Tunawakaribisha nyote kwa kipindi Maalum cha Kumbukizi ya Profesa Habwe – TV47
Tunayo furaha kubwa kuwajulisha Wasomi nyote, walimu, wanafunzi, wanasiasa, wanahabari na wadau wa Kiswahili kuhusu kipindi maalum cha TV47 kilichoandaliwa kumkumbuka Profesa Habwe, mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kiswahili ambaye mchango wake katika lugha na fasihi ya Kiswahili hautasahaulika.
Kipindi hiki kitafanyika tarehe 22/08/2025 saa tano asuhuhi na kitaleta pamoja wanajopo na wataalam wa Kiswahili wanaojulikana kwa michango yao katika lugha na fasihi ya Kiswahili wakiwemo;
- Profesa Wallah Bin Wallah – Gwiji wa Kiswahili na mwandishi mashuhuri wa Mashairi kutoka Kenya.
- Profesa Iribe Mwangi – Mwanaisimu mashuhuri na mwandishi wa vitabu kutoka Nairobi.
- Dkt. Hamisi Babusa – Babusa TV, Nairobi.
- Ndugu Ali Hassan Kauleni – Mwanahabari shupavu.
Katika kipindi hiki, tutakuwa na majadiliano ya kina kuhusu:
- Maisha na kazi za Profesa Habwe.
- Mchango wake mkubwa katika fasihi na isimu ya Kiswahili.
- Njia za kuendeleza Kiswahili kama lugha ya elimu, tafiti na mawasiliano barani Afrika.
- Jinsi urithi wa Profesa Habwe unaweza kuhamasisha kizazi kipya cha walimu, wasomi na waandishi.
Huu ni wakati wa kuungana pamoja, kujifunza na kumuenzi Profesa Habwe. Kipindi hiki kitakuwa fursa ya kipekee kwa watazamaji kuzungumza, kuuliza maswali na kupata msukumo kutoka kwa wanajopo walioguswa na mchango wa Profesa Habwe.
Tunawaalika nyote kutazama na kushiriki katika kumbukizi hii, tukihakikisha kazi, mafundisho na urithi wa Profesa Habwe unaendelea kuishi katika mioyo na akili zetu na kuendeleza Kiswahili kama lugha ya elimu na mawasiliano barani Afrika.
Usikose! Jiunge nasi TV47 na ufurahie kipindi hiki cha heshima na mafunzo.
