UTU NI VITU:

Msanii wa wa nyimbo za kidini Peace Mbabazi aliimba wimbo “TUWE NA UTU” kwasababu utu unazidi vitu ulivyonavyo:

Katika nchi moja ya bara la Afrika palikuwepo Mfalme mmoja ambaye alioa wake wanne Mbabazi, Babirye, Jubeki, na Adoko. Siku moja Mfalme aliugua kiasi kwamba alijiona anakufa, akaogopa upweke huko ahera.

Ilimbidi awaulize wake zake swali moja lakini kila moja kwa wakati tofauti. Alianza na mke wa nne Jubeki ambaye alikuwa anampenda sana, zaidi ya wake zake wengine wote. Mke huyu alikuwa anamununulia vitu vingi na vya thamani sana.

Mfalme alianza:
Mke wangu mpenzi, je nikifa leo uko tayari kufa nami na kufuatana nami ahera?

Jubeki alijibu:
“Samahani, haiwezekani hata kidogo, siwezi kufuatana nawe”, akaondoka zake.

Majibu ya mke wa tatu ambaye ni Adoko hayakuwa tofauti sana na yale ya mke wa nne, kwani alisema:
“Mimi ninayapenda sana maisha yangu, sitaweza kwenda nawe, ila itanipasa niolewe na mtu mwingine”.

Majibu ya mke wa pili ambaye ni Babirye yalikuwa hivi:
“Siwezi kwenda nawe ila nitakuandalia mazishi na nitayasimamia vizuri hadi mwisho, lakini sitafuatana nawe”.

Wakati anamjibu hivyo, ilisikika sauti ikisema:
“Nitaishi nawe milele katika raha na shida, hata kama ni maisha baada ya kufa”.

Mfalme aligundua kuwa aliyekuwa anaongea ni mke wake wa kwanza Mbabazi ambaye alikuwa hamjali wala kumtunza wakati akiwa na nguvu zake. Baada ya kutambua makosa yake, Mfalme alimwomba mke wake wa kwanza msamaha kwa kutomjali wala kumtunza kwa muda wote alioishi naye.

Mazungumzo haya yanatufundisha kuwa, kila binadamu ana wake wanne. Mke wa nne ni MWILI ambao huwa tunaugharamia na kuupamba kwa vitu vya thamani na nguo za gharama kubwa lakini baada ya kufa hatufuatani na mwili huo.

Mke wa tatu ni MALI zetu ambazo tunajikusanyia kwa wingi lakini siku ya mwisho hatuwezi kufuatana nazo. Mali zote huwa zinaachwa na kugawiwa kwa ndugu wanaobaki. Hii ni sawasawa na mke wa tatu alivyosema kuwa ataolewana mtu mwingine.

Mke wa pili anafananishwa na marafiki na familia zetu. Hawa watu huwa tunawathamini, tunawaamini na kuwapenda sana lakini nao pia hawawezi kwenda nasi zaidi ya kufika makaburini.

Mke wa kwanza ni ROHO YA UTU wetu ambao mara nyingi hatutilii maanani wala kuujali. Roho ya utu ndio pekee ambayo itatufuata hata baada ya kufa. Ndugu zangu tupiganie utu kwasababu utu ni vitu. Kudharau, kukejeli, umbeya, Kiu, uchawi na ulozi ni vya Nini?

Kwa hiyo tunapaswa kuijali miili yetu ili iwe na afya njema, kufurahia na kufaidi mali zetu tungali hai. Hali kadhalika, tuwathamini na kuwafurahia marafiki na familia zetu kwa upendo wanaotupa. Pamoja na hayo yote tukumbuke pia kutunza roho zetu kwa sababu roho ni chanzo cha maisha yetu na rafiki mwaminifu na wa ukweli. Utu ni vitu.

Hata hivyo kuwa na marafiki wengi si hoja, hoja ni kuweza kuwachambua na kuwamudu. Hapa duniani tunapita na kila moja ataenda peke yake siku zake zikifika.

Usipiganie vitu ambavyo huenda ukakosa UTU

4 thoughts on “UTU NI VITU:

Leave a comment