Sikimbilie kulea
Usinione mzazi,ukadhania rahisi
Hakika hino ni kazi,isiyo nao wepesi
Ukijaribu huwezi,ndugu utakwenda kasi
Jipe muda ndugu yangu,sikimbilie kulea.
Kulea kuna gharama,sio bwerere ni ghali
Kujituma ni lazima,changamoto kukabili
Kupo ndu yangu kukwama,sikufichi kiukweli
Jipe muda ndugu yangu,sikimbilie kulea.
Sikiliza kwa makini,nakuomba ufahamu
Kulea sio utani,tambua ni hali ngumu
Kulea ja u vitani,kujihami ni muhimu
Jipe muda ndugu yangu,sikimbilie kulea.
N’omba uwe na subira,usije ukasumbuka
Kulea kuwe ni bora,na kwepesi kwa hakika
Ukuwe mlezi bora,tena kwa kumakinika
Jipe muda ndugu yangu,sikimbilie kulea.
Namalizia kulonga,haya yatosha rafiki
Mbele mie sitasonga,ila jepushe na dhiki
Mapema anza jipanga,uipeke dhihaki
Jipe muda ndugu yangu,sikimbilie kulea
