MIFANO YA MASHAIRI YA KUCHAMBUA

              Utetezi wa Haki
Namba nawe mlimwengu, pulikiza matamko
Nikweleze neno langu, uzinduwe bongo lako
Nayo nda M'ngu si yangu, na ayani haya yako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

2
Simama uitete, usivikhofu vituko
Aliyo nayo mwendee, akupe kilicho chako
Akipinga mlemee, mwandame kulla endako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

3
Amkani mulolala,na wenye sikio koko
Isiwe mato kulola,natutizame twendako
Tuwate na kuduwala,usingizi si mashiko
Uwatapo haki yako,utaingiya motoni

4
Teteya kwa kula hali, usiche misukosuko
Siche wingi wala mali,sabilisha roho yako
Unyonge usikubali, ukaonewa kwa chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

5
Siche kifaru na ndovu, wangazidi nguvu zako
Wapempe kwa uwekevu, unusuru haki yako
Siandame wapumbavu,kilicho chako ni chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

6
Cha mtu hakifitiki,kikafungiwa kiliko
Huzuka kikawa hiki,kazana utwae chako
Uwatapo yako haki,fahamu ni dhara kwako
Leo na kwa Mola wako,utaingiya motoni

7
Fumbuwa unyang'arize, uone duniya yako
Bure sijiangamize,kuangalia wendako
Utatupa upoteze,wende ambapo si pako
Uwatapo haki yako,utaingiya motoni

8
Kadhalika nako pia,huko ambako sikwako
Huwezi kujitetea,wala huwi na mashiko
Basi iwaze duniya,kwani ya kale hayako
Uwatapo haki yako ,utaingiya motoni

9
Kadi tamati shairi,sitii la ongezeko
Mwanati iwa tayari, utete haki yako
Unyonge usiukiri,Jifunge ufe kwa chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

by Ahmad Nassir from Malenga wa Mvita

 “OWA”
                                                                   
                      Owa s'andame hadaa, moyo ukahadaiwa
                      Owa anaye kufaa, mke mwenye kusifiwa
                      Owa upate kuzaa, kama ulivyozaliwa
                      Owa ukijaaliwa, mupendane na mkeo

                                                 [2]
                      Owa aliye na kheri, muandamane kwa dini
                      Owa yai la johari, litiye nuru nyumbani
                      Owa mdomo mzuri, ukupambie lisani
                      Owa ungiye nyumbani, mupendane na mkeo

                                                [3]
                      Owa moyo wa imani, usozumbua mafuja
                      Owa usiowe duni, anayeitwa kioja
                      Owa mtenda wa dini, ndiye mke mwenye haja
                      Owa utungiwe koja, mupendane na mkeo

                                             [4]
                      Owa siowe tambara, linukiyalo vibaya
                      Owa mwanamke jura, mlekeze njema ndia
                      Owa usiowe sura, kutaka kuzangaliya
                      Owa mzuri tabiya, mupendane na mkeo

                                           [5]
                      Owa kijana kitoto, mteshi wa kutekeya
                      Owa akwandike jito, mwenye kukuhurumiya
                      Owa usiowe zito, jabali likakwemeya
                      Owa aliye na haya, mupendane na mkeo

                                         [6]
                      Owa s'andame uhuni, upate juwa kuzawa
                      Owa nami natamani, ela sijajaaliwa
                      Owa utiye chandani, pete uloiteuwa
                      Owa ujuwe kuowa, mupendane na mkeo

                                        [7]
                      Owa uvishwe kilemba, na joho na mahazamu
                      Owa wapate kupamba, ukale twiba na tamu
                      Owa upambiwe chumba, upate tanganya damu
                      Owa usijidhulumu, mupendane na mkeo

                                       [8]
                      Owa kinda la tausi, alo nadhifu mibele
                      Owa kiini cheusi, chendacho nyuma na mbele
                      Owa siowe tetesi, apaye watu uwele
                      Owa aliye lekele,  mupendane na mkeo

                                      [9]
                      Owa ualike watu, wahudhuriye arusi
                      Owa nawe uwe mtu, mkeo simnakisi
                      Owa muonyane utu, mukae mutaanasi
                      Owa mupane mepesi, mupendane na mkeo

                                    [10]
                      Owa akukubaliye, akuizao siowe
                      Owa upendane naye, zamani sizo ujuwe
                      Owa akuridhiyae, mujikubali wenyewe
                      Owa mukae mutuwe, mupendane na mkeo

                                   [11]
                      Owa chenye asimini, kikuba cha asiliya
                      Owa kilo na rihani, na waridi maridhiya
                      Owa kilicho na shani, na manukato kutiya
                      Owa ujuwe duniya, mupendane na mkeo

                                    [12]
                      Owa utukuze cheo, na jina lipate kuwa
                      Owa apate mkeo, aambiwe meolewa
                      Owa kama waowao, moyo usiliye ngowa
                      Owa ujuwe kukuwa, mupendane na mkeo
MASWALI

1. a) Katika jamii ambako ndoa nyingi zinakumbwa na migogoro, talaka na mmomonyoko wa maadili, jadili nafasi ya shairi hili kama chombo cha kurekebisha misingi ya ndoa na kuimarisha mshikamano wa kifamilia.

1.b) Kwa kurejelea shairi hili, jadili nafasi ya dini katika ujenzi wa dhana ya ndoa bora na mwenzi mwafaka katika jamii ya Kiswahili.

2. a) Kwa kutumia nadharia ya uhakiki wa kijinsia, tathmini namna mwanamke anavyowasilishwa katika shairi hili na uoneshe kama uwasilishaji huo unaendana au unapingana na dhana za kisasa za usawa wa kijinsia.

2. b) Jadili sauti ya mshairi kama mshauri wa kijamii katika shairi hili na tathmini uhalali wa mamlaka yake katika kutoa nasaha kuhusu maisha ya ndoa.

3.a) Changanua kwa kina mchango wa takriri ya mstari “mupendane na mkeo” katika kujenga muundo, maana na athari ya ujumbe wa shairi.

3.b) Kwa mifano mahsusi kutoka kwenye shairi, jadili jinsi fani (vina, mizani, mtiririko wa beti na lugha) inavyosaidia kuwasilisha maudhui ya shairi hili.

4.a) Jadili matumizi ya taswira katika shairi hili na tathmini mchango wake katika kufafanua dhana ya mke bora na ndoa yenye maadili.

4.b) Kwa kuzingatia msamiati na mtindo wa uandishi, eleza sababu zinazothibitisha kuwa shairi hili linaegemea mapokeo ya ushairi wa kale wa Kiswahili, huku ukijadili kama lina nafasi katika jamii ya sasa.

5.a) Jadili uhusiano kati ya fasihi na jamii kwa kurejelea shairi hili, ukionesha jinsi fasihi inavyotumika kama chombo cha maadili na mwelekeo wa kijamii.

5.b) Tathmini mchango wa shairi hili katika mjadala mpana wa taasisi ya ndoa katika fasihi ya Kiswahili, ukilinganisha kwa ufupi na kazi nyingine za ushairi kuhusu ndoa au mapenzi.

6.a) Kuna vipengele kadhaa vinavyoifanya kazi hii kuwa la kishairi. chambua vipengele vinavyolifanya shairi hili kuwa shairi kamili.
6.b) Mshairi ametumia mbinu tofauti kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira. Eleza vipengele vya uhuru wa mshairi vilivyotumiwa katika shairi hili.

BY AHMAD NASSIR FROM THE BOOK "MALENGA WA MVITA"

MVUVI

               Ndimi mvuvi halisi, Kulla vuvi nalijuwa
Nivuwaye mikambisi, na papa wenye khatuwa
Wala sivui vingisi, mishipi haisumbuwa
Nimekwambiya elewa

2
Sivuwi bahari ndogo, hatia nanga fuoni
Havisimbika vigogo, vilivyozama majini
Na wala Sivuwi ngogo, vidagaa na mbinini
Siwavui asilani

3

Jabali hulijilisi, jishipi nikalitupa
Haotea mifulusi, na nguru na mijipapa
Si kasikazi Si kusi, khabari yangu nakupa
Wala sivui kwa pupa

4

Na nivuapo malema, huingia ndani ndani
Maji yangu ni ya pima, thalatha u thalathini
Na ndiyo ninayozama, lema halibwaga tini
Uliza mimi n'nani?

5

Na nivuapo maziyo, mavuvi ya kizamani
Kwa hino hali niliyo, huvua kwa kutamani
Hatafuta kiteweyo, cha wali mwema kombeni
Haandaa siniani

6
Ela uvuvi wa juya, kuvua siutamani
Sababuye 'takwambiya, ufahamiwe mwendani
Ni kwambakwe huingiya, samaki waso thamani
Kama wewe mwafulani

7
Ni Kuu yangu bahari,elewa sana elewa
Huko hakwendi vihori,wala vyenu vimashuwa
Shoti nahodha hodari,kisha ende kwa ngalawa
Na milango kuijuwa

From Malenga wa Mvita by Ahmad Nassir 

NYONDA

                                       1
                     Laaziza, muhibu liakirami
                     Pulikiza, nikupe wangu usemi
                     Menikaza, sipati kunena yomi

                                
                                      2
                     Wangu moyo, una jambo uupete
                     Wayowayo, liniveme kana Pete
                     Zangu mbio, nataraji tuwe sote

                                       3
                     Si moyoni, jaraha kulla mahali
                     Na matoni, sipati lepe silali
                     Masikini, napenda kitu ki ghali

                                        4
                     U kizani, moyo umefitamana
                     Na imani, viumbe huoneana
                     Swamahani, sinifanyiye khiyana

                                        5
                     Hikuwaza, iwapo nala huata
                     Miujiza, muda hilala huota
                     Niuguza, maradhi yalonipata

                                       6
                     Yomi bui, mwenziyo nimedangana
                     Hunijui, moyoni ninavyoona
                     Sinwi shai, nisikutaje kwa jina

                                      7
                     Yomi toba, mwenziyo ni taabani
                     Kwa mahaba, yalonivaa moyoni
                     Hunikaba, wala utungu sioni.

From Malenga wa Mvita by Ahmad Nassir 

UJANA

                       

                                       1
                     Ewe ulo na busara, fikiri bibi na bwana,
                     Fikiri lilo tohara, na lile lilo dhamana,
                     Pia fikiri izara, wewe nayo kukutana,
                     Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho

                                       2
                     Ujana ni jambo bora, ameupamba Rabana, 
                     Tena umetia fora, ulitendalo hufana,
                     Basi usiwe mkora, akiba uweke sana,
                     Sihadawe na ujana na ujana una mwisho.

                                       3
                     Kuweka jambo dharura, jihimu kuweka mwana,
                     Siyo pato kulipura, kwa usiku na mchana,
                     Ukitoweka ujura, elewa umekubana,
                     Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho.
                   
                                       4
                     Hebu zituze fikara, ushike ninayonena, 
                     Akiba kwako sitam, ukiijaza shehena,
                     Na pia huwa kafara, na shida isije tena,
                     Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho.
                    
                                        5
                     Ufanyapo biashara, ewe kijana kazana, 
                     Ujihimu kila mara, na akiba kushikana,
                     Uzee ukikudara, uwe umetulizana,
                     Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho.
                     
                                        6
                     Kwa kweli Si masihara, mwanadamu hutatana,
                     Kukosa kitu ni dhara, jina hutojulikana,
                     Au uitwe fukara, mzee mja wa lana,
                     Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho.
                     
                                         7
                     Ujana hukuzingira, ukangiwa na fitina,
                     Ukafikwa na majira, uzee ukawa jina,
                     Basi na wako ujira. wa kazi weka hazina,
                     Sihadawe na ujana, na ujana una mwisho

..By Said. kizere 

WAHAKA

                        Rabbi Mola Mswifika,
                        Muumba na kuumbuwa
                        swifazo mekamilika,
                        hakuna lilopunguwa 
                        Rabbi nondosha wahaka
                        mahaba yataniuwa,

                        Ya Ilahi Mtajika
                        nakuomba we Moliwa
                        Wahadahu Ia shirika 
                        nguvu zisomithiliwa
                        Rabbi nondosha wahaka 
                        mahaba yataniuwa,

                        Enzi ni yako hakika
                        ni yupi tena wa kuwwa?
                        Bwana ulotakasika
                        na usiye shabihika. 
                        Rabbi nondosha wahaka 
                        mahaba yataniuwa.

                        Aridhi umetandika 
                        mbingu na mwezi na juwa
                        na nyota zilopambika 
                        usiku unapokuwa.
                        Rabbi nondosha wahaka
                        mahaba yataniuwa

                        Usiye na ushirika 
                        kutaka kushauriwa
                        waona usooneka 
                        tangu isotanguliwa.
                        Rabbi nondosha wahaka
                        mahaba yataniuwa.

FIKIRI

I

                                  1.
              Fikiri zako fikira, ufikiri kila tendo,
              Fikiri lilo na dhara, ufikiri na Ia pendo,
              Fikiri lilo tohara, ufikiri na uvundo,
              Fikiri fikiri tendo, Ia amani na busara.
                       
                                2.
              Fikiri sana dunia, ina mzuri mdundo, 
              Fikiri sana yalia, ina mzuri mshindo,
              Fikiri mwisho sikia, unapasuka msondo, 
              Fikiri fikiri tendo, Ia amani na busara.
                        
                                    3.
              Fikiri ndugu dahari, dunia ina mikondo, 
              Fikiri hizi habari, ni kushuka na mipando,
              Fikiri dunia pori, chaka Ia uwi na kondo,
              Fikiri fikiri tendo, la amani na busara.

                                   4.  
              Fikiri dau muundi, muunda dau muundo, 
              Fikiri lende kilindi, daule likaze mwendo, 
              Fikiri dau halendi, nguvu za dau upondo,

                                     5.  
              Fikiri ninakariri, usiwe mwenye mfundo,
              Fikiri tena fikiri, kila ovu liwe kando,
              Fikiri mno hatari, ukiwa na mbovu nyendo,
              Fikiri fikiri tendo, Ia amani na busara.

By Abdalla Kizere 

Kiburi

                               1.
              Ikiwa umeumbika, kwa uzuri ulotimu,
              Au umetajirika, pesa nyingi tasilimu,
              Kiburi ukajivika. vazi lenye uhasimu,
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                               2.  
              Mola mwenye madaraka, ndiye mwenye kurehemu
              Kukupa na kukupoka, ndiyo kaziye Karimu.
              Humpa anayetaka, jamii ya wanadamu,
              Kiburi kwa mwandamu, Si kitu chema kiburi.

                                  3. 
              Waringa na hekaheka, wenzio kuwashutumu,
              Kwa kuziona fanaka, Mola alokukirimu,
              Wazimu ukakushika, ukawa huna fahamu,
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                                4. 
              Kwanza ziondowe taka, nduguzo kuwahasimu.
              Usiipige mipaka, wazazi kuwalaumu,
              Zinduka ndugu zinduka, wewe Sio marehemu,
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                               5.  
              Kiburi ni mbaya shuka, kuivaa ni haramu.
              Yapendeza kukumbuka, msemo wenye kudumu,
              Mpanda ngazi hushuka, alacho kikawa sumu.
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                               6. 
              Na mwanadamu yataka, bongo lake kuhitimu.
              Wazee walotamka, maneno yalo muhimu,
              Kulonama huinuka, laini huwa kigumu.
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                                7. 
              Kituoni nimefika, nazikomesha nudhumu,
              Yatosha naloandika, kiburi ni jahanamu,
              Ashikae atashika, asoshika Si lazimu,
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

By – ABDALA KIZERE 

NAWAU’ZA WASWAHILI

                                    1

Risala enuka hima, sikae 'kataghafali
N'na jambo 'takutuma, ubalegheshe suali
Nipate jawabu njema, yenye amani na kweli
Nauliza Kiswahili, ni lugha ya watu gani?

2
Lugha nyingi duniyani, zatamkwa mbalimbali
Na zote ulimwenguni, zina wenyewe mahali
Si Hindi Si Uzunguni, mewaumbia Jalali
Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani ?

3
Wakamba wana kikwao, lugha yao ya asili
Na Wazungu piya nao, wana zao mbalimbali
Na Wameru wana yao, wengine ni Wasomali
Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani ?

4
Wahindi wana Kihindi, kwa kabila mbalimbali
Na Wanandi ni Kinandi, ndizo zao akuwali
Wengine ni Wakilindi, wana yao ya asili
Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
5
Kuuliza Si ujinga, musinifanye jahili
Nautafuta niuwanga, tuzinduwane akili
Ndipo shairi hatunga, kubaleghesha suali
Nielezwe Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
6
Mara nyingi husikiya, kuwa hichi Kiswahili
Hakina mtu mmoya, ambaye ni chake kweli
Na wengine huteteya, kina wenyewe asili
Ndipo ha'mba Kiswahili, ni lugha ya watu gani?

7
Masai ana kikwao, lugha ya tangu azali
Na Mahara wana yao, wengine Mashelisheli
Na Waluo lugha zao, Si sawa na Maragoli
Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani?

8
Na jamii wengineo, wana lugha mbalimbali
Na kujuwa ya wenzao, ni kujifunza ya pili
Lakini wana na zao, lugha za tangu asili
Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani?

9
Sasa ambalo nataka, kwa wenye kujuwa hili
Wa Kenya na Tanganyika, na walo kulla mahali
Nipani ilo hakika, tubalegheshe ukweli
Nambiyani Kiswahili, ni lugha ya watu gani?

10
Miye mefikiri mno, kuamuwa jambo hili
Na huona lugha hino, lazima ina asili
Kwa sababu kulla neno, lina mwanzo wa usuli
Ndipo ha'mba Kiswahili, hi lugha ya watu gani?

11
Na iwapo hivi sivyo, niliyyoamuwa hili
Nionyeshani viliyyo, mubainishe ukweli
Nijuwe ambavyo ndivyo, tutowane mushkili
Kifunuke Kiswahili, ni lugha ya watu gani?

12
Na iwapo atakuja, wa kunijibu suali
Namuomba jambo moja, twambiyane kiakili
Tusionyane miuja, jambo nisilo kubali
N'anambiye Kiswahili, ni lugha ya watu gani?

13
Tamati ndio akhiri, na jina langu ni hili
Ahmadi wa Nasiri, na Bhalo ndilo Ia pili
Mtungaji mashuhuri, mpenda penye ukweli
Nambiyani Kiswahili, ni lugha ya watu gani?

Leave a comment