Swala la uhakiki kama fasili ya fasihi ni swala ambalo limeendelea na kukua sana kihistoria. Ni swala pana sana na ni swala lenye utata mwingi.
Uhakiki ni swala lililoendelea kwa sababu kila kuchapo panatokea nadharia au maelezo mapya kulihusu. Kwa mfano, hapo jadi palikuwa na uhakiki uliohusu umithilishi, uasilia, na urasmi.
Lakini baadaye pakaingia uhalisia, uhalisia wa kijamii, na ulimbwende.
Baadaye pia pakaja umuundo, ufeministi, uhakiki-saikolojia na uhakiki- mamboleo [post-modernism]. Hii ni mifano tu, kwani kila mara panatokea nadharia mpya ya kuhakiki kazi za fasihi na hata zile za awali kuboreshwa.
NADHARIA YA UHALISIA-NAFSI
Miongoni mwa vigezo vinavyotumiwa katika kuianisha fasihi ni kuiona fasihi ile kama
zao la mtunzi binafsi. Fasihi kwa mtizamo huu huzingatia saikolojia na sifa za mtunzi huyo.
Kigezo hiki kimezingatiwa hasa katika nadharia ya tathimini saikolojia . Ni wazi kwamba chanzo cha kazi ya sanaa ni yule anayeiumba, yaani mtunzi wake, na hivyo basi maelezo yanayopatana na hulka na maisha ya mtunzi yamezingatiwa kwa muda mrefu sana kama nguzo moja ya kueleza maana ya fasihi.
Waanzilishi wa nadharia hii hushikilia kwamba kazi ya fasihi yaweza kuelezeka tu iwapo itazingatiwa kwa mkabala mmoja na maisha ya mtunzi wake. Hivyo basi fasihi huonekana kama kielelezo cha uhalisia wa maisha, jinsi yanvyotafsiriwa na nafsi ya mtu bila kujali ukweli kama unavyodhihiri kwa nje.
Jinsi mtunzi anavyojieleza kupitia kazi ya fasihi linakuwa jambo muhimu katika nadharia hii. Katika mtizamo huu huu, fasihi imezingatiwa kama hisi; yaani ni kielelezo cha
hisi za mtu binafsi (mtunzi). Jinsi mtu anavyoona na kuyahisi maisha linakuwa jambo la kuzingatiwa kama fasihi.
Wataalam wa jadi wa fasihi kama vile Aristotle wanashikilia wazo hili hili kuhusu fasihi.
Aristotle aliamini kwamba fasihi au ushairi hasa ni utanzu ambao kwao binadamu hutoa hisia zake za ndani kuhusu maisha. Hivyo basi ushairi
ukawa ni kielezo cha uhalisia wa nafsi ya mtunzi, jambo ambalo limezingatiwa katika
kueleza fasihi ni nini.
Hata wahakiki wanaozingatia nadharia ya tahakiki-saikolojia kama vile Sigmud
Freud wanashikilia kwamba kazi ya fasihi ni kielezo cha ndoto na matamanio yasiotimizwa ya mtunzi. Yaani kazi ya fasihi si chengine bali imejaa ndoto za mtunzi pamoja na majaribio ya kutimiza matamanio yake. Kwa mtizamo huu, fasihi ni hisi, hisia na mataminio ya mtunzi; yaani maisha yake. Hapa ndipo twapata hata biografia zikichukuliwa kama kazi za fasihi.
Mtazamo mkuu kuhusu fasihi haujapokelewa kwa mikono miwili na baadhi ya wataalam.
Jefferson (1982:99) anasema: Utunzi na usomaji wa fasihi hauna uhusiano wowote na nafsi halisi ya mtunzi na fasihi huwepo bila kutegemea mazingara halisi pamoja na hulka
ya mtunzi. [tafsiri yetu]
Kwa hivyo, kazi ya fasihi haina uhusiano wowote na nafsi ya mtunzi wake. Anasema kuwa kazi ya fasihi hujisimamia yenyewe kama kazi ya fasihi na haihitaji kuhusishwa na
mtunzi wake ili kueleweka ama kutungwa. Lakini hatuwezi kulitupilia mbali wazo hilo
kwani kila kitendo cha kutunga hutokana na fikira, maoni, tajiriba, na hisia za mtunzi, jambo ambalo lina ubinafsi maalum unaodhihiri, japo kwa kiwango duni, hulka ya
mtunzi huyo.
Nao Wellek na Warren (1949:78) wana maoni haya kuhusu mtizamo huo wa fasihi:
Wazo kwamba sanaa kwa ujumla ni uhalisia-nafsi unaotoa hisi na tajiriba za mtu, ni la kupotosha. Hata panapotekea uhusiano wa karibu sana kati ya sanaa na maisha ya mtunzi, hili lisichukuliwe kumaanisha kwamba sanaa ni mwigo wa maisha.
Mtazamo huu husahau kwamba kazi ya sanaa ni kazi kivyake wala si kusanyiko la tajiriba za mtunzi.
Maoni ya wataalum hawa yanadhihirisha wazo la awali kwamba fasihi ni kazi inayojisimamia na iliyo na kaida zinazoitawala.
Hivyo basi, tamthilia, riwaya au shairi huwa zinaongozwa na kutawaliwa na kaida za kifasihi zinazohusu kila utanzu.
Ukichunguza mtazamo huu kuhusu fasihi twaona kwamba unapuuza baadhi ya hoja halisi za kimantiki. Kazi ya sanaa huenda ikawa si maisha halisi ya mtunzi bali ni maoni au mtizamo wake kuhusu maisha.
Huenda ikawa pia ni kinyago cha kuficha nafsi yake halisi au huenda ikawa picha ya maisha anayotaka kuyakimbia.
Isitoshe, tusisahau kwamba huenda tajiriba ya maisha halisi ya mtunzi ikawa tofauti na ile ya sanaa; yaani tajiriba halisi maishani hutizamwa kwa jinsi ambavyo zitafaa fasihi na huwa kwa kiasi fulani zimeongozwa na kuathiriwa na kaida za kisanaa zinazotawala kazi yake. Ama kweli kazi ya fasihi inayoorodhesha matukio kama yalivyo bila usanii si sanaa bali ni kumbukumbu au historia.
Hata hivyo hatuwezi kupuuza kabisa kigezo hiki kwani kinachangia katika
kueleza fasihi ni nini. Lililo muhimu kutambua ni kwamba kigezo hicho hakiwezi kutumiwa peke yake kueleza fasihi ni nini. Ni lazima kihusishwe na vigezo vingine mbali mbali ili kutoa picha kamili na pana ya fasihi.
NADHARIA YA MGUSO.
Mtazamo mwingine kuhusu fasihi ambao twaweza kuuita wa umbo la nje ni kuitizama fasihi katika uhusiano wake na umma wake ambapo msisitizo unatiliwa mguso unaotolewa na kazi ya fasihi kwa hadhira yake.
Kila kazi ya fasihi hulenga kwa njia moja au nyengine mtu au watu fulani (hadhira) hata kama hadhira hiyo ni nafsi ya mtunzi husika. Kazi ya fasihi hutoa mguso wa aina fulani kwa hadhira ili ifikirie na kujiuliza maswali au hata kutoa funzo fulani.
Kwa kuunga mkono maoni haya, Vasquez, A.S (1973:113) anasema: …. kazi ya sanaa huathiri watu na inachangia katika kuhimiza au kupuuza dhana zao, maazimio yao, hata maadili yao – ina msukumo wa kijamii ambao huathiri watu kwa nguvu
19zake za kihisia na kiitikadi. Ama kwa hakika, hakuna anayebaki vile vile baada ya `kuguswa’ na kazi ya halisi ya sanaa.
NADHARIA ZA KI-MARX.
Anachokisema mhakiki kuhusu kazi anayoizingatia, hutegemea kwa kiwango kikubwa, dhana anazozileta katika kazi hiyo.
Aghalabu, dhana hizi haziwi za moja kwa moja, lakini mhakiki anayeegemea uhakiki wa Ki-marx huwa anafahamu kwa hakika anachokizingatia kwani kazi yake itaongozwa na falsafa fulani zilizopo.
Kazi yake itaongozwa na mtizamo wa Ki-marx kuhusu historia, ambapo mikinzano ya kitabaka huwa jambo muhimu na vile vile uhusiano kati ya fasihi na muundo wa Kiuchumi katika jamii husika lazima udhihirishwe.
Kwa jumla, twaweza kusema kwamba mhakiki wa Ki-marx hukita nadharia yake kwenye itikadi za Karl Marx na Fredrick Engels, na hasa kwenye madai ya hao wawili kuwa, katika tathimini ya mwisho kabisa maendeleo ya historia ya binadamu pamoja na taasisi zake, yatakuwa ni tokeo la mabadiliko katika njia za kimsingi za uzalishaji mali.
Kwamba mabadiliko kama hayo husababisha mageuko katika muundo wa matabaka ya kijamii ambayo katika kila kipindi huendeleza kung’anga’aniwa kwa uwezo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii; na kwamba dini, fikra na utamaduni wa jumuiya yoyote (zikiwemo sanaa na fasihi kwa kiwango fulani) huwa ni itikadi' na miundo maalum yakitabaka’ ambayo ni zao la miundo na matabaka ya kijamii yaliyomo wakati huo.
Umarx huchukua kwamba jamii zote za kitabaka huzalisha mkururo wa miundo ya urazini inayokinzana na kushindana.
Katika jamii ya kikapitolisti, kwa mfano, aina tofauti za mitizamo kuhusu maisha huwakilisha haja tofauti za kitabaka ambazo hutegemea hasa mikinzano kati ya mapato na nguvu za kutenda kazi.
Kwa hivyo Umarx huhusisha itikadi na uzalishaji mali na jukumu lake katika mivutano ya kisiasa katika jamii. Jinsi watu binafsi wanavyoelewa msingi wa maisha yao hutokea kuwa kamba ya mvutano ambapo wanaweza ama kubadilika au kuendelezwa.
Kwa mfano, chini ya mfumo wa kikapitolisti, wafanyakazi wanashurutishwa kuuza uwezo wao wa kufanya kazi kwa wale wanaotawala mazao pamoja na huduma. Katika mpangilio huu,
wanaotawala nguzo za uzalishaji mali hunufaika kupitia kwa dhamani ya ziada iliyozalishwa na wafanyakazi. Hii ni kati ya mali inayobakia baada ya kuondoa matumizi ya malighafi, mashine, na nguvukazi. Aidha faida hupatikana kwa kuwalipa wafanyakazi malipo ya chini kuliko dhamani ya kazi waliyofanya.
Uhakiki wa ki-marx hujishughulisha na tabaka la kiuchumi na sababu za kiitikadi zinazotawala jinsi mtunzi hufikiria na kuandika, lakini hasa huzingatia uhusiano wa kazi
ya fasihi na uhalisi wa kijami uliopo wakati huo. Kama tokeo basi uhakiki wa Ki-marx hudai kwamba watunzi wanapaswa kumithilisha hali halisi ya maisha ya jamii wanazotungia.
Wazo hili lilipingwa hata na wafuasi wa Marx. Mmoja kati yao ni
mtaalam kutoka Hungary, George Lukac aliyekuwa na maoni kuwa badala ya fasihi kuimithilisha hali ya maisha, fasihi na sanaa zapaswa kuwa `picha ya uhalisi’. Ambapo
picha hiyo inakiuka misingi ya kuiga moja kwa moja uhalisi.
Mhakiki wa Ki-marx, hivyo basi, tayari ametolewa picha halisi ya maisha. Shida aliyo nayo ni jinsi ya kuikabili na kuihakiki fasihi. Wahakiki wa ki-marx aghalabu
wameiona fasihi kama iliyo halisi, hivi kwamba mtunzi wake huwa anajitenga na kuonyesha makosa katika jamii.
Mbinu inayotumiwa na wahakiki wa jadi wa ki-marx ni kuunda tena mtizamo kuhusu yaliyopita kutokana na ithibati za kihistoria kisha
wakadhihirisha uhalisi wa kazi fulani kama kielelezo cha jamii na kama njia ya kuelewa uhalisi wa kijamii.
Kwa jumla uhakiki wa ki-marx huhusisha kazi ya fasihi na mtazamo wa uhalisia wa kijamii wa wakati kazi hiyo ilitungwa. Vile vile uhakiki huu zaidi huzingatia maudhui katika fasihi huku pakitolewa uhakiki wa maadili, na njia za kuyaboresha
maisha zilizoshughulikiwa. Ni muhimu kutaja kwamba pana aina mbali mbali za nadharia za uhakiki za ki-marx.
Lakini licha ya wingi wa nadharia hizi, nadharia zote za ki-marx zina nguzo moja iliyo sawa; kwamba fasihi hueleweka tu katika msingi wa
uhalisi wa kijamii hasa katika umilikaji mali. Wahakiki wa ki-marx hushikilia kwamb nadharia yoyote inayozingatia fasihi kwa kuitenga (kwa mfano kama kazi ya kimuundo
au kama zao la mkondo wa fikra za kibinafsi za mtunzi) na kuiweka katika hali hiyo huku ikitenganishwa na jamii na historia, huwa ni pungufu katika uwezo wake wa kueleza hasa fasihi ni nini.
Kwa wahakiki wa ki-marx uhalisi wa kijamii si chombo ovyo ambamo fasihi hujengeka na kutokea bali huchukuliwa kama ulio na umbo maalum, na umbo hili hupatikana katika historia ambayo kwa maoni yao ni mkururo wa mivutano kati ya matabaka yanayokinzana na njia za kiuchumi za kuzalisha mali ambazo zinazingatiwa katika jamii husika. Umbo hilo hupatikana pia katika hali yoyote ile ya jamii kwani mahusiano maalum ya kitabaka na hali halisi za kisiasa, kitamaduni na kijamii huchukuana na mfumo uliopo wa kuichumi kwa njia husishi.
Upungufu wa nadharia hizi hutokea katika kuchagua kiwango cha maisha kitakachozingatiwa kwani ni vigumu kwa kazi ya fasihi kuzingatia maisha ya jamii katika ujumla wake. Kwa mfano iwapo mtunzi atachagua kuonyesha starehe na buraha ya maisha ya tabaka tawala bila kuonyesha uchochole wa tabaka linalotawaliwa, atakuwa anakiuka misingi ya kutoa picha halisi ya maisha ya jamii? Ufinyu wa mtizamo wa kimarx ni muweka jamii katika vikundi viwili kuu ambavyo yamkinika ni sawa. Yaani yaelekea kuwa wanatabaka la juu wote wamefanana kwa njia zote, na vivyo hivyo kwa wanatabaka la chini. Hapa ndipo ahakiki wa kifeministi wanaposema kwamba umarx unaepuka kuona kwamba hata katika maisha ya tabaka la juu wanawake hawakuwa na uhuru/nafasi sawa na wanaume. Hata hivyo tutaje kwamba msisitizo wa nadharia za ki-marx kuhusu umuhimu wa
mikinzano na migongano ya kitabaka umeathiri wahakiki wengi wa kijamii ambao hawazingatii itikadi za ki-marx.

Shukrani sana, naomba Mwongozo wa Janga la werevu
LikeLike
Nashukuru…nitashughulika
LikeLike
Nilikuwa nimekutumia barua pepe angalia…
LikeLike
Sawa kakangu
LikeLike
Kb
LikeLiked by 1 person
Asante sana kwa kazi nzuri. Je, Nadharia ya Umaubo?
LikeLike
Nitaishughulikia
LikeLike
Asante Sana kufundisha dunia na kiswahili.lakini simu yako??
LikeLike
Karibu ndugu. 0778514179
LikeLike
Shukran sana, Mwalimu! Ama kweli, makala yenu hii ni ya kushibisha pia ya kushirikisha. Mjadala mkali miongoni mwa wataalam kama vile Jefferson na wengine juu ya mitazamo ya kifasihi, yaonekana kujibiwa nawe sasa.
Hongera sana mno!
LikeLike
Karibu Sana Ndugu Iradikunda.
LikeLike