RAFIKI WA KWELI NI NANI?
Katika nchi moja ya ughaibuni alitokea Mfalme mmoja ambaye alioa wake wanne. Siku moja Mfalme aliugua kiasi kwamba alijiona anakufa, akaogopa upweke huko ahera.
Ilimbidi awaulize wake zake swali moja lakini kila moja kwa wakati tofauti. Alianza na mke wa nne ambaye alikuwa anampenda sana, zaidi ya wake zake wengine wote. Mke huyu alikuwa anamununulia vitu vingi na vya thamani sana.
Mfalme alianza:
Mke wangu mpenzi, je nikifa leo uko tayari kufa nami na kufuatana nami ahera?
Mke wa nne alijibu:
“Samahani, haiwezekani hata kidogo, siwezi kufuatana nawe”, akaondoka zake.
Majibu ya mke wa tatu hayakuwa tofauti sana na yale ya mke wa nne, kwani alisema:
“Mimi ninayapenda sana maisha yangu, sitaweza kwenda nawe, ila itanipasa niolewe na mtu mwingine”.
Majibu ya mke wa pili yalikuwa hivi:
“Siwezi kwenda nawe ila nitakuandalia mazishi na nitayasimamia vizuri hadi mwisho, lakini sitafuatana nawe”.
Wakati anamjibu hivyo, ilisikika sauti ikisema:
“Nitaishi nawe milele katika raha na shida, hata kama ni maisha baada ya kufa”.
Mfalme aligundua kuwa aliyekuwa anaongea ni mke wake wa kwanza ambaye alikuwa hamjali wala kumtunza wakati akiwa na nguvu zake. Baada ya kutambua makosa yake, Mfalme alimwomba mke wake wa kwanza msamaha kwa kutomjali wala kumtunza kwa muda wote alioishi naye.
Mazungumzo haya yanatufundisha kuwa, kila binadamu ana wake wanne. Mke wa nne ni MWILI ambao huwa tunaugharamia na kuupamba kwa vitu vya thamani na nguo za gharama kubwa lakini baada ya kufa hatufuatani na mwili huo.
Mke wa tatu ni MALI zetu ambazo tunajikusanyia kwa wingi lakini siku ya mwisho hatuwezi kufuatana nazo. Mali zote huwa zinaachwa na kugawiwa kwa ndugu wanaobaki. Hii ni sawasawa na mke wa tatu alivyosema kuwa ataolewana mtu mwingine.
Mke wa pili anafananishwa na marafiki na familia zetu. Hawa watu huwa tunawathamini, tunawaamini na kuwapenda sana lakini nao pia hawawezi kwenda nasi zaidi ya kufika makaburini.
Mke wa kwanza ni ROHO zetu ambazo mara nyingi hatuzitilii maanani wala kuzijali. Roho ndizo pekee ambazo zitatufuata hata baada ya kufa. Ndugu zangu tupiganie utu kwasababu utu ni vitu. Kudharau, kukejeli, umbeya, Kiu, uchawi na ulozi ni vya Nini?
Kwa hiyo tunaaswa kuijali miili yetu ili iwe na afya njema, kufurahia na kufaidi mali zetu tungali hai. Hali kadhalika, tuwathamini na kuwafurahia marafiki na familia zetu kwa upendo wanaotupa. Pamoja na hayo yote tukumbuke pia kutunza roho zetu kwa sababu roho ni chanzo cha maisha yetu na rafiki mwaminifu na wa ukweli. Utu ni vitu.
Hata hivyo kuwa na marafiki wengi si hoja, hoja ni kuweza kuwachambua na kuwamudu. Hapa duniani tunapita na kila moja
ataenda peke yake siku zake zikifika.
MTAFUTA YOTE HUKOSA YOTE
Watu wasio na msimamo thabiti wa maisha ni watu walio na tamaa, watu wanaopenda kushiriki katika mambo ambayo ni makubwa kupita uwezo wao huishia pabaya kwa sababu ya tamaa. Watu hawa hupenda kushika hiki mara kile bila mafanikio. Tuchukue mfano wa vijana wanaotafuta ajira kwenye makampuni ama mashirika fulani. Akienda huku anaona hakufai, akienda kule anaona hakufai, badala ya kutulia mahali pamoja na kuangalia ataendeleaje mahali hapo anarukia sehemu nyingine. Huko kuruka ruka kwake kunamsababishia mwisho wa siku kukosa sehemu zote. Katika maisha yatupasa kuwa na subira, tamaa ni mbaya, pupa ni mbaya. Tuzingatie mambo tunayoyafanya na kufanya maamuzi ya busara ili mwisho wa siku tusikose yote.
ASIYESIKIA LA MKUU HUVUNJIKA MGUU
Yeyote asiyesikia analoambiwa na wakubwa wake huishia pabaya. Mtoto mmoja tangu akiwa mdogo alianza tabia ya udokozi akiwa nyumbani kwao. Wazazi walimkanya lakini hakusikia. Aliendelea na tabia hiyo ya wizi kwa majirani na shuleni, alikanywa na waalimu wake, napo pia hakusikia. Alipomaliza darasa la saba alifaulu lakini akachagua kuendelea na tabia yake ya wizi. Aliamua kujiunga na makundi mabaya, makundi ya majambazi wenye uzoefu jijini Kampala. Siku moja walienda kuiba benki, kwa bahati mbaya yule kijana alipigwa risasi na kufariki pale pale, wenzake wazoefu walitoroka. Wazazi wake walisikitika sana kumkosa mtoto wao. Lakini wana jamii walisikika wakisema ama kweli sikio la kufa halisikii. Endapo angewasikiliza wazazi na wote waliomkanya tangu utoto wake, haya yote yasingemkuta. Kwa upande wa jamii na taifa, kazi ikipotea kwenye nyanja za kielimu, kiuchumi na kisiasa., jiajiri mwenyewe. Kisa hiki kina funzo kubwa kwa vijana wetu. Yawapasa wawe wasikivu, wazingatie yale wanayoaswa na wakubwa zao kwani “asiyesikia la mkuu huvunjika mguu”.
KIKULACHO KINGUONI MWAKO.
Maranyingi binadamu huathiriwa na binadamu mwenzake. Matatizo tuyapatayo katika maisha huweza kusababishwa na watu tunaoishi nao kwa karibu. Ni watu ambao tunawaini sana na hata kuwashirikisha yale ya moyoni. Watu hawa huweza kutumia taarifa/siri zetu kama fimbo ya kutuchapia. Hii ina maana kuwa yatupasa kuwa waangalifu kwenye mahusiano yetu mbali mbali. Kumbuka, mara nyingi, adui yako ni yule yule anayekujua sana, aliyekuzoea sana na anayekula pamoja nawe.
UKIINULIWA TULIZANA
Pakitokea panya mmoja kwenye kijiji jirani jijini Mbale. Panya huyo alimeza kipande cha dhahabu cha mwenye nyumba ya jirani. Mwenye nyumba hiyo alipogundua kuwa dhahabu yake ilikuwa imemezwa na panya aliamua kumtafuta mwindaji ili amtafutie yule panya na kumuua ili aipate dhahabu yake. Kitendo hicho cha mwindaji kumtafuta panya kiliwashangaza sana wanakijiji kwa sababu panya walikuwa wengi pale kijijini kwao na walikuwa wanaishi kwenye mkusanyiko na hivyo kuwa pamoja daima. Walijiuliza, mwindaji atamtambuaje huyo panya? Lakini katika hali isiyo ya kawaida alitokea panya moja ambaye alianza tabia ya kujitenga tenga na panya wenzie.
Hivyo mwindaji alipofika wala hakupata shida kabisa kwani moja kwa moja alimlenga yule panya ambaye alikuwa hachangamani na wenzie. Mwindaji na mwenye nyumba walimpasua yule panya na kweli wakakuta kile kipande cha dhahabu. Mwenye nyumba alishangaa na kufurahi sana.
Hatimaye alimuuliza mwindaji kwamba alijuaje kama ni huyo panya aliyemeza ile dhahabu? Mwindaji alimjibu kiurahisi sana kwa kusema: “wapumbavu wakipata utajiri huwa hawapendi kujishirikisha na wenzao. (When stupid people get rich they don’t mix with others)
Somo lingine la nyongeza na la busara ni kwamba ukifanikiwa au ukibarikiwa kupata utajiri inakupasa uache majivuno ama majigambo. Ni vema ukabaki kama vile ulivyokuwa mwanzo. Utu wako utabakia kuwa wa thamani mbele za watu.
USICHEKE MWENZAKO KWA YALIYOMTOKEA
Binadamu hupitia mambo mengi katika maisha, mambo magumu na mepesi, mazuri na mabaya. Mathalan, mtu anazaliwa akiwa na viungo vya mwili vilivyokamilika, kwa bahati mbaya anapata ajali na kupoteza baadhi ya viungo vyake na kusababisha ulemavu. Tunaaswa kutowadharau au kuwacheka watu kutokana na matatizo waliyoyapata kwani hata sisi yaweza kutupata wakati wowote. Ni kweli kabisa kuwa kabla hujaaga dunia, unakuwa bado hajaumbika. Lolote linaweza kukupata wakati wowote.
Katika maisha ya mwanadamu hapa duniani majivuno na kiburi ni kikwazo cha kukurudisha nyuma kimaendeleo.
Katika nchi moja kulikuwa na mfalme mmoja mwenye maringo na dharau sana, aliwaona watu wake kama sio binadamu. Raia wake walikuwa wanamchukia sana, hata wakamwombea afe. Siku moja alipokuwa anahutubia kwenye mkutano wa wazee alithubutu kusema kuwa yeye hajawahi kuiona njaa na angefurahi sana kama angempata mtu ambaye angeweza kumuonyesha njaa ilipo na inafananaje, kwani huwa anasikia tu kuwa duniani kuna njaa.
Wazee walikasirishwa sana na kauli zake hizo za mara kwa mara. Ndipo mzee mmoja mwenye busara akajitolea na kwenda kumweleza mfalme ya kuwa, yeye yupo tayari kumpeleka na kumwonyesha njaa ilipo, Mfalme alikubali kwenda na huyo mzee ili akaione njaa kwa macho yake.
Mzee yule alitengeneza mikate yake saba na akamwambia mfalme kuwa safari imejiri. Pia alimwambia mfalme asichukue kitu chochote, kwani yeye angechukua kila kitu cha lazima pamoja na chakula kwa ajili ya safari yao. Hali kadhalika, alimwambia kuwa hawatatumia chombo chochote cha usafiri, itawabidi waende kwa miguu, maana huko kwenye njaa hakuendeki na gari, njia pekee ni ya miguu tu.
Siku ya kuondoka ilipowadia, walianza safari alfajiri na mapema. Wakaenda mbali sana na kwa vile mfalme hakuzoea kutembea, ilipofika saa sita akawa amechoka ile mbaya. Njaa nayo ikawa inamuuma sana. Yule mzee akafungua mikate yake na kuanza kula peke yake. Kwa vile njaa haina adabu, Mfalme alimuomba kipande cha mkate lakini yule mzee alimnyima. Kwa kebei alimwambia kuwa yule ambaye anasafiri kwenda kuiona njaa huwa hali chochote. Mfalme alivumilia na baada ya kupumzika waliendelea na safari. Ilipofika jioni, maskini mfalme akashindwa kuendelea na safari na kuomba chakula kwa yule mzee.
Baada ya kumuona mfalme, yule mzee kwa taratibu alimjibu swali lake mfalme ni wapi njaa ilipo. Alimwambia: “hakuna mahali maalumu ambapo ni maskani ya njaa, bali ile anayoihisi ndiyo njaa yenyewe”. Aliendelea kwa kusema: “njaa inamfanya mtu yeyote asiwe na nguvu”. Hivyo yule mzee alimsihi mfalme aweke ahadi kama hatarudia tena vitendo vyake vya majivuno na dharau kwa watu. Asipofanya hivyo kwa kuweka nadhiri yule mzee
atamwacha palepale ili afe kwa njaa. Kutokana na alivyokuwa anajisikia mfalme, wosia wa mzee huyu ulimfanya atii na kuufuata. Mfalme aliapa kwa Mungu kuwa hatarudia tena kuringa, kudharau na kukufuru kama alivyokuwa amezoea.
Hapa tunajifunza mengi nayo ni:
- Kama umejaliwa kuwa na utajiri, yakupasa umshukuru Mungu, usiwadharau wale ambao hawana.
- Usitumie madaraka uliyopewa kwa ajili ya kuwanyanyasa wengine.
- Tuwe na unyenyekevu kwa kila mtu ili siku tutakapopata matatizo wawepo wa kutusaidia..
Hadithi hii inafanana na msemo huu: ‘Adui yako muombee njaa’.
Hapa tumeona pamoja na madaraka aliyokuwa nayo mfalme njaa ilimfundisha kuwa na adabu na utu na hatimaye kuacha majivuno.
