Nadharia ya Uchanganuzi makosa na uakili.

NADHARIA YA UCHANGANUZI MAKOSA.

Stephen Pit Corder (6 Oktoba 1918 – 27 Januari 1990) alikuwa profesa wa isimu katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, anayejulikana sana kwa mchango wake katika uchunguzi wa uchanganuzi makosa. Alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Chama Cha Uingereza cha Isimu tumizi, 1967-70, na alisaidia sana katika kuendeleza taaluma ya isimu-tumizi nchini Uingereza.


Wanafunzi wanaojifunza lugha ya pili hufanya makosa mengi yakiwemo matamshi mabaya ya maneno.
Kutokana na hali hiyo, wanaisimu wamekuwa katika mstari wa mbele kubaini chanzo cha makosa na vilevile kubuni mbinu faafu zinazochangia katika kutatua matatizo hayo.
Uchanganuzi Makosa Mtazamo wa Uchanganuzi Makosa uliasisiwa na Corder na wenzake miaka ya 1960.
Mtazamo huu uliibuka kukidhi upungufu wa uchanganuzi linganuzi uliotumiwa na wanaisimu kutofautisha lugha ya kwanza na ya pili ya mwanafunzi ili kukisia makosa.
Uchanganuzi makosa ni mbinu itumiwayo kuthibitisha makosa yanayopatikana katika lugha ya mwanafunzi.
Walimu wa lugha wanaowasikiliza wanafunzi wao wakizungumza hutambua makosa. Ukweli ni kuwa kila mtu hufanya makosa anapoongea hata walimu na wazawa wa lugha hufanya makosa.
Wazawa wa lugha hawafuati kanuni za sarufi zilizoandikwa vitabuni.
Uchanganuzi makosa, huchunguza aina ya makosa na visababishi vya makosa hayo. Kulingana na mwanaisimu Corder, mtafiti hufuata hatua zifuatazo katika uchanganuzi makosa:

  1. Kukusanya sampuli ya kazi ya wanaojifunza lugha 11
  2. Kutambua makosa
  3. Kueleza makosa.
    Makosa yanawekwa katika makundi na kuelezwa kisarufi.
    Hivyo makosa yenyewe ndiyo hutumiwa katika kuainisha kategoria za kisarufi.
  4. Kufafanua chanzo cha makosa haya.
  5. Kutathmini / kuyasahihisha makosa haya ili kujua jinsi ya kukabiliana nayo.
    Tunapowasikiza wanafunzi wakizungumza tunafahamu makosa wayafanyayo. Kwa sababu hii ni vyema kujiuliza kile mzungumzaji alikusudia kukisema na angekisema vipi. Kusahihisha makosa haya sio jambo rahisi kwa sababu kuna zaidi ya njia moja ya kufanya hivyo.
    Kusahihisha makosa kunategemea kile msikilizaji anafikiri mzungumzaji alikusudia kukisema na kosa lenyewe.
    Ni vyema kufikiri namna nyingi tofauti za kusahihisha makosa. Kwa sababu huna uhakika wa kilichokusudiwa, mwache mwanafunzi akusaidie kuamua sahihisho sahihi.
    Kufafanua makosa haya, kwataka kujua kisababishi. Makosa yanaweza kutokana na kuhamisha kanuni au ruwaza za lugha ya kwanza.
    Makosa mengine yanaweza kusababishwa na jinsi mwalimu au vitabu vya kaida vinavyoeleza kanuni fulani.
    Au inaweza kuwa mikakati ya mawasiliano anayotumia mwanafunzi hata kama anajua kanuni anazotumia sio sahihi. Utafiti huu si linganishi kwa sababu hatujalinganisha lugha mbili ili kutambua makosa.

NADHARIA YA UAKILI (Ubunifu wa Lugha)
Hii nadharia inadai kwamba kila mtumiaji wa lugha ana uwezo wa kuzalisha sentensi nyingi na mpya kabisa zilizo sahihi kisarufi na ambazo hajawahi kuunda hapoawali.

Vilevile, anaweza kuelewa ujumbe uliomo katika sentensi nyingi tena mpya kabisa ambazo hajawahi kusikia hapo awali.

Hii inamaanisha kwamba, sio jambo la kawaida watu kuiga semi ambazo wamewahi kuzisikia zikisemwa bali wao hubuni semi zao mpya huku wakiongozwa na kanuni za Kifunza-Lugha.

Ukweli huu umewapelekea baadhi ya watafiti kudai kwamba ni kiasi kidogo sana cha sintaksia ya lugha ambacho mtu anaweza kufunzwa, kwani ni mambo mengi sana ambayo yeye mwenyewe hujigundulia.

UHAKIKI WA NADHARIA YA UAKILI.
Nadharia ya Uakili inatupa mwangaza zaidi kuhusu nafasi ya akili katika kumwezesha mtu kujifunza lugha.

Hata hivyo, bado haijulikani kikamilifu jinsi Kifunza-Lugha hufanya kazi. Pia sifa nyingi za sarufi bia bado hazijagunduliwa.
Isitoshe, ingawa nadharia ya Uakili imeelezea kwa kirefu jinsi watu hujifunza sarufi ya lugha, haijaelezea waziwazi jinsi watu hao hujifunza maana za maneno na sentensi katika lugha.

Nadharia hii pia ina udhaifu kwa sababu inafafanua matumizi ya lugha pasipo kuzingatia muktadha wa kijamii.
Wanaisimu-jamii wamedai kwamba matumizi ya lugha hayaathiriwi tu na akili ya mwanafunzi bali huathiriwa pia na sababu mbalimbali za kijamii.
Sababu hizi nipamoja na mielekeo, mazingira, jinsia, athari za kimakundi na utamaduni.

Leave a comment