MWONGOZO WA MAUDHUI KATIKA TUNGO ZA MUYAKA BIN-HAJI.

 Utangulizi.

Muyaka bin Haji ni kiumbe wa kihistoria na msanii mkongwe katika historia ya usanii, miongoni mwa wasanii wa kabla ya karne ya ishirini. Muyaka alizaliwa mjini Mvita katika ukoo wa Myinyi Malindi, miongoni mwa koo kumi na mbili za Waswahili, na aliishi kati ya 1776-1840.

Kitabaka,Muyaka alikuwa mtu wa wastani. Katika uhai wake, Muyaka alikuwa na mwigiliano na watu wa jamii yake katika kila tabaka.. Alikuwa mcheshi na mpenda zaha , na alifanya utafiti na wengi miongoni mwa watawala wa Mombasa – Mbari ya Mazrui, na hata watu wa tabaka lake.

Muyaka alikuwa mfanyabiashara mashuhuri, ingawaje hakufanikiwa sana katika biashara yake..

Kazi hii ya biashara ilimpeleka katika sehemu mbalimbali za  za ulimwengu wa biashara kama vile Bara Hindi, Uarabuni, Bukini, Ngazija, Pembe na Unguja. Nyingi ya tungo zake zinasimulia maisha haya.

 Kazi nyingi za Muyaka hasa zilijitenga na masuala ya kidini moja kwa moja, maudhui ambayo yalikuwa yameutawala uwanja wa tungo za nyakati hizo, na kushughulikia maswala mbalimbali ya maisha ya jamii kwa ujumla. Hata hivyo, swala la dini hakulipiga teke, bali alifunua hapa na pale katika usanii wake.

Wasanii wengi wa ushairi wa kabla ya karne ya Ishirini walijikita katika maudhui ya kidini, na wote walifuata mtindo mmoja wa kuandika ushairi wao, hasa katika utangulizi ambapo ilikuwa ni kama miongoni mwa kunga za ushairi kuwa ni lazima msanii aanze kazi yake ya kwa kumtaja Mola na kutoa shukurani kwake, na baadaye amtaje Mtume Mohamed na kumsalia, pamoja na maswahaba wake.

Kinyume na haya yote, ushairi wa Muyaka haukufuata mtindo huo wa kidini aidha

katika utangulizi wala mwili wake. Kwa kiasi kikubwa Muyaka alifaulu kuutoa ushairi nje ya maudhui ya kidini na kuanza Kutalii katika masuala ya kilimwengu , walimwengu na ulimwengu wao.

 Muyaka anatumia mashairi yake kuisawiri na kutupa picha halisi ya jamii yake.

Haya yote yanajitokeza wazi katika dhamira ya mashairi yake na yote anayoyazungumzia kuhusu jamii yake husika. Tungo za Muyaka zinajitokeza kama kio halisi cha jamii yake kwakuwa zinagusia  na kuzungumzia masuala mengi yanayoikumba na kuikabili jamii yake.

UHUSIANO WA MAISHA YA BINADAMU NA TUNGO ZA MUYAKA.

  1.  MAPENZI NA NDOA

Mapenzi na maisha ya ndoa ni mambo ambayo Muyaka ameyapa uzito sana katika kazi yake. Hili ni dhihirisho kamili la maisha ya waswahili na binadamu kwa ujumla kwamba mtu hawezi kuishi pweke kama kisiwa. Katika mashairi yake Muyaka amelijadili suala la mapenzi kwa uzito huku akitia chuku katika umuhimu wa kuwa na mpenzi na mwisho kuishia katika ndoa kwa manufaa ya mtu binafsi na kwa jamii pia.  Mfano wa tungo zake anazozungumzia mapenzi ni kama vile,

“Siupati Usingizi” (Uk. 200), anasema:

Risala wangu basiri, leo napenda kutuma,

Enenda ndiwa huuri, Mwenye cheo na heshima,

Fika ukamuhubiri, haya takayokutuma,

Namuapia karima, siupati usingizi.

Wisapo mpa salamu, ndiwa asio mfano,

Mwema wa kutakalamu, fasihi yakwe maneno,

Ni mwema wa tabasamu, mchache wa matukano,

Hasa himuwaza neno, siupati usingizi.

Wisapo mkurubia ndiwa, mwema wa mangani,

Enda kwa kunyeyekea, upomoke maguuni,

Kisa umweleze pia, yangu yaliyo mwoyoni,

Mato yangu hayaoni, kwa kukosa usingizi.

Tungo zake nyingine zinazozungumzia mapenzi ni kama vile”Mahaba” (uk. 184)), “Kitambi changu” (uk. 174), “Kwamba Wajua Mapenzi” (uk.2-4), “Tusiambiane Uongo”(uk. 221), “Kuonana na wewe” (uk. 238), “Hilo Langu Ndilo Lako”  (uk. 254), “Siuwati mtondoo” (uk. 272) “Harusi ya Bwana Muyaka” (uk. 278), “Utavaa Nguo Gani” (uk. 280),

“Mahaba nusu Wakiya” (uk. 304), “Madanganyo ni Maovu” (uk. 304) na “Musiwate Kuonana” (uk. 314) miongoni mwa mengine.

Katika tungo hizi, Muyaka anaelezea mbinu za kumbembeleza msichana na kumnasa katika mapenzi. Anayafafanua mapenzi kwa undani na kuleza ni sifa zipi zinazofaa kujitokeza baina ya wapendanao ndipo mapenzi ya kweli yawepo. Anataja sifa za binti mzuri ambaye anastahili kuwa mrembo lakini mwenye heshima, asie na matukano na myenyekevu.

 Katika shairi lake la “Siupati Usingizi” (uk. 200) anamusifu mpenzi wake kuwa ni mwema wa tabasamu na hana matukano na ni mrembo wa kulinganishwa na njiwa. Muyaka anamuomba aliyemtuma afikapo kwa yule binti kabla ya kumpa risala ambembeleze binti yule kwa kunyenyekea na kupomoka miguuni.

Haya yalikusudiwa kumchora binti yule kama mtu wa maana na kumuonyesha jinsi mapenzi yake yanahitajika na jinsi anavyopendwa.

Muyaka aliisawiri jamii ya Waswahili kama iliyojaa mahaba na yenye kuwaheshimu wanawake.

Muyaka anasisitiza suala la uzuri wa kuoa na sifa za wakuolewa anaposema:

Oa, kwamba u muozi, uzoeleo kuowa

Oa, mato maolezi, na mboni ukikodowa

Oa, Maji maundazi, meupe kama maziwa

Oa, sizi ndizi ndowa, asokuoa ni yupi?

  • UKOSEFU WA UAMINIFU

Mara kadhaa,Muyaka alionekana akiulaani ukosefu wa uaminifu katika maisha ya ndoa na mapenzi. Haya ni baadhi ya mambo yanayovunja uhusiano mwema baina ya wachumba au hata mke na mume.

Katika shairi lake la “Kwamba hutaki Nambia” (uk. 322), anamuomba mkewe

ajitoe kimasomaso juu ya fikra na matamanio yake juu ya Muyaka badala ya kupigana chenga.

Katika “Anamkejeli Mtu” (uk. 310) anazungumza juu ya ujanja aliofanya bwana mwengine mpaka akamzini bibi ya mtu mwengine. Anasema:

Nipaziwe nipaziwe, khabari zako mwandani,

Nambiwe hivi nambiwe, simba kulala shakani,

Kunyakua kama mwewe, nyamangwa kumla ndani,

Firigisi na maini, ndivyo apendavyo simba.

Hii ni ishara tosha kwamba katika jamii yake Muyaka palikuwepo na changamoto ya ukosefu wa uaminifu baina ya wanandoa na uzinifu baina ya wanajamii.

Muyaka anaelezea jinsi ukosefu wa uaminifu na uzinifu unavyosababisha kuyumbayumba kwa ndoa na hata kuvunjika na jinsi ni dhambi kuzini na suala lililopingwa na dini ya Kiisilamu.

  •  ELIMU NA JAMII.

Wakati Muyaka, watu wa Mombasa walipenda sana watoto wao wasome hasa wakati huo wakifunzwa kusoma na kuandika ili waweze kupata maarifa. Kulikuwepo na shule za kufunza kusoma na kukariri Koran pamoja na mafunzo kuhusu kazi nyingine za dini ya Kiisilamu kama vile aina tofauti tofauti za Maulidi.

Zaidi ya hayo mafunzo yaliendelezwa katika vyuo vilivyopatikana katika miskiti na mafunzo yakitolewa na Wanachuoni ama waliokuwa na elimu ya masomo mbalimbali ya Kiisilamu.

Muyaka alifahamu kuwa jamii yoyote ile ilihitaji elimu na maarifa ili kufaulu.

Wakati mwengine, Muyaka alizungumzia mambo fulani fulani tofauti ya maisha kwa kunasihi, kufundisha au hata kuonya. Wakati mwingine pia alizifuata hisia za watu na kuzichemsha bongo zao katika maswali ya jamii yaliyo na ukinzani mkuu, kama vile katika “Kasa ni Halali?” (uk.312):

Nna tembe masiala, mno yamenikikisa,

Zamani nilipolala, wavyele waliniusa,

Huzundukana akila, mato yakipesa-pesa,

Wakauza, “Huyu K’asa, ni halali, haramu?”

Kwani sikupata jibu, kwa kuchelea makosa,

Vifunueni vitabu, nyote wasomi darasa!

Munipe njema jwabu, mpatela kufuasa,

Munambie “Huyu K’asa, ni halali, ni haramu!”

Muyaka alitumia tungo kama hizi kwa dhamira ya kuwafanya kuwachochea wanajamii na wasomi  wafikirie ili wapata maarifa na kuelimika maana kila jamii huhitaji watu wenye elimu ili ifanikiwe.

  •   UTABAKA.

Katika nyakati za Muyaka, Waarabu walikuwa na ufanisi mkubwa sana mjini Mombasa lakini ufanisi wao pamoja na utawala wa Wamazrui haukudumu milele.

Kwa hivyo waliokuwa juu baadaye waliporomoka na hatimaye wakayaonja maisha ya ulitima. Ingawaje kwa kawaida baada ya kupanda marafiki huwakimbilia na kuwakata urafiki lakini wao walioporomoka urafiki hukoma, lakini Muyaka hakufanya hivyo bali aliwafariji na kuwa nao karibu sana kama walivyokuwa pamoja wakati wa ufanisi wao. Mpomoko wa ufanisi wa Mombasa anauzumgumzia katika shairi

lake la la “Ulimwengu” (uk.153):

Ai, ulimwengu jivu, ujileo vumbivumbi,

Walifile waangavu,wali na wao ujimbi,

Vianga havia mbivu, viwili vya urofumbi,

Wale walimbika kambi, leo ndio walimbikwa.

Ndiyo hali ya dunia, huleta vyema na vimbi,

Ambaye yamtatia, maninga yakwe hufumba,

Usingizihupotea, kwa mawazo tumbitumbi,

Walo walimbika kambi, leo ndio walimbikwa.

Muyaka alieleza jinsi watu katika jamii huwa katika matabaka tofauti lakini si ajabu kumuona aliyekuwa katika tabaka la juu la wenye mali na fedha ameshushwa hadhi hadi tabaka la chini la masikini.  Jamii huwa na mabadiliko kila wakati na kuna  kipindi ambapo waliokuwa maskini hupanda ngazi na kuwa wenye mali nyingi na wale waliokuwa na mali kushuka ngazi na kuwa masikini.

 Katiaka shairi lake la “Ukiwa Wako” (uk.209), Muyaka anatueleza kuhusu kijana

mmoja alieponda fedha zake hadi kuwa maskini.  Kijana huyo alirejea kwa mamaye na kudai fedha au ajidunge kwa kisu ila mamaye anamkataa na kumzomea kwa jinsi alivyozipunja fedha zake na mwishowe anamtimua Anasema:

Ndipo mamae kawaza, pamwe na kuzingatia,

Fedha zako umezizosa na leo zimekwishia

Kisu sikukutaza twaa upate jitia

Mbele zangu nondokea wende na ukiwa wako

  •  UZALENDO NA VITA

Tungo nyingi za Muyaka alizoandika wakati wa ukoloni wa Waarabu wa Omani laini ya Sayyid Said mjini Mombasa yalijikita sana katika uzalendo na vita hasa kutokana na hali halisi ilivyokuwa nyakati hizo. Katika enzi hizi, Mombasa ilikuwa kama uwanja wa vita, mara kwa mara wenyeji walijikuta katika harakati hizo za kivita. Muyaka anaonyesha jinsi wenyeji walivyopambana na kuzikata nyororo za ukoloni na dhuluma, au hata kupinga juhudi za kutawaliwa.

Katika shairi lake la , “Vikija Mtaviweza” (Abdulaziz 1979:133-134) anasema:

Kongowea haitui, hamtaki kuituza,

Mshishile uadui, kutaka kuipinduza,

Ndipo ikashika kawi, kutaka wafanikize,

Vikija mtaviweza, au mwatakia mabo?

Watani upeketefu, wa mambo kuyageuza,

Gongwa ni mji dhaifu, naona ni mwina wa Chiza,

Hutatia watifu, wasione muwangaza,

Vikija mtaviweza, au mwatakia mambo?

Muyaka anataja pia vifaa na zana walizotumia katika vita kama vile: mata, mafumo, ngao, p’anga, p’anga-kule, vitara, msu, ngurumza na fimbo. Pia anataeleza palikuwepo na ngoma na michezo mahususi ya kuwafunza vijanajinsi ya kutumia zana za vita vizuri na suala la vita kwa ujumla.

Kwa mfano, Muyaka anataja ngoma ya kizungup’ia, ambao ulikuwa ni mchezo wa vita uliohitaji matumizi ya nguvu uliochezewa katika fukwe za bahari.Mashairi mengine yalikuwa ya kuwatia ari wenyeji wa pwani kwa ujumla dhidi ya uvamizi na ukandamizaji wa Waarabu kama vile “Mjenga Nyumba Halali” (uk.124), “Kafa Li Man Hadhara” (uk.133), “Mwatupa Shauri

Gani?” (uk.136), “Mwima wa Chiza” (uk.143), “Kongowea Ja Mvumo” (uk.146).

Wakati mwingi palizuka mzozo na vita baina ya watala wa makabila ya Mombasa wenyewe na Muyaka aliyaelezea haya katika baadhi ya tungo zake na kusimulia jinsi watawala wawili wapiganiapo uongozi wananchi hushindwa ni yupi wa kufuata. Anasema:

Kwa vuma mwamba wa iwe, baharini watokota.

Ni mngumi na chongowe, wamo wawili wateta.

Hatuyui mmoyawe, tutakaye mfuata,

Zimewatatia t’ata, watatuzi tatuani.

  •  USALITI.

Jamii ilikumbwa sana na changamoto ya usaliti katika vita vya ukombozi wa Mombasa. Wakati mwingi, usaliti katika vita na juhudi za ukombozi ni jambo la kutarajiwa. Mara nyingi, Muyaka aliukashifu usaliti dhidi ya uzalendo na harakati za kujiokoa na maadui, kwa stihizai.

Katika tungo nyingine, Muyaka aliwakashifu vizalia wa Mombasa waliokwenda Zanzibar kumpongeza Sultan baada ya kushindwa kwa Mombasa na Zazinzibar katika vita.

 Anasema, “Vyema Mungelikulaje” (uk.152)

Mlio mkila nyemi, kwa furaha na urembo,

Mvuatile ulimi, wala hamsemi jambo

Na kauli hazatami, zilokuene na umbo

Viwi mwaramba vyombo, vyema mgelikulaje?

Wala hamchi kwambiwa, mmejikaza masombo

Hulaje visivyoliwa, mkiendea makombo?

Na maneno mkitowa, kama wanwaji wa tembo

Viwi mwaramba vyombo, vyema mgelikulaje?

Hula mkishindilia, ili kujaza matumbo

Shehena mkipakia, kama shehena ya chombo

Hamuoneli viwaya, mumuonela mwajimbo

Viwi mwaramba vyombo, vyema mgelikulaje?

  •  UTAMADUNI

Muyaka katika tungo zake  alizungumzia sana kuhusu suala la utamaduni na mila. Aliusifu utamaduni wa watu wa pwani na mila alizoziona zina umuhimu sana katika jamii. Alisisitiza suala la wanajamii kujikita katika utamaduni na mila na kuepuka kupotoka kutokana na mtagusano baina yao na watu wa jamii nyinginezo. Tamaduni na mila hizi ni kama zifuatavyo:

i. Chakula

Chakula kikuu cha watu walioishi Mombasa wakati huo kilikuwa ni mseto wa  mchele na mtama uliopikwa na nazi,kwa kitoweo cha samaki, nyama au mbonga. Pia, inaonekana pia katika wakati wa Muyaka, jamii yake pia ilitumia ngano, matundana samli kama chakula pia.

 Katika ubeti mmoja wa shairi lake anaeleza  jinsi ngano ilitumika kama “chakula mbadala” hasa na watu wa tabaka la juu.

Anasema:

Ai ngano na samli, viliwa vyema khiyari,

Vitu viawavyo mabali, Renu na Baunagari,

Apo mwende akali, Mola humjaza kheri,

Ai ziwa na sukari! Itakapokukutana.

Katika  shairi la “Panda” Uk. 190. Anasema:

Panda nganu na mpunga afudhali ya viliwa

Panda wimbi na kimanga vipawa vya kupewa

Panda usitunde ch’anga, tauwa mbivu tauwa

Panda ni wakouluwa, panda darajani, panda!`

ii. Mavazi

Katika baadhi ya tungo zake Muyaka anataja mavazi ya wanaume Waswahili kuwa Kanzu, vazi lenye mikono mirefu na linafika miguuni lililotengenezwa na malighafi tofauti lakini jeupe lilivaliwa sana. Chini ya kanzu  nguo iliyojulikana kama kitambi ama kikoi kilivaliwa. Baada ya kanzu vazi jingine lililojulikana kama Kizibao liliibuka ambalo haikuwa lazima liwe na mikono mirefu na lilikuwa angavu.

Kitambaa kilichofungwa kiunoni kilitumika sana ili kuzuia Kanzu kumsumbua alioivaa wakati akifanya kazi na pia kitambaa hicho kilitumika kushikia silaha kama vile visu, upanga, majambia  na pembe za unga wa bunduki.

 Muyaka anasema “jifungetoni

masombo” kuwaomba wakaze vikoi vyao. Nao wanawake wengi wa uswahilini walivalia leso ama visutu vilivyotengenezwa kwa pamba.

Wanaweka waliokuwa maskini walivalia kaniki na leso zilizotengenzwa kwa pamba hafufu na ya bei rahisi. Pia walivalia mikufu, shanga na vipuli mbali mbali.

 Katika shairi lake la “Si Wanawake wa Huja(uk.172). Anasema:

Ukiwaona kwa mbali, kwa vikuku na viganja

Wamba ni wake wa kweli ukienda wakidhi haja

Kanan ni batili swiswi na wao mamoja,

Si wanawake wa huja yalla ni yale mavao.

iii. Usafiri

Wakati wa Muyaka usafiri ulijikita sana katika matumizi ya barabara kwa kutumia wanyama kama vile punda na farasi kama inavyojitokeza katika shairi la “Mfuga Punda” (uk. 206).

 Piapalikuwepo ule usafiri wa baharini uliotumia mitumbi na mashua hasa kwa minajili ya usafiribaina ya visiwa vilivyokuwa karibu. Pia, wanabiashara waliotoka mbali  kama vile India naUarabuni walitumia meli katika usafiri wao.

Muyaka anaeleza jinsi alivyosafiri kwa mashuakatika safari zake.

 Anasema:

Simba ndume na wambuji, sikizanitatongoa,

Naketele vitongoji, na safari za mashua,

Leo nakumbuka mbiji, ya kutweka na kutua,

Ai, pato na pewa, litako kukutana.

Katika utungo wake wa “Kimbinji Changu”, (uk 168). Anasema:

Nastahabu kimbiji, kidau changu cha kwanza.

Kingwawa mlejileji, k’welea haikupanza,

Na kufa Ngozoa – Maji, yali usiku wa iza,

Ndipo leo hakiwaza haangama kazeeka.

Kiwizo changu kiwizo nilipo hikioleza

Chalikuwa cha matezo nami kikinipumbaza

Hatusa nacho Ufunzo mawimbi kutoa kweza,

Ndipo leo hakiwaza haangama kazeeka.

  •  DINI, MILA NA DESTURI.

Wakati wa Muyaka palikuwa na mila na itikadi nyingi hasa zilizotumika kama sheria za kuongoza jamii. Mfano ni kuwa mwanamke hakuruhusiwa kwenda pamoja na mumewe kwenye sherehe za kijamii na pia alihitajika kumvalia mumewe nguo mpya wala si kutoka nayo kwenda kuwaringia watu wa nje.

Mila na desturi hizi zilisisitizwa sana kwa kuwa zililinda mienendo na umoja wa jamii.

Yeyote yule aliyetenda kinyume na mila na desturi hizi alichukuliwa kama aliyepotoka na hata alihitaji adhabu kama vile kupewa talaka kwa mwanamke yeyote yule aliyepatika akizini nje ya ndoa.

Katika utungo wa “Kitambi Changu” (uk 174). Muyaka anasema:

Kitambi changu cha gomba, nilichokupa hidaya

Kumbe hivi hujipanmba ukenda kuzinginya

sikujua kana kwamba kuwa yatakuwa haya

hivi sasa nivulie nipe kitambi changu

Katika uk.176 anaendelea kusema:

Kwamba sina kazi nacho mama t’ampelekea:

ndicho kitu apendacho atakwenda jivalia

kwako nimefanya kicho siwezi kukuatia

sikuatik’ono moja! kitoe kitambi changu.

Kando na mila na desturi, dini ilichukua nafasi kubwa sana katika jamii ya wakati huo.

Dini ambayo ilikuwa imekita miziz wakati huo ilikuwa dini ya Kiisilamu. Sheria na kanuni za kiisilamu zilisisitizwa sana katika kuyangalia maadili ya wanajamii.

Dini ilitumika katika kuonya na kuelimisha wanajamii kuhusu kila suala la kila siku.

Katiaka “Mke wa Risasi” (uk. 300) anamlaani mtu mwengine aliyemhaba na kumtaka mapenzi mke wa marehemu Risasi aliyekuwa katika eda.

Kulingana na imani ya Waislamu, mjane akiwa katika eda hatakikani kuolewa wala kujiingiza katika shuguli za mapenzi, lakini bwana huyu, alivunja sheria na kumtaka mapenzi mjane wa Risasi.

  •  MAGONJWA NA KIFO

Muyaka anazungumzia pia magonjwa yaliyoikumba jamii yake na dhiki inayo ambatanishwa na magonjwa hayo. Anaeleza jinsi mtu apatwapo na ugonjwa  matokeo hayatabiriki. Yanaweza kuwa raha au huzuni, kulingana na hali itakavyokuwa , ikiwa ndwele imeshindwa nguvu na afya au kinyume chake. Abdulaziz, (1979: 156, tanbihi ya 4) anasema:

Ai, mpewa na pato lipalo mtu kukuwa,

Angawa mwana mtoto wa kutishika kachewa,

Akiwa na upasito wa kutamani ukiwa,

Ai, ndwele na afuwa, itakapo kukutana

Pana tungo amabazo Muyaka aliziandika akiwa mgonjwa sana. Katika utungo wa “Aha” (uk.188). Anasema:

Aha! Sengambile, Aha! Ndwele yaniuma.

Aha! N’ambe, sina siha, muwili wangu mzima.

Aha! Kutoona raha, ndipo aha! nikasema.

Aha! Sambile kwa wema, nasema, kwa ndwele sii

Katika shairi la “K’ongowea yaugua” (uk.202).

K’ongowea yaugua kwa kite na uguzi,

Kwa mambo kuyaugeua, kugeua mageuza,

Rabi, Ngwaipa afua! Na kuiafu si kazi,

Kutanani wamaiza shauri jema mtende.

Muyaka anazungumzia pia suala la kifo na kulielezea kama jambo lisiloepukika na mwili wa mfu huwezi ukalindwa kutokana na funza. Katika shairi lake la “Kifo Kikimbizwa Funza”

(uk.172), anasema:

Kifo kikimbizwa funza chawekwa mahali gani

Sikifakie kifunza, ukakitia shimoni,

Ndanini kujiumiza, kujitia mashakani?

Wapeni mabaniani, mahali wafakiweka.

  1.  UCHUMI.

Uchumi wa Mombasa katika nusu ya karne ya kumi na tisa ulikuwa umeimarika sana na kupanuka. Baadhi ya vitega uchumi alivyovitajaMuyaka katika tungo zake ni kama vifuatavyo:

i. Kilimo

Kilimo ni mojawapo wa vitega uchumi viliyvokuwa muhimu sana katika uchumi wa Mombasa wakati huo na familia zote zilizojiweza kifedha zilikuwa na mashamba katika sehemu za bara zilizozunguka kisiwa cha Mombasa. Mashamba haya yalikuwa chanzo cha mapato kwa familia zilizomiliki mashamba haya.

 Walikuza mpunga, mahindi, wimbi, mihogo, nazi, machungwa, maembe, ndizi na mboga za aina tofauti tofauti.

Katika  tungo za Muyaka, anataja vyakula walivyopanda wakulima wa Mombasa wakati huo.

Katika utungo wake wa “Panda” (Uk.190). Anasema:

Panda nganu na mpunga, afudhali ya viliwa

Panda wimbi na kimanga, vipawa vya kupewa

Panda usitunde ch’anga, tauwa mbivu tauwa

Panda ni wakouluwa, panda darajani, panda!`

ii. Uvuvi

Uvuvi ulikuwa miongoni mwa vitega uchumi vikubwa na maarufu  na hulka ya Waswahili .

Samaki walikuwa rahisi kupatikana na kwa wingi na samaki  walitumika sana kama chakula.

iii. Ufugaji

Wanyama kama vile  ng’ombe, mbuzi, kondoo, kanga pia walifugwa ili kuwapa maziwa na nyama. Waswahili ila hawakuweza kufikisha kiwango walichohitaji kwa matumizi yao ya kila siku na waliagizia ziada kutoka bara. Pia wanyama kama vile punda na farasi walifugwa kwa minajili ya usafiri.

Katika utungo wake Muyaka “Mufuga Punda” (uk. 206), anasema:

Mfuga hufuga ng’ombe, k’ashika bubu k”akama

Na samli lembe-lembe k’iwa na haja k’atuma

Na nyama riade nitube niwe katika hishima

Mfuga-p’unda-kilema hukujambia mashuzi

Mfuga hufuga mbuzi myama mwenye madhihala

Ukawacha yako kazi na wala pasiwe na ila

Ukaenda katika zizi kumchinja na kumla

Mfuga-p’unda, madhila hukujambia mashuzi

iv. Utengenezaji wa mashua.

Lazima palikuwepo na maeneo ambapo palitengenezwa mashua lakini si viwanda vikubwa kama vile vilivyopatikana karibu na  Lamu. Vyombo vya baharini vilivyotengenezwa katika eneo hili vilikuwa vidogo vilivyotumika katika uvuvi na usafiri baina ya visiwa vilivyokuwa karibu.

v. Ufinyanzi.

Ufinyanzi uliendelezwa sana na watu wa kabila la Wajomvu na Muyaka anawarejelea kama

“Wafinyanga Vyungu”

vi. Uhunzi.

Wahunzi wakijulikana sana kama wafua-vyuma walikuwepo na walijihusisha na utengenezaji wa majembe, mashoka, visu, misumeno, pete na kulabu. Wafua-fedha  walitengeneza vitu kama vile mikufu kama vile shanga. Wabanyanas kutoka India.

vii. Mafundi wa ngozi.

Wapo waliojihusisha na utengenezaji ngozi ili kutengeneza ndala, ngao, mishipi na majalada ya vitabu.

viii. Ushonaji.

Jukumu hili liliachiwa wanawake walioshona  mavazi kama vile kofia, jokho na aina fulani ya k’anzu na mashati.

Palikuwepo pia na utengenezaji wa vikapu, makuti ua kuezeka paa, kamba, majamvia na nyavu za kushikia samaki. Katika utungo wake Muyaka, anasema : “Ukukuu wa kamaba si upya wa

ukambaa” (uk. 260)

  1.  BIASHARA.

Biashara ilikuwa moja wapo wa shughuli iliyokuwa muhimu zaidi baina ya Mombasa na watu wa bara. Misafara ya wafanyabiashara ilitoka Mombasa kwenda magharibi kupitia Taita, Maasai na kwenda mbali zaidi hadi kiwango cha kufika katika fukwe za ziwa la Victoria.

Kaskazini magharibi, wafanyabiashara hao walisafiri hadi kufika maeneo ya ziwa Baringo. Wafanyabiashara hao walinufaika na pembe za ndovu na faru, chumvi, mikeka, kamba na mifugo wakibadilishana na bidhaa zao kama vile shaba, shanga, chuma na nguo.

Mombasa ilikuwa na uhusiano wa moja kwa moja wa kibiashara baina ya Mombasa na India na biashara hii ilihusisha ubadilishanaji wa nguo na nafaka kutoka India na Pembe za ndovu pamoja na watumwa kutoka Afrika Mashariki.

Muyaka anaisuta india katika shairi lake anapokejeli kuwa ingawa India ndiko kunakotengenezwa nguo kunao wengi wanaotembea uchi.

Muyaka anasema “Hindi ndiko kwenye nguo na wendao uchi wako” (uk.160).

HITIMISHO.

Kutokana na kuwa Muyaka aliishi na kuweza kuingiliana na watu wa matabaka mbali mbali, maisha ya jamii kwa ujumla ndiyo maswala makuu yanayojitokeza katika tungo zake. Kama tulivyoona, mashairi ya Muyaka yanatumika kama chombo cha kusawiri na kuchora  jinsi jamii yake ilivyo kwa kuzingatia maswala mbali mbali ya jamii husika.

Maswala haya ni kama vile uhusiano wa watu mbali mbali, siasa, uchumi, yanajitokeza sana katika mengi ya mashairi yake.

Maswala haya yanamuwezesha Muyaka kuihusisha hadhira kikamilifu kwani yalikuwa ni mambo ya maisha yao ya kila siku.

Kupitia tungo zake Muyaka tunaweza kuelezea jamii yake ilivyokuwa kwa kuegememea katika jinsi anavyoisawiri jamii husika.

3 thoughts on “MWONGOZO WA MAUDHUI KATIKA TUNGO ZA MUYAKA BIN-HAJI.

Leave a comment