NOVELA YA KILIO CHA TUMAINI

MUHTASARI

Mwanga wa Tumaini ni simulizi ya kusisimua inayomhusu Peter, kijana wa miaka 30 aliyelelewa kwenye familia maskini ya kidini, ambaye alirudi kijijini kwao baada ya kupata elimu mjini. Akiwa na moyo wa uongozi na ari ya kubadilisha maisha ya watu wake, Peter alikuta hali kijijini Tumaini ikiwa ya kusikitisha: watoto wakikosa maji safi, wanawake wakihangaika kusaka visima vya mbali, mifugo ikikonda kwa kiu, na vijana wakikimbia mijini kutafuta ajira. Kijiji kilikuwa kimenyamazishwa na hofu na umasikini.

Kwa msukumo wa imani na moyo wa huruma, Peter alianzisha mpango wa kuchimba visima vya maji ili kuondoa ukosefu wa maji uliokuwa umewaumiza watu kwa muda mrefu. Alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Maji-Pesa, mfanyabiashara mwenye uchu wa mali aliyekuwa akiuza maji kwa bei ya juu na kunufaika na mateso ya wanakijiji. Maji-Pesa, akihisi ameonewa na mpango wa Peter, alitumia fitina na uvumi wa sumu kudhoofisha imani ya watu kwa mradi wa visima.

Hata hivyo, Peter hakuogopa. Alisimama kidete, akihimiza umoja na mshikamano, huku akishirikiana na wanawake, wazee, na vijana kuendeleza bustani za chakula na miradi ya kujitegemea. Polepole, watu wakaanza kumuamini, wakashirikiana naye kuleta mwanga mpya wa matumaini. Shule zikapata maji, watoto wakaacha kuumwa, na familia zikapumua tena.

Pamoja na changamoto za propaganda, hujuma, na chuki, Peter aliendelea kuwa mwamba wa Tumaini jina lililomtambulisha tangu mwanzo. Alifungua macho ya jamii yake kuelewa kwamba kila mmoja ana jukumu la kulinda maisha na mali ya kijiji, na kwamba maendeleo ya kweli huanza na mabadiliko ya mioyo.

Hata hivyo, hadithi hii inabaki wazi na yenye kusisimua. Mwisho wa simulizi unatuacha kwenye mashaka, tukijiuliza ikiwa Peter ataweza kustahimili mawimbi mapya ya hujuma na tamaa za wenye nguvu, au ikiwa nuru hii ya Tumaini itazimwa na giza la chuki na ubinafsi wa wanafiki.

Mwanga wa Tumaini inagusa maisha ya kila kijana anayetamani kubadilisha jamii yake, ikionyesha kwamba uongozi wa kweli unahitaji uvumilivu, moyo wa kujitoa, na nguvu ya kuamini katika wema wa binadamu. Hii ni hadithi ya ushindi, mapambano, na ndoto ambazo hazifi ndoto za kuiona dunia bora na yenye haki kwa wote.

SURA YA 1: KURUDI KWA PETER

Jua lilikuwa linazama taratibu, likiacha anga na mwanga wa rangi ya shaba uliotanda juu ya vilima vya mbali. Nilitembea kwenye njia ya vumbi nikielekea kijijini huku miguu yangu ikipiga hatua za mashaka na moyo ukiwa na mzigo mzito. Sauti ya upepo ilikuwa ikipiga juu ya matawi makavu, kama ishara ya hali ya maisha ilivyokuwa hapa Tumaini imekauka, imechoka, imenyamaza.

Niliangalia upande wa kulia, nikaona mifugo wachache waliokuwa wamesalia wakipiga kite cha njaa, mifupa yao ikionekana wazi. Watoto walikuwa wamekaa chini ya mti mkubwa wa mkuyu, wakiangalia mbali kwa macho yaliyokosa matumaini. Akina mama walitembea kwa hatua dhaifu, wakiwa na madumu tupu ya maji waliyozoea kubeba kwa umbali mrefu. Nilihisi kama dunia imewapuuza.

Sikushangaa kuwa vijana wenzangu wengi hawakuwepo. Waliamua kutafuta kazi mijini, wakiikimbia mizigo ya familia zao. Waliobaki, walibaki kwa sababu hawakuwa na pa kwenda. Ndipo nikajua, kama kuna mtu wa kubeba mzigo huu, basi lazima niwe mimi. Nilihisi shingo yangu ikikauka, nikijiuliza kama nina nguvu ya kuanza safari hiyo.

Katikati ya mawazo yangu, nikamwona Maria mama mjane jasiri aliyefiwa mume wake kwa sababu ya njaa na tena anayeheshimika kijijini. Alikuwa amebeba kuni mgongoni, huku binti yake mdogo Esther akishika dumu la maji machafu sana kiasi cha matope. Macho yake yalikuwa yamechoka, lakini bado yalikuwa na mwanga wa imani. Nilimsalimia kwa sauti ya huruma.

Habari za jioni, mama Maria.”

Alinipokea kwa tabasamu la kinyonge, akasema:

Ni nzuri mwenzetu, Karibu nyumbani. Hapa mambo bado ni yale yale, tunavumilia tu.”

Maneno yake yaliniumiza. Tulikaa pembeni ya njia nikatazama kijiji kilichonyamaza kama kama mgonjwa wa kusinzia. Nilipumua maramoja, nikamwambia:

Mama Maria, hatuwezi kuendelea hivi. Kuna namna ya kufanya, lazima tujaribu.”

Alinikodolea macho kwa utulivu wa mama mwenye uzoefu, akasema:

Peter, kama kweli moyo wako ni wa kweli, nitakuwa nyuma yako. Bora tujaribu kuliko kukaa kimya.”

Nilihisi nguvu mpya ikinirudia. Maneno yake yalinikumbusha nilipotoka mimi, Peter, mzaliwa wa kijiji hiki cha Tumaini, mtoto wa familia maskini ya kikatoliki niliyesomea mjini kwa msaada wa mapadre. Waliniita Peter kwa imani kwamba ningekuwa mwanga kwa watu wangu. Sasa nilihisi singeweza kuwaangusha.

Lakini sikujua kama kila mtu angeona nuru hiyo. Maji-Pesa, jina ambalo wanakijiji walimpatia kwa sababu ya kuuza maji kwa bei ya juu na kuwakandamiza maskini, alianza kunipinga mara moja. Aliona mpango wangu wa kuchimba visima kama tishio kwa biashara yake. Siku moja sokoni, aliinua sauti yake kama shujaa wa vita, akasema:

Huyo Peter anajifanya msomi! Anataka kula pesa zenu na kuwaacha mkikosa maji tena! Play With him, mtaona cha mtema kuni”

Maneno ya Maji-Pesa yalinichoma moyo. Huyu alikuwa rafiki yangu wa utotoni, tuliyekula naye mihogo mibichi na kucheza mpira wa mguu uchi wakati wa mvua. Lakini sasa ananiona kama adui. Nilishindwa kulala usiku ule. Nilitazama juu ya paa la nyumba ya udongo, nikajiuliza: “Nimekosea? Nimezidiwa?”

Lakini kila nikifumba macho, niliona watoto wenye macho makavu, wenye matumbo yamevimba, nikajua siwezi kuacha. Nilipaswa kusonga mbele kwa sababu nilibeba jina la Peter na ndani ya jina hilo kulikuwa na deni kubwa kwa watu wangu.

Kesho yake, niliamka mapema nikiwa na roho nzito lakini imara. Nilitoka nyumba kwa nyumba, nikawaomba wanikubali. Sikutaka kuwaamuru, bali kuwasikiliza kwanza. Nilijifunza: watu hawabadilishwi kwa nguvu, bali kwa sauti ya upendo na usikivu. Kadri walivyohisi kwamba naheshimu mawazo yao, walinipa nafasi kueleza ndoto yangu.

Miezi michache baadaye, tulianza kuchimba kisima cha kwanza. Siku maji yalipotokea, wanawake walipiga vigelegele, watoto wakakimbia wakipiga makofi. Nilipiga magoti, nikayagusa yale matone kama baraka kutoka kwa Mungu. Nililia bila haya.

Peter neno lililosikika midomoni mwao, likiwa na heshima na shukrani. Wazee walinipongeza, wakanibariki:

“Peter, Mungu akulinde.”

Sikuhitaji sifa, bali nilitaka kuona Tumaini likiishi tena kwa heshima. Tulianzisha pia mafunzo ya kilimo bora, vijana waliokuwa wamesalia wakaanza kuungana na kushirikiana. Polepole, mashamba yalianza kutoa mazao, watoto wakaacha kulia kwa njaa.

Lakini safari bado ni ndefu. Barabara zimeharibika, shule hazina vitabu, wagonjwa wanahangaika bila dawa. Wakati mwingine ninakaa chini ya mti wa mkuyu, nikijiuliza kama nitaendelea kuwa na nguvu. Lakini kila nikikumbuka jina langu Peter najua sitaruhusu ndoto hii izimike.

Sasa, nikitazama kijiji changu kipya, watoto wakicheza karibu na kisima, Maria akiwa na uso wa furaha, najua Tumaini linaamka. Tumaini linaishi.

SURA YA 2: VIKWAZO NA MAJI-PESA

Kulikuwa na harufu ya mvua ardhini siku ya pili baada ya kuchimba kisima cha kwanza na upepo mzuri uliyeyusha vumbi kidogo. Lakini furaha ya wanakijiji haikudumu kwa muda mrefu. Niliona kwamba kadri watu walivyoanza kupata maji kwa urahisi, uso wa Maji-Pesa ulikuwa unakunjamana zaidi kila siku.

Huyu mtu alikuwa amezoea kuuza maji kwa bei ya juu sana na kupitia biashara hiyo alijenga Jumba kubwa kwa mke wake wa pili na Watoto wa Familia yake kila mtu alipata gari la kifahari aina ya Tx Landcruiser. Alijenga banda kubwa la maduka na kuajiri vijana wachache. Kisima kipya kilimfanya aanze kupoteza wateja. Siku moja alinikuta sokoni akaniita pembeni, sauti yake ikiwa na ukali ambao sijawahi kuusikia:

“Peter, kwa nini unaharibu biashara yangu? Unajua tulivyoteseka kufikisha Kijiji cha Tumaini hapa kilipo? Umekuja hivi juzi na umezaliwa na familia ya maskini Mzee Matata. Tulimsaidia baba yako hata kupata nafasi ya masomo yako halafu wewe unakuja hapa kujifanya mwerevu zaidi? Nilitumia muda wangu na nguvu zangu kuleta maji hapa.”

Nilimwangalia, nikajaribu kuelewa uchungu wake. Nikaona ni mbinafsi na hakuhusika kushabiki elimu yangu bali nilisaidiwa na mapadre wa parokia yetu. Lakini sikukubaliana na tamaa yake. Nikasema kwa utulivu:

“Maji ni uhai, ndugu yangu. Siyo bidhaa ya kuwakandamiza maskini.”

Alitetemeka kwa hasira, akaguna, akaondoka bila kusema neno jingine. Niliona wazi kwamba hakukusudia kuniacha salama.

Muda mfupi baadaye, kelele zikaanza kuenea mitaani kwamba kisima chetu kinaleta magonjwa. Ilikuwa ni propaganda chafu. Nilijua hiyo lazima imetoka kwa Maji-Pesa. Alieneza uvumi kwamba maji yalikuwa na uchafu, kwamba visima ni laana na kwamba watoto wangeugua wakiyatumia maji ya visima vyangu. Wengine walinitazama kwa shaka.

Usiku mmoja nilitembea karibu na kisima kukagua kama pampu inafanya kazi, nikakuta mipira yake imekatwa. Nikaambiwa kumekuja watu wenye bunduki na kulazimisha waliokuwepo kuondoka na wakakata pampu hiyo. Nilihisi machozi yakijaa, maana nilijua tu ni kazi ya mtu asiye na huruma. Lakini sikuweza kulala, nilikaa pale hadi alfajiri kuhakikisha maji bado yanaweza kupatikana.

Asubuhi ile, Maria alikuja akanipata nikiwa nimechoka, akaniwekea mkono begani:

“Peter, usikate tamaa. Tunakuamini.”

Maneno yake yaliniinua kama upendo wa mama. Nikapata nguvu mpya. Tulitengeneza tena pampu, tukakusanya wanakijiji na kuwafundisha jinsi ya kuilinda. Kadri siku zilivyoenda, watu walianza kuelewa uhalisia. Waliona hakuna mtu aliyeugua bali afya ilianza kuimarika. Watoto walionekana na rangi ya uso nzuri zaidi na akina mama walipunguza muda wa kutafuta maji. Siku hiyo hiyo niligundua kauli ya wahenga umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.

Maji-Pesa hakukata tamaa kirahisi. Alianza kupanga mikutano ya siri na baadhi ya wazee wenye tamaa ya pesa, akijaribu kuwarubuni waje kupinga mradi. Niliitwa kwenye kikao kimoja cha Kanisa. Padre mkuu aliniuliza kwa sauti ya upole:

“Peter, ni kweli unaleta fitina kijijini?”

Nilihisi mdomo wangu ukikauka. Nilijua hii ilikuwa nafasi ya kuanguka au kusimama imara. Nikasema kwa ujasiri:

“Padri, najua hakuna mkamilifu, ila sitawahi kumgeukia mwananchi masikini. Nilirudi kutoka chuo ili kuwatumikia, sio kuwakandamiza.”

Padre alinitazama kwa macho yenye huruma, akaona ukweli moyoni mwangu. Akatikisa kichwa taratibu, akasema:

“Peter, songa mbele. Usiruhusu uovu ushinde.”

Nilirudi nyumbani nikijisikia mzito, lakini moyo wangu ukiwa na amani. Nilijua nilikuwa upande sahihi, hata kama vita hivi vilikuwa vigumu.

Kwa muda mfupi, nilijaribu kuzungumza tena na Maji-Pesa. Nilimwita kando ya barabara nikimwomba tuungane badala ya kugombana. Lakini alinikazia macho, akaondoka bila kujibu, akibaki na chuki moyoni. Niliona ni vigumu kumgeuza, lakini nikasema kimoyomoyo: “Hata hivyo sitakata tamaa.”

Kadri wiki zilivyopita, nguvu ya mradi wa visima ilikua. Vijana wachache walijitokeza kunisaidia, akina mama walileta mawazo mapya ya bustani ndogo karibu na kisima. Tulianza kupanda mboga na shule ya msingi ya Nyahoora ikapata mradi wa upandaji miti. Furaha ikaingia tena kijijini.

Usiku mmoja, nilitembea peke yangu kuzunguka mtaani, nikawasikia watoto wakicheza na kuimba kwa sauti:

“Kisima cha Peter kimetupa tumaini!”

Nilijificha nyuma ya ua nikawatazama, nikalia kidogo kwa furaha. Nikasema ndani ya nafsi yangu:

“Sitasaliti watu hawa.”

Kijiji kilianza kuamka polepole, hata kama vikwazo vilikuwa havijaisha. Nilijua safari ilikuwa ndefu na vita na Maji-Pesa haikuwa imeisha. Lakini ndani yangu, mwanga wa uongozi ulibaki hai.

SURA YA 3: MWANGA WA KWANZA

Wiki chache baada ya kuzikabili porojo za Maji-Pesa na kurekebisha pampu iliyoharibiwa, watu wa kijiji walikuwa wameanza kuamini ukweli kwamba kisima hakikuwa laana bali baraka. Siku moja tulikutana chini ya ule mti mkubwa wa mkuyu, karibu na kisima. Akina mama, vijana wachache na hata watoto walikusanyika, kila mmoja na matumaini mapya usoni.

Nilisimama, nikakosa maneno kwa sekunde chache. Niliona macho ya watu yakinitazama kama taa zinazonitegemea kuangaza giza lao. Nikavuta pumzi ndefu, nikasema:

“Hii ni hatua ya mwanzo. Kama tungeweza kuleta maji, tunaweza kuleta mengine pia.”

Watoto walipiga makofi, kina mama wakapiga vigelegele. Nilihisi machozi yakijaa, lakini nilijizuia. Niliona Maria akitabasamu, akiwa amemshika binti yake mkononi. Uso wake ulikuwa na amani ambayo sikuwahi kuiona miaka yote aliyoteseka.

Tulichukua hatua mpya, tulianzisha vikundi vya bustani za mboga, tukatenga eneo Jirani karibu na kisima. Akina mama walianza kupanda mchicha, nyanya, na sukuma wiki. Vijana wakajitolea kusomba mbolea ya samadi kutoka mashamba ya jirani. Polepole tuliona bustani za kijani zikikua na watoto kuanza kula mboga mara kwa mara.

Wakati huo huo, shule ya msingi ilikaribia kufungwa kwa ukosefu wa maji na vyoo safi. Tulipeleka maji ya kisima pale shuleni na walimu walishukuru kwa nguvu. Tena walimu wa sana awa shule hiyo, kando na malalamishi yao ya mshahara, niliwaahidi kwamba wakati utafika pia wapate mshahara kama wa wenzao wa sayansi. Niliona watoto wakirukaruka kwa furaha wakiimba:

“Asante Peter!”

Siku moja, padre mkuu alinialika kwenye ibada ya Jumapili. Baada ya sala, aliniita katika madhabahu mbele ya waumini wote na kusema kwa sauti yenye uzito:

“Peter, Mungu akubariki. Umeleta mwanga mpya hapa Tumaini.”

Nilihisi aibu, maana sikutaka sifa, bali moyo wangu ulijaa faraja. Wazee walikuja kunishika mikono na kunipongeza. Wengine walikuwa wale ambao awali walinisema vibaya. Nilijua walikuwa wameona ukweli.

Lakini Maji-Pesa hakukoma. Siku moja alipita kwenye bustani ya mboga, akawachochea baadhi ya vijana kwamba bustani zinaharibu ardhi yao. Alitishia kwamba visima vitakauka na kuwaacha na hasara. Nilipata habari hizo, nikamfuata usiku nyumbani kwake, nikamkuta akipumzika. Nilimsalimia kwa upole:

“Maji-Pesa, ndugu yangu, naomba uniache nisaidie watu hawa. Tafadhali, tusaidiane.”

Alinitazama bila hisia, akatikisa kichwa, akasema kwa sauti ya dharau:

“Peter, mimi sifanyi kazi ya bure. Wacha nishughulikie biashara yangu.”

Nilihisi huzuni moyoni, maana nilimpenda kama ndugu yangu. Tulikulia pamoja lakini sasa tamaa ilikuwa imemfanya kipofu. Nilirudi nyumbani kwa hatua nzito, lakini nilijua bado sitakata tamaa.

Wiki iliyofuata, mvua ndogo ilinyesha na bustani zikafurahia maji. Mbegu zilianza kupunga mikono na majani yakawa yanashukuru Mungu zaidi, maua ya nyanya yakaanza kufunguka na kuweka tabasamu. Watu walipata nguvu mpya. Tulipanga kuanzisha kikundi cha vijana wa Tumaini kuwafundisha namna ya kuendeleza na kuanzisha biashara.

Siku moja nilikaa karibu na kisima, nikitazama watoto wakipiga kelele za furaha wakichota maji. Nikajikuta nawaza:

“Hii ndiyo maana ya jina langu, Peter mwamba wa matumaini.”

Nilijua mabadiliko haya hayakuwa rahisi. Barabara bado zilikuwa mbovu, wagonjwa walikuwa wanahangaika kupata matibabu, walimu wa sanaa bado wakilia, madaktari wakihama Kwenda ughaibuni na kuna watu walibaki kunipinga. Lakini kwa mara ya kwanza, niliona mwanga wa kweli kwenye kijiji change cha Tumaini. Mwanga wa kwanza, uliozaliwa kwa jasho, upendo na uvumilivu.

SURA YA 4: NGUVU ZA UMOJA

Asubuhi moja, nilikusanya watu wote chini ya mti wa mkuyu, mahali palipokuwa ni kitovu cha maisha ya Tumaini. Nilijua kuwa mshikamano ndio msingi wa kila maendeleo, na ndiyo dawa pekee dhidi ya changamoto zilizoendelea kuja.

“Ndugu zangu, Tumaini yetu inahitaji nguvu zetu sote,” nilizungumza kwa moyo mkunjufu. “Hakuna mmoja anayeweza kuleta mabadiliko peke yake, lakini sisi pamoja tunaweza kushinda kila vikwazo.”

Nilishuhudia wanawake wakipanga vikundi vya usafi wa kijiji, vijana wakijihusisha na miradi ya kilimo. Watoto walionekana wenye furaha, wakielekea shule kwa matumaini mapya, huku wakijua sasa maji safi yatakuwepo kila wakati.

Niliongoza mafunzo kwa viongozi wa kijiji juu ya usimamizi wa rasilimali na mipango endelevu. Nilisisitiza kuwa maendeleo hayatafanikiwa bila maadili mema na kwamba kila mtu anapaswa kuheshimu mchango wa mwenzake.

Maji-Pesa alijaribu tena kuanzisha fitina, lakini sasa watu walikuwa macho wazi na walimchukia mtu yeyote anayeharibu umoja wetu.

Nikiwa chini ya mti ule ule wa mkuyu, nilikumbuka changamoto zote tulizokabiliana nazo, mateso, mashaka na chuki. Lakini sasa moyo wangu ulikuwa umejaa shukrani kwa watu waliojitoa, kwa Tumaini Kijiji kilichoanza kung’aa tena.

Safari bado ilikuwa ndefu, lakini kwa nguvu za umoja, nilijua tumetimiza hatua muhimu.

SURA YA 5: HATUA MPYA, MWANGA MPYA

Siku mpya ilianza Tumaini kwa wito wa matumaini na juhudi za pamoja. Nilihisi ndani ya moyo wangu kuwa mradi wetu ulikuwa kwenye hatua mpya ya maendeleo, na hakuna kinachotuzuia kuendeleza mabadiliko haya ya kweli.

Nilikusanya wakurugenzi wa vijiji pamoja, tukapanga mikakati ya kuanzisha shule ya mafunzo ya ufundi na kilimo cha kisasa. Tulipanga kuwahamasisha vijana kuchukua nafasi kubwa zaidi katika kuleta maendeleo, ili siku moja wao wangeweza kuongoza kwa ujasiri.

Kwa mara ya kwanza, walimu walikuja kijijini kuanzisha madarasa, na watoto walifurahia kupata elimu mpya. Akina mama walijiunga katika vikundi vya ujasiriamali, wakipata mafunzo ya biashara ndogo ndogo ili kusaidia familia zao.

Wakati huo, niliona kuwa mradi wa maji haukuwa tu chanzo cha maji safi, bali pia kiini cha maisha mapya mahali pa kuamsha ndoto na kuwasha mwanga wa matumaini kwa wengi.

Lakini, bado kulikuwa na watu waliokuwa na mashaka na woga. Nilijitahidi kuzungumza nao, kueleza faida za maendeleo na kuwahimiza kuungana nasi badala ya kuendelea kupinga.

Mchana mmoja, nilitembea mtaa nikasikia watoto wakicheza na kuimba wimbo wa Tumaini, wakitangaza kwa furaha:

“Tumaini ni mwanga wetu, maji ni maisha yetu!”

Nilikumbuka kila changamoto tulizokabiliana nazo na moyo wangu ulijaa furaha isiyoelezeka. Nilijua kwamba kila hatua tuliyochukua ilikuwa ni mwanga mpya unaong’ara, ukitoa matumaini kwa vizazi vijavyo.

Niliketi tena chini ya mti wa mkuyu, nikitafakari safari hii ya Tumaini. Ndoto yangu ilikuwa kubwa na kwa nguvu za jamii, umoja na imani, ningehakikisha hatimaye Tumaini litatimiza majukumu yake kwa watu wake.

Jua lilipokuwa likizama tena, niliketi chini ya mti wa mkuyu nikitafakari. Tumaini limepata mwanga, lakini kwa kweli, safari bado ni ndefu na ya changamoto zisizo na mwisho.

Sauti za watoto wakicheza karibu na kisima zilisikika kwa furaha, lakini moyoni mwangu nilihisi kama kuna kivuli kinanijia kivuli cha hatari isiyojulikana.

Maji-Pesa, rafiki wa zamani aliyekuwa adui, bado yuko pembeni, akiwa na mipango yake ya siri. Na dunia yetu ndogo ya Tumaini, ingali ina vizingiti vikubwa vinavyokuja.

Niligusa kisima kwa mikono yangu, nikajiuliza: “Je, nitakuwa na nguvu za kuendelea? Je, ndoto yangu itaishi? Au Tumaini litazama tena gizani?”

Huko nyuma, alijitokeza mtu mmoja, mtu aliyekuwa kimya kwa muda mrefu. Yeye ndiye atakayetaamsha hadithi mpya, na kuleta mapambano mapya ambayo hayatajwi hadi sasa. Nilisimama, macho yangu yakilenga mbali, moyo ukiwa umejaa azma na mshikamano

Maswali
(a) Katika kutunga kazi yake, mwandishi ametumia mahali kadhaa ili kuunda visa
mbali mbali. Wewe kama msomaji wa fasihi fafanua namna mwandishi ametumia mahali ili kuunda visa vyake katika dondoo hili?
(b) Mwandishi wa dondoo hili alikuwa analenga kuwasilisha ujumbe muhimu, je ni
ujumbe upi muhimu unaowasilshwa katika dondoo hili?
(c) Eleza hulka za wahusika angalau wawili kutokana na dondoo.
(d)Waandishi mbalimbali wa kazi za fasihi hubuni na kuandika kazi zao kwa
kutumia lugha kwa namna tofauti. Je, mwandishi ametumiaje lugha yake
katika dondoo hili?
(e) Wewe kama kijana unajifunza nini kutokana na dondoo hili?

Leave a comment