USINGOJEE UGANDA MPYA au FULANI KUKULINDIA KESHO YAKO
.Hii ni makala maalum kwako wewe mhitimu mpya. Nakuandikia makala hii katika kipindi ambacho vyuo vingi nchini UGANDA vitakuwa katika msimu wa mahafali au graduation wakti mchache mbele hapo. Ni kipindi cha furaha kubwa kwako, na kwa ndugu, marafiki na walimu wako pia. Kifupi, hiki ni kipindi muhimu sana kwako, ambapo unavuka rasmi mstari unaotenganisha maisha ya chuo na maisha halisia nje ya darasa.
Katikati ya furaha hii, ukiwa unasheherekea kumaliza chuo na kutunukiwa cheti, stashahada, shahada ya kwanza au shahada ya uzamili, usije ukajisahau. Unapaswa kukumbuka kuwa sasa ndio unaingia rasmi kwenye ‘maisha halisia’. Ndio, una shahada, lakini hicho unachopewa mkononi ni kipande cha karatasi tu ‘kinachovutia’. Usipoweza kukibadilisha kuwa pesa kitabaki kikaratasi tu, na hakitakuwa na maana.
Juzi juzi katika gazeti moja la nchi jirani limekutana na maoni ya msomaji mmoja wa gazeti hilo yakisema, “mimi kama mmoja wa wahitimu wa chuo kikuu, BISHOP STUART wakati fulani nawaona watoto wamevalia sare zao nzuri wanaenda shule…najiuliza hivi hawa wanasoma ili waende wapi…wakati mimi nazunguka na vyeti vyangu kutoka ofisi moja kwenda nyingine mjini humu Kampala wala sijaiona hiyo ajira”.
Hapa Uganda pia katika mtandao mmoja nimekutana na bango lililobebwa na kijana mmoja likiwa limeandikwa, “ndugu zangu WanaUganda naombeni ajira…ni mimi mwalimu wa kiswahili (mtaalamu wa lugha na fasihi) ambaye sina mtu wa kunishika mkono.” Huyu ni mmoja wa vijana wengi wanaomaliza vyuo, wanaingia mtaani kutafuta kazi. Je unajua mtaani kukoje?b
Lengo la makala hii ni kukutaarifu wewe mwanachuo unayeingia mtaani, kuwa ajira (kuajiriwa) kwa sasa zinazidi kuadimika. Hii inatokana na idadi ndogo ya ajira zinazozalishwa katika uchumi kupitia sekta binafsi na sekta za umma…ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka. Vilevile nakusudia kutoa maoni ya nini cha kufanya.
Kimsingi kuna changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi kwa sasa. Ni changamoto ya ukosefu wa ‘ajira rasmi’ serikalini, katika mashirika ya umma/binafsi, au katika taasisi zingine. Na kwa kuzingatia hili ndio maana tunasema ni wakati sasa vijana wetu wajitambue, na wayajue mazingira yalivyo sasa ki-uhalisia ili wachukue hatua stahiki.
Hapa kuna vitu kadhaa vya kujadili. Wakati fulani unaweza kuinyooshea kidole serikali, kwa kushindwa kuwa na mikakati ya kuzalisha ajira katika uchumi. Tena unaweza kuwanyooshea kidole wazazi, kwa kuwasisitizia watoto njia moja tu, ya elimu ya darasani, kama msingi wa maisha yao. Au unaweza kuinyooshea kidole mitaala ya vyuo, au walimu, kwa kushindwa kuwapa watoto stadi za maisha nje ya darasa.
Kutokana na hayo, ni muhimu sasa kuzingatia kuwa, pamoja na maarifa ya darasani, watoto wajifunze pia maarifa nje ya darasa, yaani wayajue maisha halisi, ya mtaani. Haya ni maisha ya kutumia akili na ubunifu binafsi…na yakichanganywa na yale ya darasani, mseto unaopatikana una tija kubwa.
Mwandishi Scott Berkun anaandika kwamba kuna aina mbili ya watu ‘smart’ (wenye akili). Kuna Book Smart na Street Smart . Anasema book smart ni mtu mwenye akili au maarifa mengi ya darasani. Kwa bahati mbaya haya ni maarifa yaliyochaguliwa na watu fulani, kwa lengo lao fulani. Wanampatia mtu maarifa haya kwa kiasi na utaratibu fulani, ili akifaulu awafanyie kazi yao fulani kwa utaratibu fulani, halafu wanamlipa mshahara fulani.
Mhitimu huyu akiajiriwa anafanya kazi kwa miongozo maalum (rules, theories au principles) aliyofundishwa. Huyu akipata tatizo, haraka anakimbilia kusoma miongozo inasemaje, na anaifuata hiyo ili kutatua tatizo. Anapofikiria kupanda cheo anaomba kwenda kusoma shahada ya juu zaidi ambako anafundishwa theories na principles mpya ili azitumie akiwa katika nafasi ya juu kazini.
Watu ambao ni book smart , hupenda sana kijiendeleza kielimu kwenye fani zao, na wengi ni wazuri sana darasani, na ndio maana baadhi ya waajiri huwatafuta hawa inapotokea nafasi ya kazi. Tatizo la hawa, wasipoajiriwa, hawana plan B, na hii huwachanganya sana. Hawa huwa hawana macho ya kuona zaidi ya ‘upeo wa ajira’. Hawazioni fursa na wakitokea kuoneshwa hawana ujasiri wa kupambana.
Kwa upande mwingine kuna street smart. Hawa ni wale vijana ambao wanaweza kuwa na elimu ndogo tu, lakini wana maarifa ya ziada kichwani. Haya ni maarifa ya nje ya darasa. Watu hawa wana uwezo mkubwa wa kujenga fikra bunifu (imaginations), na kuziona fursa. Hawa wana ujasiri/uthubutu wa kuanza na kupambana ili kuyatafsiri mazingira yao kuwa kipato.
Maisha ya vijana hawa huwa hayana kanuni maalum wala hayaongozwi na principles – bali ujasiri na uthubutu. Vijana hawa, kwa kutumia fikra bunifu, wana uwezo wa kuanzisha biashara yoyote…wakaongeza kitu juu ya biashara hiyo…au wakapunguza, kulingana na mazingira yalivyo, na kwa kufanya hivi wakajitengenezea kipato kizuri kwa ajili ya maisha yao.Sasa jichunguze mwenyewe, hivi wewe ni book smart au street smart?
Ukiichunguza mitaala ya elimu yetu utaona kuwa bado ina misingi ile ile ya kikoloni – yaani kuwaandaa vijana wachache, kwa kuwapa elimu ya darasani inayolenga kuwapatia wahitimu maarifa yanayotakiwa katika kufanikisha shughuli zao za kiutawala, na siyo kuwapa maarifa ya kuwawezesha kujitegemea.
Kwa hiyo hata sasa vijana wanaendelea kuamini katika hili – kwamba wanasoma ili waje kuajiriwa. Kwa aina hii ya mtaala kijana akimaliza chuo anabaki na elimu ya darasani tu. Hana maono…hana fikra bunifu…hazioni fursa na hivyo hawezi kujiajiri. Huyu asipoajiriwa anaona huu ndio mwisho wa dunia!
Sisemi kwamba kujiajiri ni kitu rahisi, hapana, sio rahisi na kuna changamoto nyingi, hasa kwa wanaoanza, na hasa wanaotoka katika chungu cha taaluma, vyuoni. Kuna suala la mtaji, ushindani katika soko, uzoefu mdogo wa biashara, na uwezekano wa kupata hasara kwa kile unachokifanya.
Wala sijasema maarifa ya darasani sio muhimu, la hasha. Ninachosema ni kwamba kila mtu ajitahidi kupata elimu ya darasani, lakini wakati unaingiza maarifa haya usisahau kuwa kuna maarifa mengine muhimu pia nje ya darasa. Ukiwa na maarifa haya unakuwa na balance nzuri katika maisha, na utaepuka kuwa tegemezi wa ajira pekee.
Vijana wenye maarifa nje ya darasa utawaona jinsi ‘wanavyochacharika’ na kujaribu kila kinachowezekana. Hawa huwa hawaoni haya, hawaogopi jua, vumbi wala mvua. Vijana hawa hawachagui kazi – wao kilicho muhimu kwao ni kipato halali na matamanio ya ‘kutoboa’. Hawa si watu waoga, ni watu wenye ujasiri na uvumilivu.
Vijana hawa utawaona wakikaanga chips , samaki, chapati, pan au mihogo na kuitembeza mitaani. Wengine utawaona wakiuza juisi za miwa na wengine wakitengeneza sabuni na viungo vya mboga. Utawaona wengine wakilima bustani za mboga na wengine wakipamba maharusi na kupika vyakula vya sherehe, ili mradi kila mmoja anaingiza kipato na kuendesha maisha yake.
Wengi wa vijana hawa hawana vyeti vya kitaaluma kutoka vyuoni, wanatumia uzoefu wao wa maisha ya ‘kitaa’. Sasa wewe ‘msomi’ ukiingia mtaani na majivuno yako ya vyeti vya stashahada au shahada, utabaki unashangaa! *Wakati unamaliza soli za viatu ukizunguka na bahasha yako ya kaki, au ukijibizana na wadogo zako mkigombea remote ya TV, ukisubiri msosi, vijana hawa wako mtaani wakiingiza. pesa
Ni aibu kwa msomi wa chuo kikuu kuwa tegemezi kwa wazazi au ndugu zako. Tena wapo wasomi ambao hawana hata aibu, huwasumbua vijana waliowaacha mtaani, ambao wengine ni darasa la saba tu, wakiwaomba hadi hela ya nauli, kwenda mjini kampala kutembea kupeleka barua zao za maombi Shule fulani Kibuli🤦♀️🤦♀️, kampuni fulani Namanve😅😅 , Jibunie ndugu….
Msomi usieweza kuziona fursa na kuzichangamkia, wewe ni msomi butu. Unazidiwa na kijana wa darasa la saba, halafu unajitutumua hapa…! Mimi nilipata shahada ya uzamili MAKERERE halafu inabaki huko Kikoni ukila vikomando na kutisha mawe kwenye magari ya rais KYAGULANYI😂😂😅😅Hivi maana ya elimu ni nini? Elewa usomi sio vyeti, ni uwezo wa kutengeneza vitu au thamani katika jitihada za kujitengenezea kipato.
Hatua ya kuchukua: kijana unaliyemaliza chuo na sasa unafanya mahafali una kitu muhimu cha kujifunza. Kitu hicho ni kujitambua. Tambua kwamba wewe ni msomi, na una maarifa, lakini kwa mfumo wetu wa elimu, bado unatakiwa kujiongeza. Jiepushe na kushupaza shingo kwa kufikiria ajira peke yake…kwani ajira hazipo za kutosha sokoni. Unapaswa kuelewa kuwa watu wanakwenda shule ili kupata maarifa, siyo kazi. Kazi ikitokea… sawa!
Ile kasumba inayokumbatiwa na wazazi wengi, kwamba mwanangu nakupeleka shule/chuo kizuri, soma kwa bidii ‘masomo ya maana’ ili ufaulu vizuri mitihani, upate alama za juu, baadaye kidogo utaajiriwa na kampuni nzuri, na utalipwa mshahara mkubwa, imepita! Hali imebadilika sasa. Ndio maana tunahimiza vijana wajifunze stadi za maisha ili wawe na mbinu mbadala za kupambana na kujitengenezea kipato bila kusubiri ajira.
Eti Mimi namungojea kunilindia kesho😂😂
Angalia Uganda mpya tu✊🏾✊🏾
jifunzekiswahiliart.wordpress.com
Uyaache yasiyokuhusu.
arigumaho810@gmail.com
