SIKU YA SABA SABA TRICONA 2025

Siku ya Kimataifa ya Kiswahili huadhimishwa kila tarehe 7 Julai, kufuatia kutambuliKa kwake rasmi na shirika la UNESCO mwaka 2022. Siku hii inatambua Kiswahili kama lugha mojawapo inayozungumzwa zaidi barani Afrika na chombo muhimu cha umoja, utamaduni na ushirikiano wa kikanda. Sisi kama Waganda pamoja na ndugu zetu wa Afrika Mashariki, tunajivunia kuienzi lugha hii adhimu na wote wanaoithamini.


Katika siku hii ya tarehe 7 Julai mwaka huu, tunajiunga na wadau wa kimataifa kusherehekea Siku hii ya Kiswahili. Kiswahili ni lugha ya umoja, utambulisho na maendeleo Afrika Mashariki.

Natoa wito kwa wananchi wote wa Uganda na kila mdau kuipa lugha hii heshima inayostahili na siku hii iadhimishwe kwa moyo mkunjufu na kutambua nafasi muhimu ya Kiswahili katika kuimarisha amani, umoja na maendeleo endelevu.

Natoa shukrani za dhati kwa shirika la UNESCO kwa kuitambua lugha hii na kuipa siku hii maalum na pia nawashukuru Marais wa nchi wwanachama za Afrika Mashariki kwa kuendelea kutoa msaada wao katika kuiendeleza.

Kwa wadau wetu hapa Uganda hususan walimu wa Kiswahili na wengine wote wanaoithamini na kuchangia katika maendeleo yake, nawapongeza kwa juhudi zenu. Bila kujali kipato kilivyo, nawahimiza muendelee kusukuma mbele ajenda ya kuendeleza Kiswahili kama lugha ya pamoja kwa Afrika. Afrika ni fahari yetu na Kiswahili ndiyo sauti yetu.

Tukumbuke kwamba kupitia lugha ya pamoja, tunaweza kujenga misingi imara utakaowezesha kuunda Umoja wa Mataifa ya Afrika (USA), Afrika moja yenye nguvu ziliyoungana na yenye uwezo wa kuamua hatima yake. Mchango wenu unaweka msingi kwa vizazi vijavyo kuishi katika bara lenye amani umoja na ustawi.

Nina furaha kutangaza kuwa medali za kutambua mchango mkubwa zitatolewa kwa Waganda waliojitoa mhanga na juhudi zao kwa ajili ya Kiswahili, akiwemo Mzee Milton Rwabushaiza na wengine wengi ambao wamepitia safari hii kwa ujasiri na kujitolea.

Mwaka huu, wakati baadhi ya wenzetu watasafiri kwenda Rwanda kuungana na Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) kwa maadhimisho ya kikanda, tunawaalika kwa moyo mkunjufu wadau wote wa Kiswahili kuungana nasi katika Shule ya Sekondari ya Trinity College Nabbingo kwa ajili ya maadhimisho ya hapa nchini Uganda.

Ninawahimiza walimu wote kutoka shule zote mbalimbali kuwaleta wanafunzi wao kushiriki sherehe hizi ili kizazi kipya kipate kuona, kujifunza na kuthamini umuhimu wa Kiswahili kama lugha umoja na kikanda.

Tunatarajia programu ya kuvutia itakayojumuisha:

  • Kunyanyua mabango na bendera kutoka shule na taasisi mbalimbali
  • Kuvaa na kufurahia mavazi ya kitamaduni ya Kiafrika
  • Ngoma na nyimbo za kitamaduni
  • Hotuba maalum kutoka kwa wageni mashuhuri
  • Mashairi ya Kiswahili
  • Mashindano ya hotuba za Kiswahili
  • Tuzo na medali kwa mashujaa wa Kiswahili
  • Maonesho ya vyakula vya Kiafrika na Afrika Mashariki
  • Kuigiza na kusimulia hadithi za kuburudisha
  • Maonesho ya fasihi na kazi za sanaa za Kiswahili

Tuitumie siku hii kusherehekea urithi wetu, kuimarisha umoja na kuwahamasisha vizazi vijavyo kuendeleza gurudumu la Kiswahili kwa nguvu zaidi.

Kiswahili leo, Kiswahili kesho — nyuma haturudi!

Johnpaul Arigumaho – Watetezi wa Kiswahili Uganda (WAKIU)

Leave a comment