MIONGOZO YA TAMTHILIA MBILI=KIJIBA CHA MOYO NA MFALME EDIPODE-Timothy Arege na Sofokile.

KIJIBA CHA MOYO-TIMOTHY .M. AREGE.

Tamthilia ya kijiba cha moyo iliandikwa na Timothy M.Arege ambaye ni mwandishi mtajika wa lugha na fasihi ya kiswahili. Timothy ni mhadhiri katika chuo kikuu katoliki cha Afrika mashariki nchini Kenya.

Timothy aliandika tamthilia nyingine zikiwemo chamchela, Mstahiki meya na nyinginezo.

WACHAMBUZI

Johnpaul Arigumaho

na

Simon T Kawaida.

Utangulizi.

Moyo hupenda, moyo huchukia, moyo hukinai, moyo huhurumia, lakini moyo unapopatwa na dhiki ni rahisi kujua unaponzwa na nini.”

Tamthilia ya kijiba cha moyo ni tamthilia inayoangazia maisha ya Sele kudhaniwa kuwa mgonjwa, kunyimwa haki zake, na kutotetewa kwa namna yeyote anapopambana na waiotaka kuiba moyo wake halafu akabaki na kijiba.

Sele ni kijana ambaye amebadilika kitabia katika familia, moyo wake umepatwa na kutu, familia yake imekosa kupata utulivu kwa kughasiwa na ugonjwa wake. Sele kila tendo analiona kuwa ni uonevu , sele ana kijiba cha moyo. Je mawaidha ya bibi yatautibu ugonjwa wa Sele?

Dhamira ya mwandishi

Timothy ananuia kutuonyesha uongozi wa kiimla uliotapakaa katika nchi nyingi za bara la Afrika na kukita mizizi pale.

Tamthilia hii ni miongoni mwa kazi za kifasihi zinazo chunguza uhusiano uliopo baina ya ubepari wa mataifa na hali duni ya kiuchumi iliyojiri mataifa ya ulimwengu wa tatu kwa mtindo wa kinaya.

Mwandishi anatalii maudhui ya kiuchumi na mfumo wa kibepari ambao licha ya kuwakandamiza wakazi wa mabara ya Afrika unapunguza nafsi za wafanyikazi na kuwafanya kujihisi kuwa duni. Mahusiano haya yameendelezwa kwenye misingi ya udhalimu.

Mwandishi ameelezea maonevu haya kwa kinaya akitumia sitiari pevu ili kukejeli mfumo mzima wa uelewaji wa dhana ya uhuru katika uzalishaji mali.
Katika tamthilia hii mwandishi pia analenga kutuonyesha kuwa uongozi uliopata mashiko yake kwenye mfumo wa kibepari, umemiliki nyenzo za kimsingi za uzalishaji mali kupitia kwa ufisadi, uongo na zaidi katika kuwakandamiza wale waliopata mwangaza wa kuona njama hii ya kunyanyaswa.

Hili hutekelezwa ili kuzuia juhudi za wale waliopata mwamko mpya kisiasa dhidi ya kuwazindua wanyonge wengine katika jamii. Mwandishi kupitia kwa mhusika nguli (Sele), anasawiri uhusiano uliopo baina ya mataifa ya ulimwengu wa kwanza ambayo huyapa misaada na kuyamiliki mataifa ya ulimwengu wa tatu kwa kuyafanya yakose kujitegemea.

Mwandishi anasawiri kwa kina misaada inayotolewa kwa mataifa machanga na kuonyesha kuwa misaada hii haiwafai Waafrika ila tu ni chombo kinachotumiwa ili kuweza kupata fursa ya kuwanyonya Waafrika rasilimali zao.

Hii ni kinaya kwa kuwa Waafrika wenyewe hawaelewi hali hii.

Arege analenga kutuonyesha kuwa hali ya uhitaji katika mataifa mengi ya bara la Afrika imesababishwa na unyonyaji wa nguvu za wakazi wake kwa malipo duni.

Anaeleza kuwa mipango ya kuyasukuma mbele kimaendeleo mataifa machanga barani Afrika ambayo inaamuliwa na kuwekwa na mataifa yanayodai kujitegemea ni chanzo cha kudorora kwa maendeleo yanayotarajiwa. Hii inatokana na ukweli kwamba walioshikilia (wakoloni)
nguzo za mfumo huu wa kibepari waliwafumba macho wakazi wa nchi changa kwa kuwapa misaada isiyowafaa.

Falsafa ya mwandishi

Mwandishi ameongozwa na falsafa ya “UJinga ni Ugonjwa“Nchi zenye nguvu zinatumia aina zote za kutoa misaada ili kumiliki rasilimali za mataifa aina ya tatu juu ya ujinga na kutoelewa kinachofaa kufanywa. Hili linachorwa vizuri na mhusika sele alipojitoa kupigania haki wengine wakafikiri ni mgonjwa(ujinga).

Mtazamo wa mwandishi

Mwandishi ameegemea Mtazamo wa kisiasa yaani kiyakinifu; Kuungana, kujitahidi na kujikomboa kimawazo ni suala liwezalo kusaidia waafrika
kujiendeleza kwa misingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Hiki kinabainika baada ya kutamatisha kusoma tamthilia hii ambapo inabainika kuwa ugonjwa wa Sele si ule wa kawaida kama ulivyochukuliwa na wahusika tamthiliani bali kuzinduka kutokana na mwamko mpya wa kisiasa na kijamii.

Msimamo wa mwandishi. katika tamthilia ya kijiba cha moyo mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani amejadili matatizo yanayochangia kukwama kwa ujenzi wa jamii mpya.

Msimamo wake umebainishwa kutokana na jinsi alivyochora mhusika Sele, akijaribu kujiokoa na kujikomboa kimawazo wengine wakifikiri ni mgonjwa lakini akakosa kupata washabiki werevu. (kijiba)

Wahusika katika tamthilia ya kijiba cha moyo

Wahusika ni viumbe wa kisanaa wanaopatikana katika kazi ya fasihi na wenye sifa za kibinadamu. Aghalabu huwa na sifa za kimaadili, kitabia, kiitikadi, kifalsafa ambazo hutambulishwa na wanayoyasema (mazungumzo) na wanayoyatenda (matendo), Wamitila (2002).

  1. Sele- mumewe Aisha na mtotowe Musa na Zainabu. Sele kulingana na tamthilia ana sifa zifuatazo;
  2. Ni mdadisi: katika Kijiba cha Moyo tunaweza kusema Sele ni
    mdadisi kutokana na tabia yake ya kuuliza maswali mengi. Alimdadisi daktari alipokwenda hospitalini pia tunajuzwa kuwa Sele alimuuliza daktari maswali mengi alipokuja kwao kumtibu. Kwa mfano:
    Sele: Naelewa lakini nipe nafasi kuuliza swali
    kabla ya kuanza.
    Daktari: (Hana stahamala tena.) Sitaki maswali yako
    mengi. Siku ile nyingine umeniuliza maswali
    mengi ya kunipotezea muda. Mimi ndiye
    daktari; nakuuliza maswali wajibu. (Kimya)
    wewe ni wa kujibu, Sasa wewe unataka
    kunihoji
    .
  3. Hili tendo linadhihirisha udadisi wa mhusika Sele.
  4. Sele, Ni mwenye kughasiwa na ugonjwa wa moyo.Sele ni mgonjwa kutokana na mavazi ya wagonjwa aliyovaa na daktari si mgonjwa bali ni daktari kwa sababu amevaa sare za kazi na glovu tayari kutibu wagonjwa.(uk 52)
  5.  Ni mtetezi wa wanyonge. Sele anaonekana katika tamthilia kama mtetezi wa wanyonge wakati aliposema „vinavyoliwa huku vinatazama‟ inamaanisha vidagaa ni wanyonge hawawezi kujitetea.
  6. Hivyo basi anapinga tendo la papa la kuwala vidagaa; kwa kutokula vidagaa yeye mwenyewe. Hapa huwa anawaonea huruma na kutetea haki zao.
  7. Ni mwenye hasira. Sele amesawiriwa kama mwenye hasira na
    asiyependa kusumbuliwa.

Haya yamedhihirika kupitia namna anavyoongea kwa
ukali kama ifuatavyo:
Sele: (Kwa sauti ya juu.) Wewe umejua kama
mimi sitaki mtu kunisumbua halafu unanijia
kwa fujo. Dharau tu!
(uk.33) mazunmzo yake yalionyesha hasira na ukali.

  • Ni mwenye kujichukia. Tunamuona Sele jinsi anavyochukia maumbile yake katika tamthilia. Hivyo kumfanya kujichukia. Chuki hii ndiyo chanzo cha ndwele yake na ndicho kijiba chake cha moyo. Chuki hii ya Sele inaashiria jinsi mataifa yanayoendelea yanavyokosa kujithamini.(uk33-34)
  •  
  • Ni mwenye sura ya kupendeza. Sele kama kijana mwenye sura
    ya kupendeza yenye pua laini iliyochongeka vizuri na midomo mikubwa. Vilevile ana mataga na weusi uliokoza na kukolea. (Uk 43)
  •  
  • .Ni mkaidi. Tunamuona Sele anakaidi mashauri ya jamaa zake na pia anakaidi kumeza dawa kwamba yeye si mgonjwa.
  • Aisha-mkewe Sele.
  • Ni mwenye kupenda raha.  Hili linadhihirishwa pale alimomwambia mumewe kwamba waende kujistarehe (uk 03)
  • Ni mwenye mapenzi na kumjali mume wake. Hili linadhirika anapoingia chumba walimo wazee wake na kuwapuuza akienda mbio kutafuta vitabu kuvisoma ili aelewe ugonjwa wa mume wake ili aweze kumsaidia.(uk20)
  • Ni msomi. Amesawiriwa kama msomi. Sifa hii inadhihirika kupitia tabia
    yake ya kusomasoma vitabu. Hili linadhihirika kupitia mazungumzo baina ya Aisha,
    Zainabu na Bi. Rahma(uk18)
  • Ni mwenye heshima. Heshima ya Aisha inadhihirika pale anapowheshimu wazee wake kwa kutowaita majina.
  • Zainabu-mamake Sele na mkewe Musa.
  • Ni mwenye kumjali mwanawe Sele. Zaiabu tunamuona anatembea juu chini akimtafutia dawa la kumtibu mwanawe. Tena mwenye hamu kusikiliza muuguzi Jamila wakati alipokuwa anamtibu kwake nyumbani (uk88)
  • Ni mvumilivu kwani tunamuona katika tamthilia nzima anavumilia na ugonjwa wa mtotowe hata ingawa alimtusi wakati mwingine.
  • Ni mwenye matumaini kuwa mtoto wake atapona ugonjwa wa moyo.
  • Jamila-Bintiye Hassan
  • Ni msomi. Jamila anadhihirika kama msomi na kupitia maelezo yake
    tunaweza hatimaye kuufahamu ugonjwa wa Sele.(uk90)
  • Ni muuguzi Aliyemuugua sele.
  • Alisoma na Sele . Hili linathibitishwa kwenye (uk88) wakati zinabu na Bi:Ramhma walipokuwa wanamgojea Jamila na Bi Rahma akasema “watu waliosoma pamoja hawakosi kupatana”
  • Daktari.
  • Ni mkatili kwani tunamuona katika tamthilia ndiye aliongoza waliomtembelea sele na kumpekuapekua alipokuwa amelala. Pia alimkataa kuuliza maswali kuhusu ugonwa wake Sele.
  • Ni msomi kwani ni daktari kiutaalamu.
  • Amri-Babu yake Sele.
  • Ni mwenye mapenzi hasa Kwa Sele juu ya ugonjwa wake.
  • Ni mwenye mapenzi hasa Kwa Sele juu ya ugonjwa wake.
  • Musa-Babake Sele.
  • Hajali kuhusu ugonjwa wa sele.

MAUDHUI YALIYOMO

Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo.

  • Ubepari.

Ni mfumo wa kiuchumi unaowezesha watu wachache kumiliki rasilimali na njia kuu za uchumi wa nchi kwamfano Madaktari watatu waliomjia Sele wakati alipolala kitandani na kumpekuapekua hudhihirisha ubepari.

 Mwandishi kupitia mhusika Sele anasawiri uhusiano uliopo baina ya mataifa ya ulimwengu wa kwanza (viongozi) ambayo huyapa mataifa ya ulimwengu wa tatu misaada isiyofaa kv matibabu ya Sele, ila tu ni chombo cha kupata fursa ya kugawanya rasilimali zao.

  • Ugonjwa/Magonjwa.

Ni kuwa katika hali ya kusababishiwa hali mbaya kwamfano Sele anaoekana akivaa sare za wagonjwa na Daktari kavaa sare za udaktari maanake kuna mgonjwa na mtibu. Pia tunamuona Sele ni mgonjwa wa moyo, Jamila anathibitisha kwenda kwake hospitalini anapotoka kumhudumia (uk 88). Muuguzi jamila pia anaeleza kwamba ugonjwa wa sele haujafikia kiwango cha kutisha (uk89).

  • Elimu.

Ni mfumo wa mafunzo yanayopatikana shuleni, vyuoni, au katika maisha. Jamila ni msomi kwani ni muuguzi aliyemhudumia sele. Mazungmzo ya Zinabu na Bi Rahma kwamba Sele na Jamila walisoma pamoja unadhihirisha usomi wake.(uk 88)

  • Mapenzi.

 Ni hali ya kuingiwa moyoni kuthamini mtu au kitu zaidi ya mwingine au kingine. Aisha anamoenda sana mumewe Sele ndiposa anaingia chumba walimo wazee wake na kuwaluuza akitafuta vitabu akikusudi kusoma ili aelewe ugonjwa wa Sele aweze kumsaidia(uk18)

  • Mabadiliko. Ni hali ya kubadilika kutoka hali moja kwenda hali nyingine.

Sele tunaona alibadilika baada ya kugundua kwamba anagandamizwa lakini wengine hawakumuelewa ili wamtolee msaada ya kujikomboa na kuwatetea wanyonge -mambo hayakufaulu.

  • Ukoloni.  Ni hali unapokuta nchi moja inatawaliwa na nchi nyingiine.

Tendo la madaktari kumzungukazunguka na kumpekuapekua Sele mara wakishauriana na kumuashiria kisha kusema kwa pamoja “bado amelala” kinaashiria wakolni walivyokuja bara la Afrika wakachunguza rasilimali, na wakaona bado waafrika wamelaala na ndipo kuamua kutwaa rasilimali hizo. (Uk79)

  • Unyanyasaji.  Ni hali ya kudharau mtu kwa kiburi au kwa kujiona bora dhidi yake.

Tendo la madaktari watatu kuja kumpekuapekua huku na kule mwili mzima ni ishara ya kudharau na kumnyanyasa. Tena kunyimwa fursa ya kuuliza daktari na kutopewa habari kuhusu tests zake hospitalini ninishara ya kumnyanyasa kiakili.

  • Ukatili.  Ni hali ya mtu kutokuwa na huruma.       

Ukatili unajitokeza pale daktari anapompiga dawa sele akiwa anajua sele si mgongwa ila  kwa hamu ya kumyakua pesa zake.(uk52-53) “staki kupoteza muda, time is money bwana” ni ishara ya ukatili.

  • Utumwa.

Ni mfumo unaotoa fursa kwa binadamu kumiliki binadamu mwingine kama mali ya Utumwa unadhihirika pale ambapo Sele ananyimwa fursa ya kupata matokea ya habari kuhusu “tests” zake hospitalini (uk60, 61)

  • Utabaka.

 Hi ni hali ya ubaguza wa kiuchumi, kisiasa na kijamii inayotenganisha watu wa hali duni na wale wa hadhi ya juu. Utabaka unadhihirika pale tunapoona Sele anahudumiwa lakini kwa ghari na akasema nipe “deposit yangu”

Ndoa. Ni maafikiano rasmi baina ya mwanamke na mwanamume. Ndoa inashihirika kati ya Sele na Aisha pamoja  Musa na Zainabu.

  • Ukosefu wa nidhamu.

Ukosefu wa nidhamu katika tamthilia ya kijiba cha moyo unaonyeshwa pale Aisha alipoingia chumba waliomo wazee wake na kuwapuuza baada ya kuwasalamia tu na akaingia kwenye chumba kingine akaaanza kutafuta vitabu vya kusoma iki aelewe ugonjwa wa sele. (Uk20)

TAMATHALI ZA USEMI:


Kazi ya fasihi, haihusiani na kuwasilisha mawazo tu, bali kuyawasilisha mawazo hayo kisanaa. Habari au wazo fulani haliwezi kuelezwa au kuwasilishwa kwa wasomaji bila kuzingatia hali ya kuwepo kwa usanii wowote.

Mawasiliano yote ya kisanaa huhitaji kuwasilishwa kwa mbinu za kimvuto, ile njia inayompa raha au ladha tamu msomaji anapojaribu kuufuatilia ujumbe wa mwandishi wa kazi ya fasihi.

 Nakwahivyo, zifuatazo ndizo baadhi ya tamathali za Usemi nilizoweza kuchambua katika tamthilia ya kijiba cha moyo;

  • Tashbihi ni tamathali ya usemi ambapo watu ama vitu viwili au zaidi hulinganishwa au hufananishwa na watu ama vitu vingine.

 Kwa mfano, Sele akielezea umahiri wake katika uogeleaji
anasema: … Kisha nikapumzika juu ya mawimbi kama gogo huku chini yangu maji yakipiga na kutoa povu. (uk. 2)

“Na mimi nahisi kama sisi tunayumbishwa mithili ya miti
msimu wa kipupwe… “(uk. 29)

“Linaweza kuwa dogo na athari zake ziwe kubwa, kama tone la
mafuta ya taa kisimani- huhangaisha mtaa mzima… “(uk. 50)

  • Tashihisi. ni tamathali ya kukipa kitu kisichokuwa na uhai mkamilifu sifa za kitu chenye uhai kinachojitegemea katika mazingira yake.

Katika tamthilia ya Kijiba cha Moyo, Sele anatuchorea taswira ya starehe ya bahari na uzoefu wake katika uogeleaji. Anaeleza:
“…Nikapiga mbizi. Nikapambana na Mawimbi chini kwa chini. Nikayapenya. Nikataka nitokezee huko wanakokaa papa.
Nilipoibuka nilikuwa palee! Mbali huko.
Kisha nikapumzika juu ya mawimbi kama gogo huku chini yangu maji yakipiga kutoa povu. Mimi juu, papa chini. Siku hizo nilitaka
niwe bingwa wa dunia”. (uk. 2)

Mtindo huu pia unajitokeza katika maelezo ya Aisha kuonyesha namna ilivyomwia vigumu katika kutambua ugonjwa anaougua Sele. Anaonyesha kuwa hali hii ni ngumu anaposema:
“…Kama lililotiwa hamira, linafura na kujaa fikirani. Kichwa kinakuwa kizito kama nanga…” (uk. 20)
Jambo limepewa uwezo wa kufura na kujaa na pia kufanya kichwa kuwa kizito.

Hii ni tashhisi ambayo mwandishi ametumia ili kuonyesha namna mchanganyiko wa mawazo ulimpata.

  • Methali ni kifungu cha maneno yanayotumiwa pamoja kisanii, kwa njia ya kufumba na kupigia mfano jambo fulani.

Tamthilia ya Kijiba cha Moyo imetawaliwa na methali mbalimbali kwa nia ya mwandishi ya kukuza ujumbe wake. Bi. Rahma analalamikia mapishi ya kisasa na kushuku kuwa huenda ndiyo yanamkosesha Sele hamu ya chakula. Anamwambia Zainabu:
“… Watavilaje vyakula vya kuharakishwa?
Heri huvutwa kwa subira mama. Vyakula
visivyopata kutua sufuria, vipi vitatua
moyoni?” (uk. 14)

Methali anayoitumia Bi. Rahma ina maana kwamba kizazi cha kisasa hakina subira katika kutekeleza majukumu hasa kimapishi.

Mwenye nguvu mpishe (uk 29)

Mchana watasema usiku watalala(uk 34)

Pole pole ndio mwendo (uk26)

Methali nyingine katika tamthilia ni “mhitaji zote ni mtumwa” (uk25).

  • Tabaini ni mtindo wa kiusemi wa kulisisitiza jambo kwa kutumia maneno yanayoelekea kutoonyesha msisitizo huo waziwazi kwamfano; Mwandishi katika kuelezea hali mbalimbali kwa msisitizo wa kitabaini. Aisha anaelezea jinsi muziki unavyoweza
    kutuliza na kuburudisha watu wa umri wowote.

 Katika kuelezea athari hii anasema hivi:
Sina shaka.Viumbe wote hufurahia
muziki; si binadamu, si wanyama,
si miti; ndoo maana hata kizee utakiona
kikitingisha kichwa kwa mlio wa uzi dhaifu
wa gitaa…” (uk. 6)

  • Taswira. Ni hali ya kupiga picha ubongoni ukirejelea tendo fulani.

Katika tamthilia ya Kijiba cha Moyo, mwandishi ametuchorea taswira nzuri Zaidi inayoonyesha uhusiano wa mabepari na wanyonge katika jamii. Sele anamweleza Aisha:
Yapo mengi mengine. Ni kweli papa ana kiburi kikubwa maana yu mfalme wa bahari. Mwili wake una uwezo wa kuzuia mawimbi ya bahari navyo vidagaa hujificha nyuma yake kujisitiri.
Vidagaa vinajua ni hatari lakini afadhali hatari ya papa kuvila badala ya kuangamizwa na mawimbi makali. Wajua ni kama kuku ambaye anakiona kisu cha mchinjaji afadhali kuliko maisha vichakani…” (uk. 37)

  • Takriri ni mtindo wa uneni wa ufasaha ambao msanii hutumia
    kwa maksudi au nia mahususi, hurudia neno, sauti au maneno yale yale ili kutilia mkazo au msisitizo zaidi juu ya jambo asemalo kwamfano

“Alosema kuna uhuru nani? Unajidanganya. Hata katika uhuru wako huo mna utumwa. Kiungo kimojawapo cha uhuru ni utumwa. (uk. 66) Amri anakariri neno „uhuru‟ kwa Sele akitaka kumweleza kuwa hamna uhuru kamili katika dunia hii.

  • Nahau ni fungu la maneno ambayo yakipangwa pamoja huleta maana isiyo ya kawaida ya kuonekana wazi kwamfano

 Sele anaeleza kutoridhika moyoni licha ya kujitahidi kwake. Anamweleza Aisha:
…”Ni kama unanikodolea macho.
Ni kama unanisaili kimyakimya.” (uk. 9)

Bi. Rahma anamweleza Sele kama mtu asiye na matumaini. Anamwambia hivi:
“umekata tamaa kwa kufutwa kazi…” (uk. 28)

  • Mseto au Kuchanganya ndimi. Ni kuweka maneno yasiyo ya kiswahili katika lugha ya kiswahili. Kwamfano Aisha anasema “sisi hatwendi “private beach” twenda “public beach” pia kwenye ukurasa (04) Aisha alitoa kauli ” life savers si wapo lakini” sele anasema “kweli hata mapolice wapo wale mapatrol police“… Sele anasema “… Juzi aliniambia nahitaji plastic surgery (uk35). Mikanjuni secondary (uk59).
  •  
  • Maswali ya balagha. Ni maswali yanayoulizwa na msimulizi au mhusika ambayo hayahitaji majibu kwamfano sele anajiuliza maswali kama “Mimi ni nani ? Nimekuwa wapi? Niko wapi? Ninakwenda wapi? (Uk 96)
  • Uzungumzaji nafsi. Ni pale mhusika anapozungmza mwenyewe bila kukusudi kusikiwa na mtu yeyote, kwamfano(uk96) sele anazugmza mwenyewe anapojiuliza maswali, mimi ni nani? Niko wapi? Nimekuwa wapi? Ninakwenda wapi?

Uthibitisho wa madaKIJIBA CHA MOYO.

Hadithi ya Sele ya madaktari na mganga katika tamthilia ya Kijiba cha moyo ni sitiari ya maisha yalivyo katika ulimwengu wa kihadithi (ulimwengu wa hadithi kuu) ambamo hadithi imeegemezwa.

Daktari mrefu anawakilisha nchi za magharibi (Waingereza), naye daktari mfupi mwenye misuli anawakilisha nchi za mashariki (China), mganga mwenye viguo vilivyoparara na kumbana na kibuyu cha dawa mkononi anawakilisha nchi za bara la Afrika na (Sele) vilevile akiwakilisha nchi ya Kiafrika.


Kule kuja kwa daktari mrefu akifuatiwa na daktari mfupi na nyuma yao wakifuatiwa na mganga wakati Sele amelala inaashiria majio ya wakoloni wakati Waafrika wenyewe hawatambui.

Kujibizana kwa furaha na kukumbatiana na kisha kuzozana kwa madaktari wakiwa karibu na Sele kunaashiria kutoafikiana kwao kuhusu ugawaji wa rasilimali kutoka kwa nchiya Kiafrika (Sele) iliyokuwa bado imelala mbele yao.
Wakati wote huu nchi zingine za Afrika (mganga) zilikuwa kando zikitazama.


Tendo la madaktari la kumzungukazunguka Sele, mara wakishauriana na kumuashiria kisha kusema kwa pamoja, “Bado amelala” na kumpekuapekua kila mahali na walipokosa chochote wakaondoka. (uk.80)


Hiki kinaashiria namna wakoloni walivyokuja bara la Afrika wakachunguza rasilimali zilizoko na wakaona bado Waafrika „wamelala‟ na hivyo kuamua kutwaa rasilimali hiyo ili kujigawia. Sele kuona hivyo akawatapikia moyo wake.

Moyo wa Sele unaweza kuwakilisha madini yanayopatikana ndani ya ardhi. Wakoloni walipopata walichokijia hawakuijali tena nchi ya Kiafrika.

Hadithi ya papa na vidagaa katika Kijiba cha Moyo, imetumika kufafanua maisha halisi yalivyo katika ulimwengu wa kihadithi. Ambapo wenye vyeo na mamlaka wanawagandamiza wanyonge.

Nao wanyonge licha ya kudhulumiwa na wenye vyeo bado wangali wanawategemea hao hao. Tunaelezwa, “…Mwili wake una uwezo wa
kuzuia mawimbi ya bahari navyo vidagaa hujificha nyuma yake kujisitiri. Vidagaa vinajua ni hatari lakini afadhali hatari ya papa kuvila…” (uk.37).

Hali hii ndiyo iliyompelekea Sele kutafakari upya juu ya uhusiano wao na wafadhili wao na hiki ndicho kijiba katika moyo wa Sele.

Nakwahivyo, Kijiba hiki ndicho kinachomfanya kudhaniwa
kwamba yeye ni mgonjwa lakini yeye anafanya juu chini kujiokoa, kujikomboa na kutetea wanyonge wakati wenzake hawatambui na ndio maana wanasema “KIJIBA CHA “MOYO

TAMTHILIA: MFALME EDIPODE

MWANDISHI: SOFOKILE

MWAKA: 1969

MFASIRI: SAMUEL S. MUISHI

Utangulizi:

Mchezo huu wa mfalme edipode uliandikwa na sofokile na kuchapishwa mara ya kwanza mwakani (1969). Lakini imekisiwa kuwa ulitungwa kati ya mwaka 429 na mwaka 420 kabla kristo, na ni mojawapo wa mfululizo wa hadithi zinazohusiana na ufalme wa Thebe huko Ugiriki.

Mchezo huu ulitafsiriwa katika lugha ya Kiswahili na Samuel S. Muishi umetoa mchango mkubwa katika fasihi ya Kiswahili. Ni mchezo wa aina yake wenye muundo wa kishairi na ambao haupangwi kwa maonyesho na vitendo kama ilivyo katika michezo mingine. Yote yaliyomo hutendeka maskani mwa mfalme Edipode.

Uchambuzi wa kichwa cha mchezo:

Kichwa cha mchezo huu ni “Mfalme Edipode”. Mfalme maana yake ni mtawala mwanamume aliyepata nguvu za utawala kwa njia ya urithi au uwezo mwingine kama vile ushujaa. Edipode kulingana na mchezo huu, humaanisha ‘miguu iliyovimba’.

Kwa hivyo, mchezo huu ukapewa kichwa hicho kulingana na yaliyo mtukia Edipode kwanzia pale anapofungwa miguu mpaka ikapata uvimbe, kupelekwa koronto na kurudi kwake ugiriki. Kwa kifupi, unayazunguka maisha yake Edipode tangu utotoni mpaka laana yake inapomfika na kufunuliwa kwake mpaka ikasababisha utoboaji wa macho yake kwa mikono yake mwenyewe.

Uchambuzi wa picha ya jalada:

Jalada la mchezo huu wa mfalme Edipode huonyesha kichwa cha mfalme ambacho kimechorwa kwa rangi nyekundu. Kichwa chenyewe kimetobolewa macho. Kulingana na yaliyomo, picha hii ya jalada huelezea giza analoliishi mfalme edipode kwa kufurahia ndoa na mwili wa mamake bila kujua, kitendo ambacho kinamfanya yeye kujitoboa macho yote mawili kwa kutumia vifungo vya vazi lake dhahabu, ili macho yake yasione tena aibu yake baada ya ukweli kufunuliwa kuwa ndiye najisi muuaji wa Laio babake mfalme wa Thebe na mwoaji wa mama mzazi kama ilivyotabiriwa na Apolo huko Delfi.

Dhamira ya mwandishi/Mtunzi:

Sofokile alidhamiria kuonyesha kuwa la mungu ni la mungu, haliwezi kuepukanwa. Kupitia tamthilia hii, anaonyesha utabiri kuwa mtoto atazaliwa katika nyimba ya mfalme na kuwa mtoto huyo huyo, atamuua babake na amwoe mamake mzazi. Lakini wazazi wa kitoto hicho baada ya kukizaa, wakahofu kukiua kwa mikono yao na kukipa mchunga wanyama akipeleke msituni huko kitaroni na akitupe huko. Kwa nguvu za mungu, mchunga wanyama naye vile akakihurumia kitoto na kukipa mchunga mwenzie akipeleke ugaibuni kikulie huko kisije kikarudi ugiriki. Huko alikopelekwa, katiwa kwenye ufalme wa korinto, nguvu ya mungu bado ingali. Mtoto kakuzwa kama mfalme mpaka anaposikia habari kutoka kwa m mpita njia mlevi kuwa polibo na merope hawakuwa wazazi wake edipode.

Kwa wasiwasi, edipode kawaendea polibo na merope kuwauliza juu ya yale aliyoyasikia na wao wakamdanganya kuwa ndio wazazi wake halisi. Edipode kaenda kuuliza kwa miungu, na habari alizopata zikamshutua. Habari zenyewe zikawa zinasema kuwa alizaliwa na laana ya kumuua babake na kumwoa mamake. Kwa hofu nyingi, akakimbia kwao ili aje aepukane na msiba huo huo. Na kukimbilia ugiriki akidhani amekimbia nyumbani bila kujua alikokimbilia ndiko palikuwa nyumbani. Na mwishowe akamua babake na kumwoa mamake na kuzaa naye wana wawili na mabinti wawili.

Kama ilivyotabiriwa, vikatukia na mji wa Thebe kuanza kuambukizwa na maradhi ya tauni  na majonzi yakajaa ufalme wote. 

Ploti ya Mchezo:

Mchezo huu unaanzia maskani kwa mfalme Edipode na mkewe Jokasta ambapo kunakuja umati mkubwa wa raia wa Thebe na kukaa kama wahitaji. Edipode anakuja na kufika walipo na kuwaomba wamwambie linalowaudhi…..(uk 1). Raia wakiongozwa na Kahini, wanamwelezea linalowakefyakefya kuwa ni mkondo wa mauti yasiyoepukwa kwanzia rutuba, malisho ya wanyama, tumbo la uzazi na maradhi yaliyo maambukizi……(uk 2). Baada ya maneno yake yote kahini, Edipode anawaonyesha kuwa anawasitikia na kuwa ashaanza mipamgo ya kutambua chanzo cha hayo yote. Anawaelezea kuwa amemtuma kreoni kwa Apolo apate kuchunguza nini ni sababu ya kuambukizwa kunakoizingia mji wa Thebe……… (uk 4). Kreoni anaingia huku akitabasamu na kuwaelezea yaliyotoka kwa Apolo kuwa chanzo cha yote ni maluuni muuaji wa Laio, na kuwa kunatakiwa atafutwe na afukuzwe ufalmeni. Edipode anaapa kuwa ataanza kufichua siri ya kifo cha mfalme Laio……(uk 7).

Anaingia ndani na jamii ya wazee wa Thebe wanaosema kwa kupokezana wanaingia huku wakiwaomba miungu wawaondolee maambukizi wote kwa utatu wao. Baada ya muda Fulani, Edipode anaingia na kusimama mbele ya wahitaji na kuanza kuwauliza ikiwa miongoni mwao kuna anayejua kuwa alihusika na kifo cha mfalme Laio. Kila mtu yu kimya…..(uk 13). Teresia anafika na kuwambia kuwa hatasema kitu na kumwambia Edipode asafishe nyumba yake. Lakini kutokana na mvutano wea maneno kati yake Edipode na Teresia, Teresia anaishia kusema kuwa Edipode ndiye najisi……(uk 15). Akaendelea kumwambia kuwa “siku ya leo itakufunulia kuzaliwa kwako na ajali pia…….” (uk 19). Wanaondoka na kunabaki wazee wakijiuliza maneno kwa kupokezana . harafu, anaingia kreoni na kuvutana na Edipode kwa maneno huku wazee wakiwatuliza pamoja na Jokasta, mpaka kreoni anapotoka….(uk 27). Edipode anamwuliza Jokasta juu ya kifo cha mmewe Laio, na Jokasta anamwambia yote yaliyofika mmewe, na kuwa kuna mtumishi aliyewambia kuwa Laio aliuawa na msafiri huko njia panda. Edipode kwa hofu anamwagiza Jokasta kumwita huyo mtumishi mchunga wanyama….(uk 32). Hapo ndipo Edipode anapowambia Jokasta na wazee yanayomhusu toka korinto kwa nyumba ya polibo na mkewe Merope, mpaka kufika kwake Thebe Ugiriki. Wazee waonyesha kutishwa na yaliyosemwa na Edipode….(uk 35).  Hapo ndipo mjumbe kutoka korinto anapoingia huku akiuliwa kwa Edipode. Wazee wanamwambia kuwa ndipo hapa….(uk 38). Habari anazowaletea akina Edipode ni kuwa babake mfalme polibo alifariki na kuwa umma wataka kumpa ufalme Edipode. Mambo yaendelea kuwachanganya wazee, Edipode na Jokasta. Lakini mjumbe kutoka korinto anawafafanulia kuwa Edipode hakuwa mwana wao polibo na merope, na kwamba kalelewa tu pale na ushahidi unaletwa na mchunga wanyama aliyemkabidhi kitoto(Edipode) kwa hofu klukiacha kiangamie huko kitaroni kama alivyoagizwa na mfalme Laio na malkia Jokasta.

Baada ya Edipode kujua kuwa alimwua babake na kumwoa mamake, Jokasta anatoka na kujifungia chumbani huku akilia na kujinyonga. Naye vile Edipode aingia chumbani na kukuta mkewe akininginia ukambani na kumtoa na kutumia vifungo vya vazi lake kujitoboa macho kwa kuvipigilia macho vifungo hivyo ili yasije tena kuona aibu yake…..(uk 51). Edipode sasa yaingia akliwa kipofu huku akilaani aliyemsaidia alipokuwa amefungwa miguu, akisema, “kufa wakati huo Baraka yangu”….(uk 54). Akaomba atolewe nje ya mji wa Thebe. Kreoni anaingia. Edipode anamwomba kuwantunza vizuri wana wake na mabinti zake wapendwa Ismene na Antigone. Akamsihi kumzika jokasta na kumwomba kumtoa nje mbali na mji wa Thebe, huku akijutia kuzaliwa kwake. Mwishoni mwa mchezo, wazee, baada ya edipode kupelekwa ndani ya nyumba na kreoni ili waanze kupata maamuzi ya mungu, wanaanza tena kusema kwa kupokezana, wakilinganisha uwezo aliokuwa nao Edipode na msiba uliomwangukia.

Wakisema……..

Kwa hiyo jueni kila mtu yampasa

Klutazamia hatima ya maisha yake

Na hakuna yeyote awezaye kuitwa

Mwenye furaha hadi siku ile ambayo

Atakwenda nayo kaburini kwa amani                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                 

MAUDHUI YALIYOMO:

Ni mambo muhimu yanayoelezwa kama vile katika hadithi, mchezo, hotuba au makala. Kwa mujibu wa mchezo huu, maudhui na mambo muhimu au makuu ambayo mtunzi Sofokile anayaeleza kupitia maandishi yake. Na ni kama yafuatayo:

  • Utabiri
  • Huruma
  • Ndoa
  • Vifo
  • Safari
  • Malezi
  • Uongozi
  • Malalamishi
  • Utumikiaji
  • Soni/haya/aibu
  • Heshima
  • Woga
  • Majuto
  • Hasira
  • Uchungaji
  • Maradhi
  • Utamaduni
  • Laana

Utabiri: ni jinsi au namna ya kubashiri mambo yatakayotokea. Katika mchezo huu, kuna utabiri kutoka kwa Apolo kuwa motto atazaliwa katika jumba la mfalme Laio na atamwua babake na amwoe mama mzazi. Na kulingana na yaliyomo, tunaona utabiri huu ukitukia kutokana na ufunuaji wa siri ya maambukizi yaliyouzingira na kuangamiza mji wa Thebe.

Huruma: humaanisha moyo wa wema. Kulingana na yaliyomo mchezoni, mchunga wanyama anakihurumia kitoto (Edipode)  baada ya kutiwa mikononi mwake na mfalme Laio pamoja na malkia Jokasta ili akitupe huko kichakani kitaroni. Anakihurumia na kukipa mchunga wanyama mwenzie akipeleke koronto kikakulie huko ili kisije kikaleta maangamizi kama utabiri ulivyosema.

Huruma nyingine ni zake Edipode baada ya kufunuliwa siri za kuzaliwa kwake, anawahurumia mabinti zake Ismene na Antigone akimwomba kreoni mjomba wao ili awatunze watoto wake wasione tabu…..(uk 59).

Ndoa: ni makubaliano rasmi ya mwanamke na mwanamume kuishi pamoja kama mume na mke. Na mara nyingi ndoa husababisha kuzaliwa kwa watoto na hujaa mapenzi tele. Katika mchezo huu, kuna ndoa kati ya mfalme Edipode na malkia Jokasta inayopelekea kuzaliwa kwa wana wawili na mabinti wawili.

Vifo: kifo ni tukio au tendo la kufikia mwisho wa uhai. Katika mchezo huu, kuna vifo mbalimbali. Kwanza kabisa, kuna kifo cha mfalme Laio kinachosababishwa na mkono wa mwanawe Edipode kama ilivyotabiriwa na Apolo.

Pia, kuna kifo cha mfalme Polibo huko Korinto ambako Edipode alilelewa. Vile vile kuna vifo vya watumishi waliotembea na mfalme Laio ambao waliuawan msafiri huko njia panda nchini Foki.

Kuna kifo cha malkia Jokasta kinachosababishwa na mikono yake mwenyewe kwa kuhofu aibu ya kuzaa watoto na mwanawe halisi, baada ya kufunuliwa siri za chanzo cha maambukizi yaliyouzingira mji wa Thebe na kusababisha maafa mengi. ….(uk 50)

Safari: ni tendo la kwenda mahali Fulani ambapo ni mbali na pale mtu alipo. Katika mchezo huu, kuna safari yake Edipode kutoka korinto kwenda Ugiriki. Kuna safari yake mfalme Laio kutoka Ugiriki kwenda Foki. Pia kuna safari yake mjumbe kutoka korinto kwenda Ugiriki huko thebe kumtafuta Edipode ili arudi kwao korinto na aurithi ufalme wa Polibo.

Malezi: ni njia ya ukuzaji wa mtoto kwa kutarajiwa kufuata tabia na mwenendo unaostahiki. Katika mchezo huu, kuna malezi anayopewa Edipode kutoka kwa wazazi wake wa kambo akina Polibo na Merope. Malezi mengine yaliyomo ni ya Jokasta na mmewe wanayowapa wana wao na hasa mabinti zao.

Uongozi: ni madaraka anayopewa mtu ya kusimamia shughuli au asasi. Katika mchezo huu kuna uongozi wa kifalme ambapo tuna mfalme Edipode kama kiongozi wa ufalme wa Thebe huko ugiriki. Kuna mfalme Polibo kam kiongozi wa ufalme huko korinto. Pia kuna mfalme Laio aliyeuawa na mwanwe Edipode kama kiongozi wa ufalme wa Thebe kabla kuja kwake Edipode.

Malalamishi: ni maelezo yaonyeshayo kutoridhika na jambo Fulani au yaliyofanywa. Kulingana na mchezo huu wa mfalme Edipode, kuna kundi ra raia wa Thebe wanaolalamikia maambukizi yanayoawfika huku wakiongozwa na kahini. Wanamlalamikia mfalme wao Edipode huku wakimwomba usaidizi ili awaondolee m,auti yanayowasimanga.

Utumikiaji: ni hali ya kutenda kazi ya kuajiriwa kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa. Kulingana na mchezo huu wa mfalme Edipode, kuna utumikiaji ambapo tunaona watumishi katika jumba la mfalme Edipode wakimtumikia malkia Jokasta na Edipode. Pia tunaona mjumbe kutoka korinto akitumikia jumba la mfalme Polibo na mkewe malkia Merope. 

Soni/Haya/Aibu: Ni jambo livunjialo mtu heshima. Kulingana na mchezo huu, kuna aibu kwa wahusika mbalimbali. Kwanza, kuna aibu kwa mfalme Edipode baada ya kufunuliwa siri za kuzaliwa kwake na kuwa ndiye najisi mwuuaji wa kipenzi mfalme Laio aliyerithi mkewe/ mamake malkia Jokasta. Jambo hili linapelekea kujitoboa macho kwake Edipode. Pili, kuna aibu kwa malkia Jokasta baada ya kugundua kuwa mtu aliyekuwa akifurahi naye kimapenzi kawa mwanake wa damu. Na kwa hivyo anaamua kujinyonga.

Heshima: ni thamaniya utu. Katika mchezo huu, tunaona raia wa Thebe wakimheshimu mfalme Edipode kwa kumtaja kama “habibi mkuu, mfalme wangu”__maneno yake kahini akiwasilisha yaliyowaleta yeye na raia wengine kwa mfalme Edipode…..(uk 2). Pia, tunaona Jokasta malkia wa ufalme akimheshimu bwana wake…..(uk 31)

Woga: ni hali ya kuwa na hofu ya kufikwa na jambo la kutisha au la tabu. Au, hali ya kutoweza kustahimili vitisho. Kulingana na mchezo huu, woga unabainika pale mfalme Laio na mkewe malkia Jokasta baada ya utabiri wa Apolo kuwa mwanao atamwua baba na amwoe mama. Kwa woga wa kitendo hicho kuwafika, wanaamua wakiue kitoto chao kichanga. Vile vile, kuna woga unaowafika pale wanaposhindwa kukiua kile kitoto kwa mikono yao ili wasije wakapata laana, na kuamua kukipa mchunga wanyama akitupe kitaroni.

Vile vile, woga unamshika Edipode baada ya kusikia utabiri kuwa atamwua baba na amwoe mama, na anaamua kutoroka korinto ili asije akamua Polibo na kumwoa Merope akidhani kuwa ndio wazazi wake halisi.

Majuto: ni huzuni inayosababishwa na kosa lililotokea. Kulingana na jinsi ilivyo mchezoni, kuna majuto ya Edipode baada ya kufunuliwa siri kuwa yeye ndiye chanzo cha mateso, anajutia kunusurika kwake kwa kifo babake na mamake walichokuwa wamempangia. Tunamwona akijutia kila kitu…………………

Ee mwanga! Laity nisikuone tena,

Kwa kuwa wazi nimekwishaonekana,

Mwenye dhambi katika kuzaliwa kwangu,

Tena mwenye dhambi katika ndoa yangu

Na mwenye dhambi kwa kumwua baba yangu!………(uk 48)

SIFA ZA WAHUSIKA:

Wahusika ni viumbe wa kisanaa wanaotumiwa na mwandishi au mtunzi kuwasilisha ujumbe wake. Katika mchezo huu wa mfalme Edipode kuna wahusika wafuatao pamoja na sifa zao:

Edipode: ni mwanao mfalme Laio na malkia Jokasta na kwa upande mwingine ni mmewe malkia Jokasta na baba yao Ismene na Antigone.

  • Ni kiongozi mtawala wa ufalme wa Thebe kwa kuwa tunamwona akisimama kama mfalme na kupewa heshima na raia wa ufalme wote wa Thebe.
  • Ni shujaa kwa kuwa anamshinda mwanamke aliyetia foara kuwanyanyasa na kwafanya watu wa Thebe watumwa kwa makafara baada ya kifo cha mfalme Laio . anawaokoa watu wa Thebe kotoka mikononi mwake.
  • Ni mwenye hekima kwa kuwa anajibu mafumbo ya mwanamke aliyetia for a kuwaangamiza wakazi wa Thebe na kuwafanya watumwa kwa makafara.
  • Ni mwenye mapenzi. Mapenzi yake kwa mkewe Jokasta na wanawe pamoja na mabinti zake. Anawaonyesha mapenzi mpaka ile saa ya mwisho wa furaha yake. Mapenzi yake kwa familia yake yanabainika pale anapowaachia kreoni awatunze wana wake na mabinti zake.
  • Ni mwenye huruma. Kwa kuwa anawahurumia watu wa Thebe kwa sababu ya maambukizi yanayowazingira na kujaribu kutafuta chanzo cha maambukizi hayo pamoja na suluhisho.
  • Ni najisi kwa kuwa anamwua babake mfalme Laio kwa kutojua huko nchini Foki kwenye njia panda moja ikielekea Delfi.
  • Ni mwenye laana ya kumwua babake na kumwoa mamake kama utabiri wake Apolo ulivyosema.
  • Ni mwenye hasira na hasira zake zinapatikan pale anapomfokea Teresia kwa maneno makali baada ya kuambia kuwa yeye ndiye chanzo cha kila teso lipatikanalo mjini Thebe.
  • Ni mwenye aibu/soni,haya.

Jokasta: ni mkewe mfalme Laio na mkewe mfalme Edipode baada ya kifo cha Laio na kurithiwa na Edipode. Ni mama yao Edipode, wana wawili na Ismene na Antigone. Ni dada yake kreoni na pia malkia wa ufalme wa Thebe.

  • Ni mwenye heshima kwa mmewe mfalme Edipode
  • Ni mwoga na woga wake unabainika pale anapoamua yeye na mfalme Laio kukiua kitoto chao kichanga ili kisije kikamwoa yeye baada ya kumwua baba.
  • Ni mpole na upole wake unapatikana pale anapojaribu kumtuliza moyo mme wake Edipode kuachana matusi kati yake na kreoni.
  • Ni mwenye mapenzi kwa mmewe Edipode.
  • Ni mwenye aibu kwa kuwa anajinyoga baada ya kufichuliwa kwa siri kuwa Edipode mmewe ni mwana wake halisi. Aibu inamfanya ajinyonge.

Kreoni: ni kaka yake Jokasta na mjomba wao Ismene na Antogone.  Ni mkwewe Edipode na Laio. 

  • Ni mpole. Na upole wake uanapatikana pale anapofokewa na Edipode baada ya kuletwa kwa Teresia. Anamjibu kwa upole ingawa yeye Edipode anamfokea.
  • Ni mwenye huruma kwa kuwa anamhurumia Edipode baada ya kujitoboa macho huklu akiomba kuwashika mabinti zake mikonono. Tunamwona anawamletea.
  • Ni mtu mwenye kukubali kazi. Kwanza anakubali kazi ya kwenda kwa Foibo mkuu kuuliza chanzo cha mateso yanayowakabili raia wa Thebe. Pia, anakubali kazi ya kuwatunza  na kuwalea wana wake Edipode hasa mabinti zake Ismene na Antigone…(uk 59)

Teresia: ni mtabiri kipofu mwenye uwezo wa kuona kile binadamu wa kawaida hawezi kuona.  Ni mzungumzaji na miungu yaani anauwezo wa kuzungumza na mungu jambo ambalo haliwezekani kwa watu wakawaida. Anaonea mbali mambo kabla hajaambiwa. Na ni mficha siri.

  • Ni mwenye hasira na hasira zake zinapatikana pale anapoamua kusema aliyokataa kusema mwanzoni baada ya kusimangwa na mfalme Edipode huku akimtwanga maswali.

Kahini: ni mmoja wao raia wa Thebe wanaolalamikia mfalme Edipode ili awaondolee mateso yanayowazingira.

  • Ni msemaji kwa niaba ya raia wengine anayeteuliwa na mfalme Edipode kuwasilisha yanayowaudhi raia wa Thebe.
  • Ni mwenye umri mkubwa na ndio sababu anateuliwa nas mfalme Edipode ili awasilishe yanayokefyakefya raia wote.
  • Ni mwenye kuheshimu. Anamheshimu mfalme wao Edipode kulingana na maneno anayotaja mwanzoni mwa hotuba yake…….(uk 2)

Mjumbe: mtumishi katika ufalme wa korinto huko kwa mfalme Polibo na mkewe malkia Merope.

  • Ni mwenye huruma kuwa kuwaalihurumia kitoto(Edipode) baada ya kukipokea kutoka mikononi mwa mchunga wanyama na kukipeleka ka Polibo kilipopatia maisha bora.
  • Ni mchungaji kwa kuwa anakutana na wachunga wanyama wengine huko kitaroni kulingana na misimu mbalimbali.

Mchunga: analisha wanyama wa mfalme Laio na mkewe malkia Jokasta.

  • Ni mwenye huruma kwa kuwa anakihurumia kitoto baada ya kukipokea mikononi mwa wazazi wenye nia ya kukiangamiza. Kwa huruma zake, anakiweka mikononi mwa mchungaji kutoka korinto ili akipeleke mbali na kwao.
  • Ni mwoga. Woga wake unapatikana pale anapotwangwa maswali na Edipode akitaka kujua asili yake. Na kwa woga, anamwambia yote yanayomhusu ambayo alifyatia ulimi miaka mingi.
  • Ni mficha siri. Ufichaji siri wake unapatikana pale anapofyata ulimi baada ya kutoka huko kataroni alikodhaniwa alikitupa kile kitoto. Vile, baada ya Edipode kupewa uongozi pale Thebe, anaamua kutoka ufalmeni akaenda kijijini kuchunga wanyama ili afiche siri yake vizuri.

Mtumishi na Watumishi: wanatumikia jumba la mfalme Edipode na mkewe malkia Jokasta.

Wazee: Jamii ya wazee wa Thebe wanaosema wote kwa pamoja na kupokezana.

  • Ni wenye upole. Upole wao unabainika pale wanapowatuliza nyoyo akina Edipode na Kreoni baada ya Teresia kufichua mambo yanayohusiana na kifo cha mfalme Laio.
  • Ni waombelezi kwa kuwa wanaonekana wakimwomba mungupamoja na miungu wao wote katika utatu wao, ili waje na wakawaondolee kuteswa na huzuni na maafa yanayowazingira.
  • Ni wenye hekima. Maneno wanayoyasema mwishoni mwa mchezo huu yenye kufundisha na yenye ujumbe mzito.
  • Ni washikaji wa imani pamoja na washikaji utamaduni.
  • Ni wazee wenye umri mkubwa.

Ismene na Antigone: wanao mfalme Edipode na mkewe malkia Jokasta.

  • Ni wenye huruma. Wanamhurumia na kumlilia baba yao kwa yote yanayomfika.
  • Ni watoto wa dhambi waliozaliwa kutokana na ndoa ya dhambi iliyolaaniwa. Ni watoto wa kaka yao.

Raia wa Thebe: ni wakazi wa ufalme wa Thebe, wenye kufikwa maambukizi ya maradhi, maafa, mateso na huzuni kutokana na laana aliyopata mfalme wao Edipode kabla hajazaliwa.

MBINU ZA UTUNZI

Hizi ni njia mbalimbali mwandishi/mtunzi anazotumia kuiunda kazi yake ili ujumbe anaolenga uwafike walengwa wake. Au, ni vipengele vinavyotumiwa na mwandishi kuwasilisha ujumbe wake. Na kulingana na mchezo huu wa mfalme Edipode, Sofokile alitumia mbinu zifuatazo:

Ushairi: hii ni sanaa ya utunzi wa mashairi. Kwanzia mwanzo wa mchezo huu mpaka mwisho wake, mwandishi ametumia ushairi huku akifuatia usawa wa mizani. Hasa pale wazee wanapozungumza kwa kupokezana.

Mazungumzo: ni hali ya kusema kwa watu wanaohusika kwa zamu. Mmoja anasema huku mwenzake akisikiliza na baadaye, anampa nafasi naye kusema huku akisikiliza. Katika mchezo huu, mwandishi ametumia hii mbinu kwanzia mwanzo hadi mwisho wake. Kwa mfano, Edipode anazungumza huku kahini na raia wengine wanasikiliza. Na baada yake, kahini anazungumza huku Edipode na raia wengine wakisikiliza.

Taswira: mbinu hii hujihusisha na ujenzi wa mawazo au picha akilini mwa msomaji kuhusu kile kinachoendelea mchezoni. Kwa mfano mtoto kuzaliwa na laana ya kumwua babake na kumwoa mamake hujenga hiyo picha ya jambo hilo kutokea akilini mwa msomaji.

Majazi: Mbinu hii huhusika na kumpa mhusika jina kulingana na sifa au tabia na matendo yake. Katika mchezo huu, mwandishi amemchora Edipode na jina lake lenye kumaanisha miguu iliyovimba kutokana na yaliyomfita alipokuwa bado kitoto kichanga.

Pia, watumishi na mjumbe wamepewa majina hayo kulingana na kazi wanazozifanya kutumikia nyumba za falme mbalmbali. Kahini haye kapewa jina lake kutokana na matendo yake ya uongo na udanganyifu. Wazee nao pia wamepewa jina kutokana na umri pamoja na matendo yao ya kizee.

Methali: Ni usemi wa kisanaa wa kimapokeo unaofikiriwa na jamii kuwa kweli na unaotumiwa kufumbia au kupigia mfano na huwa umebeba maana pan kuliko maneno yanayotumiwa.

Katika mchezo huu, mwandishi ametumia methali kama vile; hakuna refu lisilo na mwisho….(uk 60), kisichotafutwa hakionekani……(uk 6). Na kadhalika.

Taharuki: Ni mbinu ya kumwacha msomaji na hamu ya kuendelea kujua namna kitu Fulani au tukio Fulani lilivyoisha. Katika mchezo huu, mwandishi ametuacha na hamu ya kutaka kujua kilichotokea baada yake Edipode kujitoboa macho, baada ya kifo cha Polibo, baada ya kifo cha Jokasta, yaliyowafika Isamene na Antigone. Na kadhalika.

Na mbinu nyinginezo. Ukisoma mchezo huu utajaribu kuzichambua moja kwa moja ili kukuza Nyanja ya uhakiki.

N.B: Ikumbukwe kwamba mwongozo huu haubebi yote namna inavyojitokeza katika mchezo, kwa hivyo inakubidi wewe kama mtumiaji kusoma mchezo kwanza na kasha ukasome mwongozo kukusaidia kuelewa vipengele mbalimbali vinavyopatikana na ambavyo vimeangaliwa hapa ndani. Asante!!!

arigumaho810@gmail.com. +256778514179/757223817.

2 thoughts on “MIONGOZO YA TAMTHILIA MBILI=KIJIBA CHA MOYO NA MFALME EDIPODE-Timothy Arege na Sofokile.

Leave a comment