Neno “utendi” linatokana na kitenzi “kutenda” maanake huwa ni kutenda jambo Fulani.
Chaligha (2013), anaeleza kuwa, kumetumika fomula, kuelezea maana ya Utendi kuwa ni E = M + Ms yaani (Epic= Mars + Music/muse), yaani Utendi ni mungu, Muziki na Vita (U=M+V). Akifafanuwa maelezo hayo, Chaligha (kashatajwa), anasema Utendi ni tukio la kimuziki linalozungumzia vita na miungu.
Mawazo hayo yana mashaka, kwa upande wa Utendi/Utenzi wa Kiswahili. Uswahilini, Utendi na Utenzi, tofauti ni matamshi. Tendi Uswahilini si lazima zizungumzie miungu kama aonavyo Chaligha. Uswahilini kote, neno “miungu” ni kufuru.
Chaligha (ameshatajwa), alieleza kuwa, tendi simulizi ni tungo simulizi zenye mtindo wa kifomula, zinazohusu mambo ya ajabu, ya watu wasio wa kawaida. Masimulizi hayo yanasimuliwa kwa njia ya mdomo. Utendi/Utenzi wa Kiswahili hughaniwa katika miktadha mingi kama vile, sherehe na msiba.
Mulokozi (1999), anaeleza kuwa, Utendi ni utungo mrefu wa kishairi wenye kusimulia hadithi ya ushujaa na mashujaa. Kwa jumla, Mulokozi anaona kuwa, Utendi lazima uwe na mhusika shujaa. Mawazo hayo, hayana ukweli wa moja kwa moja kuhusiana na Utendi wa Kiswahili.
Wamitila (2010), anaelezea kuwa, Utendi ni aina ya Utenzi ambao, unazungumzia maisha na matendo ya ushujaa au ya mashujaa wa jamii fulani. Tendi ni simulizi, ambazo husimuliwa na mtunzi na ambazo huchukuwa mkondo unaofanana katika kazi za kishairi. Mawazo ya Wamitila yametoa mwelekeo tofauti na wa Mulokozi (ameshatajwa), juu ya dhana ya Utendi. Utendi/Utenzi na Nathari au Tutumbi hukutana kwenye maudhui lakini si kwenye fani, kila utanzu una mitindo, miundo, kanuni, ada na taratibu zake. Uswahilini, hakuna Utendi ama Utenzi wa kinathari au kitutumbi.
Utendi/Utenzi ni bahari kuu na kongwe ya Ushairi wa Kiswahili. Kusilazimishwe swala na mbuzi- mmoja na wapili ni wa majumbani.
Mawazo ya Wamitila (2010), yana upungufu. Kuna vielezea vya Utendi, havikuhusishwa katika ufafanuzi wake. Vielezea hivyo ni sifa za pekee za fani za Utendi wa Kiswahili, kama vile; muundo wa beti, bahari ndogo ya kila ubeti, vina na mizani pamoja na urefu wa Utendi huo..
Baada ya kutalii mawazo ya wanataalimu waliotangulia, dhana ya Utendi imeweza kuelezeka kwa kupambanuliwa kwa sifa ya Utendi/Utenzi ambao hufuata kaida ya urari wa vina na mizani na huweza kuwa na mhusika shujaa au asiyekuwa shujaa.
Mhusika huyo mkuu, huitwa nguli. Vile vile, tendi, huelezea masuala yanayoihusu jamii, kama vile, masuala ya kijamii, ya kisiasa, ya kiuchumi na ya kiutamaduni.
Masimulizi hayo, hutolewa kwa lugha ya kishairi, ambayo ujumi wa lugha hiyo, hutegemea jamii inayohusika na masimulizi yenyewe yanayotolewa huwa kwa ajili ya jamii, ili kuwa katika mwenendo bora wa maisha ya hapa Duniani na Akhera.
Utendi ni aina ya ushairi na tanzu moja wapo wa fasihi simulizi ambao husimulia Maisha na matendo ya mhusika shujaa au wa visasili.
Utenzi ni ni utungo mrefu wa kishairi unaoelezea juu ya mambo Fulani na maranyingi huwa na pande moja yaani huwa na vina vya kati tu. Utenzi haufuati urari wa mizani.
Katika Kiswahili, kuna tenzi kuu maarufu kama vile utenzi wa tambuka(Bwana mwengu karne ya 18), utenzi wa mwanakupona(mwanakupona karne ya 19), utenzi wa inkshafi(Abdallah bin ally), utenzi wa hayati sokoine(kazi ya Charles mloka karne ya 20), utenzi wa hati na adili(shaban robert), utendi wa Fumoliyongo (muhamad kijumwa 1913)
Utangulizi wa utendi wa Fumoliyongo.
Utendi wa fumoliyongo unamhusu shujaa liyongo. Baadhi ya wataalamu (mbele 1986:138-140) hudai kuwa jina lake lilikuwa “liyongo fumo” sio Fumoliyongo yaani Fumo alikuwa ni babake. Wengine wataalamu wakiwemo (knappert 1983:144)”fumo” ilikuwa tu wadhifa wake sawa na mfalme. Bado kuna utata na mjadala mkubwa kuhusu tarehe ya liyongo, na wengine wanadai kuwa yaweza kuwa kiumbe tu hadithini ambaye hajapata kuishi.
Hata hivyo, kuenea kwa hadithi yake na umashuhuri wake katika mapokezo na matendo ya kiimla ya waswahili yanaashiria kuwa huenda mtu huyo aliishi kweli hata kama habari zake za kuishi zimetiwa chumvi na waenezaji.
Baadhi ya wataalamu (Nabhany 1987, Mbele 1986) wanasema liyongo aliishi karne ya 9 masihiya (miaka ya kikristo)
Wengine wakiwemo Chiraghdin (1973) naKnappert (1983:167) wanasema liyongo aliishi baina ya miaka ya 1160-1204 lakini tarehe inayoelekeya kukubaliwa ni ile ya karne ya 13-14. Hii ni kwasababu kitabu cha Tarekhe ya Pate(Freeman Greenvile 1962:241-299) kinamtaja mtawala wa jimbo la Ozi aitwaye Fumoliyongo aliyeishi kati ya utawala wa Fumomari.
Fumoliyongo alikuwa shujaa wa kitaifa aliyeishi eneo la mto wa Tana kaskazini mwa Mombasa. Babake alikuwa kiongozi wa mji wa shaka.
Babake liyongo alikuwa na watoto wawili yaani Liyongo mwenyewe na kakake Daudi mringwari.
Fumoliyongo alikuwa kiongozi mkuu kaskazini mwa pwani ya Afrika mashariki hapo karne ya 9-13. Anajulikana kama shujaa, kijudu, na mshairi wa mashairi ya jadi, hadithi na nyimbo za waswahili na hasa zilizohusu mila, harusi na densi za gungu. Miji kadhaa pwani huko Tanzania inadai kuwa ndiko alizaliwa. Baadhi ya nyimbo, mashairi na hadithi zake huzungmzia sherehe za harusi za kale, vita, na densi za gungu kama vile wimbo wa “sifu uta wangu (song of the worrier)”. Pengine liyongo anatambulika kama mjuzi wa upiga pinde.
Hadithi za kale za liyongo nyingi zilibeba sifa lingani na zile za ulaya kv Achilles, Sigurd, na Robinhood. Tena aliandika gungu nyngi kama “Sifa la Uta” au “Wimbo wa Mapenzi”
Fumo Liyongo wakati mwingine alikuwa askari na mwandishi wa mashairi katika pwani ya kaskazini ya Afrika Mashariki kati ya karne ya 9 na karne ya 13.
Fumoliyongo alikuwa kijana mwenye kusifiwa mjini kote, mrefu, mwenye matendo ya kishujaa, nguvu zisizo za kawaida aliyeishi ungwana na mashaha eneo la shaka jimbo la ozi.
Kama alivyoeleza Sigurd, liyongo alikufa kutokana na usaliti. Liyongo alisalitiwa na mtoto wake aliyetoboa siri ya nguvu za babake. Liyongo aliweza tu kufa akidundwa sindano ya shaba kitovuni. Hiyo ilikuwa siri kati ya liyongo na mamake aliyejulikana kwa jina “Mbwasho”.lakini liyongo alipoifunua kwa mtotoke, akaangamizwa na damu yake yenyewe.
Inasemekana kwamba, baada ya kifo chake, mwenye nguvu zake Liyongo alizikwa mji wa shaka jimbo la Ozi.
Kuhusu mwandishi wa utendi wa fumoliyongo;
Katika mwaka wa 1913, mwandishi wa mashairi Muhamad bin Omar Al-Bakry aliyejulikana sana kwa jina la Muhamadi Kijumwa aliandika juu utendi maarufu uitwao utendi wa Fumo Liyongo, utendi ambao ulikuwa ukielezea maisha ya Fumo Liyongo, aliyekuwa mshairi na pia mtawala katika eneo la Pate. Kijumwa kama yeye siye mwandishi bali alipata hadithi hiyo kutokana na simulizi za waswahili wa mwambao wa Kenya. Kijumwa hakuiandika hadithi bali alisimulia upya kwa njia ya utendi.
Muhamad kijumwa aliishi 1855-1940 alikuwa mwenyeji wa lamu nchini Kenya. Alikuwa msanii mashuhuri ambaye mbali na kutunga mashairi na tendi, vilevile alikuwa mjomi (mchongaji wa milango yenye nakshi), msanii-msanifu, msawidi (copyist) na mnukuzi wa miswada ya zamani.Habari za maisha yake hazijulikani bali anaanza kujitokeza kwenye miaka ya 1890 ambapo alikuwa anawasaidia watafiti wa kizungu kv Alice werner (1900-1935), William Hichens (miaka ya 1930).
Inasemekana kuwa, muhamad kijumwa alifariki mwanzoni mwa mwaka wa 1940 japo tarehe kamilii haitambuliki wazi mtoto wake Elesha aliishi Lamu. Kijumwa alitunga masahiri mengi yakiwemo utendi wa helewa.
Muhtasari wa utendi wa Fumoliyongo;
Utendi wa Fumo Liyongo unahusu mgogoro kati ya Fumo Liyongo na kaka yake, sultan wa Pate ambaye hajatajwa kwa jina. Mwanzoni utenzi unamdokeza Liyongo akiwa ana umri wa makamo hivi, aidha kimo na nguvu zake za mwili ziliwashangaza wengi kwa hivyo walimsifia mno.
Watu wa kabila la Wagalla walipofika Pate kutafuta chakula ili wanunue, walielezwa sifa za Liyongo na wananchi, halikadhalika Sultani wa Pate alimsifu Liyongo. Kwa kusikia sifa hizo za ajabu, Wagalla walitamani sana kumwona Liyongo, kwa hivyo wakamwandikia Liyongo warakawakimwomba aje ili wamwone.(beti 18,19)
Liyongo akaitikia wito huo, hivyo akapanga safari yake ya kwenda Pate huku amebeba mizigo chungu nzima.(beti 37,38)Kati ya vitu alivyovibeba ni panda, kinu na mawe. Kwa mwanadamu wakawaida, safari hiyo ni ya siku nne lakini Liyongo alichukua siku mbili tu na kufika Pate.
Alipokaribia jijini Pate, alipuliza panda ya kwanza hadi ikapasuka.Alipuliza ya pili nayo vile vile ikapasuka. Alipuliza ya tatu na kuingia mjini hadi barazani kwa sultani.(beti27,30, 31) Watu walishangaa mno kwa sauti kubwa ya panda. Watu wengi wakakusanyika kumwona, alipotua mzigo wake umejaa vitu vingi ambavyo vilitosha kuijaza nyumba nzima. Moja kwa moja, Wagalla wakakiri kuwa kweli Liyongo ni mtu mnene na mwenye nguvu. Wagalla wakatamani sana kuipata mbegu yake, hivyo walimwomba sultani awaruhusu kupata mbegu hiyo, kiongozi huyo akakubali.
Wakafanya mpango wa kumwoza mke wa Kigalla ambaye alimzalia mtoto wa kiume. Sifa za Liyongo zilivyozidi kusambaa ndivyo mgogoro kati yake na Sultan wa Pate ulivyozidi.
Mfalme alihofia kuwa huenda Liyongo angemnyang’anya ufalme hivyo akatafuta njia ya kumwangamiza.
Liyongo alipogundua njama ya Sultan ya kutaka kumwangamiza, akatoroka Pate na kwenda kuishi nyikani pamoja na Wadahalo, Watwa, Wasanye na Waboni.
Mfalme akafanya mpango wa kisiri pamoja na Wasanye na Wadahalo ili wamuue huko mwituni kwa kuwahidi malipo ya reale mia moja iwapo wangemletea kichwa cha Liyongo. Watu hao walifanya urafiki na Liyongo kisha wakashauri wawe wakicheza kikoa
pamoja. Hivyo wliachaguana kwa kupeana zamu ya kuangua makoma kutoka mtini. Walipanga kuwa ikifika zamu ya Liyongo, wamngojee apande mkomani kisha wamfume kwa mishale yao wamuue akiwa mtini.
Kwa uwezo wa kiakili aliokuwa nao Liyongo, akagundua njama hiyo. Badala ya kupanda mtini aliangua makoma akiwa chini aridhini hivyo wakashindwa kumuua.Watu hao walimpelekea Sultani ripoti kuwa haiwezekani kumuua Liyongo.
Mfalme aliwaambia warejee alipo Liyongo wamweleze kuwa mjini ni salama na hapana hatari yoyoyte ili waende naye huko. Waliporudi wakamweleza Liyongo uwongo huo ambao aliuamini kuwa kweli, kwahivyo akawafuata na kuenda nao mjini Pate.
Sultan akaandaa ngoma ya Gungu na mwao na kuwaalika wapenzi wa aina hiyo ya ngoma, Liyongo alikuwa mmoja wao. Ngoma iliposhika kasi, askari walimnasa Liyongo na kumtia korokoroni.
Mfalme na watu wake waliamua kumuua Liyongo akiwa gerezani.
Siku ya mauaji kutekelezwa zilipokaribia, Liyongo akapewa muda wakutoa ombi kwa kitu chochote apendacho. Liyongo akaomba apigigwe ngoma ya mwao naGungu.
Ombi hili likakubaliwa na ngoma ikaandaliwa. Ngoma ilipoandaliwa, Liyongo akatuma ujumbe wa kishairi kwa mama yake kupitia kwa kijakazi Saada ambaye humletea chakula.(beti 104, 105)
Katika ujumbe huo alieleza kwamba siku hiyo ya ngoma apike mkate wa wishwa na ndani yake atie tupa ya kukatia minyororo. Mama yake akafanya vivyo hivyo.
Kijakazi Saada alipompelekea chakula, walinzi wakachukua mikate waliyodhania kuwa mizuri na kuutupilia mbali ule wa wishwa ili umwendee Liyongo. Ngoma iliposhika kasi, Liyongo akatumia nafasi hiyo kukereza minyororo, hivyo akafaulu kuikata. Akavunja Lango kuu la jela na kutorokea msituni.
Mfalme alipoona kuwa ameshindwa kumuua Liyongo, akamshawishi mwanawe Liyongo aende amuulize babake kiwezacho kumdhuru.
Sultani alimpa ahadi ya kumwoza bintiye, kumpa uwaziri katika uongozi wake na mali nyingine ikiwa angefanikiwa.
Mwanawe Liyongo akafululiza hadi Shaka alipokuwa babake na kumtaka amweleze siri ya yeye kutodhurika na kitu chochote.
Ingawa Liyongo alitambua njama ya mahasidi wake ya kupitia kwa mwanawe, alikubali kumfichulia siri.
Alimweleza kuwa kiwezacho kumuua ni sindano ya shaba ikitiwa kitovuni mwake. Sultan alijawa na furaha sana, alipopewa taarifa hii na kijana huyu wa Liyongo.
Kwa hivyo akampatia sindano ya shaba, akampa ahadi zaidi na kumpa zawadi tele.
Akarejea Shaka tena alipo babake, akamngoja alipokuwa usingizini, akamchoma sindano ya shabakitovuni. Liyongo alizinduka na kuamka kwa hasira, akachukua mshale wake na kuelekea kisimani akimtafuta adui.
Akiwa amepiga goti, akatia mshale katika upinde huku akiuelekeza mjini na kukata roho. Umati wa watu walipomwona akiwa katika hali hiyo, wakadhani yuko hai na kaudhika mno. Kwa hivyo walijawa na hofu ya kwenda kuchota maji kisimani.
Walipozidiwa na ukosefu wa maji, walikwenda kumwomba mama yake Liyongo aje ambembeleze aondoke wateke maji. Mama yake akawa anaenda kumpembeleza mara kwa mara lakini alikosa kufanikiwa.
Hatimaye maiti yake iliaanguka ndipo watu wakabaini kuwa alikuwa ameshakufa.
Sultani alipopata habari ya kifo cha Liyongo alijawa na furaha. Akamwarifu mwanawe Liyongo kuwa babake amefariki. Badala ya kuwa na maskitiko, huzuni na maombolezo, yeye alifurahi.
Kitendo hiki kinamuudhi mfalme ambaye alichukua mali yote aliyokuwa amempa. Wanajamii wakamfukuza kijana huyu asitangamane nao. Siku chache baadaye akakumbana na maradhi yasiyokuwa na tiba ambayo yalimwangamiza.
Sifa za Fumo Liyongo;
Mwandishi Kijumwa (1973), amemsawiri mhusika Fumo Liyongo kishujaa katika utendi wenyewe. Kwa upande wangu nachukua mtazamo huo huo wa kishujaa alioutoa mwandishi ili kubaini sifa zake.
Kwa mujibu wa Wamitila (2003), neno shujaa hutumika kueleza mhusika mkuu katika kazi ya kifasihi ambaye anaweza kuwa wa kike au wa kiume.
Kimsingi neno hili haliashiri wema tu. Kwa upande wake, Mulokozi (1996), anasema kuwa mashujaa wa utendi ni wa aina tatu: Mashujaa wa kijadi wa kiafrika kwa mfano, Fumo Liyongo katika Utendi wa Fumo
Liyongo, mashujaa wa kidini kwa mfano, Mtume Muhammed na masahaba wake katika Utendi wa Ras‘lghuli na mashujaa wa kubuni kwa mfano Tajiri mbaya katika Utendi wa Masahibu.
Mtunzi anamtaja Fumo Liyongo kama jitu nene, lenye kimo kinachozidi cha mtu wa kawaida.
Kimo cha Fumo Liyongo kimeelezwa kwa kina, huku mtunzi akidhamiria kuweka wazi uwezo wa nguvu alizo nazo na umbo lake la kipekee. Alijulikana mno kwa unene wake kiasi cha kuwashangaza watu wengi. Watu walitoka mbali kuja kumtazama, kwani Vimo vyao vilimfikia magotini: (beti za 6 na 16).
- Liyongo kitaka,mali
akabalighi rijali
akawa mtu wa kweli
na haiba kaongeya.
- Wagalla wakipulika
kwa dhihaka wakateka
wakanena “twamtaka”
na sisi kumwangaliya. Mtunzi anaeleza alivyosafiri safari ya mbali kwa siku chache mno, hali ambayo ni tofauti na ya mwanadamu wa kawaida. Kwa mfano, aliwahi kutembea kutoka Shaka hadi jijini Pate, safari ya siku nne lakini yeye akachukua siku mbili tu. Liyongo ni mwenye vipaji kadhaa: Anawashinda maadui katika kulenga shabaha anapotumia upinde na mishale kuchuma mikoma bila kukwea mkomani.
Juu ya yote alikuwa muungwana sana na mfano wa kuigwa na watu. Talanta inayojikeza hata zaidi ni, ufundi wa kutunga nyimbo na mashairi yaliyojulikana kama Gungu. Kwa mfano, akiwa kizuizini, aliitumia talanta hii kumtumia mamake ujumbe wa kishairi huku akiomba tupa ambayo aliitumia kukata minyororo ili kujiweka huru: (beti za 104 na 108).
- kama sada nakutuma
Enda kamwambie mama
Afanye mkate mwema
Kati tupa aitiya.
- zilizo kikaza kusi
alikikata upesi
hata zikikoma basi
inukani kawambiya.
Liyongo alikuwa hodari katika vita, aliwashinda maadui wake wote hata Wagala walishindwa vita na Liyongo. Vimo vyao vilimfikia magotini hali hivyo ikawawia vigumu kumshinda vitani.
Pia katika nguvu za kiakili, Liyongo alitumia akili kukataa kupanda mkomani ili aangue makoma(ubeti wa 65).
- Akawambia ngojani
akatowa mkobani
chembe katiya ngweni
makoma kiwanguliya.
Alikuwa na nguvu za kimwili yaani ubabe na mabavu, kama inavyodhihirika katika (beti za 40, 41, 46).
Pia, Liyongo likuwa na nguvu za kiakili na kivita. Liyongo alikuwa na uwezo wa kiakili, kuvumbua mambo mbalimbali na nguvu za kivita alikuwa nazo.Vilevile sifa ya uganga na sihiri, Liyongo ana sifa ya uganga. Hivyo alisema hawezi kudhurika kwa njia ya kawaida inayomdhuru mwanadamu yeyote. Kile ambacho kingemdhuru yeye ilikuwa siri ambayo aliifichua kwa mwanawe. Yaani nikwa kudungwa sindano ya shaba kitovuni: (ubeti wa 143)
Liyongo ana mshikamano na kundi au makundi ya watu. Aliishi porini na Watwa na kushirikiana nao. Ushirikiano wake ndio unaomnusuru na njama za mfalme za kutaka kmuua. Liyongo anapokufa watu wengi waliompenda wanaomboleza kwa masikitiko makubwa: (ubeti wa 224).
Vilevile kulikuwa na ushirikiano wa kifamilia kati ya Liyongo na mamake, ushirikiano huu unamsaidia kutoroka gerezani baada ya mamake kumpelekea mkate wa wishwa uliotiwa tupa ndaniye: (beti za 107, 110)
Nakwahivyo, utendi wa fumoliyongo unafunza hasa wanaume kuwa washujaa na wababe, rijali (ub 13), kukiimu mahitaji ya jamii na familia (ub 25), kuwa masihiri ( ub 143) na masuala hayo yana msingi ya kiume katika jamii ukizingatia nadharia ya ubabedume inayojikita katika kutambua na kuchunguza nafasi na majukumu ya mwanamume katika jamii ya waswahili.
Mambo kuhusu utamaduni katika utendi wa fumoliyongo;
Utamaduni ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake. Hivyo inajumlisha imani, ujuzi, sanaa, maadili, sheria, mila na desturi, ambavyo mtu anapokea kutoka jamii anamoishi.
Kama sifa maalumu ya binadamu inayomtofautisha na wanyama wengine, utamaduni ni suala la muhimu katika anthropolojia ukihusishwa na yale yote kama vile lugha inayowaunganisha watu wanaohusika, fasihi, mafungamano, ndoa, michezo, ibada, sayansi na tekinolojia (ustaarabu).
Utamaduni pia ni mkusanyiko wa maarifa, itikadi, na tabia za wanadamu ambazo hutegemea sana uwezo wa kuwasilisha mawazo na mafunzo ya kijamii kwa njia ya ishara.
Utamaduni ni jumla ya tabia za watu pamoja na akili, imani, sanaa, sheria, mila, dsturi, na tabia za watu wa waishio katika jamii moja.
Nakwahivyo, Utamaduni ni jumla ya mitazamo , kaida, malengo na maadili yanayotambulisha asasi, shirika, au kundi fulani la watu.
Ukilinganisha fasili hizo, utagundua kuwa utamaduni huwa ni tabia na mienendo ya watu wa jamii fulani.
Mambo kuhusu utamaduni katika utendi wa fumoliyongo yatagusia vipengele kama imani, mila, desturi, ndoa, lugha, michezo na burudani yapatikanayo katika utenzi huo huo. Yafuatayo ni baadhi ya mambo hayo;
Utendi wa fumoliyongo umeegemea utamaduni wa imaani ya dini ya uislamu. Utendi wa Fumo Liyongo, unatumia mianzo maalumu na kumalizia kwa miisho maalumu yenye dalili za dini ya kiislamu. Utendi huo umeanza kwa duwa na kumalizia kwa duwa. Duwa hiyo, anaombwa Mwenyezi Mungu Mmoja, ambaye ndiye Mwenye uwezo wa kila kitu. Aidha, katika duwa hizo, ametajwa Mtume Muhammad (S .A .W), ambaye ndiye Mtume wa mwanzo na wa mwisho katika ulimwengu huu. Kwa mfano, ubeti wa kwanza, kuna duwa:
Bismillahi nabutadi
Kwa ina la Muhammadi
Nandikie auladi
Nyuma watakaokuya
Kutokana na ubeti huo wa kwanza, Utendi wa Fumo Liyongo, mtunzi anaanza jina tukufu la Bismilahi, kisha, anamtaja Mtume Muhmmad (S.A.W). Hii ni desturi ya waumini wa Dini ya Kiislamu, ambapo, kila jambo, hulianza kwa mtajo wa Allah (S.W), yaani Bismi Llahi Rahmani Rahimi.
Vile vile, katika Utendi wa Fumo Liyongo, mtunzi anamalizia kwa kumuomba Mwenyezi Mungu (S.W), katika ubeti wa 228 na wa 229, ili akirimiwe, na AIlah (Mwenyezi Mungu). Mfano;
- Tumeziya kukhitimu
Hapo ndio wasalamu
Ilahi tatukirimu
Kwa Baraka na afiya
- Rabbi tatusahiliya
Na uzito wa duniya
Tena tatujaaliya
Kuwa njema yote niya
Katika mifano hiyo hapo juu, mtunzi anamuomba Mwenyezi Mungu, Amuepushie uzito wa dunia. Pia, anamuomba Mola, Aifanye vyema niya yake. Mwenyezi Mungu, Ameoneshwa kuwa, ndiye Mwenye uwezo wa kila jambo kwa mja wake. Mifano hiyo inadhihirisha utamaduni wa imani ya dini ya uislamu katika utendi wa fumoliyongo.
Kuna utamaduni wa serikali ya utawala wa kifalme katika utendi wa fumoliyongo.
Inasemekana kuwa babake liyongo alikuwa mfalme wa pate na alipofarika, kakake liyongo ajulikanaye kama Daudi mrinngwari ndiye alilithi uongozi wa babake. Sultwani alikuwa mtawala wa Pate. Mwanzo alikuwa na mapenzi na Fumo Liyongo.
Hata hivyo, mwisho alijenga uwaduwi mkubwa juu ya Fumo Liyongo. Mtawala huyo, ndiye aliyefanya kila hila, ili amwangamize Liyongo;
- Mfalume kipulika
Liyongo ametoweka
Nde mui meanguka
Haya aliazimia.
Mfalme huyo alikuwa ni muuwaji.
- Fitina zikamngiya
Mfalume miya miya
Kwa hila kakusudiya
Kumuuwa fahamiya.
Beti hizo zinathibitisha serikali ya utawala wa ufalme katika utendi wa fumoliyongo.
Utamaduni unazingatia mfumo wa kuumeni.Tamaduni za waswahili zinamtaja Mwanamume kama Mkimu Jamii katika utenzi wa fumoliyongo. Hili linadhihirika na tukio la kikoa na makoma, Fumo Liyongo anapata usawiri wa kuwa mkimu jamii. Anajiunga na wanaume wenzake kukidhi hitaji la jamii la chakula. Wanashirikiana kutungua makoma kwa zamu.
Katika beti zifuatazo tunafahamishwa namna walivyounda kikoa ili kuhakikisha jukumu lao la kukidhia jamii linatekelezwa kwa utaratibu:
- Siku moya wakanena
natuleni waungwana
kikowa ni tamu sana
karamu ‘sotindikiya
- Likisa shauri lao
wakenenda kwa kikao
mkoma waupatao
hupanda mtu mmoya
Doyle (1985:107) anadokeza kuwa mwanamume anapaswa kukimu familia kikamilifu kulingana na matakwa na matarajio ya jamii ya kiasili. Wanakikoa walitaka kutumia tukio la kuunda kikoa kwa nia mbaya ya kupata nafasi ya kumdhulumu Liyongo kwa kunuia kumwangamiza. Imebainika wazi kwamba, Liyongo ametimiza matakwa na matarajio ya jamii kuwa mkimu wa jamii akiwa mwanamume. Kwa hivyo, katika jamii ya kitamaduni ambayo huzingatia mfumo wa kuumeni, Liyongo ana hadhi na haki ya kudai nafasi yake kama mwanamume, hususan katika jamii ya Waswahili kwa sababu ametekeleza wajibu wake wa kukidhi jamii kama mwanamume. Asingepata tunuku la hadhi ya mwanamume pasipo kutimiza jukumu hili.
Utendi wa fumoliyongo umetumia lugha ya kiamu. Utendi huo umetumia lugha ya asili, kutokana na uasili wa kisa cha Fumo Liyongo.
Aidha, wanajamii, hiyo ndiyo lugha yao, waliyokuwa wakiitumia, na bado inatumika hadi leo katika eneo hilo. Beti za 14 na 50 zinadhihirishia misamiati ya lugha ya Kipate kama ifuatavyo:
- Ghafula kikutokeya
Mkoyo hukupoteya
Tapo likakuwiliya
Ukatapa na kuliya
- Liyongo akatambuwa
Huzengea kuuwawa
Pale Pate kayepuwa
Barani akitembeya.
Beti hizo hapo juu, yaani ubeti wa 14 na 50, kuna matumizi ya maneno ya lugha ya Kiamu. Kwa mfano, katika ubeti wa 14, neno mkoya, lina maana ya mkojo, na neno “ukakuwilia,” lina maana ya “kutetemeka”. Aidha, katika ubeti wa 50, neno “kapepua” lina maana ya “akajiepusha”. (Mulokozi, 1999) anasema kutoka ubeti wa kwanza hadi 56 zimetumia lahaja ya kiamu.
Utendi wa Fumo Liyongo umetumia, kwa kiasi kikubwa, misamiati ya Kiswahili cha Kiamu kama beti
- kuwa liyongo mekwima
Uko nde ya kisima
Sasa watu wamekoma
Mai hawapati ndiya.
Utamaduni katika utendi wa fumoliyongo unaheshimu muda wa michezo na burudani. Hili linadhihirika tunapoona fumoliyongo anaomba achezewe densi za gungu kabla ya kuuawa. kwamfano katika ubeti wa 98.
98. Akajibu “usikhini”
Kamwambie sulutwani
Mwao nieutamani
Na gungu liwe pamoya.
- Liyongo nikwambiao
Shaha wa gungu na mwao
Tena ni mkuu wao
Huwashinda wut’e pia.
Beti hizi zinaonyesha aina za nyimbo na burudani kama kipengele kimoja cha utamaduni katika jamii yao.
Mambo kuhusu uislamu katika utendi wa Fumoliyongo;
Utafiti unaonesha kuwa, Utendi wa Fumo Liyongo umebeba mambo ya dini ya Kiislamu wakati Utendi huo unapoanza kwa mtunzi kuomba duwa kwa Mweyezi Mungu mmoja na kumaliza kwa duwa. Nabii Muhammad (S.A.W), pia anasifiwa katika utendi huo.
Dua inatangulia maandishi ya utenzi wa fumoliyongo (ub 01) pia huwa ni njia mojawapo ya kuimarisha imani ya Kiislamu.Aidha kwa mujibu wa Koran tukufu, dua ni kigezo muhimu sana katika kuimarisha imani ya waumini wa dini ya kiislamu:
Kwa mfano;(ub 01)
- Bismillahi nabutadi
Kwa ina la Muhammadi
Nandikie auladi
Nyuma watakaokuya
Kutokana na ubeti huo wa kwanza katika Utendi wa Fumo Liyongo, mtunzi anaanza kwa jina tukufu la Bismilahi, kisha, anamtaja Mtume Muhmmad (S.A.W). Hii ni desturi ya waumini wa Dini ya Kiislamu, ambapo, kila jambo, hulianza kwa mtajo wa Allah (S.W), yaani Bismi Llahi Rahmani Rahimi.
Vile vile, katika Utendi wa Fumo Liyongo, mtunzi anamalizia kwa kumuomba Mwenyezi Mungu (S.W), katika ubeti wa 228 na wa 229, ili akirimiwe, na AIlah (Mwenyezi Mungu). Mfano;
- Tumeziya kukhitimu
Hapo ndio wasalamu
Ilahi tatukirimu
Kwa Baraka na afiya
- Rabbi tatusahiliya
Na uzito wa duniya
Tena tatujaaliya
Kuwa njema yote niya
Katika mifano hiyo hapo juu, mtunzi anamuomba Mwenyezi Mungu, Amuepushe na uzito wa dunia. Pia, anamuomba Mola Aifanye vyema niya yake. Mwenyezi Mungu Ameoneshwa kuwa ndiye Mwenye uwezo wa kila jambo kwa mja wake.
Chittick na Murat (1994) vision of Islam, wanasema “Kuwa mwanadamu kamili ni kutekeleza matendo ya mungu alivyotenda.” Ni wazi kuwa maandishi yaliyomo, kwenye Koran yanatoa mwongozo wa maisha jinsi mwislamu alivyostahili kuishi. Aidha mandishi yanamtaja fumoliyongo kama kielelezo bora cha kuigwa hasa kwa waislamu.
Kuimarishwa kwa dini ya kiislamu; Matukio ya kushangaza katika Utendi wa fumoliyongo yamejengwa ili kuimarisha imani ya waumini wa Kiislamu.
Mwandishi anaonyesha adhabu mbalimbali ambazo watu wanapewa ilikulipia matendo yao maovu. Kwa mfano mtotowe liyongo alipomaliza kumsaliti babake na kumdunda shindano ya shaba, alifukuzwa mjini pate na mwishowe akakumbwa na madhabu yaliyomwangamiza. (ub 179
- Kamtiya kitovuni,
Naye ulele kwa t’ani
Achamka hamuoni
Kiyana amekimbiya. 216, 213
- mfalme kabaini
Kabisa huna imani
Epuka mwangu matoni
Na nyumbani nitokeya.
- mfalme kamtowa
Nguo zakwe kamvuwa
Na watu akatukiwa
Khabari ikaeneya.)
Hayo yote yanatokana matendo maovu.Tukio hili na mengine ni kama onyo kali kwa waislamu wasitende maovu ya aina hiyo.
Kwa hivyo imani ya dini yaoinaimarika.Waislamu wana imani kuwa wanadamu wote wanaotenda kinyume na matakwa ya Allah wataadhibiwa vikali:
Utetezi wa binadamu ni ishara ya matendo mazuri katika Koran na hadith. Fumoliyongo katumwa na nabii muhamed kama Mtume. Hili ni dhihirisho kuwa katika maisha ya sasa, Mungu huwateua watu wake ambao anawatwika kusimamia binadamu, kama vile,fumoliyongo. Mungu ana mamlaka ya kuchagua awapendao, na kuwapa majukumu yampendezayo. Liyongo ametumiwa kudhihirisha utukufu wa Mungu kwani Mungu hapendezwi na nyoyo chafu, za akina Daudi mringwari na mtoto wake liyongo aliyemsaliti.
Nguvu za mwenyezi mungu pia ni somo hasa kwa waumini waisilamu; Matukio yanayomkumba Liyongo ni dhihirisho la nguvu za Mwenyezi Mungu. Kutokanana sifa tele za Fumoliyongo, tunatoa rai kuwa yeye ametumiwa kama mwongozo bora kwa waumini wote wa Kiislamu. Jukumu lake kuu ni kuwa kilelezo au mfano bora wa kuigwa kwa kila muumini kama watume.
Wakatimwingine, utendi wa Fumoliyongo umekiuka matakwa ya dini tukufu ya uislamu, kinyume na mafundisho ya hadith na koran tukufu kama;
Matendo ya Sultan wa pate Bw Daudi mringwari kakake Fumoliyongo ya kumpangia njama za kumwangamiza Liyongo yanayodhihirishwa na mwandishi katika utenzi wa fumoliyongo (beti 87, 71,53) yanakiuka na kuvuka mipaka na kuvunja sheria za hadith pamoja na Koran tukufu. Mtume Mohamed(SAW) Alikuja kuokoa watu kuhubiri utendaji mazuri kwa wengine sio kutenda maovu, kwamfano
- Mfalme kawambiya
‘‘Liyongo kunipatiya
Kitwa mukanieteya
T’awapa riale miya’’
- Mwambieni tusafiri
Hata pate tukajiri
Hapana tena khatari
Habari tumesikiya.
- Akatiwa gerezani
Kafungiwa kijumbani
Asikari mlangoni
Kwa zamu wakachangaliya.
Mipango hiyo yote inayooneshwa kwenye beti hizi yanakiuka matakwa ya mtume muhamadi kutendea watu maovu.
Pia, tendo la kumuoza liyongo kiholela na mke wa kigalla linakiuka mipaka ya ndoa katika dini ya kiislamu ambapo muislamu anapaswa kuozwa kirasmi na kiongozi wa msikiti. (ubeti 45
- Sharuti wakatimiza
Liyongo wakamuoza
Kwa furaha na kuteza
Nyumbani akaingiya.
- mke katukuwa mimba
Akazaa mwane simba
Mwanamume wa kutamba
Mwane liyongo sikiya.
Tendo la mtoto wa liyongo la kumsaliti kwa kumdunda sindano ya shaba na kumuua haliambatani na mafundisho ya dini ya kiislamu. (ubeti 179)
- kamtiya kitovuni
Naye ulele kwa t’ani
Achamka hamuoni
Kiyana amekimbiya.
Mungu hapendezwi na nyoyo chafu, za akina Daudi mringwari na mtoto wake liyongo aliyemsaliti. NakwahivyoWaislamu wana imani kuwa wanadamu wote wanaotenda kinyume na matakwa ya Allah wataadhibiwa vikali.
Katika utenzi wa Fumoliyongo, kuna maswali ambayo pengo halijazibika ama hakika haikutambulika wazi kama;
Muhamad kijumwa aliandika kuhusu utenzi wa Fumoliyongo kutokana na wenyeji wa mwambao wa Kenya, je matendo ya liyongo ni ya kweli au mwandishi kaongeza utamu kwa kuweka zaidi ya aliyoambiwa?
Hadithi inaanza kwa kutuelezea kuwa liyongo alikuwa anaishi mwituni hata kabla ya kuwa na ugomvi na kakake mringwari, je kama mtoto wa kifalme kwanini aliamua kuishi mwituni na wadahalo pamoja na makabila mengine sio pate kwenye Ufalme, huenda ulikuwa uongo?
Hatimaye, nakamilisha mjadala huu kwa kusema, uchunguzi zaidi kuhusu maisha na matendo ya liyongo unahitajika kwa kutembelea hasa panaposemekana kuwa aliishi halafu historia yake ikagunduliwa rasmi na wenyeji.
Share this: Kiswahili leo kiswahili kesho