalamu na wakiwemo Mwalimu Abaho Rogers, Simon kawaida, Ariiho Edwin, Vicent Muhereza, Earnest Muwuta Mwase. Mwenyezi Mungu awabarike na kuwapa kila la kheri.

SHUKRANI.

Mchakato mzima wa kukamilisha kazi hii haukuwa kwa bidii zangu kama Johnpaul Arigumaho bali iliweza kukamilika kutokana na michango pamoja na misaada ya watu wengine.

Kwanza mwenyezi mungu sina kikomo kumshukuru kwa kila kitu.

Tena, shukrani zangu za pekee zimwendee Mh.Innocent Agume aliyebobea sana na kuangalia kwa undani kilichomo katika kizazi cha leo kwa kutunga tamthilia ya Chema Chajiuza, shukrani sana mheshimiwa.

Vilevile, sina budi kuwashukuru wa ambao hawaniachi nyuma bali kila mara nikiwafikia wananielekeza katika njia inayostahili na hao ni Mh.Mhadhiri Bwana Kubakurungi Abraham, Mh.Mhadhiri Bi-Asiimwe Caroline PamojaMh.Mhadhiri Bi-Ninsiima Betty. Moyo wangu ndio unaojua jinsi ninavyojihisi juu ya ninyi.

Tamthilia hii ya chema chajiuza iliandikwa na Innocent Agume aliyezaliwa wilayani Ntungamo magharibi mwa Uganda. Innocent ni mwandishi aliyeinukia kwa kasi na mwenye jicho la ndani katika uga wa fasihi na lugha.

Tamthilia hii ya chema chajiuza inazungumzia juu ya unafiki na wema unaopatikana katika kizazi cha leo.

Mwandishi anasema kwamba wengi wanapoajiriwa wanajidai ni wafanyakazi waadilifu na wenye bidii kwelikweli, kumbe ni vinyonga wanaogeuza rangi ili wawasaliti marafiki na kuwaibia waajiri wao!

Tunaona injinia Bakehena anaonyesha unafiki wake kwa kupunja na kuiba pesa za mwajiri wake kabaila Bumaali na mwishowe akafutwa kazini halafu maisha yake yakabadilika kuwa magumu sana.

Lakini miongoni mwa watu wengi, kuna wachache wazuri na wenye wema.

Yeye Bwana Kwatampola katika tamthilia tunamuona anaonyesha wema wake kwa kuwa mfanyakazi mwadilifu na mwaminifu kwa mwajiri wake kabaila Bumaali na kisha akatunukiwa na zawadi kubwa Iliyokuwa ndoto yake kila siku na ndio sababu chema chajiuza.

PLOTI/ MUUNDO WA TAMTHILIA.

Muundo huwa ni mtiririko wa visa na matukio katika kazi za kifasihi. Hapa, tutaangalia jinsi mwandishi Innocent alivyofuma matukio kwa muhtasari kutoka kitendo cha kwanza hadi kitendo cha nne na mawazo makuu yaliyomo.

KITENDO CHA KWANZA.

ONYESHO LA KWANZA.

Hapa, tunamuona Bwana Kwatampola nyumbani kwake kakoba anazungumza na mke wake Kunihira juu ya kukosa kumkuta Mzee Bumaali.

Bwana Kwatampola tunamuona baada ya kuambulia patupu anapanga miadi na mtumishi kumpigia simu ili amkute Kabaila Bumaali.

Pia, tunamuona Injinia Bakehena anafutwa kazini na analalamika juu ya kabaila Bumaali kwa kumfukuza.

Vilevile, tunamuona Kunihira analalamika juu ya mume wake kwamba labda alirogwa kwakuwa pesa anazozipata kutoka kwa Bumaali hazitumiki vyema iwezekanavyo.

ONYESHO LA PILI.

Hapa tunamuona Bumaali na Kwatampola wameketi uani. Bumaali anamwelezea Kwatampola kwamba alipata kidosho na anataka akitengenezee jumba huko Nyamitanga. Bumaali amempa Kwatampola milioni thelathini (30) ili ashughulikie kazi nzima ya kujenga ugo halafu atajenga jumba zima. Milioni thelathini ni za vifaa na vibarua. Bumaali anamwambia Kwatampola kwamba injinia bakehena alimuibia pesa na asimsaliti kama yeye.

ONYESHO LA TATU.

Hapa, tunawaona Mzee Bahemuka na mke wake Bi-Shogora njiani wanamtembelea mwanao Kwatampola

huko kwake Kakoba. Mzee Bahemuka anatembea kwa kuinama na na kuiweka mikono yake juu ya mkongoji alioulaza mabegani kwake. Bi-shogora na mumewe Bahemuka wanatembea wakizungumuzia juu ya mtoto wao kwamba ni maskini mzuri tena mwadilifu. Tunawaona wamefika Kakoba nyumbani kwa Kwatanpola mtoto wao, mke wake Kwatampola Kunihira anawakaribisha kwa heshima na kumpa mcheja wake Bi-Shogora maji ya Rwizi ya kunywa kupuuza joto la njia. Papo hapo, Kunihira anawaelezea kwamba mtoto wao babake Ben yumo kitandani na Ben mwenyewe ameenda shuleni.

Vilevile, Kwatampola anakuja kutoka kitandani na kuwasalamia badaaye anaondoka nje na babake halafu Kunihira akabaki nyumbani na mcheja wake Bi-shogora wakijadiliana.

Baada ya muda mchache, tunawaona Bahemuka na mke wake bi shogora wanaondoka kurudi kwao Rwampala.

KITENDO CHA PILI.

ONYESHO LA KWANZA.

Hapa, tunawaona Kwatampolana mkewe Kunihira nyumbani kwao wanazungumuza pamoja. Kwatampola anamwambia mkewe kwamba Mzee Bumaali amemuita asubuhi na kumpa kandarasi ya mradi kujenga ugo na badaaye atajenga jumba zima huko Nyamitanga.

Tunawaona pia Kwata na mkewe Kuni wanaondoka kwenda kule Nyamitanga pale jumba litakapojengwa. Tunaona Kuni amepewa kazi ya kupikia wajenzi wote na kwata anawasimamia wajenzi wake.

ONYESHO LA PILI.

Hapa, tunamuona kabaila Bumaali anamshukuru kwatampola kwa kujenga ugo vizuri na kwa muda uliokuwa unatakikana. Bumaali anampa kwata bunda la noti ya shilingi milioni mbili ili azigawanyie vibarua wake kwa kazi waliyoifanya na Kwata anashukuru sana.

Pia, tunamuona Bakehena anazungumuza na Kwatampola kuhusu masuala ya pesa alizopewa na kabaila Bumaali halafu anaenda maramoja hadi nyumbani kwa kwata na kumwelezea Kunihira kwamba mume wake Kwata amepewa hela nyingi sana na ameenda mjini mbarara kuzitumia ovyoovyo.

Tunamuona Kunihira baada ya kusikia ujumbe huo anashutuka na kumuita Ben kwa kumtusi kwamba ni mjinga kama babake kwa hasira.

 Papohapo, tunamuona Kwata anaingia. Mkewake anaanza kulalamika juu ya ujumbe alioupokea ya kwamba amepewa hela na ameenda mjini kuziharibu kumbe kwata alikuwa ameenda kuvinunua vifaa vya ujenzi.

Tunamuona Kunihira maramoja anaingia nyumbani na kuchukua begi yake kubwa na kurudi kwao Kabale. (talaka inafanywa). Tunamuona Ben mtoto wao analia juu ya kuachwa na mamake lakini babake Kwata anambembeleza na halafu anamtwaa Rwampala kwa mzee Bahemuka na Bi-shogora ili wamlee hadi mamake atakaporudia.

ONYESHO LA TATU.

Hapa, tunamuona Kwatampola na wajenzi wake mkutanoni huko Nyamitanga katika uwanja wa ujenzi. Kwata anawagawanyia hela alizopewa na kabaila Bumaali juu ya kazi nzuri waliyoifanya ya kujenga ugo.

Tena, Kwata anawaelezea wajenzi kwamba alikumbwa na vita vya kibinafsi, tamaa na mwishowe mke wake akamuacha.

Wajenzi wanakabidhiwa hela na kila mtu akachukuwa shilingi 36956.52. Wote wajenzi wanamshukuru kwata na kabaila Bumaali.

KITENDO CHA TATU.

ONYESHO LA KWANZA.

Hapa, tunamuona Kunihira Nyamitanga katika uwanja wa ujenzi tena jikoni kwa upishi anawahudumia wajenzi.

Tunawaona wajenzi wote na mainjinia wanafanya kazi kwa bidii.

ONYESHO LA PILI.

Hapa, tunawaona kwata na mainjinia watatu wanaongea kwa sauti za chini sana.

Injinia wa tatu anamwambia kwata kwamba yeye ni msomi hataki vitu vya upesiupesi. Pia tunamuona injinia huyo anamshukuru kwata kwa kazi nzuri.

ONYESHO LA TATU.

Hapa, tunamuona Injinia Bakehena nyumbani kwake chumbani mwake anazungumuza na mke wake Nabaganzi. Nabaganzi anamwambia mume wake kwamba Kabaila Bumaali anamtangaza kwa marafiki zake wote ya kwamba alimuibia pesa.

Pia, tunamuona Bakehena anapanga kuelekea mjini Fortportal kutafuta kazi ya kufanya ili naye aajiriwe kama wengine.

KITENDO CHA NNE.

ONYESHO LA KWANZA.

Hapa, tunamuona Nabaganzi anaongea na kwatampola katika uwanja wa ujenzi huko nyamitanga. Tunaona kwatampola amempa Nabaganzi kazi ya ufagizi na anashukuru sana.

ONYESHO LA PILI.

Katika onyesho hili, tunawaona Bumaali, Akello na wajenzi wote huko Nyamitanga katika kasri na wanakagua kazi waliyoifanya kwa muda.

Kabaila Bumaali anashukuru sana Kwata hadi kiasi cha kumbusu mkononi juu ya kazi nzuri aliyoifanya na wajenzi wake wote.

Pia, tunamuona injinia wa pili anahakikisha uzuri wa Bwana Kwatampola kwa kusema kwamba hata mitaimbwa, rangi na mabati viliibwa lakini Kwata alitumia pesa zake mwenyewe kununua vipya.

ONYESHO LA TATU.

Hapa, tunaona wageni washerehekeaji wakiendelea kumwajika wakiwemo wafanya biashara mashuhuri, wanasiasa, wanadini wake na waume wote Nyamitanga uani wa kasri la Machu.

Pia, tunawaona wageni waalikwa na wasioaalikwawote wanakaribishwa. Mziki unaendelea kupigwa polepole na Mc-bob king. Watu wote wamefurahi sana.

Bwana harusi Bumaali na Bi-harusi Machu nao wanakaribishwa. Mziki unadundwa tena na Mc.Bob king mfawidhi.

Vilevile, tunaona Bumaali anatoa hotuba kwa kushukuru kila mtu na mke wake wa kwanza Bi-Akello.

 Bumaali anazawadia kwatampola juu ya wema wake kwa kumpa kisanduku chenye funguo na hati ya maandishi yaliyo ya kumpa jumba hilohilo alilojengea Machu la Nyamitanga.

Bila shaka tunamuona Kunihira anatoka shoti juu ya yale aliyoyasikia na wanakuja kumhudumia kwa kumuzoea pale alipokuwa ameanguka. Kunihira anapelekwa Mbarara Regional Referal hospital.

Vivyohivyo, Bumaali anahitimisha kwamba atarudi kwake Makenke na wake wake wote wawili na kumwachia kwata jumba la Nyamitanga.

WAHUSIKA NA SIFA ZAO KATIKA TAMTHILIA YA CHEMA CHAJIUZA.

Wahusikani viumbe hai au visivyohai vinavyoshirikishwa katika kazi yeyote ya kifasihi ili kujenga maudhui na dhamira ya mwandishi.

Wahusika wanaweza wakawa kama vile wanyama, ndege, wadudu, nakadhalika. Tunaainisha wahusika hao kwa makundi tofauti kama vile wahusika wakuu, wahusika wadogo na wahusika wasaidizi.

Hivyo basi, katika tamthilia hii ya chema chajiuza, kuna wahusika kadhaa mwandishi aliowatumia kufikisha ujumbe wake kwa hadhira na baadhi yao ni;

KWATAMPOLA: Mhusika huyu ana sifa zifuatazo;

  • Ni mhusika mkuu kwani tunamuona anajitokeza aghalabu katika tamthilia nzima.
  • Ni mzazi kwani tunamuona katika tamthilia anambembeleza mtoto wake aitwaye Ben. (uk 23)
  • Ni mume kwani katika tamthilia tunamuonandiye aliyeoa Kunihira.
  • Ni mwanake Mzee Bahemuka na Bi-Shogora kwani tunawaona wanakiweza wakati walipomtembelea kwake Kakoba.(uk 23)
  • Ni mfanya kazi kwani tunamuona hata alizawadiwa juu ya wema wake katika kazi ya kujenga jumba la Machu huko Nyamitanga.(uk 115)
  •  Ni mtiifu kwani tunamuona katika tamthilia anamtii mwajiri wake Kabaila Bumaali hata kufika kiwango cha kutomuita jina lake bali kumuita Mzee.
  • Ni mwenye mapenzi kwasababu kinawekwa wazi katika tamthilia na mke wake Kunihira wakati alipo toka shoti akaacha karamu akaenda naye hostitalini. Pia anampenda mtot wake Ben kwa kumuimbia nyimbo za kumbembeleza baada ya mamake kufanya talaka(uk 47)

KUNIHIRA: Mhusika huyuni mhusika mkuu na ana sifa zifuatazo kulingana na jinsi anavyochorwa katika tamthilia.

  • Ni mke wake kwatampola kwani hata tunaona katika tamthilia anamuita Bi-Shogora mcheja wake tena ndiye anayechorwa kama mke wake kwata katika mchezo. (uk 49)
  • Ni mhusika mkuu kwani tunamuona anajitokeza aghalabu katika vitendo vyote.
  • Ni mamake Ben kwani tunamuona katika tamthilia anamuacha mtoto Ben na kufanya talaka. (uk 25)
  • Ni mjasiri kwani tunamuona katika tamthilia anajiunga mkono na wafanya kazi wa kiume na kuwapikia au kuwahudumia kama mpishi. (uk 32)
  • Ni mvumilivu kwani tunamuona anavumilia maisha yao ya kimaskini na mume wake Kwata hadi walipobadilika kuwa watajiri.(uk 27)
  • Ni mtiifu kwani anamtii mume wake Kwatampola kwa kuitika wito wa kupikia na kuishi na vibarua.
  • Ni mwenye mapenzi kwani kinawekwa wazi katika tamthilia ya kwamba alivumilia umaskini wao pamoja mumewake Kwatampola, hakuna mapenzi yanayozidi uvumilivu huo. (uk 27)
  • Ni mfanya kazi kwani tunamuona anahudumia vibarua kwa kuwafanyia kazi ya kuwapikia huko Nyamitanga. (uk 32)

BUMAALI: Mhusika huyu ana sifa zifuatazo kulingana na jinsi anavyochorwa katika tamthilia ya chema chajiuza;

  • Ni mume kwani alimuoa Bi-Akello na Bi-Machu hasa katika sherehe za kumuoa mke wa pili (uk 113)
  • Ni kabaila au mtajiri mkubwa sana kwani ana nyumba nyingi mjini Mbarara na tena alipompa Kwata milioni 30 ni ishara ya utajiri. (uk 13)
  • Ni mume wao Bi-Machu na Bi-Akello kwani anawatambua wakati wa sherehe za kumuoa Machu mke wake wa pili huko Nyamitanga. (uk 113)
  • Ni mwenye mapenzi kwani tunaona katika tamthilia anamjengea jumba Machu na anakiweka wazi pale ambapo tumemuona anamsimulia Kwata kuhusu kidosho chake alichopata huko Rwebikona, huo ni upendo wa kiwango kikubwa kubwa. (uk 116)

BI-AKELLO: Mhusika huyu ana sifa zifuatazo kulingana na jinsi anavyochorwa katika tamthilia ya chema chajiuza;

  • Ni mkewe wa kwanza wa Bwana Bumaali kwani kinaoneshwa katika tamthilia katika sherehe za kumuoa mke wa pili Bi-Machu. (uk 113)
  • Ni mvumilivu kwa kuvumilia maisha ya kuolewa kwa mke wa pili kwani si rahisi hata hakipatikani  mtu kuvumilia kama yeye hasa katika kizazi cha leo.(uk 112)
  • Ni mtiifu kwani anamtii mume wake Bumaali kwa kukubali yote aliyomwambia.
  • Ni mwenye moyo wa kupa kwani tunamuona anakubali kumpa zawadi kwatampola kwa kazi aliyoifanya.(uk 105)

BI-MACHU: Mhusika huyu ana sifa zifuatazo kulingana na jinsi anavyochorwa katika tamthilia ya chema chajiuza;

  • Ni mtoto wa Daudi kwani tunawaona Kwata na mke wake wanasema kwamba, kunihira atakuwa mcheja kwake kwani wana uhusiano yao na Daudi.(uk 29.)
  • Ni mwenye mapenzi kwani alikubali harusi juu ya mapenzi.(uk 113, 116)

NABAGANZI: Mhusika huyu ana sifa zifuatazo kulingana na jinsi anavyochorwa katika tamthilia ya chema chajiuza;

  • Ni mke wake Injinia Bakehena kwani tunawaona kwao baada ya kufutwa kazini wanazungumuzia jinsi ya kutafuta kazi (uk 81)
  • Ni mjasiri kwani anajiunga na wajenzi huko Nyamitanga kwenye uwanja wa wajenzi na kufanya kazi ya ufagizi bila kuogopa. (uk 90)
  • Ni mwenye mapenzi kwani tunamuona anakubali kuishi na mume wake Bakehena hata baada ya kufutwa kazini.(uk 81)
  • Ni mvumilivu kwasababu ukweli unaonekana pale alipoamua kufanya kazi ya ufagizi huko kwenye uwanja wa ujenzi Nyamitanga. (uk 90)
  • Ni mfanya kazi kwani tunamuona anaacha familia yake na kwenda huko Nyamitanga kwenye uwanja wa ujenzi na kufanya kazi ya ufagizi bila kuaibika kama mwanamke aliyekuwa mtajiri muda mchache nyuma. (uk 90)

BAHEMUKA:Mhusika huyu ana sifa zifuatazo kulingana na jinsi anavyochorwa tamthiliani chema chajiuza;

  • Ni mume kwani ni mume wake Bi-Shogora kwani tunawaona wote wanakaribishwa nyumbani kwa kwatampola. (uk 23)
  • Ni babake kwatampola kwani tunamuona Bahemuka alipokuwa anaelekea kakoba anazungumuza na mke wake kwamba walimzaa mtoto maskini mwadilifu na mwema na atazikwa na wengi. (uk 21)
  • Ni mwenye mapenzi. Je kwatampola alitoka wapi? Ni juu ya mapenzi kati ya Bahemuka na Bi-Shogora. Pia, anampenda mtoto wake Kwata ndipo akamtembelea (uk 23)

BI-SHOGORA: Mhusika huyu ana ssifa zifuatazo kulingana na jinsi anavyochorwa katika tamthilia ya chema chajiuza;

  • Ni mke wake mzee Bahemuka.
  • Ni mzazi kwani ndiye mamake Kwatampola kulingana na tamthilia.(uk 23)
  • Ni mwenye mapenzi kwani isipokuwa mapenzi asingemtembelea mtoto wake Kwatampola kumuona huko Kakoba, huo ni upendo wa mama kwa mtoto. (uk 23)
  • Ni mtiifu kwani anamtii na kumheshimu mume wake Bahemuka.

BAKEHENA: Mhusika huyu ana sifa zifuatazo kulingana na jinsi alivyochorwa katika tamthilia ya chema chajiuza;

  • Ni mwizi kwani tunamuona katika tamthilia aliiba pesa za kabaila Bumaali mwajiri wake na kufutwa kazini. (uk 13)
  • Ni mwenye mapenzi kwani anampenda mke wake Nabaganzi. (uk 81)
  • Ni mfanya kazi kwani tunamuona ni injinia mjenzi wa nyumba. (uk 13)
  • Ni mvumilivu kwani anavumilia maisha ya umaskini hata bila kujiua baada ya kufutwa kazini.
  • Ni mume kwani ni mume wake Nabaganzi.(uk 13, 81)

MAUDHUI KATIKA TAMTHILIA YA CHEMA CHAJIUZA:

Maudhui ni jumla ya mambo, mawazo, mafunzo, maoni na ujumbe unaowasilishwa na mwandishi wa kazi ya kifasihi.

Hivyo basi, Johnpaul (2019) kwa maoni yangu nasema maudhui ni ujumbe, mawazona mafunzo yanayopatikana katika kazi yeyote ya kifasihi na jinsi msanii anavyosisimua hisia kuhusu kazi hiyohiyo.

Katika tamthilia ya chema chajiuza, mwandishi Innocent Agume alishughulikia maudhui kadhaa, na baadhi ya hayo ni kama vile;

  • MAPENZI: Mapenzi ni hali ya mvuto na upendo alionao mtu kwa mtu mwingine. Katika tamhilia hii ya chema chajiuza upendo huonekana kati ya Kwatampola na mkewe Kunihira (uk 27), Mzee Bahemuka na Bi-Shogora (23), Bakehena na Nabaganzi (uk 81), Bumaali na wake wake wawili yaani Bi-Machu na Bi-Akello (uk 116) (uk…)
  • UJASIRI: Hii ni hali ya kutokuwa na uoga aukutoogopa kitu chochote kwamfano, katika tamthilia hii ya chema chajiuza ujasiri unaoneka pale Nabaganzi na Kunihira walipojivunia na kufanya kazi na wajenzi wanaume bila uoga. (uk 32, 90)
  • UTUMISHI: Ni hali ya kufanyishwa kazi kwa malipo au kutolipwa. Katika tamthilia hii, Kwatampola anasema kwa kumjibu Bumaali ‘’ taja mtumishi wako yuko tayari kutimiza wajibu’’ (uk 12), Bakehena, Nabaganzi, Kunihira na wajenzi wengine ni watumishi. r
  • UZAZI: Hii ni hali ya kuzaa. Kwamfano katika tamthilia hii ya chema chajiuza mwandishi Innocent anatuonyesha kwamba Kwatampola na Kunihira walimzaa Ben (uk 47), Bahemuka na Bi-Shogora walimzaa Kwatampola (uk 21), lubengula alimzaa Bumaali nk rejelea(uk 12)
  • NDOA: Ni mafanikio rasmi baina ya mwanamume na mwanamke ili waweze kuishi pamoja kama mke ne mume. Katika tamthilia hii ya chema chajiuza, ndoa inapatikana kati ya Bwana Kwatampola na Kunihira, Bumaali na wake wake wawili (uk 116, 113), Bakehena na Nabaganzi nakadhalika.
  • WIZI: Ni tendo la kuchukua kitu kisicho chako bila ruhusa la mwenyewe. Kwamfano mwandishi anatuonyesha kwamba mitaimbwa, rangi na mabati yaliibwa huko katika uwanja wa ujenzi(uk 102) Pia, injinia Bakehena alimuiba Bumaali mwajiri wake na kisha akafutwa kazini. (uk 13) rejelea tena (uk 55)
  • MABADILIKO: Ni hali ya kugeuka kwa mambo. Katika tamthilia hii, mwandishi Innocent anatuonyesha wahusika wengi ambao maisha yao yalibadilika kama vile Kwata kutoka umaskini kuwa mtajiri (uk 115), Bakehena alibadilika toka utajiri kuwa maskini alipofutwa kazini (uk 81).
  • UTAJIRI: Ni hali ya kuwa na mali au fedha nyingi sana. Kwamfano tamthilia hii ya chema chajiuza inatuonyesha kwamba kabaila Bumaali ni mtajiri kwakuwa anamiliki nyumba nyingi na pia anampa kwata milioni thelathini za kununua vifaa vya kujenga ugo na kulipa vibarua (uk 13) Kwatampola ni mtajiri baada ya kupewa jumba la Nyamitanga (uk  115)
  • Kinyume cha utajiri, pia kuna maudhui yaUMASKINI katika tamthilia hii ya chema chajiuza: Umaskini ni hali ya kutokuwa na hela au mali. Kwamfano tunaonyesha wahusika wengi ambao ni maskini kama vile Kwatampola alikuwa maskini kabla ya kuzawadiwa na jumba kwani tunaona alikuwa analala katika kiota kama ndege (uk27), Bakehena badaaye aligeuka kuwa maskini hadi kufika kiwango cha kutafuta kazi huko Fortportal (uk 13), Nabaganzi hadi kufika kufanya kazi ya ufagizi (uk 90), Kunihira anasema Ben ameenda kwa jirani kuona Runinga na huo huonesha umaskini. nk.
  • NDOTO: Ni maono yanayotokea usingizini. Kwamfano katika tamthilia ya chema chajiuza, tunamuona Kwatampola aliota kuwa mtajiri halafu akawa (uk 02)
  • UTIIFU: Ni tabia ya adabu au nidhamu, hali tendo au uwezo wa kufuata amri au kutii. Kwamfano Kunihira anamtii mume wake Kwatampola, Kwatampola anamtii Bumaali kwani tunamuona anampa hata kutomuita jina bali humuita ‘’Mzee’’
  • UVUMILIVU: Ni hali ya kuvumilia maisha magumu. Kwamfano katika tamthilia ya chema chajiuza , mwandishi Innocent anachora Nabaganzi kama mvumilivu kwakuwa anavumilia hali ya umaskini na kfanya kazi ya ufagizi baada ya mume wake kufutwa kazini (uk 13), kwatampola na mkewe wanavumilia maisha ya umaskini (uk 27) nk
  • ELIMU: Ni mafunzo yanayotolewa na jamii kwa watu ama darasani au pasipokuwa darasani. Kwamfano tunamuona Injinia wa tatu ni msomi (uk…), Ben anasoma(uk 09)nk
  • UTENGANO: Ni hali au tendo la kuachana na kukaa mbalimbali na kitu kingine  bila kushirikiana. Kwamfano katika tamthilia ya chema chajiuza, tunaona utengano kati ya Kwatampola na Mke wake Kunihira alipofanya talaka, Machu anatengana na familia yake na kuolewa kwa Bumaali (uk 47, 113)
  • NYIMBO: Ni sauti zilizopangwa kimziki. kwamfano katika tamthilia ya chema chajiuza, mwandishi Agume Innocent anatuonyesha mziki unadundwa na mc.Bob King katika sherehe ya harusi ya kumuoa Bi-Machu (uk 111).
  • UTAMADUNI: Hii nimila, asili, jadi na desturi zinazofutwa na kundi la jamii Fulani. Kwamfano tunamuona Bumaali anasema ‘’kulingana na mila na desturi zetu, Kwatampola hatalajiwi kuwa katika kalamu hii’’ (uk 113). Hii ni kwasababu katika tamthilia mwandishi anatuonyesha kwamba Kwata ni ami yake Machu.

MBINU ZA KIFANI, LUGHA NA SANAA KATIKA TAMTHILIA YA CHEMA CHAJIUZA.

Mbinu au fani na uteuzi wa maneno na kuwekwa katika kazi za kifasihi ili kuifanya lugha iwe ya kuvutia na kupendeza.

Mwandishi wa tamthilia hii ya chema chajiuza Innocent Agume ametumia mbinu kadhaa kuvutisha na kupendesha kazi yake, na baadhi ya mninu hizo ni kama;

  • METHALI: Ni misemo ya hekima yenye maana iliyofumbwa. Kwamfano Katika tamthilia hii, tunaona methali kama haraka haraka haina Baraka (uk 02), kila mbwa na siku yake (uk 13), hakuna siri ya watu wawili (uk 17), dawa ya moto ni moto (uk 49), akufanyia kwa dhiki ndiye rafiki (uk 43), mtenda mema hulipwa mema (uk 105).
  • SEMI NA NAHAU: Ni fungu la maneno yanayotumika kutoa maana nyingiine badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha maneno makali au kupamba lugha. Mwandishi katika tamthilia hii hutuonyesha semi kam vile vuta nikuvut (uk 21), siku ayami (uk 21), cha mtema kuni (uk 58), kata kauli (uk 14) nk.
  • MASWALI YA BALAGHA: Haya ni maswali au masimulizi yasiyohitaji majibu. Kwamfano katika tamthilia hii ya chema chajiuza mwandishi anatuonyesha maswali kama vile ‘’una nini ambacho ulininunulia nikisahau?’’ (uk 85), ‘’wamejigamba kama wewe, wakajuta badaaye?’’ (uk85), ‘’jina lako sasa halina soko?’’ (uk 87) nk..
  • TAKRIRI: Hii ni mbinu ya kurudirudia neno au fungu la maneno ili kusisitiza ujumbe ulani. Kwamfano katika tamthilia ya chema chajiuza tunaona urudiaji wa maneno kama vile, leo ni leo (uk 14), Kwata anasema ‘’kwa hizo hizo nitafanya kazi yako’’ (uk 14), wasiwasi (uk 13), nyumba ni nyumba bora imesimama (uk 30), dhiki ni dhiki hata iwe ndogo (uk 43), Ben Analia kwi kwi kwi, ‘’mama usiniache mama usiniache’’ (uk 47).
  • TASHIBIHI: Hii ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha kama vile, kama, mithili ya, sawa na, nk. Na katika tamthilia tunaona mbinu ya tashibihi inajitokeza pale kwamfano ‘’tufe kama mtakatifu Stefano aliyekubali kifo cha kosa ambalo hakulifanya’’ (uk 4), na leo pia nimekuita  kwa kazi ngumu kama mawe (uk 12), amejenga nyumba kubwa kama dunia ya wamasaba wa Bugisu (uk 13), mjinga kama baba yako (uk 45), wanamziki ni kama mbwa (uk 108).
  • KUCHANGANYA NDIMI: Hii ni hali ya kutumia maneno yasiyo ya Kiswaahili katika lugha ya Kiswahili. Kwa mfano, katika Tamthilia hii ya chema chajiuza, kuna maneno kama radio west (uk 99) na posho (uk 99). Pia kuna Balya hardware (UK 14) na ok one two three (UK 108). Mbarara Regional Referal pia inatajwa (uk 116).
  • UTOHOZI: Hii ni mbinu ya kuwasilisha maneno ya lugha nyingine yatamkwe katika Kiswahili. Kwamfno mwandishi anatumia maneno kama hospitalini (uk 115), dereva (uk 116), korasi, sinema nk
  • CHUKU: Hii ni kutilia chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani. Kwamfano katika tamthilia hii ya chema chajiuza, mwandishi anatuonyesha chuku kama Bumaali alipomwambia Kwata ‘’nakuamini kushinda ninavyojiamini’’ (uk 13), shogora anasema ‘’maji yamepita kiwango cha baridi, sijabakiza hata jino moja’’ (uk 24)
  • MAJAZI: Hii ni mbinu ambayo mtunzi wa kazi ya fasihi hutumia kufananisha tabia za wahusika na majina yao halisi. Kwamfano katika tamthilia mwandishi alitumia majina kama ‘’Bakehena’’ maana ya kwamba mjifanyia mabaya. Tena kabaila Bumaalai kwakuwa alikuwa mjajiri sana. Kwatampola kwa maana ya kutenda mambo yake kiupole bila kuruka ruka.
  • TASWIRA: Hii ni mbinu inayomfanya msomaji kupiga picha ubongoni. Kwamfano (uk 115) kwatampola tunamuona anapewa zawadi la jumba.
  • UZUNGUMZAJI NAFSI: Hii ni mbinu inayomhusu mhusika anapojizungmzia au kwa kuongea au kuwaza bila kukusudia kusikika na yeyote. Kwamfano tunamuona Kwatampola katika tamthilia anazungmza mwenyewe baada ya kupewa pesa za kujenga ugo (uk 14).
  • HOTUBA: Hii ni mbinu inayotoa mazungmuzo yanayohusu jambo maalumu, kwamfano tunamuona Bi-Akello anatoa hotuba (uk 113), hotuba ya Bumaali (uk 112).
  • KISENGERE NYUMA: Hii ni mbinu ya Sanaa ambayo mwandishi hutumia kusimulia mambo yaliyotokea huko nyuma, kwamfano Bumaali anamuelezea kwata jinsi babake lubengula alivyopenda mchezo huo wa kuoa wengi (uk 12).
  • TAHARUKI: Hii ni mbinu inayoibuka baada ya msomaji kusoma na kubaki na hamu ya kuendelea kusoma. Kwamfno kunihira anapotoka shoti na wakamhudumia pale alipoanguka na kumpeleka hospitalini (uk 115), taharuki inawabakia watu wakijiuliza je, alipofika huko hospitalini palitokea nini? Nk
  • MAZUNGUMZO: Ni majadiliano kati ya watu wawili au Zaidi kuhusu jambo Fulani, kwamfano kuanzia ukurasa wa kwanza hadi ya mwisho ni mazungmzo kwani kuna maogezi kila onyesho.
  • TASHIHISI: Hii ni mbinu ya kupatia kitu kisicho na uhai kuwa na sifa za kiumbe mwenye uhai. Kwamfano Injinia wa kwanza anasema ‘’mawingu yanapiga makofi kwa furaha zako’’ (uk 102) Pia, Bakehena anasema ‘’jina lako litaanza kusafiri mawinguni kama ndege’’ (uk 75).
  • NYIMBO: Ni mbinu ya kutumia nyimbo katika kazi ya kifasihi kufikisha ujumbe kwa hadhira, kwamfano kuna nyimbo katika sherehe za harusi unaoogozwa na Mc-Bob King Mfawidhi (uk 111, 110).

Hivyo basi, ninahitimisha kwa kusema kwamba, ni kweli mwandishi Innocent Agume jicho lake liliangalia ndani ya uga wa fasihi na kuelezea ukweli uliopo katika kizazi cha leo ambacho kimejaa na unafiki kwa wale wanaojidai kuwa ni waadilifu kumbe ni vinyonga vinavyojigeuza rangi na kusaliti wenzao hasa katika uwanjani tunapofanyia kazi, kwamifano Bakehena.

Tena kwakuwa anaelezea kuhusu wema anapotumia mhusika Kwatampola, shukrani kwake kwakuwa hata katika kizazi cha leo wema upo nakwahivyo wale wenye uadilifu ndio wanaoajirika na kufaulu katika maisha ya leo.

Vilevile, napenda kusema kwamba, kwa kweli CHEMA CHAJIUZA na KIBAYA CHAJITEMBEZA.

Hvyo basi nahitimisha kwa kutoa methali katika lugha ya kinyankore inayosemwa kwamba ‘’Nyakwehena akeenyampira naarya’’ yenye maana kwamba mtenda mabaya anajiharibu mwenyewe nikirejelea jinsi Innocent anavyomchora mhusika Bakehena na namna anavyoishia na maisha yake.

Tena wanawake ambao mmepata wanaume wa aina hiyo kama Bakehena, ushauri wangu ni kwamba muwashauri wawe waadilifu na waaminifu ili kujiokoa na matatizo kama haya. 

Kazi hii inaelezea kwa muhtasari Vipengele muhimu yaani ploti/muundo, wahusika, maudhui pamoja na mbinu za kifani na kisanaa vinavyojitokeza katika tamthilia ya chema chajiuza iliyoandikwa na Innocent Agume.

Bila shaka, kazi hii itawafaa walimu na wanafunzi wa somo la Kiswahili katika shule za sekondari, vyuo vya walimu na vyuo vikuu ambao wamekuwa wakipata changamoto ya kuvisoma vitabu vizima, chema Chajiuza kimeisha chambuliwa.

Vilevile, kazi hii itawanufaisha na kuwafurahisha wapenzi wa lugha ya Kiswahili kwa kupata marejelo halisi katika tamthilia yenyewe.

Kwa mantiki hiyo, kazi hii itatoa mchango mkubwa katika harakati za kusoma na kuchambua kazi nyingine za kifasihi.

Hivyo basi, mwandishi wa kitabu hiki Mh.Innocent Agume anafaa zawadi kama ile iliyopewa na Kwatampola kwa kuandika kazi nzuri na inayorejelea mazingira halisi ya kizazi cha leo.

Kazi hii imetengenezwa namwalimu Johnpaul Arigumaho mpenzi halisi wa fasihi na lugha ya Kiswahili.

                                      arigumaho810@gmail.com.

0778514179..

Kila la kheri.

kazi hii bado ni mbegu. ni mwongozo tu sicho kitabu halisi.

11 thoughts on “MWONGOZO WA TAMTHILIA YA CHEMA CHAJIUZA-Innocent Agume.

Leave a reply to Mwalimu Arigumaho Johnpaul Cancel reply