SUBIRA NI NGAO

SUBIRA NI NGAO

JOHNPAUL ARIGUMAHO2025

TABARUKU

Ninaitabarukia kazi hii kwa mama yangu mpendwa Beatrice Katushabe kwa upendo na ujitolea kwake ambavyo vimenifanya niwe hivi nilivyo leo. Ninakitolea wakfu kitabu hiki kwako mama nikiwa na shukrani za dhati kwa juhudi zako. Wewe ni mwamba.

SHUKRANI

Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa mke wangu mpendwa, Lydia Nitwesiga, kwa usaidizi wake usioyumbayumba na kunitia moyo katika safari hii yote. Uwepo wake katika maisha yangu umekuwa chanzo ufanisi huu.

Pia ninawashukuru sana walimu wenzangu katika idara ya Kiswahili shule ya upili Uganda Martyrs Namugongo ambao wamekuwa sehemu muhimu ya ukuaji wangu wa kitaaluma. Hasa, napenda kumshukuru Chrispus Mukama, Joseph Bikorwomuhangi na Peter Nuwajuza kwa ushirikiano wao, utaalam na urafiki wao. Michango yao imekuwa muhimu kwangu na ninathamini usaidizi wao katika kufanikisha mradi huu.

SUBIRA NI NGAO

Katika Shule ya upili Wazalendo, mapenzi, urafiki na simanzi vinagongana. Mapenzi kati ya Alex na Daniella yanalazimishwa kusubiri wakati siri ya kushangaza ya rafiki yao Chris inabadilisha kila kitu. Maelezo ya kutisha na ya hatari za mapenzi kabla ya ndoa  kati ya Chris na Emily kuwa nguzo imara katika kuwasaidia kuishi maisha mazuri ya baadaye.

Soma kisa cha kuhuzunisha kuhusu Mapenzi kabla ya ndoa. Je, Alex na Daniella watakuwa tayari kusubiri au watafuata nyayo za Chris? Furahia safari yao kuanzia chini hadi kikomo. Je, kweli subira ni ngao?

Onyesho la kwanza

Kitendo cha kwanza

[Katika ua la shule ya upili Wazalendo  mvua inanyesha. Wanafunzi wanatembea na miavuli pamoja na mifuko wakielekea darasani kwa masomo ya asubuhi. King’ora kinalia ikionesha kuanza kwa shughuli za siku shuleni. Alex na Daniella wote wanatembea pamoja na wameshika miavuli wakitabasamu na kuzungumza]

Alex:           Haya, Daniella, umeona habari kuhusu densi ya shule? Inakuja hivi karibuni!

Daniella:     Ndio mpenzi wangu Alekuu, niliona! Nimefurahi sana. Lazima  tutakuwa pamoja, sawa mpenzi?”

Alex:           Hakika! Siwezi kwenda na mtu mwingine yeyote ikiwa si wewe Daniella.”

[Wote wanatabasamu pamoja. Katika kutembea pamoja kuelekea darasani kwao, Daniella anamgusa Alex kwa mzaha]

Daniella:     Leo tutasoma Kiswahili asubuhi hii. Unajua Mwalimu Busta alitupa kazi ya kufanya?

Alex:           Naam, ninajua. Wewe umefanya kazi hiyo?

Daniella:     Hahaha! Hapana bwana. Sikufanya kazi yake. Nilikuwa ninakuota usiku kucha.

Alex:           Hahaha! Wewe wewe, wacha wewe! Unadandanya wewe! Lakini Asante. Na mimi nilishindwa kufanya. Leo mwalimu atatucharaza viboko kabisaaa.

Daniella:     Whatever! After all sitachukua Kiswahili kidato cha tatu. Mimi ukiniambia Kiswahili kwangu ni kama kutembea miibani bila viatu.

Alex:           Haha… Mimi nuo ndio mlo wangu. Mimi siwezi kuacha Kiswahili. Ninafurahia wimbo wake wa “Kiswahili leo Kiswahili kesho nyuma haturudiThats why nitachukua Kiswahili kidato cha tatu.

Daniella:     Kwa hivyo, na mimi nitachukua Kiswahili kwa sababu yako tu.

Alex:           [akitabasamu] Kweli? Natumai sio kwa mzaha Daniella!

[Wote wawili wanacheka na kuendelea kutembea, kuzungumza na kufanya mzaha pamoja. Wanaingia darasani, wanaona marafiki zao, Tendo na Sarah, tayari wameketi na mwalimu Busta ameanza kufundisha tayari]

Tendo:        [akiita] Hey, guys! Kwa nini mmechelewa?

Sarah:         [akitabasamu] Ndio, tulikuwa tumeanza kufikiria kuwa may be mmenda maktabani!

[Alex na Daniella wanatabasamu na kuchukua viti vyao na kuanza kipindi]

Onyesho la pili

[Mlango wa darasa unafungwa baada ya Daniella na Alex kuingia. Mwalimu Busta anaandika  mada ya siku “Mapenzi Kabla ya Ndoa” katika ubao. Alex na Daniella wanatazamana kwa tabasamu zaidi]

Mwalimu Busta: Leo, tutasoma mada muhimu sana: “mapenzi kabla ya ndoa” Nini maoni yako kuhusu hili?”

Alex:           [kwa kusitasita] Nadhani ni sawa kumpenda mtu kabla ya ndoa mwalimu, lakini ni muhimu pia kuwa mwangalifu na sio kuharakisha mambo.

Daniella:     [akitabasamu] Ninakubali na mpe……….samahani, ninakubaliana na Alex. Mapenzi ni mazuri, lakini ni muhimu pia kutanguliza masomo yetu na mustakabali wetu.

[Mwalimu Busta anaitikia kwa kuwashukuru kwa michango. Anawaomba wengine kutoa maoni yao kuhusu mada]

Onyesho la tatu

[Wakati wa mapumziko ya chakula cha mchana, Alex na Daniella wamekaa pamoja katika chumba cha maakuli]

Alex:           [akiwa na tabasamu la upendo] Halo, Daniella, ungetaka chakula chochote kutoka kwenye kantini? Labda chipsi au sosegi?”

Daniella:     [akitabasamu] Hapana, mimi niko sawa. Lakini asante kwa kunijali wakati wote.

Alex:           Hiyo ndiyo kazi ya mpenzi wako, sivyo? Wewe kuishi njaa bora nilale bila chakula wiki nzima. Ninakujali sana mpenzi wangu.

Daniella:     [Anaongea peke yake] Nina bahati kubwa sana kuwa naye Alex. Ananifikiria kila mara. Mungu ambariki hadi anioe. Nitameza maneno moyoni kwa mama yangu kuhusu hili.

[Alex anarudi na sahani ya chipsi na sosegi na wanaanza kula pamoja]

Alex:           Halo, Daniella, mama yako anaendeleaje? Ulisema ni mgonjwa wiki iliyopita.

Daniella:     Ndiyo, sasa yuko vizuri zaidi. Amepata nafuu. Asante kwa kuuliza, Alex. Siku zote unajua jinsi ya kunifanya nijisikie vizuri.


Onyesho la nne

[Jioni, Alex na Daniella wameketi na marafiki zao chini ya mti mbele ya maktaba]

Tendo:        [kwa mzaha] Haya, Alex, utamfurahisha lini Daniella?

Sarah:         [akicheka] Ndio, nyie mmekuwa wapenzi kwa muda mrefu! Kwa nini kweli kweli?

Alex:           Ndugu zanguuu! tunachukua mambo polepole. Hatuko tayari kwa hilo tafadhali. Sisi bado wanafunzi wa kidato cha tatu! Unataka tuingie mambo hayo tushindwe kuendelea na masomo na ndoto zet ziangukie patupu?

Daniella:     Ndio, tunataka kumaliza masomo yetu kwanza kabla ya hayo. Mshika mbili moja humponyoka. Itatubidi tungoje hadi wakati ufike.

Tendo:        Mmekuwaje nyie! Nyinyi si watoto wachanga. Mnahitaji kupata utamu wa maisha kabla ya kufa! Tafuta siku mlale pamoja wakati mmoja, utanishukuru baadaye.  Maana hamjaonja asali nyie.

Sarah:         Ndiyo kabisaa. Wewe Alex hujui methali inayosema “Chelewa chelewa utakuta mtoto si wako” Fanya kitu kwa sababu kinaongeza mapenzi. Nyinyi mnakosa utamu jamani!

Alex:           Hatuko tayari, Tendo. Maisha ni mazuri sana tukimaliza masomo kwanza. Yaliyomfikia Annet tulipokuwa kidato cha kwanza hamkuyaona? Si alifukuzwa shuleni? Sasa mnataka na sisi tuingie mtego huo utunase?

Daniella:     Ndio, tunahitaji kufanya maamuzi yetu wenyewe, si tu kufuata kile ambacho wengine wanafanya. Simba mwenda pole ndiye mla nyama. Msitukimbize sipiidi.

Tendo:        Sawa, sawa. Lakini nyie mnakosa utamu. Mimi nimewaambia!

Sarah:         [kwa mzaha] Ndio, labda nyie mnaogopa sana kujaribu! Wewe Alex ngoja ngoja tu, utagonga mwamba.

Onyesho la tano

[Katika likizo, mbele ya duka kuu la Akamwesi Kyebando, Tendo na Sarah wanakutana na wapenzi wao, Jake na Mike. Ghafla, Daniella na Alex wanatokea na Tendo anawashawishi wajiunge]

Tendo:        Hii ni sadfa kwa kweli! Hallo jamaani! Njooni mjiunge nasi! Leo tutakuwa na wakati mzuri sana. Siku ingekuwa mbaya bila nyinyi wawili. Tumefurahi sana kuwaona.

Sarah:         Ndio, msiwe na shaka! Tumefurahi sana kuwakuta hapa. Tunataka kutumia vyema likizo hii. Tumekuwa tukingojea wakati huu kwa muda mrefu, na hatimaye tuko hapa!

Daniella:     Sijui kama…….Alex anataka. Tumekuwa tukichukua mambo polepole na sitaki kuharakisha.

Tendo:        Hey guys, mnaweza kuamini sisi hatimaye ni wanafunzi wa kidato cha pili? Mnakumbuka mwaka wetu wa kwanza wakati mvulana mmoja alifika shuleni mara ya kwanza na kaptura yake ya shule ya msingi?

Sarah:         Oh jamani, hiyo ilikuwa epic! Nadhani alikuwa anaitwa Tenge?

Tendo:        Hahaha…Alitufanyia siku huyo. Unawezaje kuja katika shule ya sekondari na chupi….. Sitasahau jambo hilo kamwe.

Sarah:         Na ni nani anayeweza kuusahau mkoba wake wa rangi nyekundu kama damu? Kila mtu alikuwa namuona. Wanafunzi walipiga msururu kumuona akiingia chumba cha maakuli.

Alex:           Nashangaa hakupotea njia ya kwenda darasani mwake kwa sababu ya ushamba wake…

[Wote wanakimbia hadi mahali tulivu wakicheka na kufanya mzaha]

Tendo:        Ila nimefurahi sana Alex na Daniellah kujiunga nasi! Sisi ni kama ni kama chanda na pete? Upendo lazima udumu hadi milele.

Sarah:         Kabisa! Na sasa tuna wapenzi wetu! Tunaweza kufanya mambo yote ambayo tumekuwa tukitaka kufanya. Shuleni hakuna fursa kama hizi.

Jake:          Ndio, sisi ni timu sasa! Hatuwezi kushindwa. Hakuna mwalimu yeyote kutuingilia. Tumepaa kama ndege angani.

Mike:          Na sisi sio timu tu, sisi ni familia.

Daniella:     Sikuwahi kufikiria ningesema hivi, lakini nimefurahi sana kuwa hapa. Mwanzoni nilisitasita, lakini sasa nina furaha nitamhisi mpenzi wangu Alex.

Alex:           Ndio, mimi pia. Ninahisi kama tumekuwa tukikosa mengi lakini sasa tumeyapata. Tunaishi maisha mazuri sasa.

Tendo:        Nimejifunza mengi sana kutoka kwenu nyote. mmenisaidia kutoka kwenye ganda langu. Ndugu zangu tafadhali nipigie wimbo wa Zuchu mimi nifurahie Maisha. Waliokufa wakiharakishaa….. (Anaanza kuimba huku kabla ya Dj kuweka wimbo)

Nampenzi wangu honey. Simuoni tafrani namwita honey haonekani

Honeey, Honey, Honeey, Honey, Honeey, Honey, Honeey

Aah honey, Nakupendaa honey we unanitesaa

Bolo bolo bolo (bolo)

Kushney bolo (bolo)

Tumsepyale bolo (bolo)

Polokina bolo (bolo) Nampenzi wangu honey

Simuoni tafrani namwita honey haonekani

Honeeeey……….

(Wote wanasimama na kuanza kucheza mziki na boyfriends wao)

Tendo:        Hebu tutazame filamu pamoja! Nani anataka kuja?

Sarah:         Mimi ninataka! Ninajua filamu za kufurahisha.

Daniella:     Hakuna filamu za mapenzi! Hebu tuangalie filamu za Action.

Alex:           Ndio, na mimi ninapenda Action.

Jake:          Nina filamu za mashujaa. Nizitafute?

Mike:          Sawa! Hebu tupate chakula na tuwe na siku ya kutazama filamu.

[Wote wanaenda chumba kimoja kutazama silamu na kula vyakula]

Tendo:        Nani anataka pizza?

Sarah:         Mimi nintaka! Nina njaa.

Daniella:     Mimi pia! Hebu tuagize kutoka sehemu hiyo mpya.

Alex:           Sawa, inaonekana vizuri!

Jake:          Nitaenda kuchukua chakula. Ni nani aliye na filamu tayari?”

Mike:          Mimi! Hebu tuanze kutazama!

[Wanatumia siku kutazama sinema, kula na kujiburudisha pamoja.]

Kitendo cha pili

Onyesho la kwanza

[Muhula wa shule umeanza, Alex na Daniella wamerudi darasani. Wamekaa kwenye madawati yao wakionekana na waswasi]

Tendo:        [akimnong’oneza Sarah] Hallo Sarah, umeona namna Alex na Daniella wana wasiwasi?

Sarah:         [akinong’ona] Ndio, wanafanya mambo ya ajabu sana. Kila mara wanatukana.

Tendo:        Najua, sawa? Na hata hawazungumzi na sisi tena.

Sarah:         Nadhani ni kwa sababu ya kile kilichotokea wakati wa likizo. Alex alijaribu kumshawishi Daniella kuingia kitendo cha ngono, lakini Daniella alikataa. Bora sisi tulifurahia.

Tendo:        Ndio, na sasa wanatuingiza sisi. Wanafikiri tunawahukumu kwa bure?

[Mwalimu anaingia ndani na kipindi kinaanza. Alex na Daniella hawana furaha na wenzao wanaanza kuona]

Nina:           [ananong’ona] Halo, nini kinaendelea kati ya Alex na Daniella? Wanagombana kila wakati.

Kofi:           [akinong’ona] Sijui, lakini nilisikia wana matatizo fulani. Kitu kuhusu ngono.

Akua:          [akijiunga] Ndio, nilisikia Alex alijaribu kumshinikiza Daniella lakini akakataa.”

[Minong’ono ilienea darasani kote na kila mwanafunzi anazungumza kuhusu hali ya Alex na Daniella.]

Alex:           [akisimama] Tafadhali tunaweza kuzingatia somo? Hili halihusiani na mtu mwingine yeyote.

Daniella:     [akisimama pia na darasa inaanguka na vicheko ni minong’ono] Ndio, Can we please mind business that brought us here!! Sawa?

Tendo:        [kwa sauti ya chini] Oh, jamani. Tunajaribu tu kusaidia.

Sarah:         [kwa upole] Ndio, tunawajali ninyi wawili.

[Mwalimu anaingilia kati, akiuliza kila mtu kutulia na kuzingatia somo. Alex na Daniella wameketi chini lakini wanaonekana kutostarehe na kusononeka.]

Mwalimu:   Sawa, tuendelee na mada ya leo. Tafadhali fungua vitabu vyenu kwenye ukurasa wa 37.

[Darasa linaanza, lakini Alex na Daniella bado wanaonekana kukasirika. Hawazingatii somo na wenzao bado wananong’ona kuhusu hali yao.]

Nina:           [akimnong’oneza Kofi] Sielewi kwa nini wanakuwa hivi?. Ni ngono tu?

Kofi:           Ni hivyo tu, Lakini nadhani hawako tayari kwa hatua hiyo.

Akua:          Ndiyo, na sasa wanatusumbua tu. Wajisaidie, hebu tusome jamani.

[Wakati huohuo, Tendo na Sarah wanajaribu kuwa makini kwa somo lakini pia wanajali kuhusu marafiki zao.]

Tendo:        [akimnong’oneza Sarah] Tunapaswa kuwasaidia wenzetu hata kama wametuchukia. Si Daniella akue naye…aiseee!!

Sarah:         Ndio, labda tunaweza kuwaona baada ya kipindi.

[Somo linaendelea, lakini minong’ono chumbani inaendelea na vijana wenzao bado wanaongea porojo kuhusu hali yao]

Alex:           Itanibidi niondoke hapa.

[Wote wawili wanatoka darasani wakiwaacha wenzao na mwalimu katika ukimya na hali ya kushangaza!]

Onyesho la pili

[Katika karamu ya Watahiniwa, Alex na Daniella wako pale wakijaribu kusogeana ili kusahau masuala yao ya nyuma. Mziki unadundwa na wengine wanafurahia.]

Alex:           [akitabasamu] Njoo, Daniella, tuache ya nyuma na tufurahie.

Daniella:     [akisitasita] Sijui, Alex. Sitaki kufanya jambo lolote ambalo nitajuta.”

Alex:           Tutacheza wimbo mmoja tu, njoo! Ni sherehe tu, wacha tufurahie.

[Daniella anaonekana kuwa na wasiwasi kisha Tendo na Sarah wanatokea wakicheza mziki.]

Tendo:        Hallo, jamani! Jiunge nasi tucheze mziki!

Sarah:         Ndio, njooni tufurahie Tarmac gance!

[Daniella anamtazama Alex kisha anawatazama tena Tendo na Sarah. Anaanza kuhisi kujaribiwa]

Daniella:     [akitabasamu] Sawa, nitacheza naye wimbo mmoja tu.

[Wanacheza na kucheka pamoja, lakini karamu inavyoendelea, Alex anaanza kumkaribia Daniella, na anaanza kujisikia vibaya tena.]

Daniella:     [akimsukuma Alex] Alex, acha! Usirudie! Usirudie!

Alex:           [amekata tamaa] Sawa, samahani. Naomba unisamehe. Ni kwa ajili ya mapenzi tu.

Daniella:     Mapenzi ya kutaka kunibusu hapa shuleni na kufanya hivyo ni mapenzi ya aina gani hayo? Mimi nilikuja kusoma si kufanya hivyo, mvumilivu hula mbivu, umesikia?

[Karamu inaendelea, lakini Alex na Daniella sasa wanakabiliwa na changamoto nyingine. Je, watakubali kushawishiwa au?]

Onyesho la tatu

[Siku iliyofuata, Chris rafiki yake Alex na Daniella anawakaribia shuleni, akionekana kusononeka.]

Chris:         Halo ndugu zangu, naweza kuzungumza nanyi kwa dakika moja?

Alex:           [anadadisi] Kuna nini, Chris?

Chris:         [anapumua mara moja] Nilitaka tu kuzungumza nanyi nyote wawili. Nimekuwa katika uhusiano wangu na Emily, na ninajuta kufanya naye ngono mapema hivi.

Daniella:     [akiwa na mshangao] Kweli? Kwa nini? Najua nyinyi mlikuwa mnapendana sana, lakini sikufikiri kwamba ingekuwa hivyo.

Alex:           [ameshtuka] Lo! Chris, ooh, pole ndugu yangu. Siwezi hata kufikiria. Ninamaanisha, tumekuwa tukizungumza juu ya kuwa waangalifu lakini nadhani hatujawahi.

Daniella:     [akiwa na wasiwasi] Chris, unaendeleaje? Najua hili haliwezi kuwa rahisi kwako. Na vipi kuhusu Emily? Anaendeleaje?

Chris:         Hali ni ngumu jamani. Natamani ningerudi nyuma na kufanya mambo kwa njia iliyo sawa. Lakini nataka ninyi nyote mjifunze kutokana na kosa langu.

Alex:           Umesema nini Chris?

Chris:         Hakikisha uko tayari na uhakikishe kwamba kila unachofanya kinalenga tu masomo kwa sasa. Ukimwi ni hali ya maisha na ARVs ni ukumbusho wa kila siku wa makosa yangu.

Alex:           Kwa sasa nimeogopa kabisaa!!

Chris:         Je, mtu anaweza kusonga mbele bila kujifunza kutokana na yaliyopita? Je, mafanikio yanaweza kuwa matamu bila ladha chungu ya majuto?

[Daniella anamtazama Alex, na wote wawili wanaonekana kufikiria sana maneno ya Chris.]

Daniella:     Asante, Chris kwa ushauri wako mzuri. Asiyefunzwa na mamaye funzwa na ulimwengu….lazima tujifunze kitu kwa kweli.

Alex:           [akitikisa kichwa] Ndio, asante kwa kutushauri ndugu Chris. Kwa sasa ninamshukuru Daniella kuwa mwangalifu zaidi……nimefikiria kuacha haya mambo hadi labda nimalize masomo…

[Chris anatikisha kichwa huku machozi yakimtoka na anaondoka akiwaacha Alex na Daniella wakitafakari uhusiano na maamuzi yao wenyewe.]

Chris:         [akiwapungia mkono akilia] Bye Bye ndugu zangu. Kwa sababu hiyo, maisha yangu yamekuwa magumu. Ukimwi hautibikiiiii…..(akiangusha kilio kikubwa zaidi)

Onyesho la nne

[Katika ukumbi wa shule. Bw. Johnson, mshauri wa shule anasimama kwenye jukwaa, akiwasalimu wanafunzi wa kidato cha pili]

Johnson:    Habari za asubuhi wanafunzi wa kidato cha pili? Natumai nyote mko salama?

Wanafunzi: (kwa pamoja) Ni nzuri Bwana Jonhson, shikamoo Bw Johnson?

Johnson:    Marahabaa…. Hamjambo nyote?

Wanafunzi: Hatujambo Bw Johnson. Karibu sana.

Johnson:    Asanteni sana. Jina langu ni Bw. Johnson Atabaki kwa wale ambao hawanijui. Mimi ni mshauri wa shule hapa katika Shule ya Upili ya Wazalendo. Ninafanya kazi ya kushauri wanafunzi, walimu na wazazi ili kusaidia maendeleo yenu hapa shuleni.

[Wanafunzi wanaitikia kwa vichwa kuonesha umakini]

Johnson:    Leo, ninataka kuzungumza juu ya mada muhimu sana: Mapezni kabla ya ndoa. Lakini kabla hatujaanza, hebu tupate maombi kutoka mmoja wenu? (Desire mwanafunzi wa kidato cha pili kaskazin ambaye ni kiongozi wa chama cha kiswahili shuleni anaamsha mkono)

Desire:        (anasimama ili kujitolea kuomba) Hebu tunyenyekee tuombe. Jina la baba, mwana na roho mtakatifu, Amina. Eh Mungu tunakushukuru kwa zawadi ya maisha, wazazi wetu, walimu wetu, mshauri wetu Bw Johnson na watu wengine wote. Tunaomba utuongoze katika shughuli hii ya ushauri na umuongoze mshauri wetu ili aweze kutuokoa kutoka hali mbaya ya kushiriki katika mapenzi kabla ya ndoa. Nimeomba haya yote kupitia jina la mtoto wako Yesu Kristo.

Wanafunzi: (Wote kwa pamoja) Amiina…..

Johnson:    Naomba tumpigie makofi Kiabo Desire kwa kutuombea vizuri. Nitampa zawadi baada ya kipindi hiki kwa sababu ameomba vizuri na ametumia Kiswahili kizuri sana. Asante Desire. Tuko sawa sasa?

Wanafunzi: Naam, tuko sawa mkubwa.

Johnson:    Sawa, kwa hivyo naomba tufafanue maana ya mapenzi kabla ya ndoa inamaanisha nini. Mapenzi kabla ya ndoa inamaanisha kushiriki mapenzi ya dhati  na mtu ambaye hujafunga naye ndoa. Kwa nini ushiriki katika mambo ya kijinga huku hujamaliza kusoma?

[Wanafunzi wanasikiliza kwa makini, wengine wakionesha hamu ya kujua zaidi.]

Wanafunzi: (Wote kwa pamoja) Mada nzuri saana….. Tutafurahiaaa…..

Johnson:    Sasa, ninajua baadhi yenu huenda mnajaribu kufikiria mada hii. Kwa nini hili ni jambo kubwa sana? au Kuna ubaya gani kufanya mapenzi kabla ya ndoa? Lakini niko hapa kuwaambia kuwa kuna hatari zinazohusika na ni muhimu sana kuzielewa.

[Wanafunzi wanashika vijitabu vyao na kuanza kuandika]

Johnson:    Hebu tuchunguze mada hii pamoja, na nitaomba maoni yenu? Je, nyote mko tayari?

Wanafunzi: (Kwa pamoja) Ndiyo Bwana Johnson, tuko tayari.

[Bw. Johnson anatabasamu, akianza uwasilishaji wake]

Johnson:    Kwa hiyo, hebu tuzungumze kuhusu baadhi ya hatari zinazohusiana na mapenzi kabla ya ndoa. Kwanza kabisa, kuna hatari ya kupata mimba isiyotarajiwa.

[Kila mwanafunzi anatikisa kichwa akichukua maelezo.]

Johnson:    Unaposhiriki katika shughuli za ngono bila ulinzi unaofaa, unajiweka katika hatari ya kupata mimba au kumpatia mimba mtu mwingine. Na ikiwa hauko tayari kuwa mzazi, hilo linaweza kubadilisha maisha yako kuwa mabaya.

[Daniella na Alex wanatazamana kwa umakini.]

Johnson:    Hatari nyingine ni magonjwa ya zinaa. Haya ni magonjwa ambayo yanaweza kuenea kwa njia ya kujamiiana na baadhi ya magonjwa hayo yanaweza kuwa na madhara makubwa ya muda mrefu kwa afya yako.

[Wanafunzi wanaonekana kuogopa]

Johnson:    Na kisha kuna kipengele cha mvurugiko wa akili. Mapenzi kabla ya ndoa yanaweza ya hatari kubwa kwa ubongo wako kama mwanafunzi na inaweza pia kusababisha hisia za majuto, hatia na aibu.

[Wanafunzi wanaanza kufikiria huku wakinong’onezana]

Johnson:    Sasa, ninajua baadhi yenu mnajiuliza, je mtu asipende mwenzake? Na jibu langu ni kwamba, penda mwenzako kwa nmna inayostahili.

(Wanafunzi wanaonekana wakicheka na kulifikiria)

Johnson:    Upendo wa kweli unasubiri. Ikiwa mtu anakupenda kikweli, atakuwa tayari kungoja hadi nyote wawili muwe tayari.

(Daniella na Alex wanatabasamu kila mmoja, akiwa anafikiria)

Johnson:    Sasa, ninataka niwasimulie hadithi ya wanafunzi wawili waliohusika katika mapenzi kabla ya ndoa. Kuna wanafunzi walikuwa hapa na walikuwa wanapendana sana. Kila mmoja alikuwa anamwahidi mwenzake dunia na ardhi. Siku moja walienda wakajificha katika ukumbi baada ya prep. Waliingia katika matendo mabaya na kwa bayati mbaya Kamera zilikuwa zinarikodi kila kitu.

[Wanafunzi wanaonekana wakiwa makini zaidi]

Johnson:    Asubuhi iliyofuata, waliitwa katika ofisi ya mwalimu mkuu. Walifukuzwa shuleni na kwa bahati mbaya, mvulana alikuwa amezaliwa na ugonjwa wa ukimwi. Baada ya mwezi mmoja msichana alikuwa na mimba pamoja na Ukimwi. Yaliyomtokea baadaye sikutaka kuwaambia kwa sababu mtalia nyote…

(Wanafunzi wanaonekana wameogopa sana na wengine kuanza kulia machozi)

Johnson:    Kwa hivyo, kinga ni bora kuliko tiba. Maisha yao yalisambaratika na kwa sasa mvulana anabeba mizigo katika soko la Owino na msichana anapika chipsi katika soko la Kalerwe. Wote walitengana na kila mtu yuko anapambana na maisha yake.

[Wanafunzi wanapiga makofi, wametiwa moyo.]

Johnson:    Hoja yangu ni kwamba, matendo kama hayo ukiwa bado mwanafunzi ni mabaya, lakini kwa kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii tunaweza kuyashinda.

[Daniella na Alex wanatazamana huku wakitafakari]

Johnson:    Kwa hiyo, nawaomba nyote mfikirie kwa makini maamuzi yenu. Kumbuka, mapenzi kabla ya ndoa yanaweza kuwa na madhara makubwa. Lakini ikiwa uko tayari kungoja, unaweza kujenga msingi thabiti wa uhusiano mzuri na wa upendo.

Wanafunzi: [Wanafunzi wanaitikia wote] Asante sana, tumejifunza.

Johnson:    Na daima kumbukeni, niko hapa kuwasaidia.

[Wanafunzi wanatabasamu wanashukuru. Kusanyiko linaisha na wanafunzi wanaanza kutawanyika.]

Daniella:     (kwa Alex) Nimependa mawasilisho yake. Nimetiwa moyo.

Alex:           Na mimi kabisa. Nimejifunza kungoja na kuacha haya mambo hadi muda ufike.

[Wanashikana mikono wakiondoka ukumbini pamoja]


Onyesho la tano

[Katika nje ya mlango wa ukumbi wa shule. Daniella, Alex na Chris wanatembea pamoja, wakipiga soga na kucheka]

Daniella:     Habari ndugu zangu? Hebu tusimame pale tuongee mawili matatu.

Alex:           Kabisa.

Chris:         (akitabasamu) Ndio, hilo ni wazo zuri.

[wanaondoka wakiwa wameshikana mikono wote watatu]

Daniella:     Hebu tuombe jamani. Mungu mpendwa, asante kwa kutuongoza vizuri. Tusaidie kuzingatia malengo yetu na kuipa elimu yetu kipaumbele. Utupe nguvu ya kusubiri muda wa mapenzi kamili baada ya kusoma.

Alex:           (akiongeza) Na utusaidie kuwaacha wanafunzi hawa wapumbavu wanaotuingiza katika hali ya kushawishika, Bwana. Tunajua ni shetani na wanataka kutuharibu.

Chris:         (Amina) Ndiyo, Bwana Mungu. Pia, wanawake walioumbwa na kuumbika Bwana, akipita unabaki ukitazama nyuma Mungu, utusaidie na utuokoe mashakani Mungu. Mungu wetu, kuna hili jambo la Makalio maarufu kama Nyash Mungu. Limetuweka wengi matatani. Hiyo ndiyo sababu sasa ninapambana na ukimwi kwa sababu ya Nyash niliyoona inazidi mlima wa Rwenzori Mungu, Tuokoeeee…

[Wanaomba kwa ukimya kwa muda wa dakika tatu. Baadaye wote wanaitikia Aminaaa…..]

Daniella:     (akitabasamu) Asanteni ndugu zangu. Ninahisi kama sote tuko kwenye ukurasa mmoja sasa. Lakini Chris, kwa kweli la Nyash lilikuwa linahitajika?

Alex:           (akitikisa kichwa akicheka pia) Kwa kweli ulipoombea Nyash nikaona ndiyo ilinisukuma kumwendea Daniella. Lakini kwa sasa nimeokoka na nimetambua umuhimu wa kungonja baada ya mwawasilisho ya Johnson. Hakika. Hebu tuachane na mapenzi haya ya shule za upili na tuzingatie mustakabali wetu.

Chris:         (anacheka) Alikuwa moyo mtakatifu ndugu zangu.

[Wote wanaangusha kicheko na kila mmoja anatawanyika kwenda darasani]

Kitendo cha tatu

Onyesho la kwanza

(Katika maktaba, Alex na Daniella wameketi katika meza wakiwa wamezingirwa na vitabu )

Daniella:     (akitabasamu) Nimefurahi tuliamua kuwa marafiki tu Alex. Tunaweza kuzingatia elimu yetu sasa.

Alex:           (akitikisa kichwa) Mimi pia, Daniella. Urafiki huu utatujengea msingi bora kesho.

Daniella:     (kwa kudadisi) Je, unafikiri tungefanya vizuri katika masomo kweli tukiwa katika mambo ya mapenzi kweli?

Alex:           (Katika mawazo) Kusema kweli, sidhani.

Daniella:     (anacheka) Ndio,  na mimi naona hivyo.

Alex:           Lakini kama marafiki, tunaweza kufanya vizuri katika masomo yetu.

Daniella:     (akitabasamu) Ndio, lazima. Kwa hivyo, ni upi mpango wako wa siku zijazo?

Alex:           Ninataka kuwa mhandisi. Je, wewe?

Daniella:     Waoo, nimefurahishwa. Nina hakika utafanya mhandisi mzuri. Mimi ninataka kuwa mwalimu na tena mhadhiri katika vyuo vikuu.

Alex:           Waoo, utakuwa mwalimu mzuri kabisa. Hebu basi tugange yajayo…. yaliyopitwa si ndwele…

Daniella:     Kwa hivyo, ni nini kilikufanya uamue kuwa mhandisi?

Alex:           Nimekuwa nikipendezwa na sayansi na hesabu kila wakati na nikagundua kuwa uhandisi unachanganya zote mbili. Je, wewe kwa nini uliamua kusomea ualimu?

Daniella:     Nimekuwa nikipendezwa na namna Mw Busta alikuwa anachukua mambo yake darasani. Pili, nimeona ni tajiri na ualimu unakupa muda wa kufanya biashara zako nyingine. Tatu, walimu wanakuwa werevu na tena maridadi.

Alex:           (akitabasamu) Asante, Daniella. Nadhani utakuwa mwalimu mzuri kabisa.

Daniella:     Asante Alex. Nitafanya kazi kwa bidii.

[Chris anajiunga nao, akiwa amebeba rundo la vitabu]

Chris:         Jamani! Nini kinaendelea?

Daniella:     Kujadili tu mipango yetu ya baadaye.

Chris:         Lo, ndio! Nimekuwa nikifikiria hilo pia. Nataka kuwa mwanahabari. Ninataka kuzingatia somo la Kiswahili ili niweze kuwa mzungumzaji mzuri kwenye Televisheni.

Alex:           Hilo ni wazo zuri, Chris! Umekuwa mzungumzaji mzuri kila wakati. Nadhani hadi sasa wewe ndiye spika wa viranja wote wa shule hii?

Chris:         (akitabasamu) Hakika, unajua nilichaguliwa bila kipingamizi. Asante Alex. Nitafanya kazi kwa bidii ili niweze kufanya kazi na NBS TV. Sawa, wacha tuanze safari hii ya masomo pamoja kama meli tatu zinazosafiri katika ziwa zikielekea upande mmoja.

Daniella:     Nina furaha kuwa katika safari hii nanyi nyote wawili. Ni kama kuwa na nanga mbili katika dhoruba kuniwekea msingi na kuwa mlengaji.

Alex:           Na mimi ni dira inayotuelekeza kila wakati katika mwelekeo sahihi. Je, Dniella unakumbuka Tendo na Sarah ambao walikuwa wanatusawishi kuingia vitendo vibaya katika kidato cha pili? Unajua sasa wote walishindwa mitihani na kwa sasa wote wanateseka huko mtaani?

Daniella:     Una uhakika Alex? Niliwaona hao, hawangefaulu kabisaa. Walionja mambo ya watu wakuu wakiwa bado wachanga.

Alex:           Ni ukweli. Kwa sasa ukiwaona, huwezi kula chakula.

Chris:         Hayo kando, ni nani anayeweza kupinga mwito wa king’ora cha kubadilisha mambo?

Daniella:     Je, kweli tunaweza kulaumu king’ora au ni udhaifu wetu wenyewe unaotupotosha?

Alex:           Lakini kama mgomba unaokulia katika mchanga, tunaweza kutambua makosa yetu na kupata nguvu zaidi.

Chris:         Na tukizungumzia urembo, je, ujuzi si urembo wa hali ya juu unaostahili kutafutwa zaidi ya yote?

Daniella:     Hakika ni hivyo.

Alex:           Lakini kuna umuhimu gani kuwa na mawazo mazuri kama haya na tukashindwa kuyatumia katika jamii?

Chris:         Je, kweli tunaweza kutenganisha nadharia kutoka kwa vitendo, au je, zimeunganishwa kama nyuzi za utepe?

[Wote wanatafakari swali hilo]

Onyesho la pili

(Katika ua la shule baada ya matokeo ya kidato cha sita, Alex, Daniella na Chris wakikaribishwa na walimu pamoja na wanafunzi kwa kufanya vizuri katika mitihani)

Alex:           (kwa msisimko na tabasamu kubwa) Ole, Mungu wanguuuu!! Jmaani! Tulikipiga kabisaaa! Sote tumepata pointi 20 chini ya 20!

Daniella:     (kwa kupiga kelele ya furaha) Ahhh! Siwezi kuamini! Tulifanya kazi kwa bidii kwa hili jamani!

Chris:         (anacheka kwa futaha) Jitihada zafua dafu jamani! Sisi ni tishio mara tatu la ufanisi!

Alex:           (akitabasamu tena) Tunapaswa kusherehekea! Nani yuko huru leo twende tunywe chupa ya maji?

Daniella:     Ni mimi! Twende kwenye mkahawa huo mpya ambao umefunguliwa hivi punde katikati mwa jiji la Kira.

Chris:         Na kisha tunaweza kupiga kilabu na kucheza mziki usiku kucha!

Alex:           (kwa mzaha) Na labda hata upate ice cream ili uiongeze kwa maji!

Daniella:     (akicheka) Wewe na uchu wako wa ice cream, Alex!

Chris:         Jamani tunastahili, walahi!

[Wote wanakumbatiana na kuanza kupanga mipango yao ya siku]

Alex:           Leo itakuwa siku ya shamra shamra! Tutasherehekea kama mabingwa!

Daniella:     (akitabasamu) Kwa sababu sisi ni mabingwa! Tumeshinda S6!

Chris:         (anacheka) Na sasa tuko tayari kwenda chuo kikuu!

[Wote wanashangilia na wanaendelea kupangia siku yao na wezao]

Onyesho la tatu

(Ndani ya mkahawa mmoja jijini Kampala, Alex, Daniella na Chris wamekutana kuzungumzia nafasi za kujiunga vyuo vikuu)

Daniella:     (Kwa msisimko) Ee Mungu wangu, siwezi kuamini nilipata ufadhili wa masomo katika Chuo Kikuu cha Makerere! Jamani kozi yangu ya ualimu ilikubaliwa na sasa nimeitwa Chuo Kikuu Cha Makerere kusoma shahada yangu.

Alex:           Inashangaza kabisaa, Daniella! Hongera! Hongera! Umejitahidi sana kwa hili.

Daniella:     Asante, Alex! Bado ninashangaa kwa hili. Na wewe vipi? Unaelekea wapi?

Alex:           Na mimi siwezi kuamini ndugu yangu. Nimepata ufadhili Chuo Kikuu cha Gulu kwa shahada ya uhandisi! Nimefurahi sana kuanza sura hii mpya. Nimesikia mambo mazuri kuhusu programu zao.

Daniella:     Wow, hiyo ni kozi nzuri! Utafanya mambo ya ajabu Alex ninajua. Utabadilisha jamii kwa ujuzi wako wa uhandisi!

Alex:           (anacheka) Nina matumaini! Na Chris, vipi kuhusu wewe? Unaenda wapi? Naona furaha imekuzidi ni kama ya mchinjaji wa kondoo, twambie basi.

Chris:         (anaonesha tabasamu na furaha) Nimepata ufadhili katika Chuo Kikuu cha Bishop Stuart kwa shahada ya uanahabri na mawasiliano! Nani alijua tutaishia katika vyuo vikuu tofauti? Mungu ni mwema kabisaa….

Daniella:     Maisha yanageuka jamani. Ni sisi hakuna wengine. Lakini tutafanya kazi ninaamini. Tutawasiliana na kusaidiana wakati wote hata kama tuko katika vyuo tofauti.

Alex:           Kweli kabisa. Tuko pamoja katika kila kitu. Tutahakikisha kuwa tumepanga zoom meeting mara kwa mara ili kusaidiana kuhusu maisha yetu.

Chris:         Sawa. Na ni nani anayejua, labda siku moja tutafanya kazi pamoja kwenye mradi ambao unabadilisha ulimwengu!

Daniella:     Hakuna! Ni Mungu tu! Tunaweza kuanzisha shirika lisilo la faida au kuanzisha miradi inayosaidia nchi yetu. Pia, tumeshuhudia uongozi mbaya kwa karne nyingi, huenda Rais wa miaka ya mbele yuko miongoni mwetu.

Alex:           Uwezekano hauna mwisho. Lakini kwa sasa, tuzingatie tu maisha ya chuo kikuu na tuombe tufanikiwe vizuri.

[Wote wanashiriki katika maombi na kuaagana]

Onyesho la 4: Mtandaoni

(Daniella, Alex na Chris wako kwenye mkutano wa Zoom wakiongea kuhusu maisha yao)

Daniella:     (akiwa mwenyekiti wa mkutano) Ndugu zangu natumai mko salama? Naomba niwasimulie ufanisi wangu huku chuoni. Lo! nilipata mkutano wa kushangaza zaidi na Profesa Nakku mtaalam mkuu wa sayansi na mazingira! Alinishauri na kunitambulisha kwa watu wengine katika mkutano uliokuwepo hapa chuoni Makerere.

Alex:           (kwa shukrani) Hongera sana Daniella. Hiyo ni achievement , Daniella! Nilipata uzoefu kama huo kwenye maonyesho ya kazi wiki iliyopita. Nilikutana na mtu kutoka kampuni ya ndoto yangu, na akanipa mafunzo mengi zaidi kuhusu kazi ya uhandisi!

Chris:         Na hivi punde tu mimi nimemhoji mwanahabari mashuhuri, Zambaali Burasio Mukasa kwa gazeti letu la chuo kikuu! Alitoa maarifa mengi juu ya uandishi wa habari za uchunguzi. Nilifaidika sana.

Daniella:     (kwa udadisi) Wow, Alex, kazi inahusu nini? Utakuwa unafanya nini?

Alex:           Nitafanya kazi kwenye miradi ya nishati, kubuni na kutekeleza mifumo ya nishati mbadala. Hiyo ndiyo ilikuwa ndota yangu kutoka zamani.

Chris:         (alivutiwa) Hiyo ni nzuri! Na Daniella, inakuwaje kufanya kazi na Profesa Nakku?

Daniella:     Utaalam wake na mapenzi yake kwa sayansi ya mazingira ni ya muhimu kwangu. Tayari amenitambulisha kwa fursa kadhaa za utafiti.

Alex:           Nyie mnanitia motisha ndugu zangu! Nani anajua fursa zingine huko nje?

Chris:         Sawa! Tunapaswa kuhudhuria mkutano wa Rais Museveni alioita kukutana na wanachuo mtandaoni ili tujifunze mengi.

Daniella: (akikubali) Kweli kabisa!

Chris:         Jamani!  Nimepokea tu barua pepe kutoka kwa Zambaali Burasio Mukasa mwanahabari niliyemhoji. Anataka nifanye naye kazi katika kampuni yake ya Next media hata kama sijamaliza kusoma. Hii ni fursa ndugu zangu….

Alex:           Wow, Chris, hiyo ni fursa kabisaa! Kweli umejitengenezea jina katika ulimwengu wa uandishi wa habari.

Daniella:     Hongera sana ndugu Chris. Na la kushangaza zaidi, sasa hivi pia nimepokea email kutoka chuo kikuu cha Havard ili niende kuwasilisha utafiti wangu kwenye Kongamano la wanazuoni. Visa na kila kitu kimefadhiliwa! Naona Profesa Nakku amenitumia ujumbe wa Whatsap eti naye atakuwepo pia!

Alex:           Hongera sana jamani! Mungu hamsahau mja wake kiukweli. Mnanitia moyo kufanya kazi kwa bidii zaidi.

Chris:         Hivyo ndivyo marafiki walivyo, Alex. Tuko pamoja katika hili.

Daniella:     Kweli kabisa. Tunapaswa kuanzisha blogi au chaneli ya YouTube pamoja ili tutangaze uzoefu wetu na hdahira pana zaidi.

Alex:           Hilo ni wazo zuri, Daniella!

Chris:         Naipenda.

[Wote wanaanza kuchangia mawazo kwa blogu yao na chaneli ya YouTube]

Onyesho la  tano

(Mwaka Mmoja Baadaye. Danella, Alex na Chris amekutana katika hoteli kuu ya Serena jijini Kampala)

Daniella:     Je, mnaweza kuamini kuwa ni mwaka mmoja umepita tangu tuhitimu? Naipenda kazi yangu katika kampuni ya ushauri wa mazingira. Malipo ni makubwa na imesaidia kuleta mabadiliko katika maisha yangu.

Alex:           Najua kabisa? Hata wa kwenu nyumbani sasa wameanza kufurahia.  Ninafanya kazi kama mhandisi mkuu katika kampuni ya juu na mshahara wangu ni mzuri. Ninaishi ndoto yangu!

Chris:         Ndugu zangu nimeongezewa unga kazini. Sasa mimi ni meneja wa kampuni ya Next media. Nilijaribu kufanya kazi yangu hai kwa kuandika yanayofaidi nchi.

Daniella:     This is good! Chris! Sote tunafanya vizuri sana.

Alex:           Tulijitahidi kwa hili. Tunastahili.

Chris:         Na bado hatujamaliza. Tuna mengi zaidi ya kufikia.

Daniella:     Kweli kabisa. Tuendelee kujitutumua tuone maisha yanatupeleka wapi.

Alex:           Hongereni nyote!

[Wote wanagonganisha glasi zao pamoja za vinywaji wakifurahia mafanikio yao]

Daniella:     (kwa udadisi) Kwa hiyo, ni nini kinachofuata kwetu? Kuna mipango mikubwa?

Alex:           Ninafikiria kuanzisha kampuni yangu ya uhandisi. Vipi kuhusu wewe, Chris?

Chris:         Ninafikiria kuanzisha kampuni yangu mwenyewe pia. Nimeishakusanya hela.  Na wewe, Daniella?

Daniella:     Ninafikiria kuanzisha shirika lisilo la faida linalozingatia elimu ya mazingira. Kwa sasa ninakaribia kumaliza shahada yangu ya uzamili. Ninapanga mwaka kesho niende kwa shahada ya uzamifu (PhD) katika utunzaji wa mazingira.

Alex:           Jambo zuri sana Daniella. Itabidi tusaidiane kila hatua. Utaanza PhD mwaka ujao? Itanibidi nikulipie mwaka mmoja wa shahada yako hiyo kwa sababu uwezo ninao. Naona sote tumefua dafu.  

Onyesho la……

(Katika hoteli kuu ya Pearl of Africa. Daniella na Alex wanarejesha mapenzi yao. Wanapanga ndoa rasmi)

Alex:           (akitabasamu) Unajua, Daniella, nilikuwa nikifikiria tu… hadithi yetu ya mapenzi ilianza tulipokuwa bado shule ya upili.

Daniella:     (anacheka) Hahaha! Najua. Tulikuwa watoto tu wakati huo.

Unakumbuka jinsi tulivyokuwa tukisoma pamoja kwa ajili ya mitihani na kutazamana kwa siri?

Alex:           (akicheka) Ningewezaje kusahau? Nilivutiwa sana na wewe, lakini sikujua jinsi ya kukwambia.

Daniella:     (akitabasamu) Kisha tukaamua kuwa marafiki baada ya Bw Johnson aliyekuwa mshauri wa shule kutusimulia kuhusu madhara ya mapenzi kabla ya ndoa. Lakini urafiki wetu uliendelea kuwa imara tulipoanza kusoma vitabu.

Alex:           Lakini moyoni, siku zote hisia zangu kwako zilizidi urafiki.

Daniella:     Wacha weweee… Huenda.. lakini ilitubidi kungoja hadi wakati ufike.

Alex:           Ilistahili kusubiri, kwa sababu sasa tumekomaa zaidi na tuna hekima zaidi na tayari tuna kazi sote.

Daniella:     Kweli kabisa. Ninashukuru sana kwa safari yetu, haijalishi imetuchukua muda gani kufika hapa?

Alex:           Mimi pia mpenzi wangu. (akatulia na kumshika mkono)

Daniella:     (kwa kudadisi) Kuna nini Alex? (Kwa upole sana na sauti ya chini) Mbona unanishika mkono kwa upole?

Alex:           (Kwa jazba) nilitaka kusema……. tangu nilipokutana na wewe katika shule ya upili, nilijua utakuja kuwa mtu maalum katika maisha yangu. Na sasa ningeomba unikubali nimalize maisha yangu yote na wewe?

Daniella: (Kwa machozi) Ah, Alex …….kweli uko serious?

Alex:           (akitabasamu) Je, utakubali nikuoe Daniella? (anatoa pete mfukoni na kumvalisha)

Daniella:     (akiwa na furaha tele) Ndiyo, ndiyo, ndiyo mara milioni! Nitakuwa mke wako nikuzalie mapacha, nikuoshee nguo na nikupikie chakula kwa sababu umekuwa mvumilivu.

[Wanakumbatiana sana na Chris akishangilia na kupiga makofi chinichini]

Chris:         (akitabasamu) Hongereni nyinyi wawili! Nina furaha kubwa kuwa karibu na nanyi katika safari hii. Tuapngie ndoa rasmi mwezi ujao.

(Pazia)

Leave a comment