
Katika makala yake ya tarehe 6 Aprili 2025, iliyoandikwa na Caesar Jjingo katika gazeti la Daily Monitor, mtaalamu huyu kutoka Chuo Kikuu cha Makerere anatoa hoja nzito kuhusu nafasi ya Baraza la Kiswahili nchini Uganda, akieleza athari hasi za kukosekana kwake.
Mwandishi anaelezea uzoefu wake wa kushiriki katika mijadala miwili tofauti ya WhatsApp kuhusu maendeleo ya istilahi za Kiswahili. Mjadala wa kwanza ulifanyika asubuhi na ulihusisha washiriki kutoka sehemu mbalimbali duniani. Mjadala huo ulikuwa wa kisayansi na ulilenga kutafuta neno sahihi la Kiswahili kwa ajili ya teknolojia ya Artificial Intelligence, yaani akili bandia. Hili lilikuwa jaribio muhimu kuonyesha jinsi Kiswahili kinavyoendelea kuingia katika maeneo ya taaluma na teknolojia ya kisasa, jambo ambalo linahitaji uratibu wa kitaalamu na wa kitaasisi.
Kwa upande mwingine, mjadala wa pili ulifanyika usiku na ulikuwa na washiriki kutoka Uganda pekee. Tofauti na ule wa asubuhi, mjadala huu ulitawaliwa na hisia binafsi na maoni yaliyojaa ukosefu wa uelewa wa msingi kuhusu lugha. Mada kuu ilikuwa neno la Kiswahili “Mganda,” ambalo kwa mujibu wa lugha hiyo humaanisha mtu kutoka Uganda. Wachangiaji wengi walitaka neno hilo lihusishwe tu na kabila la Baganda, wakipuuza kuwa Kiswahili kama lugha ya kitaifa na kikanda, lina utaratibu wake wa kisarufi wa kuunda majina ya watu kulingana na mataifa yao.
Nukuu moja inayobeba mzizi wa hoja ya Dkt Jjingo ni pale anaposema:
“Bila chombo rasmi kama Baraza la Kiswahili la Taifa, Uganda itaendelea kuwa nyuma katika utekelezaji wa sera ya lugha ya Kiswahili…”
Kauli hii si ya kupuuzwa hata kidogo. Jjingo anaweka wazi kuwa kukosekana kwa mwongozo wa kitaifa kunatoa nafasi kwa tafsiri potofu na hisia binafsi kutawala mijadala ya lugha, badala ya hoja za kitaalamu. Mfano wa neno “Mganda” kutafsiriwa na wengi kama mtu wa kabila la Baganda, badala ya raia wa Uganda, unaonyesha pengo kubwa katika uelewa wa sarufi na historia ya Kiswahili.
Kwa mtazamo wangu, Dkt Jjingo anazungumza kwa niaba ya wengi wanaohangaika kuona Kiswahili kikikuzwa kitaasisi. Sauti yake ni ya kitaalamu lakini pia ya uchungu – uchungu wa kuona lugha hii adhimu ikikosa msimamo madhubuti nchini Uganda, licha ya kuwa lugha rasmi ya pili.
Makala yake inapaswa kuchochea mjadala wa kitaifa. Uganda haiwezi kuendelea kujinasibu kuwa sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bila kuwa na chombo rasmi cha kusimamia maendeleo ya lugha ya Kiswahili. Lazima hatua ichukuliwe.
Katika mjadala wa usiku, wachangiaji wengi walionekana kulazimisha neno hilo “Mganda ” lihusishwe na kabila la Baganda badala ya taifa zima jambo lililoonyesha ukosefu wa uelewa wa msingi kuhusu matumizi ya lugha na historia ya Kiswahili.
Mwandishi anaeleza kuwa hali kama hii ni matokeo ya kukosekana kwa chombo rasmi cha kuongoza maendeleo ya Kiswahili nchini, jambo linalosababisha mkanganyiko mkubwa. Anafafanua kuwa mataifa mengine kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (zamani Zaire) na Jamhuri ya Czech (zamani Bohemia) yamebadilisha majina au maandishi rasmi ya lugha kwa kufuata taratibu sahihi, na hivyo haipaswi kuwa ajabu kwa neno kama Mganda kupitiwa au kufanyiwa marekebisho kisayansi.
Dkt Jjingo anasisitiza kwamba bila chombo rasmi kama Baraza la Kiswahili la Taifa, Uganda itaendelea kuwa nyuma katika utekelezaji wa sera ya lugha ya Kiswahili, ambayo tayari imetangazwa kuwa lugha rasmi ya pili nchini.
Baraza hilo linapaswa kuwa na jukumu la kuratibu, kushauri na kutoa mwelekeo wa kitaaluma juu ya matumizi ya Kiswahili nchini, badala ya kutegemea maamuzi ya kihisia au ya watu binafsi.
Dkt anamalizia kwa kusisitiza kuwa lengo la baraza hilo halitakuwa kudhibiti watu bali kuhimiza matumizi sahihi na yaliyo thabiti ya Kiswahili nchini Uganda kama ilivyo katika mataifa mengine jirani yanayopiga hatua kubwa katika kukuza lugha hiyo.
Kwa maoni yangu, kuanzishwa kwa Baraza la Kiswahili nchini Uganda ni jambo la lazima na linahitaji kuungwa mkono na wadau wote. Uganda, ikiwa ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, inahitaji kuleta mabadiliko madhubuti katika jinsi Kiswahili kinavyoendelezwa na kutumika.
Hivyo, Baraza la Kiswahili litakuwa ni chombo muhimu si tu katika kutoa miongozo ya kitaaluma na kisayansi, bali pia katika kuleta umoja wa kitaifa na kuboresha mawasiliano kati ya wananchi wa Uganda na majirani zao. Kutokuwa na chombo hiki kumeweka taifa katika hatari ya kurudi nyuma katika harakati za kukuza na kuimarisha Kiswahili, lugha ambayo ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.

Kiswahili Leo kiswahili kesho nyuma haturudi. Kazi nzuri sana
LikeLike
Nyuma haturudi
LikeLike